Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Felister Aloyce Bura

Supplementary Questions
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mgogoro uliopo kati ya Wananchi wa Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara ni sawasawa na mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi wa vijiji 11 vya Wilaya ya Kondoa. Katika mgogoro huo wananchi wameuawa, Askari wa Hifadhi ya Mkungunero wamekufa na mgogoro huu ni wa muda mrefu na tumeiomba Serikali washughulikie mgogoro huo na wananchi wanaomba kilometa 50 tu ili mgogoro umalizike.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri waliopita wametembelea na wamefanya mikutano na wananchi wa vijiji 11 wa Wilaya ya Kondoa pamoja na Chemba. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini mgogoro wa wananchi wa Wilaya ya Kondoa, vijiji 11 utaisha kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi hao?
MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Dodoma ilijengwa mwaka 1923 na ilipojengwa ilikuwa na wakazi wasiozidi elfu hamsini lakini kwa sasa Dodoma ina wakazi takribani laki sita na majengo yako vilevile wala hayajaongezeka. Bima ya Afya waliamua kujenga jengo kwa ajili ya kupunguza wingi wa watu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambalo lina miaka mingi halijakamilika, limekabidhiwa lakini hakuna samani ndani yake.
MWENYEKITI: Uliza swali sasa.
MHE. FELISTER A. BURA: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuishawishi Bima ya Afya ambayo ipo chini ya Wizara yake kuleta samani na kukamilisha jengo lile ili lianze kutumika kwa wagonjwa wa Dodoma?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ni sehemu ya Great North Road iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na Watanzania; na kwa kuwa ni sehemu ya Tanzania tu ambayo haijakamilika mpaka sasa; na kwa kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua; kazi zimesimama kwa baadhi ya maeneo; je, Serikali inatuhakikishiaje Watanzania kwamba barabara hii itakamilika kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Ujenzi katika Mkutano wa Wadau uliofanyika Saint Gaspar aliwaahidi Wanadodoma kwamba atajenga ring roads ili magari yanayotoka mikoa mbalimbali yaishie nje ya Mji kupunguza msongamano wa magari; je, ni lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ajili ya kujenga barabara hizo za ring roads?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali
la nyongeza.
Pamoja na njaa iliyowakumba wananchi wa Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chemba,
Kondoa na maeneo mengine ya ukame katika Mkoa wa Dodoma, lakini mvua iliyonyesha na
inayoendelea kunyesha imeleta mafuriko makubwa kwa baadhi ya vijiji na vyakula ambavyo
wananchi walikuwa navyo vimesombwa na maji, mahitaji ya ndani, magodoro, vitanda,
vyombo vimesombwa na maji.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao kwa kushirikiana na Wabunge?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na kwa kuwa vyuo vikuu vinazalisha vijana asubuhi na jioni wenye elimu nzuri ya kufanya ujasiriamali, lakini tatizo ni wapi watapata mikopo kwa njia rahisi zaidi na kwa riba nafuu zaidi? Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa vijana kupata mikopo kwa urahisi na kwa riba nafuu zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajira ambayo ni rahisi kwa vijana na hasa kwa wanawake pia ni kilimo; lakini kilimo kinacholimwa kwa sasa hakina tija; kwanza, masoko hayapo kwa urahisi, mazao mengine yanaoza mashambani; lakini la pili, maeneo ya kulima. Vijiji vingi havijatenga maeneo kwa ajili ya kilimo kwa vijana na hata kwa wanawake ambao wameshajiunga kwenye vikundi mbalimbali. Je, Serikali iko tayari kutenga maeneo na kuzihimiza Halmashauri zetu kutenga maeneo kwa ajili ya vijana na hata kwa wanawake ambao wako tayari kuwa wajasiriamali kupitia kilimo?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yetu ya Kondoa haina ultra sound na kuna Kata zaidi ya 30, lakini wanawake wanapopata shida, wanaletwa Dodoma Mjini. Kituo cha Afya cha Chamwino lkulu, kiko katika geti la Ikulu pale Chamwino hakina ultra sound, na wanawake wanatoka kilometa 50, 80, 90 wakija Dodoma Mjini,kwa ajili ya matibabu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuongea na Bima ya Afya ili tupate mkopo huo wa shilingi milioni 72 kwa haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari kuisaidia Hospitali ya Kondoa, ambayo pia haina kifaa tiba hicho; na wanawake wengi wa Kondoa, wanabebwa kilometa 150 kuja Dodoma Mjini kwa ajili ya ultra sound. Je, wako tayari kuisaidia hospitali hii ya Kondoa wakapata kifaa hicho?