Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Ignas Aloyce Malocha

Supplementary Questions
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyomudu nafasi yake na anavyochanganua majibu mbalimbali. Hata hivyo, nataka kumshauri aiangalie sana ofisi yake inayotoa majibu ya maswali, ni jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameelekeza taratibu tunazotakiwa kuzifuata na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishazifuata, Mikutano ya Vijiji, Mikutano ya Madiwani, Mikutano ya DCC, Mikutano ya RCC na vigezo vipo na Bunge linajua hivyo na tulishaomba. Nataka aniambie ni lini wananchi wale watapata Wilaya mpya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, haoni kwamba kitendo cha kuunganisha Wilaya, Sumbawanga Mji na Sumbawanga Vijijini ambazo jiografia zake ni ngumu kunamfanya Mkuu wa Wilaya asiweze kumudu nafasi yake na hatimaye wananchi wa Wilaya wa Sumbawanga Vijijini kucheleweshwa kimaendeleo?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilishatuma maombi ya kugawa Halmashauri ambayo iliambatana na maombi ya Wilaya, Jimbo na kupitia vikao vyote kuanzia Vijiji, WDC, DCC, RCC na kuonekana kwamba, ina vigezo vyote na hata watawala ambao wametawala maeneo hayo wanaujua ukweli huo; kwa mfano Mheshimiwa Manyanya, Mheshimiwa Mkuchika, hata baadhi ya Wabunge ndani humu, hata Waziri Mkuu aliyepita alishashuhudia ndani ya Bunge. Je, ni lini wananchi hawa watapata haki yao ya kugawanya Halmashauri?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ahadi nyingi zilizotolewa na viongozi kuanzia Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na sasa Awamu ya Tano. Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuandaa ahadi hizo kwa kutengeneza kitabu cha mpango wa utekelezaji na sisi Wabunge tukagawiwa?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Sera ya Serikali ni kuwa na chuo cha ufundi VETA kila Wilaya lakini hadi sasa ipo baadhi ya Mikoa haina hata chuo kimoja cha ufundi VETA kwa mfano Mkoa wa Rukwa.
Je, Serikali ina mpango gani, wa kiuwiano wa kuhakikisha Mikoa yote ambayo haina vyuo vya ufundi VETA inapewa kipaumbele kwanza?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya 2016/2017, miradi mingi ya umwagiliaji iliyokuwa imeanza katika hatua za awali katika Halmashauri zetu na kuombewa fedha haikupangiwa fedha; kwa mfano, katika Jimbo langu, mradi wa Nkwilo, mradi wa Uzia, mradi wa Nzogwe, mradi wa Mkanga na mradi wa Momba.
Je, Serikali ina mpango gani mbadala wa kuifanya miradi hii iweze kuondelea ili wananchi waweze kuondokana na tatizo la njaa na kukuza uchumi wao na Taifa zima kwa ujumla?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kumekuwa na taarifa zilizotapakaa katika mitandao ya kijamii zinazoeleza ugunduzi wa gesi aina ya helium. Je, Serikali inaweza kutueleza nini juu ya taarifa hizo, ni za kweli au ni za uongo?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanzishwa kwa pori hilo mwaka 1959 hadi sasa ni miaka 57; je, Serikali inaweza kusema kwa kipindi hicho, imepata faida gani zaidi ya Askari Wanyamapori kukodishia wafugaji na wakulima wasio na uwezo kuruhusiwa kulima halafu baadae wanagawana mazao?
