Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Supplementary Questions
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mamlaka ya Maji ya Tabora Mjini (TUWASA) ina matatizo makubwa ya malimbikizo ya madeni zaidi ya bilioni mbili ambayo inawadai Taasisi za Serikali na hasa majeshi yetu na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema katika majibu yake ya msingi kuna pesa zimetengwa kulipa katika miradi mbalimbali. Je, ni lini Mamlaka ya Maji Tabora watalipwa pesa zao ambazo zinawafanya sasa wasifanye kazi kwa ufanisi?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, ninaomba kumuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa kwenye bajeti ya Serikali mwaka huu moja ya vitu vilivyoainishwa mle ni pamoja na kufanya review ya mikataba mingi kwa hawa waliobinafsishiwa viwanda. Sasa ni lini Serikali itafanya review ya kujua uwezo wa huyo mwekezaji kuhusu kuwekeza Tabora Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna tuhuma zinazomuhusu mwekezaji huyo wa kiwanda cha Nyuzi kwamba kuna mashine mbalimbali ambazo aliziuza kama vyuma chakavu, ambazo zilikuwa mle kwenye kiwanda na kwamba kuna mashine nyingine ambazo tayari zilishasafirishwa, hazipo kabisa pale;
Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi ili kujiridhisha kwamba mwekezaji yule kweli hajaziuza mashine hizo au kuzihamisha nje ya nchi?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa mazungumzo na hawa wawekezaji mahiri wa kusindika tumbaku na mambo ya sigara yanaendelea. Je, mazungumzo hayo yakifanikiwa, ana uthibitishia Mkoa wa Tabora kwamba utapata upendeleo kwa kujengwa Kiwanda cha Tumbaku? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameonesha nia ya Serikali kuwashirikisha mashirika ya kijamii kama NSSF kushiriki kwenye ujenzi wa viwanda na biashara, je, ni lini mazungumzo hayo, Serikali itaanza na haya mashirika ya kijamii?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, tatizo linalowakabili wananchi wa Maswa Magharibi kuhusu bwawa lao, linafanana kabisa na tatizo la bwawa la Kazima Mjini Tabora ambalo maji yake yanapungua mara kwa mara hasa wakati wa kiangazi, kutokana na tope pamoja na mchanga uliojaa pale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha lile tope pamoja na mchanga linaweza kuondolewa ili wananchi wa maeneo yale waweze kupata maji ya kutosha?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikopwa na pesa zao zinachukua muda mrefu sana kuja kulipwa, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wananchi hawa wanaolima tumbaku hasa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kwamba wanalipwa pesa yao na riba kama wanavyofanya mabenki?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Raphael Michael, Mbunge wa Moshi Mjini ametoka nje, naomba nitumie nafasi hii kwa sababu swali alilouliza linafanana kabisa na suala ambalo liko Tabora katika Hospitali yetu ya Mkoa ya Kitete, naomba niulize swali kwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Hospitali yetu ya Mkoa wa Tabora ya Kitete ina tatizo lile lile la mlundikano wa wagonjwa kama ambavyo iko Moshi Mjini. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Hospitali ya Wilaya inajengwa Tabora ili kuweza kupunguza huu mlundikano wa wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete ina upungufu mkubwa sana wa Madaktari, tuna Daktari Bingwa mmoja tu. Serikali inajipanga vipi kuhakikisha Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete inapata Madaktari Bingwa wa kutosha?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kutokana na msongamano huo wa magereza na mahabusu ambao hata Mheshimiwa Waziri ameukiri hapa, kunasababisha magonjwa mengi hasa ya mlipuko; nimewahi kutembelea Gereza la Uyui pale Tabora, kulikuwa na wagonjwa wengi wa upele; na sasa hivi kuna tatizo kubwa sana la upatikanaji wa madawa sijui Serikali ina mkakati gani wa kufanya upendeleo kuhakikisha wale mahabusu na wale ambao ni wafungwa wanapata dawa za kutosha?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililopo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, linafanana kabisa na tatizo ambalo lipo kwenye Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Rufaa ya Kitete. Kuna tatizo kubwa sana la wagonjwa na hasa akinamama wanapoenda kujifungua, wodi ile ni ndogo na wengi wanalala chini wakiwa hata wale wachache wanakuwa wana-share kitanda kimoja:-
Je, Serikali inajipanga vipi kutatua hili tatizo la muda mrefu la msongamano wa akinamama wanapojifungua pale Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mkoa wa Tabora hususani Tabora Mjini tuna mabwawa makubwa mawili, Bwawa la Igombe na Bwawa la Kazima, pia tuna mradi wa bwawa ambalo lipo Kata ya Ndevelwa ambalo limeigharimu Serikali zaidi ya shilingi bilioni moja ambalo mpaka sasa hivi halifanyi kazi kwa sababu linavuja.
