Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Halima Abdallah Bulembo

Supplementary Questions
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara haijataja asilimia ngapi itakwenda kwa vijana wa kike na wa kiume; naomba Wizara ichukue ushauri wangu kwamba zile fedha zitakapopelekwa halmashauri waweze kusema asilimia kumi itakuwa kwa vijana wa kike na wa kiume na hii itapunguza mkanganyiko katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa (credit guarantee scheme for youth)?
(b) Je, Serikali inaona kuna umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii ili kuwezesha vijana kuweka akiba yao ya uzeeni, kupata bima ya afya na hata kuweza kupata mikopo katika biashara zao?
MHE. HALIMA A.BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya madhara ya Madaktari feki wamekuwa wakisababishia wagonjwa hawa vilema vya maisha au kupoteza maisha kwa ujumla.
Je, kuna utaratibu wowote wa fidia kuwafidia watu hawa?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yaliyoko Longido yanafanana kabisa na ya mkoani kwangu Mkoa wa Kagera Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangeleko ambapo kumekuwa na mradi mkubwa wa maji uliojengwa tangu miaka ya 60 mpaka 70 na mradi huu uliweza kufanya kazi kwa miaka 10 na uliwahudumia wananchi wengi. Mradi huu tayari una vyanzo, una matenki, kinachohitajika katika mradi huu ni ukarabati. Je ni lini mtaukarabati mradi huu ili uweze kuwahudumia wananchi wa Bukoba Vijijini?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa fursa hii. Watafiti Joel Lugala na Jesse Mbwambo katika andiko lao la kitafiti linalosema au lililoandikwa street children and street life in urban Tanzania; the culture of surviving and its implication for children health la mwaka 2013; watafiti hawa katika hitimisho lao wanasema, Serikali ya Tanzania hailijui tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Na kwa majibu ya Serikali ni dhahiri tatizo hili halieleweki na hitimisho hili ni thabiti. Je Serikali itachukua hatua gani kulielewa tatizo hili kwani linazidi kukuwa siku hadi siku? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatambua mfumo wa uchumi umebadilika hayo yanayosemwa kwamba watoto watalelewa na ndugu, au walezi hayapo kwa sasa. Watoto yatima wamekuwa wakinyanyaswa, wakidhulumiwa mali zao na ndugu wa wazazi; je, Serikali ipo tayari kubadili mtazamo wake kuhusu watoto wanaoishi katika mazingira magumu?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna raia wa kigeni ambao wamekuwa wakitumia udhaifu wa mfumo wa hati za kusafiria na kuwawezesha kusafiri kinyume cha utaratibu na kuwawezesha kutenda makosa kwa kigezo cha Utanzania. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wanapatikana lakini hatujajua wala hatujawahi kusikia ni hatua gani ambazo zimekuwa zikichukuliwa. Je, Serikali imewachukulia hatua gani maofisa hawa wanaojihusisha na utoaji wa hati hizo?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Tumekuwa tukiona mapori mengi ya hifadhi yakiingiliana na makazi ya watu katika jamii na mapori hayo yamekuwa yametengwa kwa muda mrefu sana.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mapori haya ya hifadhi yaliyotengwa kwa muda mrefu kwa wananchi, ili waweze kufanya shughuli za kijamii kama kilimo, na mifugo na hii itaweza kuwaondolea adha ya migogoro ya wafugaji na wakulima?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na swali zuri lililoulizwa juu ya ajira ya kilimo kwa vijana wa Mkoa wangu wa Kagera, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017, ilionesha nia na dhamira ya dhati ya kuinua ajira kwa vijana. Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wake katika sera ya ajira ya vijana katika sekta ya kilimo?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, changamoto kubwa katika kuanzisha Benki za Maendeleo ni mtaji. Hivi sasa nchini kwetu tumejiwekea utaratibu kwamba kila Halmashauri hutenga 5% kwa ajili ya vijana. Bajeti ya mwaka huu katika Serikali za Mitaa imekusanya takriban shilingi bilioni 600 ambapo katika ile 5% ya vijana ni sawasawa na shilingi bilioni 30. Iwapo fedha hizi zitatumiwa vizuri, tunaweza kuanzisha Benki ya Vijana zenye matawi katika kila Halmashauri na tukiweza katika hili, tutaweza kutatua suala zima la mikopo kwa vijana.
