Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Yahaya Omary Massare

Supplementary Questions
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, ilizuia usafirishaji wa mazao ya misitu ambayo hayajachakatwa ikiwemo asali, mbao na hata wanyamapori. Naomba kuuliza swali langu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya zuio hilo Serikali imeruhusu kusafirisha mbao ya sentimita 15 tu unene na wakati huo wadau na masoko yanahitaji zaidi ya sentimita 15. Je, Serikali iko tayari sasa kuwaruhusu wafanyabiashara ambao wanafanya export ya mbao hizi, wakiwemo wafanyabiashara wa mitiki, pine na mbao za miche ya asili angalau wafikie katika sentimita 20 ili nao wapate tija na kushindana na wafanyabiashara wenzao katika masoko?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi na Wilaya nzima ya Manyoni, imezuia uvunaji wa mbao na mazao ya misitu kwa ujumla, Je, Serikali sasa ipo tayari kushirikiana na Halmashauri yangu mpya ya Itigi uvunaji uendelee, badala ya watu sasa kuiba ili walipe kodi za Serikali na maduhuli na pia kusaidia pato la Halmashauri wakati misitu ipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, matatizo yaliyoko Mpwapwa yanafanana sana na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Itigi. Watu wanaenda kilometa nyingi sana kufuata maji hasa katika vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Chabutwa na Mabondeni;
Je, Serikali itasaidiaje kutatua tatizo hili katika Jimbo la Manyoni Magharibi;
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi hasa Mtanzania kupitia kodi zao kusikiliza redio ya Taifa hasa TBC. Je, ni lini Serikali sasa itaweka booster yake ya TBC katika Mji Mdogo wa Itigi ili na wananchi wale wasikie redio yao ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenye gari yake yenye redio nzuri ili atakapofika Itigi asikie matatizo yaliyoko pale?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nimuulize swali dogo tu Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa swali la msingi linafanana sana na Jimbo langu la Manyoni Magharibi ambapo kuna zahanati tatu tu. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga vituo vya afya katika Kata za Idodyandole, Aghondi, Sanjaranda, Majengo, Tambuka Reli, Kitaraka, Mgandu, Kalangali, Mwamagembe na Ipande?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mkiwa - Itigi, Rungwa - Makongorosi aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi wenye vijiji vya Songambele, Majengo na Itigi Mjini na kwa majibu haya, maana yake barabara hii imeshushwa daraja. (Makofi)
Swali, wakati sheria inabadilika kutoka mita 45 kuja mita 60, wananchi hawa waliwekewa alama za “X” kwamba wasiendeleze maeneo yale. Sasa kwa majibu haya; je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutamka kwamba wale wananchi waendelee na ujenzi? (Makofi)
Pili, Naibu Waziri anaweza kuthibitishia wananchi wa Itigi kwamba itakapoanza kujengwa kilometa 35 za kwanza na kipande kile kitakajengwa pamoja nacho? Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona ili niulize swali dogo tu la nyongeza, kwa kuwa swali la msingi wananchi wa Morogoro linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi hususan Mji mdogo wa Itigi. Je, ni lini Serikali itasaidiana na Halmashauri yangu kuhakikisha Vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Kingwi, Dodiandole, Mbugani, Mabondeni, Njirii, Gurungu, Majengo, Songambele, Kitalaka, Kihanju na Tambuka Reli vitapatiwa maji? Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pamoja na Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa masikini ambayo inahitaji usaidizi wa Serikali. Sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusaidia wananchi wa mikoa hii ya Dodoma na Singida kwa ushawishi wake mkubwa na weledi wake kufanya basi angalau kiwanda kimoja kiwekezwe katika Mkoa wa Singida, hususan katika Jimbo la Manyoni Magharibi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea wananchi wa Itigi ili kujionea fursa zilizopo ili kushawishi wawekezaji waweke kiwanda katika eneo la Itigi? Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Korogwe yanafanana sana na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Itigi; kuna shamba lililokuwa la Shirika la Tanganyika Packers lipo katika eneo la Kitaraka, lilitelekezwa na shirika hili baada ya shirika hili kufilisika mwishoni mwa miaka ya 1980.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo yale katika vijiji vya Kitaraka, Kaskazi Stesheni, Doroto, Majengo, Tambukareli, Kihanju na Sanjaranda wamelitumia shamba lile kulima na linawasaidia sana kupata mahitaji yao ikiwemo mazao ya chakula pamoja na mazao ya biashara, lakini kuna taarifa kwamba Serikali ina mpango wa kulibinafsisha shamba lile kwa wawekezaji.
Je, ni nini kauli ya Serikali kwamba haitaonesha inaleta mgogoro na wananchi ambao shamba lile sasa linawanufaisha wananchi wengi sana wazawa na wananchi wa nchi hii kuliko kuweka mwekezaji, ni nini kauli ya Serikali juu ya suala hilo?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona ili niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa askari hawa ambao wanatekeleza kufanya nchi hii iwe na amani kuhakikisha wahalifu wanakuwa hawafanyi vizuri wako katika Jimbo langu la Itigi na wanakaa katika nyumba ya railway ambayo ni mbovu sana. Kituo kile kiko katika nyumba za railway; Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaboreshea Kituo cha Polisi na Mheshimiwa Waziri anajua kabisa kituo kile ni kibovu na hakifai na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wamejitahidi kwa nguvu zao wameshindwa. Nini kauli ya Serikali na je, itawasaidia wananchi wa Halmashauri ya Itigi?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa katika barabara hii korofi kipindi chake cha kuharibika sasa kimekaribia, kipindi cha mvua ambacho katika maeneo ya Lulanga, Itagata, Ukimbu, Mitundu, Kiombo, Mwamaluku, Mwamagembe, Kintanula hadi Rungwa udongo huo aliousema ni mbaya na ukarabati uliofanyika kipindi cha nyuma ulikuwa haukidhi kiwango. Je, sasa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kutosha katika kipindi hiki kabla mvua hazijaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika ujenzi wa kipande hiki cha kilometa 57 ambacho Meshimiwa Naibu Waziri amekisemea hapa, watakapoanza wanatarajia ni muda gani utachukua kukamilika? Maana yake wananchi wanahamu kubwa ya kuona barabara ya lami katika kipande hiki nikiwemo mimi Mbunge wao.
Mhesshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo tu kwa kifupi. Kwa kuwa matatizo yaliyopo huko Kyerwa yanafanana sana na yaliyopo katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi katika Mji wa Itigi ambao hauna maji kabisa toka nchi hii imepata uhuru. Je, sasa Serikali iko tayari kusaidiana na Halmashauri ya Itigi ili wananchi wa Itigi Mjini pale wapate maji?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa
kunipa nafasi. matatizo yaliyopo huko Segerea yapo pia katika Jimbo langu la
Manyoni Magharibi katika Halmashauri ya Itigi kuna msitu unaitwa Chaya Open
Area, ni kitalu cha uwindaji ambacho muda mrefu hakina Mwekezaji. Sasa
Serikali inataka kuondoa wananchi ambao wamekaa pale kwa ajili ya kulima na
wanafuga vizuri sana. Je, Serikali inaweza ikaona umuhimu wa wananchi wale
kuendelea kutumia Chaya Open Area ambapo ni eneo ambalo halina kabisa
faida kwa ajili ya uwindaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi kuna vijiji vya Mbugani, Agondi, Mabondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitalaka, Kaskazi Stesheni, Kintanura, Lungwa na Kalangali havina umeme. Je, Serikali inaweza kutoa tamko kwamba REA Awamu ya Tatu wananchi wa vijiji hivi watafikiwa na umeme?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's