Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Hussein Mohamed Bashe

Supplementary Questions
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nisikitike na samahani kwa kauli nitakayosema, ni aidha Manaibu Waziri wanapokuja kutujibu au Mawaziri hawako serious, wanatuchukulia for granted ama hawafanyi kazi yao ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Naibu Waziri anasema majengo ni mali ya mkandarasi hayawezi kurejeshwa Serikalini. Anataka kutuambia mimi na Rais tarehe 14 Oktoba, 2015, tuliwadanganya wananchi wa Nzega tukijua kwamba majengo yale ni mali ya mkandarasi na hakutakuwa na chuo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mji wa Nzega una sekondari inayoitwa Bulunde, majengo yalikuwa ya mkandarasi. Je, Serikali utaratibu ule ule iliyotumia kuyapata majengo yaliyotumika kwa ajili ya sekondari ya Bulunde, inakuwa na ugumu gani leo kuyapata majengo yanayotumiwa na mkandarasi anayejenga barabara ya Nzega - Puge ili kuanzisha Chuo cha VETA.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa msingi wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kutazama uwezo wa Halmashauri, kwamba haina uwezo wa kujenga madaraja haya pamoja na barabara zake, thamani ya madaraja haya mawili ni zaidi ya milioni 800.
Je, Waziri yupo tayari kuthibitishia Bunge lako na wananchi wa Jimbo la Nzega kwamba miradi hii itapalekwa TANROAD kama ambavyo Rais aliahidi?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na commitment ya Serikali kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya sekondari ya Bulunde na kutoa fedha kwa ajili ya sekondari ya Chief Itinginya. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo moja;
Kwa kuwa, jitihada za wananchi na Mbunge wa Jimbo la Nzega ni kumalizaS ya Bulunde ili tuwe na high school, na kwa kuwa, mahitaji ya fedha yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya shule ya Chief Itinginya hayatoweza kumaliza ujenzi wa shule ile kuwa na high school katika sekondari ya Chief ya Itinginya, mahitaji halisi ni shilingi milioni 250.
Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ya Chief Itinginya, ili katika Halmashauri ya Mji wa Nzega tuwe na shule mbili za A-level ?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza naishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Nzega, Mheshimiwa Profesa Muhongo na Mheshimiwa Kalemani wametekeleza ahadi ya kuturudishia machimbo ya Na. 7 na wiki hii wachimbaji wadogo watakabidhiwa maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali moja tu. Mwaka 2005 Rais wa Awamu ya Nne aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Nzega, hasa wa Jimbo la Bukene ujenzi wa kilometa 146 wa Barabara ya kutoka Tabora, kupita Mambali, kuja Bukene, kwenda Itobo, kwenda Kahama na Kilometa 11 kutoka Nzega Mjini kuunganisha mpaka Itobo kuweza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ya mwaka 2014/2015 Serikali ilitenga fedha za upembuzi yakinifu na tenda ikatangazwa, Wakandarasi wote walioomba wakawa wame-bid zaidi. Je, Serikali iko tayari sasa kuongeza fedha ili barabara ile upembuzi yakinifu ukamilike na ujenzi uweze kuanza? Ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mgodi mkuu uliokuwepo katika Mji wa Nzega wa Resolute ulishafungwa na kwenye ripoti ya TMAA inaonyesha Mwekezaji huyu aliondoka na fedha za Halmashauri ya Mji wa Nzega, ten billion shillings ambazo zilikuwa ni service levy: Je, kama Wizara, imefikia wapi kulifuatalia suala hili kuhakikisha haki hii ya wananchi wa Mji wa Nzega inarudi? ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Igunga pamoja na upatikanaji wa maji kitakwimu wa asilimia 60, lakini kutokuwepo kwa umeme wa uhakika kunapelekea upatikanaji wa maji katika Mji wa Igunga kuwa angalau kwa wiki mara mbili. Je, Waziri ama Serikali wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria, inaweza kutusaidia katika Mji wa Igunga kuwapatia angalau generator ili liwe pale ambapo umeme haupo, basi waweze kupata maji ya uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo la Igunga linafanana sana na tatizo la Mji wa Nzega; na upatikanaji wa maji katika Mji wa Nzega kwa sasa ni asilimia 30 tu ya maji na maji haya yanapatikana kwa wiki mara tatu: Je, Serikali ni lini itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa matenki matano na kuweka chujio la maji katika bwawa la Kilime na pampu ili wananchi wa Mji wa Nzega wasiendelee kupata shida wakati tunasubiri mradi wa maji wa Ziwa Viktoria?