Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Supplementary Questions
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua ushirikishwaji wa vikao vya Wilaya ya Maswa, kwa sababu jibu lake la mwanzo ameeleza kwamba vijiji vilishirikishwa, lakini nina hakika kabisa ushirikishwaji wa vijiji hivi na Kamati hizi zilizoorodheshwa hapa sina hakika navyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuniridhisha kwa kunionesha vikao hivi vilifanyika lini na wapi ili watu wa Maswa waweze kulitambua hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mwenyekiti wa RCC ni Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa wakati ule alikuwa ni Dkt. Balele ambaye naye anatokea Bariadi, huoni naye alikuwa labda ni sehemu ya kufanya Serikali iingie kwenye matumizi makubwa, kupeleka sehemu ambapo hakuna majengo mengi ikilinganishwa na Maswa ambayo ni Wilaya kongwe iliyozaa Bariadi na Meatu?
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Swali langu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, kuna wastaafu wengine baada ya kupewa pensheni wanapewa kila baada ya miezi mitatu na ukitazama kuna walimu wengine wastaafu na wafanyakazi wengine, kila baada ya miezi mitatu wanapewa kiasi cha shilingi 150,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba je, pesa hizi wana mpango wowote wa kuwaongezea na je, anaonaje kama ikawa kila mwezi mkawapatia kila mwezi badala ya kuwapatia miezi mitatu?
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini napenda kujua, kwa sababu maendeleo hayana utengemano yaani ni maendeleo kwa jumla bila kujali mipaka na itikadi ya kisiasa, miradi hii inakwenda kwa wananchi wote. Baada ya kutandaza mabomba mpaka maeneo ya Kishapu, je, mradi huu mnaweza kuupeleka mbele zaidi hadi vijiji vya Mwamashindike mpaka Lalago wakapata maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Maswa nayo inasubiri Mradi wa Maji ya Ziwa Viktoria ambao utakuja katika phase two ya ule mradi wa maji kutoka Lamadi. Je, Wizara ina mpango gani kuwasaidia wananchi ambao hawana maji hivi sasa kwa kutumia mabwawa yaliyopo katika Wilaya ya Maswa kwa mfano Bwawa la Sola, Nyangugwana, Mwantonja kwa kuyasafisha na kuyafanya kuwa chanzo cha maji katika Wilaya ya Maswa ili wananchi waweze kupata maji kwa sasa wakati wanasubiri mradi wa Ziwa Viktoria ukamilike? Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, swali la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Maswa imekwishatenga eneo zaidi ya heka 110 na tumekwisha kuandika barua kwa EPZA kuja kuwekeza Maswa. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atatusaidia Maswa, EPZA kuja ku-facilitate maeneo ya uwekezaji ili tuweze kukaribisha wawekezaji kwa maana ya kuwekeza viwanda vidogo vidogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali. Kwa kuwa tunataka kwenda kwenye nchi ya viwanda na tunataka kuwawezesha kimtaji wafanyabiashara na wakulima, je, Wizara ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha kwamba mashamba ya wakulima hasa wa Mkoa wa Simiyu na Mikoa ya jirani yanapimwa na kupatiwa hati ili kusudi wakulima waweze kwenda kwenye mabenki na kukopa? Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, ahadi nyingi zinazotolewa na Mheshimiwa Rais, kuanzia Awamu ya Nne na mpaka sasa awamu ya Tano, tunavyotambua ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kama amri.
Je, ni kwa nini ahadi zinazotolewa na Rais wetu hazitekelezeki mapema? (Makofi)
Swali la pili, kuna ahadi vilevile ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne katika Halmashauri ya Mji wa Maswa, ilisemekana kwamba zitajengwa kilometa tatu ilitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete; je, ni lini ujenzi huu utaanza? Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa mpango huu wa hizi nyasi bandia zinazotolewa, je ni mpango wa kila Mkoa na kama ni kila Mkoa, je, ni lini Mkoa wa Simiyu mtatupa uwanja wa namna hii? Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza napenda kujua usanifu huu wa kina umeanza lini na utaisha lini?
Swali la pili ningependa kujua kwa sababu nimefuatilia kwa muda mrefu ahadi hii ya Mheshimiwa Rais kumekuwa na mkanganyiko wa kutokujua, kwamba fedha za ujenzi wa barabara hizi kilometa tatu zitatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa au zitatoka katika Serikali Kuu? Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi siridhiki kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya ushindani yanayosemwa kwanza hajawekewa mazingira mazuri ya ushindani na nauli kwa tunaosafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam mara kwa mara, nauli kwa mfano za Shirika la FastJet, wanapoaihirisha safari wewe abiria hawakulipi na ukichelewa ndege unalipa zaidi ya nauli. Je, TCAA na Mheshimiwa Waziri wanalijua hili na kama wanalijua wana mpango gani wa kuliondoa? (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri.
Swali la msingi linauliza kwamba pesa hizi zitaanza kutolewa maana yake toka mpaka sasa ni kwamba uchaguzi umeshapita, mwaka mzima umeisha quarter ya kwanza ya bajeti imeisha ni lini? Swali la msingi linauliza.
Swali la pili la nyongeza ni kwamba hili Baraza la Mawaziri litakaa lini kupitisha hii pesa kwa sababu tayari ilishajulikana pesa hizi zinakwenda kwa kila kijiji, ni nini kinakwamisha Baraza hili kukaa na kupitisha pesa hizi au mpango huu ili wananchi waweze kupata hizi pesa?
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na mikakati na Sheria na Sera za Kitaifa za Mazingira ya Mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mkakati wa Hatua za Kuhifadhi Mazingira 2008, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Swali langu la nyongeza dogo, Serikali ina mpango gani maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu kwa sababu hizi sheria na mikakati yote inaonekana ni ya Kitaifa zaidi? Ninachotaka ni kupata commitment ya Serikali maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Simiyu kweli unategemea kupata maji kutokana na huu mradi wa Simiyu Resilient Development Programme wa kutoka Ziwa Victoria, lakini katika Mkoa huu Maswa itapata maji katika mradi huu katika phase ya pili. Vilevile jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri linasema kwamba utekelezaji wa kupata maji maeneo haya kutoka Ziwa Victoria unatekelezwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Wizara ya Maji, ni lini itafufua mabwawa ya Wilaya ya Maswa kwa sababu itachelewa kupata maji. Kuna mabwawa mengi zaidi ya mabwawa 35 na yamefanyiwa upembuzi yakinifu yanahitaji shilingi bilioni 1.2 tu kufufuliwa ili watu waweze kupata maji na waweze kuotesha na kumwagilia miti yao. Nashukuru.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nikazie kusema kwamba, Mradi wa KASHUWASA wa Shinyanga sio mamlaka ni mradi na vilevile wananchi wa Mji wa Maswa leo sasa wanakwenda wiki ya tatu wanakosa maji kisa TANESCO imewakatia umeme kwa sababu hawajalipa bili ya umeme na wananchi wa Maswa wanalipa bili zao kwa muda unaostahili na maji wamekatiwa kwa sababu ya makosa sio ya kwao. Je, Mhesimiwa Waziri unawahakikishia ni lini wananchi wa Maswa na Shinyanga watapata maji? Ahsante.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Kinondoni (CUF)

Contributions (7)

Profile

Hon. Kunti Yusuph Majala

Special Seats (CHADEMA)

Supplementary Questions / Answers (1 / 0)

Contributions (4)

Profile

Hon. Silvestry Fransis Koka

Kibaha Mjini (CCM)

Questions / Answers(3 / 0)

Supplementary Questions / Answers (3 / 0)

Profile

View All MP's