Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Daimu Iddi Mpakate

Supplementary Questions
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini katika miradi miwili aliyosema imekamilika, mradi wa Nandembo na Nalasi tarehe 22 Julai, 2014, Rais wa Awamu ya Nne alifungua miradi ile, lakini cha kusikitisha hadi leo maji hayatoki katika miradi yote miwili. Je, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia miradi ile kama alivyosema imekamilika wakati maji hayatoki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi wa Mbesa umesimama kwa takribani kwa mwaka mmoja na nusu na vifaa viko pale, vina-hang hovyo bila usimamizi wowote. Je, ni lini Serikali itapeleka mkandarasi mwingine ili aweze kumalizia mradi ule?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa mazingira ya Mchinga yanafanana kabisa na Wilaya ya Tunduru yenye kilometa za mraba 18,776; na kwa kuwa tayari kuna majimbo mawili na taratibu zote za kuigawa Wilaya ile zilishafanyika siku za nyuma; na kwa kuwa zilitolewa ahadi za viongozi wa Awamu ya Nne kuigawa Wilaya ile na Mkoa kwa ujumla. Je, ni lini taratibu za kuigawa Wilaya ile na Mkoa mpya wa Selous zitafanyika?
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa matatizo ya ushirika yameenea katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania, na kwa kuwa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2013 ilianzisha rasmi Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Je, ni lini Serikali itaifanya Tume hii iwe na uongozi wa kudumu kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume pamoja na Makamishna wa Tume ili ushirika usimamiwe vizuri?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Makambako - Njombe - Songea, ilijengwa tangu mwaka 1984, na sasa ina hali mbaya sana kila siku inawekwa viraka lakini hali imekuwa ni mbaya sana.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile upya ili kuwahudumia watu wa Mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa ujumla?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kama alivyozungumza, kuna kata 15 kati ya hizo ni vijiji vinne tu vya Kata ya Chiwana na Kata ya Mbesa ndivyo vimepata umeme. Je, kati ya kata hizi zifuatazo ni lini watapatiwa umeme wa REA, Kata za Mtina, Nalasi, Mchoteka, Malumba, Mbati, Ligoma, Namasakata, Mchesi, Lukumbule, Chiwana na Msechela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tabia ya mkandarasi anayejenga laini ya Mbesa kuwadai wananchi wetu Sh.200,000/- mpaka Sh.300,000/- kwa ajili ya kupelekewa nguzo na kuunganishiwa umeme katika nyumba zao. Je, ni hatua gani imechukuliwa ili mkandarasi huyu asiendelee na tabia hiyo kwani umeme huu ni haki yao wananchi kupewa bure kwa kulipa Sh.27,000/-? Ahsante
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika vivuko vilivyotajwa; Kivuko cha Chaulesi kilichopo Makande na Chamba kilichopo Wenje kinaunganishwa na barabara mbili za mkoa ambazo zipo chini ya barabara ya ulinzi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika muda wote wa mwaka kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ambapo watu wa Msumbiji na Tanzania wanatembeleana kwa ajili ya kupata huduma kutoka Tunduru Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa eneo la Chaulesi na Chamba watu wengi wanapita sana kutoka Msumbiji kuja Tanzania kufuata huduma za mahitaji ya muhimu kutoka Tunduru Mjini: Je, Serikali haioni haja ya kuweka Kituo cha Uhamiaji katika maeneo hayo mawili ili kuondoa kero ya Watanzania ambao wanapata tabu wanapovuka Msumbiji kwa ajili ya kukosa hati na kusumbuliwa na askari wa Msumbiji?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Tarime yanafanana kabisa na mazingira ya barabara zilizopo katika Jimbo la Tunduru Kusini kutoka Mtwara Pachani, Msewa na Rasi mpaka Tunduru Mjini iliahidiwa na Makamu wa Rais wakati wa kampeni kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini mchakato wa ujenzi wa barabara hii utaanza?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa chuo kile hakikukidhi haja ya kukikarabati na kwa kuwa katika majibu ya msingi yamesema kwamba eneo la chuo lilikuwa dogo. Je, Serikali haioni haja ya kujenga chuo kipya kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina maeneo mengi ambayo yangeweza kujengwa chuo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi katika Idara ya Afya kwa zaidi ya 70%. Ni kwa nini sasa Serikali isitoe upendeleo maalum kwa ajili ya Wilaya ya Tunduru na kwa vijana wa Tunduru ili waweze kuhudhuria mafunzo hayo katika vyuo ambavyo vimefufuliwa?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mazingira ya barabara ya Mtwara yanafanana kabisa na mazingira ya barabara ya kutoka Masasi – Mangaka – Tunduru - Songea - Mbinga kutokana na machimbo yanayoendelea ya makaa ya mawe pale Ngaka, Mbinga. Makaa yale yanasafirishwa kwa malori makubwa yenye zaidi ya tani 30 kupitia barabara ya Tunduru – Mtwara