Je, Serikali haioni ni vyema sasa, Halmashauri zote nchini kuwa wanahisa wa Benki za Vijana na kutumia fedha hizi kama mtaji wa kuanzisha benki hii?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo linalozikabili zahanati nyingi nchini siyo upungufu wa dawa tu, bali pia huduma kwa akinamama wajawazito, hususan katika wodi zao huduma ni mbaya, ni hafifu, vifaa stahiki hakuna: Je, ni lini Serikali itahakikisha inaboresha afya kwa akinamama wajawazito katika hospitali na zahanati zote za Mkoa wa Kagera?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, Serikali haioni umuhimu wa kugeuza Kambi za JKT kuwa vyuo vya VETA ili pamoja na mafunzo ya Kijeshi, vijana pia hasa wale wa kujitolea waweze kupata mafunzo ya ufundi? Ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ilani ya Chama cha Mapinduzi moja ya ahadi kubwa iliyotolewa ilikuwa ni kujenga VETA katika kila Wilaya Tanzania nzima. Kwa kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne lakini wanashindwa kujiendeleza kutokana na ukosefu wa vyuo hivyo. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha vijana hawa wanajengewa vyuo hivyo angalau hata katika Wilaya tatu za Mkoa wao? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingi duniani stesheni za reli ni vituo vya biashara tofauti kabisa na nchini kwetu Tanzania. Serikali inaweza kueleza ni kwa nini stesheni kubwa kama Morogoro, Dodoma, Tabora na Mwanza huduma huwa zimedumaa na hakuna huduma za biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, TRL ipo tayali kushirikiana na sekta binafsi kuendesha stesheni za reli kwa kuziboresha ikiwemo kuweka hoteli, huduma za maduka na kadhalika? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. RCC ya Mkoa wa Kagera ilishatoa kibali kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karagwe, lakini suala hilo linakwamishwa na Wizara ya TAMISEMI kwa sababu haitaki kutoa usajili ili hospitali hiyo itengewe bajeti na ujenzi uanze mara moja. Je, ni lini Wizara ya TAMISEMI itaamua kutoa usajili huo ili ujenzi uanze mara moja ili kuokoa akina mama na watoto?
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri, migogoro ni moja ya sababu inayokwamisha jambo hilo, lakini migogoro hiyo haijazuia wananchi wetu kufanya biashara. Ni kwa nini Serikali isirahisishe movement ya wananchi wetu hasa hasa vijana wa Kitanzania kuchangamkoa fursa ya soko kubwa la Congo ikizingatiwa Congo ni land locked country? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera kuna vijiji ambavyo vimewekwa katika mpango wa Rea Awamu wa Pili, vijiji kama Songambele, Kitwe, Mulongo lakini havikupatiwa umeme. Vijiji hivi hivi pia vimewekwa katika Mpango wa REA Awamu ya Tatu. Je, Serikali itahakikisha katika Mpango huu wa REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi havitakosa umeme? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya asilimia 56 mpaka 60 ya watanzania ni vijana lakini vijana wanashindwa kutimiza malengo yao ama ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya upangaji wa nyumba za makazi hasa mijini kuwa kubwa na wamiliki kutaka kupewa kodi za mwaka au miezi sita.
Je, ni lini sasa Serikali itafuta utaratibu huu na sisi kama Bunge tutunge sheria itakayowalazimisha wamiliki wote kupokea kodi ya kila mwezi badala ya mwaka ama miezi sita kama ilivyo sasa? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa naibu Spika, mwaka jana tumeshuhudia Serikali yetu ikijaribu kupunguza tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji jambo lililosaidia kupunguza lakini siyo kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mwaka jana Serikali yetu ikijaribu kupunguza tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya kwa kuwataja hadharani watumiaji na wauzaji lakini jambo hili halikumaliza tatizo bali ilipunguza tu, suala hili bado lipo tena kwa wingi zaidi na wanaoathirika ni vijana wa Kitanzania ambao ni nguvu kazi ya nchi. Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga rehab zitakazotambulika ili kumaliza janga hili? Nashukuru.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Septemba, 2016 niliuliza swali kama hili na nikatoa utafiti nikampa Naibu Waziri ambao ulionesha Serikali ya Tanzania haijui tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Baada ya kusikiliza majibu ya Serikali, nalazimika kusema kwamba bado Serikali haijalijua kwa undani suala la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Je, ni lini sasa Serikali itaamua kufanya utafiti na kuja kutupa namba sahihi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini? (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo wagonjwa wote wa akili wanaranda mitaani hata miongoni mwetu tunaweza kuwa wapo wagonjwa wa akili. Kwenye nchi za wenzetu wamefanya utafiti wa wagonjwa wa akili nchi kama Marekani, Uingereza na Australia, tafiti zao zinasema katika kila watu wanne kuna mgonjwa mmoja mwenye tatizo la akili. Je, ni lini sasa nchi yetu itamua kufanya utafiti kama huu ili kubaini tuna wagonjwa wangapi wa akili nchini? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Rev. Dr. Getrude Pangalile Rwakatare

Special Seats (CCM)

Contributions (4)

Profile

View All MP's