Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Supplementary Questions
DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa, Mkoa wa Tabora ni kati ya Mikoa ambayo tunalima pamba sana hususan Wilaya ya Igunga, na kwa kuwa miaka ya nyuma tulikuwa na kiwanda hicho cha nyuzi lakini pia tulikuwa na kiwanda cha kuchambua pamba kule Manonga ginnery katika Jimbo la Manonga.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua hicho kiwanda ili kiweze kulisha kiwanda cha nyuzi cha Tabora?
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika swali la msingi, Wilaya ya Igunga nayo ina zahanati kama Jogohya, Mbutu, Mwazizi na Kalangale ambazo hazijakamilishwa. Je, Serikali nayo itaelekeza jicho lake huko kwenye Wilaya ya Igunga pia?
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu ambayo hayatoshelezi.
Kwa kuwa mimi nimezaliwa na kukulia katika mbuga hii, ni mashahidi kwamba mbuga hii ilitelekezwa, kwa hiyo, wananchi wengi wakulima na wafugaji walihamia katika mbuga hii. Matokeo yake wanyama na hao ndege anaosema wametoweka; kama wamebaki ni sehemu ndogo sana; na kwa kuwa eneo hili mwaka 2014 lilisababisha mauji ya wakulima watano kutokana na mgogoro wa wakulima: kwa nini Serikali isikubali ombi hili? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi nchi inakabiliwa na migogoro ya wafugaji na wakulima, sisi sote ni mashahidi; na kwa kuwa mwaka 2011 Serikali hii ilifanya tathmini ya mbuga zile ambazo zimepoteza sifa na Wembere ilikuwa ni mojawapo; kwa nini Serikali isilitazame upya jambo hili na kuitenga mbuga hii ili wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo waweze kulima na kufuga bila kugombana; lakini pia wanaweza kubakiza eneo dogo kwa ajili ya hawa ndege hawa anaowasema? Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utafutaji wa madini katika eneo la Kalambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, sasa hivi kule mitaani kuna malalamiko kwamba utafutaji umepungua sana, wawekezaji hawaji kwa sababu ambazo hazielezeki. Kwa nini Serikali sasa isichukue hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba utafutaji unakua na tuweze kupata migodi mingine siku za usoni? Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa matatizo ya maji vijijini, Serikali imekuwa ikifanya miradi mingi kama ilivyo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Mradi wa maji wa Kata ya Itunduru - Igunga, ulitekelezwa, miundombinu ikakamilika, lakini maji hayakupatikana, miundombinu imebaki white elephant. Nauliza ni lini Serikali itatafuta chanzo cha maji ili miundombinu hii iweze kutumika?
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kule Wilaya ya Igunga Jimbo la Igunga kulikuwa na Kata za Kiningila, Sakamaliwa na Kinungu, zilikuwa zimewekwa kwenye Mpango wa Mawasiliano kwa Wote, lakini pia Jimbo la Manonga Kata ya Goweko na Kata ya Mwanshiku. Ni lini sasa mradi huu utatekelezwa kwa maana yake tulitegemea mwaka 2015 na mwaka 2014 yafanyike? Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yasiyotosheleza sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Swali la kwanza; kwa kuwa kutunza dhahabu kwenye hazina ya nchi yoyote ni kuashiria utajiri wa nchi hiyo; kwa mfano, nchi ya Marekani ina dhahabu zaidi ya tani 8,100 kwenye hazina yake, lakini nchi ya Ujerumani 3,300 na nchi ya Italia ina tani 2,450. Kwa nini Tanzania tunachelea chelea kutunza dhahabu wakati sisi sasa hivi ni wazalishaji wa dhahabu duniani?
Swali la pili, kwa kuwa Tanzania ni nchi inayozalisha dhahabu kama Ghana, ina tani nane kwenye ghala yake, lakini Afrika ya Kusini ina tani 125. Na kwa kuwa kwa kipindi cha muda mrefu dhahabu imekuwa ikipanda thamani. Miaka ya 1900 dhahabu ilikuwa zaidi ya dola 200, miaka ya 2000 ilikuwa zaidi ya 500; sasa hivi ni zaidi ya dola 1000. Kwa nini Serikali inachelea kwamba dhahabu inatelemka bei. Kwa nini sasa Serikali isifanye utafiti ikaangalia nchi zingine zinafanyaje na ikatunza dhahabu kwenye hazina yake kwa ajili ya kupandisha uchumi wa nchi yetu? Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo hayatoshelezi kwa
sababu niliwahi kuuliza swali hili lakini nimepata majibu yale yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi, ni kwa nini tuendelee
kutumia dola katika kununua, siyo uhuru wa soko. Sasa swali la kwanza, kwa nini
Tanzania isitumie utaratibu wa nchi zingine kama Zambia, South Africa, Ghana,
Dubai na Ulaya? Wote tumesafiri tumeona ukifika tu kwenye nchi hizo
unaachana na matumizi ya dola lazima ubadilishe na ukalipe kwa hela yao.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa nini au ni lini Serikali sasa
itakagua haya maduka ya fedha ambayo kwa kweli kuna taarifa za ki-intelijensia
zinasema wanatumika kutorosha fedha zetu? Wakaguliwe, mapato yao
yajulikane na ijulikane pia ni jinsi gani wanazitumia hizi fedha na kuziweka kwenye
soko letu la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali kwamba mwaka 2013 Mji Mdogo wa Igunga ulianzishwa na tumekuwa na tatizo hili ambalo wanalisema wote kwamba umeanzishwa lakini haufanyi kazi. Namshukuru Waziri ameeleza kwenye swali namba 142 kwamba ni Halmashauri inatakiwa isimamie, lakini sisi tumejaribu kuishauri Halmashauri isimamie jambo hilo na nimeweza kufika ofisini kwake mara moja na akaahidi kwamba angeweza kuandika Waraka wa kumwambia Mkurugenzi au kuiambia Halmashauri ifanye jambo hilo na halijafanyika.
