Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Musa Rashid Ntimizi

Supplementary Questions
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Wananchi wa Jimbo la Igalula hususani Kata ya Loya na Halmashauri yetu imefanya kazi kubwa sana kujenga kituo hicho cha polisi na nguvu kwa sasa imetuishia na kazi kubwa imefanyika. Serikali kupitia Wizara haioni umuhimu wa kusaidia nguvu hizi za wananchi katika kumalizia kituo hiki cha polisi na kiweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Igalula na Kata ya Kigwa kuna vituo vya polisi ambavyo vingeweza kutoa huduma katika Kata ya Loya kipindi hiki hatuna kituo kituo cha polisi katika Kata ya Loya. Tatizo letu kubwa lililopo pale katika vituo hivi viwili vya polisi havina usafiri. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuvipa usafiri vituo hivi vya polisi ili viweze kuendelea kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana vituo vya polisi?
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nia nzuri ya Serikali ya kumpunguzia mkulima wa tumbaku makato mengi ambayo yanafanya mkulima huyu asipate tija ya zao la tumbaku, kuna shida ya makato ya mkulima yanayotokana na ujenzi wa ma-godown ambayo ma-godown yale yalijengwa kwa mkataba wa CRDB na kupatikana mkandarasi kwa kupitia CRDB. Ma-godown yale hayana tija yamedondoka mpaka sasa hayafanyi kazi lakini mkulima wa tumbaku anaendelea kukatwa mpaka sasa. Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru pia kwa juhudi nzuri za Mheshimiwa Waziri anazozifanya katika kuhakikisha kwamba Mikoa ambayo inalima mazao mbalimbali, inakuwa na uwezekana wa kupata viwanda vya ku-process hayo mazao. Mkoa wetu wa Tabora una zao la tumbaku, na juhudi ambazo anazifanya Mheshimiwa Waziri tunaziona;
Je, Mheshimiwa Waziri anatuelezaje kuhusu uwezekano wa kupata mwekezaji wa kuja kuweka kiwanda katika cha kuchakata kuchakata zao la tumbaku katika Mkoa wetu wa Tabora?
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri na majibu yanaleta matumaini kwa hawa askari wetu, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika mpango huu wa Serikali wa kujenga nyumba za askari wetu, Wilaya yetu ya Uyui itaangaliwa kwa macho mawili? Kwa sababu Halmashauri yetu ya Tabora kwa maana ya Uyui imetumia zaidi ya shilingi milioni 300 kujenga kituo kile cha polisi, kwa sasa kama nilivyosema kwenye swali la msingi askari wetu hawana makazi ya kukaa wanakaa kwenye nyumba za mabati.
Lakini la pili, Serikali ina wajibu wa kuwapatia makazi bora askari wetu, ukiangalia nchi nzima askari wetu wanakaa katika nyumba za kupanga mitaani kwa sababu hakuna makazi ya askari wetu.
Je, Serikali inawalipa posho ya makazi askari hawa au ina mpango gani wa kuwalipa posho za makazi askari hawa kwa sababu wanakaa nyumba za kupanga uswahilini? Ahsante.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Shida ya maji ya Kilindi inafanana na shida ya maji katika Jimbo letu la Igalula. Tuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaokuja katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora, lakini mradi huu hauleti maji katika Jimbo letu la Igalula. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuchepusha mradi ule kuleta katika Jimbo letu la Igalula ili kuondoa matatizo ya maji?
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tatizo la barabara hii ya Kilombero linafanana na tatizo la barabara yetu ya Tabora - Itigi. Kipande cha Chaya - Nyahua kilomita 89 ambacho kinaifanya barabara hii mpaka sasa isiweze kupitika na tunaelekea katika kipindi cha mvua.