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wa Shabiby round about, Arusha Road walifanyiwa tathmini mwaka 2006 na waliambiwa wakati wowote Serikali itabomoa nyumba zao na kujenga barabara pale lakini mpaka leo wananchi hawa hawajalipwa na huu ni mwaka wa 10 hata choo kikibomoka hawajengi. Naomba Waziri aniambie, ni lini wale watu watalipwa fidia zao halali kwa maana zinazostahili kwa leo ili waondoke?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi suala la Pori la Mukungunero ni tofauti na maeneo mengine kwa sababu mauaji yamekwishatokea, maaskari watatu walikwishauawa pale, wananchi walishaandika barua mpaka kwa Waziri Mkuu na Waziri Mkuu akapeleka suala hili Wizara ya Maliasili lakini tangu mwaka 2013 suala la Mukungunero halijashughulikiwa. Naomba suala la Mkungunero sasa litazamwe kwa jicho lingine la haraka. Je, ni lini sasa Wizara ya Maliasili itaishughulikia barua iliyoandikwa kwao na Waziri Mkuu aliyepita?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa lengo la Serikali la kuanzisha benki hii ni kuwasaidia wanawake wanyonge waliopo vijijini; na kwa kuwa masharti ya Benki ya Wanawake haina tofauti na masharti ya mabenki mengine; na kwa kuwa riba inayotozwa na benki hii pia haina tofauti na riba inayotozwa na mabenki mengine. Je, lengo la Serikali la kuanzisha benki hii kuwasaidia wanawake wanyonge limefikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wanawake wengi wao wapo vijijini na benki hii haijaweza kuwafikia wanawake hao wa Tanzania waliopo vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawake wengi wanyonge waliopo vijijini wanafikiwa na huduma ya benki hii?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililoko Mara la ambulance ya kuwachukua wagonjwa, ni sawasawa na tatizo lililopo Wilaya ya Kondoa ambako Kituo cha Afya cha Wilaya ya Kondoa hakina ambulance kwa muda mrefu sasa; iliyopo ni mbovu ya mwaka 2008 na inahitaji matengenezo makubwa sana kiasi kwamba Halmashauri haiwezi kumudu. Je, Serikali iko tayari kutuletea ambulance Wilaya ya Kondoa ili wagonjwa ambao wanatakiwa kupata Rufaa ya kuja Dodoma Mjini wapate usafiri?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kupanua uwanja wa ndege wa Dodoma, lakini upanuzi huo umeathiri sana barabara ya Area D round about ya Shabiby, na wananchi wanaotoka Area D na Majengo Mapya
hurudi mpaka Kisasa kuja mjini kilometa nyingi.
Je, Serikali iko tayari kujenga barabara nyingine ya
lami kuwapunguzia safari ndefu wananchi wanaokaa maeneo ya Area D na Majengo Mapya?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufungua Benki ya Maendeleo ya Kilimo Mkoani Dodoma na kukubali kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo Mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeanzishwa kwa malengo ya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa masharti nafuu na kwa haraka zaidi. Je, Serikali iko tayari kupunguza sasa riba ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili wakulima wengi wapate kufaidika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwa wakulima. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba mikoa yote wanapata matawi ya benki hii ili wakulima wasihangaike kwenda Dar es Salaam na Dodoma kufuatilia mikopo?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kibaigwa unakua
kwa kasi sana na kwa sasa mji ule ni Mji Mdogo. Hata hivyo, kwa kuwa hatuna watumishi wa kutosha na mji ule haujafanywa kuwa mamlaka, naiomba Serikali sasa ituambie ni lini Mji wa Kibaigwa utapewa mamlaka ili waweze kupanga shughuli za mji wao na kupewa watumishi wa kutosha kuendeleza Mji ule Mdogo?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza naipongeza Serikali kurudisha Ardhi ya Dodoma mikononi mwa wananchi yaani Baraza la Madiwani. (Makofi)