Namuomba Mheshimiwa Waziri hebu utusaidie kwa sababu DED sasa hivi hataki kabisa kuisikiliza hiyo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga na hawana bajeti, hawana gari, wana mtendaji tu. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie kama ikiwezekana njoo Igunga ili mamlaka hii iweze kuanza. Ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali ya nyongeza kwamba barabara ya kutoka Igurubi mpaka Igunga kwenda Loya tuliiombea na tulishapeleka maombi kwamba ipandishwe hadhi. Leo mwaka wa tano kuna shida gani?
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mengi ya masalia ya Wafalme pamoja na majengo; kwa mfano, Mtemi Shomali Mwanansali wa Igurubi, kuna majengo ya Mtemi Humbi Ziyota Mwanantinginya pale Ziba. Kwa nini Serikali sasa isiyatambue maeneo haya yote yenye majengo na masalia ya Watemi nchini kote na kuyatangaza? Najua wenzetu kutoka Ulaya watakuja kuyaangalia. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa muda sasa nchi za SADC ili kukuza fursa za uwekezaji na soko la pamoja zimeendesha mradi wa ku-harmonise au kuwianisha sera na sheria za nchi hizi ili kuweza kuvuna rasilimali hizi, lakini pia soko liwe la pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ya Tanzania imeshirikije kwenye mradi huu mpaka sasa? Tumefikia wapi? Maana bila ku-harmonise sheria zetu, soko hili haliwezi kuwa la pamoja na wala hatuwezi kuvuna rasilimali hizi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yametoa matumaini kwamba watafanyia research udongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, Jimbo la Igunga ni Jimbo ambalo udongo wake hauwezi kujengwa kwa kukwangua barabara lazima uweke tuta kwahiyo hela zinazotengwa kwa Halmashauri hizi hazitoshi kabisa kujenga hizi barabara.
Swali la kwanza, je, kwa nini Serikali isilete upendeleo kwenye Jimbo hili la Igunga ikasaidia kujenga barabara za vijijini?
Swa li la pili, kwa azma ya Serikali ya kuunganisha Mikoa Tanzania, kwanini Serikali isijenge kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Kolandoto kupitia Igurubi kwenda Igunga, Mbutu na kwenda mpaka Loya kwenye Jimbo la Igalula na mpaka Tura kwenye barabara ya lami itokayo Tabora kwenda Dodoma?
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mengi ya masalia ya Wafalme pamoja na majengo; kwa mfano, Mtemi Shomali Mwanansali wa Igurubi, kuna majengo ya Mtemi Humbi Ziyota Mwanantinginya pale Ziba. Kwa nini Serikali sasa isiyatambue maeneo haya yote yenye majengo na masalia ya Watemi nchini kote na kuyatangaza? Najua wenzetu kutoka Ulaya watakuja kuyaangalia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna dhuluma sana miongoni mwa wananchi wetu, ni lini sasa Serikali itachukua hatua kwa sababu kuna matukio mengi sana ambayo siwezi kuyaorodhesha hapa, yako kule kwenye Jimbo la Igunga ambapo wananchi wengi sana wamedhulumiwa. Ni lini sasa Serikali itachukua hatua hizo badala ya kutoa onyo tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kwenye Kijiji cha Lugubu, kijiji kiliamua kutenga eneo moja kuwa eneo la hifadhi, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watendaji waliwaruhusu wananchi wawili waingie kwenye hilo eneo na kukazuka mgogoro mkubwa sana wa ardhi ambao Mahakama ya Ardhi na Mahakama ya Mwanzo wameshindwa kuurekebisha huo mgogoro. Je, ni lini sasa Serikali itatusaidia jambo hili ili tuweze kutenga eneo katika Kijiji hicho cha Lugubu? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa Wilaya ya Ugunga na Jimbo la Igunga kwa ujumla lina uhitaji mkubwa sana wa mabwawa kama ilivyo Lupa; na kwa kuwa mabwawa ya Mwanzugi na Igogo sasa yamefikia uhai wake, yalijengwa miaka ya 1970, hayana nafasi tena ya kuendelea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea mabwawa mengine mawili kwa ajili ya umwagiliaji kama yalivyokuwa haya mabwawa mawili? Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Igunga kwenda Mwanzugi hadi Itumba ilikuwa na mkandarasi wa TARURA aliyewekwa na TARURA anaijenga, lakini uharibifu ulikuwa mdogo sana. Sasa hivi kutokana na mvua kama ulivyosema barabara hiyo imeharibika sana, naiomba Serikali itakuwa tayari kweli kuongezea bajeti kwa ajili ya kuijenga hiyo barabara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Igunga? Ahsante sana. (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's