Swali la pili, kwa majibu yaliyotolewa ninapata imani kuwa, Mheshimiwa Waziri anadanganywa na wataalam wa chini yake. Je, yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kwenye Mbuga hiyo, ili akajionee changamoto zilizopo na baadae asiweze kudanganywa na watumishi wake?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina vituo vya afya vitano ambavyo havina magari ambavyo ni Laela, Kayengeza, Msanadamungano, Mpuwi na Milepa, na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imejitahidi sana katika kuweka bajeti kwa mwaka 2013/2014, 2014/2015 ili kukabiliana na adha hii lakini Serikali haijatoa fedha ili halmashauri iweze kununua magari hayo. Sasa Serikali inaithibitishiaje halmashauri kwamba ikitenga fedha inaweza kuipatia ili iweze kununua magari kukabiliana na tatizo hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia tatizo la msongamano wa wingi wa wagonjwa katika Kituo cha Afya Laela, na amezungumzia utatuzi wa tatizo hilo kwa mpango wa muda mrefu, wakati kwa sasa tatizo hilo ndiyo lipo na ni kubwa sana kutokana na wingi wa watu na kupanuka kwa mji mdogo. Nataka Serikali inieleze, kwa sasa inafanyaje mpango wa dharura ili kuokoa wananchi wanaosongamana katika kituo cha afya?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri na ufafanuzi wa swali langu la msingi umeeleweka lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Jimbo la Kwela? Nauliza hivyo kwa vile Ukanda wa Ziwa Rukwa haujaguswa kabisa karibu Kata 13 na Kata saba za Ukanda wa Juu na zenyewe hazijaguswa kabisa, jumla Kata 20 hazijaguswa hata kijiji kimoja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itamalizia kupeleka umeme katika REA III katika vijiji 68 ambavyo havijapelekewa umeme katika Kata za Mpwapwa, Jangwani, Mpuhi, Likozi, Kalambanzite, Lusaka, Lahela na Sandurula?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana; lipo tatizo kubwa kati ya Uwanda Game Reserve na vijiji vya Kilangawana, Maleza, Legeza, Mpande, Ilambo, Mkusi, Iweliamvula na Ngomeni. Kwa watu wa TFS
kuhamisha mipaka inayotambulika toka enzi za nyuma na kusogeza katikati ya vijiji. Tatizo hili ni kubwa sana na mimi nilishaenda mara kadhaa kumwambia Waziri kwamba naomba afike asikilize pande zote mbili kwa sababu ninachokiona hawa askari wa TFS ni kama wanagandamiza wananchi wakati jambo lipo wazi. Je, ni lini Serikali itatuma uongozi wa kwenda kuangalia haki juu ya wananchi wale?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara hii nimekuwa nikiulizia mara kwa mara na hii ni kutokana na umuhimu wake. Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ukurasa wa 62 inaeleza kuwa itafanyiwa upembuzi yakinifu na hivi sasa ni miaka miwili sioni dalili ya kutenga pesa kwa ajili ya kufanya usanifu katika barabara hiyo. Je, ni lini sasa Serikali itatenga pesa kwa kuanza kazi hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mawaziri wote wawili ni wapya, yawezekana hawajatambua vyema umuhimu wa barabara hii. Naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara ya kutembelea barabara hii toka Mlowo hadi Kibaoni ili ajionee fursa zilizopo katika barabara hiyo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza katika swali la msingi umuhimu wa ujenzi wa daraja la Mto Momba kwamba ni kiungo muhimu katika kuunganisha mikoa mitatu. Kwa kuwa Sera ya Serikali katika ujenzi wa barabara za lami inazingatia barabara zinazounganisha mikoa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii muhimu kwa kiwango cha lami inayounganisha mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Serikali imejenga mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Laela ulioanza mwaka 2014 na umetumia takribani shilingi bilioni moja na milioni mia nne; na mradi huu unaonekana umekwisha, lakini cha ajabu hautoi maji, jambo ambalo limeleta taharuki kubwa sana kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Laela. Je, ni lini Serikali itahakikisha maji yanatoka katika mradi huo?
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni mahakama iliyojengwa toka enzi za mkoloni na kutokana na hali hiyo imechakaa na inahatarisha maisha ya wananchi. Ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ni miongoni mwa mahakama iliyopangwa kujengwa upya. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuipa kipaumbele cha pekee kunusuru hali inayoweza kutokea kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa vile vikwazo ulivyovieleza vya upatikanaji wa kiwanja na hati miliki vyote vilishakamilika na uongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga ulishathibitisha. Je, ni lini sasa Mahakama hiyo itaanza kujengwa? (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kushika nafasi hiyo mpya na kwa kweli ameanza kuifanya vizuri Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza aendelee kuifanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza sisi sote tunafahamu wazi kwamba maeneo yaliyo na madini yanatoa fursa kwa vijana wengi kujiajiri kwa machimbo madogo madogo kwa kujipatia kipato na vilevile Serikali kukusanya kodi. Tunafahamu kwamba Serikali ilishafanya utafiti katika maeneo mengi, lakini utafiti huo uko ndani ya vitabu mpaka uende maktaba jambo ambalo sio rahisi wananchi wa kawaida vijijini kutambua wapi kuna madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa nini Serikali isiainishe maeneo yote yenye madini kwa uwazi ili wananchi waweze kuyatambua na kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo?
La pili umesema kwamba wananchi wanaweza kutumia ofisi za kanda za Magharibi zilizopo Mpanda na Dodoma, jambo ambalo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida hasa wa vijijini kuzitumia ofisi hizo kutokana na umbali uliopo. Kwa nini Serikali isiweke branch katika mikoa yote ili kurahisisha wananchi kuzishilikia ofisi hizo?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's