Kwa kuwa CDA imevunjwa na ndio mamlaka iliyokuwa na madaraka juu ya ardhi ya Dodoma na wakati inavunjwa wapo wananchi ambao walishapata barua za kumiliki ardhi, lakini walikuwa hawajaonyeshwa maeneo yao na wapo wananchi ambao wanalipa kidogo kidogo pale CDA, je, Serikali imeweka utaratibu gani wa dharura wa kuhakikishwa kwamba wananchi wa Manispaa ya Dodoma wanahudumiwa wakati taratibu zingine zinaendelea?(Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chemba ni kati ya Wilaya mpya katika Mkoa wetu wa Dodoma. Ukitoka Kondoa kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 50 na ukitoka Dodoma Mjini kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 100 lakini Kituo cha Afya kilichopo pale hakikidhi mahitaji na Kituo cha Bahi ambacho kinahesabika kama Hospitali ya Wilaya bado kina upungufu makubwa. Je, lini Serikali itaungana na wananchi wa Chemba kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Wilaya inapata hospitali ya Wilaya?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali na kuipongeza kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Naamini mwaka ujao wa fedha barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali; kwa kuwa mji wa Dodoma na viunga vyake unakua kwa kasi sana kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, na kwa kuwa tusingependa mji wa Dodoma ukawa na msongamano kama Dar es Salaam; je, Serikali iko tayari na ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kwamba barabara za mzunguko katika mji huu zinaanza kujengwa kupunguza Msongamano unaoweza kuwepo mji utakapokua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga barabara nyingine baada ya barabara iliyokuwa inatoka Shabiby Petrol Station na Area D kufungwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege na sasa wananchi wa Area D, Mlimwa, Majengo Mapya na maeneo mengine wanazunguka mpaka Swaswa ndipo waje mjini, je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, takribani zaidi ya vijiji 12 vinavyozunguka Pori la Akiba la Mkungunero hawafanyi kazi ya kilimo kwa sababu ya mgogoro mkubwa ambao umedumu zaidi ya miaka 10, kati ya wafanyakazi wa pori la Akiba la Mkungunero na wakulima wanaozunguka pori lile. Suala hili limeshafika Serikalini, lakini hakuna hatua zinazochuliwa. Wabunge wa Majimbo Mheshimiwa Juma Nkamia na Mheshimiwa Dkt. Ashatu wanapata shida sana wakati wa kampeni na hata wakati wa kuwatembelea wananchi wao.
Je, ni lini sasa matatizo haya yatakwisha mpaka halisi wa pori la Mkungunero litabainishwa ili wakulima wale wafanye kazi yao kwa uhuru na kwa amani?(Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kero ya maji iliyopo Nyang’hwale inawasumbua sana wanawake wa Wilaya ya Kongwa na Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuuliza mara nyingi ukipita hapa jirani yangu kuhusu Wilaya ya Kongwa na ukaniambia umetoa fedha kwa ajili ya maji Wilayani Kongwa. Visima vinavyotoa maji Wilayani Kongwa havizidi vitatu, visima vingine vilivyobaki vilivyochimbwa na World Bank havitoi maji. Ni jana tu nimeongea na Mkurugenzi wa Kongwa akaniambia shida ya maji ya Kongwa ipo palepale, maji yanayotoka ni kwa maeneo machache sana.
Naomba leo Naibu Waziri aniambie maji yatatoka lini Kongwa ya kuwatosha wanawake wa Kongwa? (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ilianzishwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Halmashauri hii Makao yake Makuu yako karibu sana na Chamwino Ikulu. Kwa hiyo, nilitegemea Serikali ingeliangalia hili suala kwa jicho la kipekee kabisa. Idara za Halmashauri hii zimetawanyika, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Ofisi ya Ardhi ni kilometa tano.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Idara nyingine ambazo nyingine ziko kwenye shule za msingi, nyingine ziko kwenye nyumba za watu binafsi kwa hiyo, ufanyaji kazi na huduma kwa wananchi uko katika hali ngumu kabisa kutokana na jengo lile kutokamilika. Halmashauri waliwafuata TBA wakafanya tathmini wakaona kwamba, zinahitajika shilingi…

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa shilingi bilioni 2.3 na Serikali imetenga shilingi milioni 600 tu kukamilisha lile jengo.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha za kutosha kwa ajili ya lile jengo la Halmashauri na likamilike kwa wakati, japo floor ya chini, ili watumishi wahamie wakafanye kazi pale?
Swali la pili, Halmashauri ya Chemba iliomba shilingi milioni 950 kwa mwaka huu wa fedha na wamepata shilingi milioni 450 tu. Je, shilingi milioni 500 zilizobaki watapata lini ili waendelee na ujenzi wa jengo la Halmashauri?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's