Barabara hii ni muhimu sana kwa sisi wakazi wa Tabora, Katavi na Kigoma. Tunaomba Serikali ituambie ni lini barabara hii itatengenezwa ili kufungua barabara hii na kusaidia wakazi wa mikoa hiyo? Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru wewe na pia kwa kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri; lakini katika majibu yake Serikali imekiri kwamba wanunuzi hawa wa tumbaku wana muungano wa ukiritimba katika kupanga bei na kiasi cha tumbaku cha kununua. Wanapenda kuangalia gharama za mkulima katika kuzalisha zao lake ndipo wapange bei, lakini sisi hatujui wao wanauza shilingi ngapi katika Soko la Dunia. Je, ni hatua gani Serikali inachukua katika kumsaidia mkulima huyu wa tumbaku katika kupata bei nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ililitangazia Bunge kwamba kupitia WETCU wana mpango wa kufufua Vyama 64 vya Wakulima wa Tumbaku ambapo wanachama wa vyama vile walichangishwa sh. 100,000/= kila mmoja katika kufanikisha zoezi hilo, lakini leo WETCU na makampuni wamewanyima wakulima hawa pembejeo, lakini vile vile wanasema kwamba soko la kununua tumbaku ile hakuna. Wakulima tayari wameshalima na utaratibu wote wameshamaliza na hawajui watauzia wapi tumbaku hiyo. Je, Serikali inawaambia nini wakulima hawa wa tumbaku ambao tayari sasa wemeshalima tumbaku yao na wanasubiri mauzo? Ahsante sana.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa TIC kuhusu kunadi fursa hiyo kwa wawekezaji kuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Tabora lakini wawekezaji wa Philip Morris wanaozalisha sigara duniani wanatarajia kuja kujenga kiwanda hiki mkoani Morogoro. Pamoja na kwamba Serikali kupitia Halmashauri yetu ya Nzega, Tabora Manispaa na Wilaya ya Uyui tulishatoa maeneo kwa ajili ya kiwanda hiki kuja kujengwa Tabora, lakini bado tunasikia Philip Morris wanakuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kwamba haiwatendei haki wana Tabora ambao ndiyo watoka jasho wakubwa katika zao hili la tumbaku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, Serikali imekiri asali bora na nyingi inazalishwa katika Mkoa wa Tabora hususani katika Jimbo la Igalula. Kwa nini Serikali kwa makusudi makubwa kabisa isingesaidia uongezaji wa thamani wa zao hili la asali kwa maana ya kupata utaalamu na packaging ili kusaidia kipato cha wana Igalula na nchi kwa ujumla? Ahsante.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya matatizo ya Walimu wetu ni kukosa makazi katika maeneo wanayofundishia katika vijiji vyetu. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za kutosha kwa Walimu wetu ili kuwapa motisha kufundisha vizuri katika maeneo yetu?
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nazungumzia shule hizi ambazo tunazijenga kutokana na umbali wa shule mama. Kuna maeneo ni zaidi ya kilometa 20 watoto wanatembea, hata hawa kuanzia darasa la nne mpaka darasa la saba wanatembea zaidi ya kilometa 20 kwenda na kilometa 20 kurudi, tunasababisha wasichana kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba, lakini pia tunasababisha wavulana kuona hakuna umuhimu wa kwenda kusoma kwa sababu ya umbali wa shule hizi.
Je, kwa nini sasa Serikali haioni umuhimu wa kutumia kigezo hicho kuzisajili shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili Mheshimiwa Waziri amesema moja ya sababu ya vigezo vinavyoweza kufanya shule hizo zisisajiliwe ni kutokuwa na ofisi za Walimu Wakuu na kadhalika kama alivyovitaja. Baadhi ya shule zetu nyingi hizo tunazoziita za satellite zimeshajengwa kwa asilimia zaidi ya 80 zimekamilika lakini bado hazisajiliwi. Wakaguzi wakija wanatoa kila siku sababu mpya. Kwa nini shule hizi ambazo zimetimiza zaidi ya 80% ya vigezo zisijaliwe? Ahsante sana.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Wakati tunasubiri utaratibu wa kupata maji hayo ya uhakika ya hiyo progamu ya pili ya maji hayo kutoka Ziwa Victoria, je kwa sasa Serikali ina utaratibu gani wa haraka wa kusaidia kutatua maji katika Jimbo la Igalula?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kwisha, kuambatana na mimi kwenda katika Jimbo la Igalula kuona shida kubwa ya maji ya wananchi wa Jimbo la Igalula? Ahsante. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini shida ya ya maji Longido ni sawasawa na shida ya maji iliyopo Jimbo la Igalula. Maeneo mengi ya Jimbo la Igalula maji chini hayapatikani kwa urahisi, visima vingi vimechimbwa lakini havitoi maji na kusababisha kupotea fedha nyingi za Serikali; lakini yako maeneo mengi ambayo yanaweza yakachimbwa mabwawa na yakasaidia upatikanaji wa maji katika Jimbo la Igalula.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umeshafanyika, upembuzi yakinifu na usanifu katika Kata ya Goweko na Igalula umeshafanyika, lakini mpaka sasa miradi hii haijafanyika na miradi hii ilikuwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, lakini mpaka sasa hakuna kinachofanyika. Sasa naomba kujua miradi hii ni lini itatekelezwa? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Halmashauri ya Chamwino linafafana na tatizo la Halmashauri ya Tabora Uyui. Tuna zaidi ya miaka kumi tumeamia Isikizya, lakini jengo la Halmashauri yetu lina zaidi ya miaka mitano halijakamilika kutokana na kutoletewa pesa.
Je, ni lini Serikali itatusaidia ili kumalizia ujenzi wa jengo hilo. Ahsante.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya matatizo ya Walimu wetu ni kukosa makazi katika maeneo wanayofundishia katika vijiji vyetu. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za kutosha kwa Walimu wetu ili kuwapa motisha kufundisha vizuri katika maeneo yetu?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's