Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Supplementary Questions
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Morogoro Kusini Mashariki linafanana na tatizo la Mbinga Mjini, hasa maeneo ya Mbinga „A‟, Mbinga „B‟, Ruwiko, Bethlehemu na kadhalika; ile 5% inayotolewa kwa ajili ya vijana, pamoja na kwamba inaonekana inawasaidia vijana na maeneo mengine haiwafikii, bado inaonekana ni hela ndogo sana ukilinganisha na mahitaji ya vijana na hasa ukizingatia mabenki yetu hayajawa marafiki kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza, ukiondoa ile 5% inayotoka kwenye Halmashauri, Serikali Kuu kutengeneza fungu maalum kwa ajili ya kuwasaidia vijana, hususan vijana wa Mbinga? (Makofi)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza. Mradi unaokusudiwa kujengwa au kukamilishwa Mbinga ni mradi mkubwa; na fedha zilizoainishwa ambazo zinatafutwa, Dola milioni 11.86 ni nyingi, zinaweza zisikamilike kwa wakati:-
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kutengeneza mpanga wa dharura kwa kukarabati miundombinu ya maji ulioko sasa ili watu wa maeneo ya Frasto, Kipika, Masumuni, Lusonga, Mbambi, Bethlehemu, Luiko na Misheni waweze kupata maji safi na salama?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuvishirikisha Vyama vya Msingi na AMCOS kwenye hiyo contract farming badala ya ku-deal na wafanyabiashara binafsi ambao wale hawamgusi moja kwa moja mkulima, wao wako zaidi kwa ajili ya ununuzi wa kahawa siyo uzalishaji wa kahawa.
Mheshimiwa Waziri huoni sasa ni wakati muafaka kwa ile AMCOS ya Kimuli ya kule Utili sasa ishirikishwe na zile „AMCOS’ nyingine za Miyangayanga, Utili na sehemu nyingine?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la Kata ya Rasbura linafanana na tatizo lililoko Kata la Lusonga Jimbo la Mbinga Mjini ambapo Halmashauri ilitwaa eneo ambalo lilikuwa linamilikiwa na wananchi kwa malengo ya kupima viwanja na kuliboresha eneo lile lakini mpaka sasa fidia bado haijalipwa na viwanja bado vinaendelea kugawanywa kwa watu wengine. Serikali haioni sasa hiyo formula inayotumika kule Lindi ikatumike na Mbinga yaani kulirudia tena kulipima upya na wale wananchi wa Lusonga wapate haki yao?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, tatizo la Hospitali Teule ya Muheza linafanana na tatizo la Hospitali ya Wilaya ya Mbinga Mjini, mapema mwaka huu Waziri Mkuu alipofanya ziara yake Mkoa wa Ruvuma aliahidi kwamba Hospitali ya Wilaya ya Mbinga itaboreshwa katika maana ya theatre, nyumba ya kuhifadhia marehemu pamoja na kuhakikisha kwamba Madaktari wanaongezeka na gari ya wagonjwa. Ni lini ofisi yako itahakikisha hizo ahadi za Waziri Mkuu zinatekelezwa? (Makofi)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kibamba na Ubungo katika ujumla wake ni Mji unaokua kwa kasi sana na ongezeko kubwa la watu linalohatarisha usalama wa mali na raia kitu ambacho Kituo cha Kibamba kinapochelewa kujengwa kinahatarisha usalama wa eneo hili. Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia hili jambo katika udharura wake ili kituo kijengwe kwa haraka?
Pili, kwa kuwa tatizo la maslahi ya askari wa Kibamba na maeneo mengine hayatofautiani na yale ya Mbinga, Nyasa, Songea Vijijini, Namtumbo Tunduru na Madaba; haoni kuna ulazima sasa kwa Serikali kuboresha maslahi ya watumishi katika maeneo niliyoyataja ikihusisha fedha maalum kwa ajili ya operation za ulinzi na usalama pamoja na kuboresha makazi yao hususan maeneo ya kulala ili kusitiri utu wao?
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri hasa eneo la kutoa milioni 50 kwa ajili ya wodi ya watoto, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni lini Serikali itaboresha wodi ya akinamama wajawazito pamoja na sehemu ya kujifungulia hasa ukizingatia hali ya sasa pale hospitalini, akinamama wanakaa katika mazingira magumu na wanalala watatu watatu? (Makofi)
Swali la pili la nyongeza; kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi, Hospitali ya Wilaya ya Mbinga inahudumia Halmashauri nne, yaani Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Mbinga Vijijini, Mbinga Mjini na sehemu ya Halmashauri ya Songea Vijijini. Gari ambalo limetolewa na waterreed liko kwa ajili ya kitengo cha UKIMWI na linawasaidia wale wagonjwa wa UKIMWI tu, maeneo kama ya Mpepai kwenye zahanati na vituo vya afya Kihungu, Kilimani, Kigonsera, Mkumbi ambao hao wakipata mazingira magumu katika maeneo yao wanahitaji kuletwa katika hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatuletea gari la wagonjwa kwa sababu hilo lililosemwa hapa haliko kwa ajili ya kuwasafirisha wagonjwa wa hali ya kawaida, ni wale tu kwenye kitengo cha UKIMWI?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's