Mheshimiwa Spika, sijui Serikali ina mkakati gani wa kufanya mradi huu ambao kwanza umekwama, lakini pamoja na haya mabwawa mengine yaweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili wananchi kwa ujumla waweze kupata ajira pamoja na kuweza kupata mazao kwa ajili ya kujikimu kutokana na hali mbaya ya chakula ambayo inaikabili nchi yetu kwa sasa?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu
Waziri, nauliza swali ambalo kama ilivyo Rungwe ule mradi wa Masoko, Tabora
Mjini ule mradi wa Ziwa Victoria, kuna vijiji ambavyo niliviorodhesha kwenye swali
Na. 57 lililojibiwa hapa Bungeni ambavyo ni Vijiji vya Itetemla, Uyui, Ntalikwa,
Kabila, Mtendeni, Itonjanda na baadhi ya maeneo ambayo ni ya Kata za Tumbi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji hivi na hizi Kata havijaorodheshwa kwenye
huu mradi wa Ziwa Victoria na vina shida sana ya maji. Sijui vitapitiwa lini na
mradi huu wa Ziwa Victoria? Naomba swali langu lipatiwe majibu. Ahsante.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa kuwa huu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaonekana unaendelea kusuasua na hauna uhakika exactly lini utaanza na wananchi wa Tabora wanaendelea kuteseka kwa shida ya maji na sisi pale Tabora Mjini tuna bwawa kubwa la Igombe ambalo lina-access ya maji kwa maana ya lita za ujazo ambazo Serikali kama itaweka mpango mkakati wa kusambaza maji yale ya Igombe na kwa unafuu, Wananchi wa Tabora Mjini watapata nafuu ya tatizo la maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba yale maji ya Igombe yaweze kusambazwa kwa bei nafuu kuliko kusubiri huo mradi wa Ziwa victoria ambao haujulikani utaanza lini? Hilo la kwanza
Swali la pili, moja ya tatizo lingine linalosababisha ile Mamlaka ya Maji (TUWASA) Tabora inapata matatizo katika uendeshaji wake ni pamoja na kutolipa deni ambalo Mamlaka ya Uendeshaji ya Maji - TUWASA pale Tabora inaidai Serikali kwa muda mrefu zaidi ya shilingi bilioni 2.3 ambazo zinadaiwa hasa kwenye taasisi zetu za majeshi pamoja na taasisi zingine za Serikali.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha TUWASAwanalipwa pesa hizo ili Tabora iweze kupata maji ambayo yatakuwa ni ya uhakika? Ahsante.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa hii biashara ya vyuma chakavu inavikumba pia viwanda vilivyobinafsishwa kwa muda mrefu sasa kikiwemo Kiwanda cha Nyuzi Tabora, na kwa kuwa kuna taarifa kwamba mashine nyingi mle ndani zimeuzwa kama chuma chakavu na kimefungwa kile kiwanda, je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu nimewahi kulalamika hapa Bungeni na kutoa taarifa kuhusu kufanyika kwa vyuma