- Lindi - Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kujenga reli ili makaa yale yaweze kusafirishwa kwa njia ya reli kwa sababu magari yale yanahatarisha usalama wa barabara yetu?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Serikali imetambua urefu mkubwa uliopo kutoka Ofisi ya Uhamiaji ilipo mpaka Wenje, Makande na Kazamoyo; na kwa kuwa wananchi hawa wa maeneo haya hawana uwezo mkubwa wa kuweza kufuata huduma hii ya uhamiaji zaidi ya kilometa 90 ziliko ofisi; na kwa kuwa Serikali inakosa mapato kutokana na tozo zinazotolewa kwenye hati hizi ya kusafiria; je, kwa nini Serikali haioni umuhimu kwa sasa wa kuweza kutoa huduma hii kwa njia ya mobile ili wananchi hawa waweze kupata huduma hii kwa haraka?
Swali la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Ofisi ya Uhamiaji ina gari ambalo kwa muda mrefu ni bovu halina huduma yoyote katika maeno yote yaliyopo. Je, Serikali ni lini itatoa gari kwa ajili ya kurahisisha huduma hii ili wananchi wale wahudumiwe kwa urahisi zaidi?
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo. Tatizo la Manyoni linafanana kabisa na mazingira ya tatizo la barabara ya Mtwaro - Pachani - Lusewa - Mchoteka - Nalasi - Mbesa - Tunduru Mjini ambayo iliwekewa alama za ‘X’ zaidi ya miaka saba iliyopita. Je, ni lini ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Makaimu Watendaji wa Vijiji karibu maeneo mengi ya Tanzania hawapewi posho. Je, Serikali haioni haja ya kuwapa posho Makaimu Watendaji wa Vijiji ili waweze kufanya kazi zao vizuri?
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyotoa Naibu Waziri, lakini Jimbo langu la Tunduru Kusini vituo vyake vya afya vimechakaa na vina hali mbaya na vina matatizo lukuki pamoja na uhaba wa wafanyakazi,hakuna gari, wala chumba cha upasuaji.
Swali langu, ni lini Serikali itahakikisha vituo hivi vya afya vinapata watumishi wa kutosha ili viweze kuhudumia wananchi wa Tunduru?
Swali la pili, katika kampeni ya uchaguzi mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Mji wa Nalasi ambao una zaidi ya watu 25,000. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya kujenga kituo cha afya pale Nalasi ili kuweza kuwahudumia wananchi wale ambao wako katika vijiji sita katika Mji ule wa Nalasi? Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante na Mheshimiwa Naibu Waziri asante kwa majibu mazuri. Kwa kuwa kituo hiki kinahudumia zaidi ya Kata Tano, Kata ya Mtina, Lukumbulem Mchesi, Masakata na Tuwemacho.
Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kuboresha kituo hiki ili kiweze kutoa huduma za upasuaji kwa wakina mama na wajawazito?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kampeni ya mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kata mbili za Nalase ambazo zipo katika Mji mmoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imekuwa inatenga kila mwaka na mpaka sasa imeishia kujenga msingi tu. Je, ni lini Serikali itaona haja ya kutimiza ahadi ile ya Rais wa Awamu ya Nne ili wapate kituo cha afya pale Nalasi? Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Mheshimiwa Mpakate. Napenda kuuliza swali la nyongeza. Katika maeneo yanayozalisha korosho, mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia sana wakulima kuongeza kipato, lakini moja ya changamoto inayokumbana nayo ni matatizo ya maghala katika vijiji vyetu katika maeneo yote ambayo yanalimwa korosho. Mradi wa MIVARF ungeweza kusaidia kujenga maghala kila Kata angalau ghala moja moja ili kuwapunguzia wakulima gharama ya kusafirishia korosho. Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa kujenga angalau ghala moja kila kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili kuwapunguzia wakulima wa Tunduru gharama ya kusafirisha korosho.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's