Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Supplementary Questions
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya kweli. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kumekuwepo na malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi wa Mwakata walioathirika na hiyo mvua ya tarehe 3 mwaka jana kwamba usimamizi wa misaada mbalimbali nje ya ile iliyotoka Serikalini umekuwa na harufu mbaya, umekuwa na dalili za ufisadi. Nataka kujua Serikali iko tayari kufanya uchunguzi maalum wa Kiwizara ili kujua misaada yote iliyokusanywa na jinsi ambavyo ilitumika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, maafa haya yalikuwa na madhara makubwa sana kwa wananchi wanaoishi kwenye nyumba za tope. Serikali katika Ilani yake inayoitekeleza sasa hivi moja ya mkakati ni kujenga nyumba bora kwa maana nyumba za saruji. Nataka kujua Serikali imefikia wapi katika kupunguza ushuru wa vifaa vya ujenzi hasa simenti na kuweka standardization ya bei ili wananchi wanaoishi upande wa Magharibi mwa nchi yetu ambako hakuna viwanda na huipata bidhaa hiyo kwa gharama kubwa waweze kuipata kwa bei rahisi ili waweze kujenga nyumba bora na kuepuka majanga kama haya ambayo yanaweza yakawa yanajirudia endapo nyumba zitaendelea kutokuwa na ubora?
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kupeleka fedha hizi kwenye shule za bweni zilizoko kwenye Wilaya ya Hanang. Pamoja na hatua hiyo nzuri na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa kushirikiana na Mbunge wao wamefanya kazi kubwa sana ya kujenga shule pamoja na hosteli kwenye shule za Isaka, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya pamoja na Busangi. Lakini shule hizi au hosteli hizi hazitambuliki kabisa na Serikali kwa maana ya kutolewa au kupewa msaada wa aina yoyote kama inavyofanyika kwa wenzao wa Hanang. Je, Serikali inaweza sasa ikaziingiza shule hizi kwenye mpango wa kupatiwa huduma ya chakula kama ilivyofanyika kwenye maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa tatizo la mabweni kwenye shule nyingi za sekondari za kata ni kubwa sana hasa kwenye shule zilizoko kwenye maeneo ya wafugaji ambao wengi wao wanaishi kwenye maeneo ya pembezoni na yenye mazingira magumu, na kwa kutambua mazingira hayo wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa kushirikiana na Mbunge wao wameanza juhudi au wanaendelea na juhudi za kujenga hosteli kwenye shule ambazo bado hazijapata ikiwemo shule za sekondari za Isakajana, shule za sekondari za Ngaya pamoja na zingine.
Je, Serikali inaweza ikachangia namna gani au ikaunga mkono namna gani juhudi hizi nzuri za wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala pamoja na Mbunge wa eneo hilo?
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Swali la kwanza; tarehe 3 Machi, 2015 kulitokea maafa ya mvua kwenye eneo la Mwakata kwenye Jimbo langu na watu 47 wakafa na misaada mingi ilikusanywa. Kwa bahati mbaya sana kumekuwepo usimamizi usioridhisha wa matumizi ya misaada ile na wananchi wamekuwa wakiwatuhumu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Bwana Ali Nassoro Lufunga na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, lakini pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Bwana Benson Mpesya, aliyekuwa Mkuu wetu wa Wilaya kwamba, misaada ambayo ililenga kuwafikia waathirika wa Mwakata haikuwafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali itasaidiaje kuhakikisha kwamba, taarifa sahihi ya fedha zilizokusanywa na misaada mingine kwa ajili ya maafa ya Mwakata inapatikana kutoka kwa watuhumiwa hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, Serikali inakiri kwamba, maafa ni jambo ambalo halitabiriki na pia inakiri kwamba Serikali ina wajibu wa kusaidia wananchi. Hatutaki Serikali ilipe fidia au kufanya chochote, lakini ni kwa nini isiangalie uwezekano wa kuwa na Mfuko, kama tulivyopendekeza kwenye swali la msingi, ambao unakuwa unachangiwa kwa njia endelevu ili likitokea janga hata mnapokwenda kusaidia angalau mna mahali pa kuanzia kuepuka aibu ambayo inajitokeza kwa sasa kwamba, zinafika mpaka nchi nyingine kuja kusaidia, sisi kama Serikali tunawaomba na kuitisha harambee sisi hata shilingi moja ya kuanzia hatuna. Hivi Serikali haioni kwamba, ni aibu katika mazingira ya namna hiyo?
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la uhaba wa vyuo vya ufundi
na ahadi imekuwa ni ya muda mrefu na tatizo ni la muda mrefu. Katika
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala tumekwishaanza juhudi za kufanya au
kutekeleza jambo hili. Kwa bahati nzuri kwa mazingira yetu tuna mgodi wa
Bulyanhulu ambao vijana wengi sana wanakosa fursa za kufanya kazi pale kwa
sababu ya kukosa elimu fulani ya ufundi na mgodi umeonesha nia ya kushirikiana
na Serikali kuutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwomba au kumuuliza swali
Mheshimiwa Waziri kwamba anaonaje akitusaidia katika kutia chachu
mazungumzo kati ya Halmashauri ya mgodi ili kuweza kutekeleza mradi huu kwa
yeye mwenyewe kufika na kukaa na watu wa mgodi ili kuona namna gani
tunaweza tukatekeleza mradi ambao tayari eneo lilishapatikana muda mrefu
kwenye Kijiji cha Bugarama?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's