chakavu, ni lini tunaweza tukaenda tukakagua kile kiwanda kwa sababu sasa hivi umetoka kusema utakula nao sahani moja, tuweze kujua kama vile zile mashine hazijauzwa kama vyuma chakavu?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongezana ninaomba kuiuliza Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba hii migogoro kweli ipo na ni ya muda mrefu, Jimbo la Tabora Mjini linazungukwa na kambi nyingi za Jeshi ambazo migogoro mingi inapelekea kuhatarisha amani miongoni mwa wanajeshi pamoja na raia. Ni lini sasa Serikali au Serikali ina mpango gani wa kuwakutanisha wanajeshi wahusika ili waweze kukaa na wananchi kuweza kutatua migogoro hiyo ya ardhi iliypo Tabora Mjini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inafanya uhakiki mbalimbali kuanzia watumishi wa Serikali na mpaka leo tumeona wale wa vyeti, lakini ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa Maafisa wa Ardhi ambao wanaingiza migogoro kwa makusudi kati ya wananchi pamoja na Serikali kwa kufanya mpango wa kugawa viwanja; kwa mfano kiwanja kimoja kutolewa zaidi ya mtu mmoja (double allocation). Maafisa hao wapo na hawajafanyiwa uhakiki ili wachukuliwe hatua. Ni lini Serikali itafanya uhakiki wa hawa maafisa wanaoleta migogoro ili na wao wachukuliwe hatua?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyopo Kwera yako sawasawa kabisa na matatizo ambayo yapo kwenye Manispaa ya Tabora kwenye barabara ile ya Mambali ambayo inapita Misha, Kata ya Kabila, Kata ya Ikomwa mpaka kutokea Bukene. Barabara hii kwa kiwango kikubwa eneo kubwa lipo eneo la halmashauri na haijapandishwa daraja pamoja na maombi ya muda mrefu. Hata hivyo, kwa kuwa Halmashauri ya Tabora uwezo wa kuitengeneza barabara hii kwa lami unaonekana haupo kabisa, Serikali ina mpango gani kuhakikisha barabara hii inawekwa kiwango cha lami ili iweze kuwa endelevu katika uchumi wa Mkoa wa Tabora? (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali inakiri kwamba ujenzi wa bwawa hili ulikamilika mwaka 1958, kwa maana hiyo ujenzi huu uliwakuta wananchi wengi ambao walikuwepo pale kwa miaka mingi kabla ya hapo na kwa kuwa wananchi wanaendelea kunyanyasika maeneo yale na hasa kwa kukosa sehemu ya kilimo; na kwa kuwa kuna wananchi ambao wao ni waaminifu na hawaharibu mazingira.
Je, Serikali iko tayari angalau kuwapa wananchi maeneo mbadala ya kuweza kufanya shughuli zao za kilimo maeneo yale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa maeneo yale kumekuwa na matatizo ambayo yanahusiana pia na mifugo ya wananchi hao hao wamekuwa wakikamatiwa mifugo yao na maafisa wa wanyamapori na wengine wala siyo maafisa wa wanyamapori wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi, wakikamata ng’ombe zao na wengine kuwapiga fine ambazo hazina hata receipt.
Nini tamko la Serikali kuhusu hawa maafisa wa wanaymapori hewa ambao wanakuwa wanafanya uhalifu ndani ya maeneo yale?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la kutolipa wakandarasi au wazabuni katika sehemu mbalimbali za nchi hasa wale ambao wanatoa huduma kwenye vituo vya polisi limekuwa ni kubwa kwa muda mrefu. Kwa mfano, mkoani Tabora kuna wazabuni wengi ambao wanaidai polisi malimbikizo ya muda mrefu ya huduma wanazotoa na hasa utengenezaji wa magari.
Kwa mfano Tabora yapo malalamiko ya muda mrefu ya mzabuni ambaye anatengeneza magari ya polisi hajalipwa sasa hivi ni zaidi ya miaka mitatu, anadai zaidi ya shilingi milioni 222. Sijui Mheshimiwa Waziri anazo taarifa hizi na kama hana, atasaidiaje mkandarasi huyu ambaye ndiye anatengeneza magari ya polisi pale Tabora Mjini alipwe fedha zake?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tabora Manispaa tuna tatizo kubwa la msongamano wa wagonjwa katika Hospitali Teule ya Kitete na kwa kuzingatia hilo, Tabora Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani pamoja na wananchi wengine tumetenga eneo kwa ajili ya kujengwa Hospitali ya Wilaya ambayo mpaka sasa hivi ujenzi wake unasuasua kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali inajipanga vipi katika kusaidia uwezeshaji wa kuweza kujenga hospitali hiyo ya wilaya?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nukipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Tabora una vivutio vingi vya utalii ukiwemo uwandaji. Ni lini Serikali itafanya uhakiki wa vitalu vya uwindaji vilivypo Tabora? Kwa sababu kuna taarifa kwamba vitalu vya uwaindaji vilivyopo vinasomeka ni vichache kuliko uhalisia wa vitalu vilivyopo?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Tabora Manispaa imeathirika sana na migogoro ya ardhi. Kuna kata ambazo zinapakana na maeneo ya jeshi, ambazo ni Kata za Cheyo, Mbugani, Tambuka Reli, Uyui na Micha. Maeneo yale yamekuwa na migogoro ya mipaka ya muda mrefu. Je, Wizara ya Ardhi imejipangaje kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi ili waweze kuoanisha sasa mipaka halisi ili kuweza kutatua migogoro hii ya mipaka katika kata hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Tabora kama nilivyosema manispaa imekuwa na migogoro mikubwa ya ardhi na hasa bomoa bomoa. Tabora imeathiriwa sana na zoezi la bomoa bomoa; si maeneo ya reli tu lakini hata maeneo mengine yanayopaka na mashule kama Tabora Girls…
Wananchi wale na maafisa kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri wengine si waaminifu. Je, Serikali kwa kuwa hawa wananchi wengi waliobomolewa hayakuwa makosa yao, inawachukulia hatua gani hawa ambao wamesababisha wananchi wamepata hasara kubwa na sasa hawana hata amani na wamekuwa katika hali isiyoeleweka?
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, tatizo la akina mama kujifungua mara nyingi wakati mwingine linaletwa pia na matatizo ya baadhi ya ma-nurse ambao huwa wanawanyanyapaa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua.
Sasa sijui Serikali ina mpango gani au huwa inachukua hatua gani kuwadhibiti hawa akinamama ambao wana tabia za kuwanyanyasa akina mama wenzao wanapotaka kujifungua? (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza mradi mkubwa sana wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwenda Tabora na mradi huo kuna kipindi vifaa vya ujenzi vilikuwa vina mikwamo kwamo. Swali langu ni dogo tu, je, mradi huo umefikia kwenye hatua gani ya utekelezaji na wananchi wa Tabora wategemee kupata maji hayo lini? (Makofi)

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Chamwino ndiyo tatizo lililopo Manispaa ya Tabora. Ofisi mpya ya Halmashauri imekwama kwa muda mrefu sasa kukamilika kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Kwa kuwa ombi maalum kupitia Hazina Serikali iliahidi kutoa shilingi bilioni mbili ili kuweza kukamilisha ujenzi huo pamoja na kumlipa mkandarasi anayedai karibu shilingi bilioni moja Masasi Construction.
Je, Serikali ni lini italeta pesa hiyo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ili jengo hili liweze kukamilika? (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Tabora Mjini, Kata ya Ikomwa maeneo ya Kapunze; Kata ya Kabila, maeneo ya Igosha; Kata ya Ndevelwa, maeneo ya Ibasa; na mengine ambayo kwa muda mrefu hayana mawasilino, Halotel inaonekana inasuasua hata kwenda kufanya survey tu maeneo yale. Sijui Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hawa Mameneja wa Mikoa wa Halotel wanafanya kazi ipasavyo ili maeneo hayo yapatiwe huduma ya mawasiliano? Serikali ina mkakati gani kwa kuwa hiyo pesa inalipwa na Serikali kuhakikisha hawa Mameneja wa Mikoa wa Halotel wanafanya kazi yao kwa ufanisi.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's