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naomba kumuuliza swali fupi Mheshimiwa Waziri pamoja na jitihada alizozifanya katika Mgodi wa Resolute, Nzega. Je, sasa Serikali iko tayari leseni iliyokuwa chini ya MRI iweze kugawia kwa wachimbaji wadogo wa Mwaishina ambayo maarufu kwa namba saba original katika mji wa Nzega?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningeomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la Itobo linafanana kabisa na tatizo la Kata ya Lusu kuwepo kwa kituo cha afya ambacho kilijengwa na ADB chenye vifaa na vitendea kazi vya namna hiyo. Je, Serikali haioni wakati umewadia wa kuhakikisha wanapeleka Wataalam na katika kituo cha afya cha Lusu ili kuweza kutatua tatizo linalowakabili wananchi wa Lusu kwa sababu wanatembea zaidi ya kilometa 20?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kituo cha afya cha Zogolo kilichopo katika Kata ya Nzega ndogo ambacho majengo yake yamekamilika na baadhi ya majengo kwa ajili ya wodi kwa akinamama na theatre yanahitaji kumaliziwa na kituo cha afya kilichopo Kata ya Mbogwe ambacho hutumika kwa ajili ya kuhudumia Kata zaidi ya saba, je, Serikali haioni wakati umewadia wa kutenga fedha kwenda kusaidia nguvu za wananchi katika vituo hivi vya afya vya hizi Kata mbili cha Zogolo na Mbogwe ili wananchi wa maeneo hayo waache kusafiri masafa marefu kwenda kufuata huduma katika hospitali ya Wilaya ya Nzega?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Kwa kuwa tatizo linalowakabili wananchi wa Mufindi Kusini linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Nzega Mjini; nilitaka kusikia kauli ya Waziri, katika kata ya Migua, jimbo la Nzega Mjini, Kata za Mwanzoli, Mbogwe, maeneo ya Bulunde pamoja na Kashishi yote haya yalikuwa yapekelewe umeme kwa miradi ya MCC na miradi hii imefutwa. Je, Naibu Waziri anasema kauli gani kuwaambia wananchi wa jimbo la Nzega wa maeneo haya juu ya upatikanaji wa uhakika wa umeme katika maneo niliyoyataja? Ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru. Nilitaka kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shilingi bilioni 5.2 ni sawa sawa na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa zaidi ya miaka mitatu, na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Nzega haina uwezo wa kifedha na ndio ilikuwa mantiki ya kumuomba Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na baadaye Rais John Pombe Magufuli kwamba miradi hii ya ujenzi wa kilometa 10 iende chini ya TANROADS.
Je, sasa Serikali iko tayari kuwaambia wananchi wa Jimbo la Nzega kwamba miradi hii ya kilometa 10 itajengwa chini ya utaratibu wa TANROADS na si kwa kutumia fedha za Halmashauri ya Mji?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa maeneo mengi ambayo wawekezaji wakubwa wamewekeza wameacha athari kubwa katika maeneo hayo na mojawapo ni Wilaya ya Nzega katika Mgodi wa Resolute, wananchi wameachiwa mashimo makubwa bila manufaa yoyote. Je, Serikali sasa iko tayari kumnyima mwekezaji Kampuni ya Resolute, certificate ya kumruhusu kuondoka nchini ambayo anatakiwa apewe mwezi wa sita kabla hajalipa deni ambalo anadaiwa la shilingi bilioni 10 na Halmashauri ya Mji wa Nzega?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kujenga Taifa la Viwanda na sekta ya kilimo kuwa ni muhimu. Katika Halmashauri ya Mji wa Nzega tumekuwa na mradi uliokuwa unasimamiwa na Shirika lililokuwa linaitwa NZEDECO miaka ya 1970 na miaka ya 1980 la umwagiliaji katika Kata ya Idudumo, mradi huu sasa hivi umekufa. Vilevile katika Halmashauri ya Mamlaka Ndogo ya Mji wa Igunga nako katika Bwawa la Imamapuli limejaa tope.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali iko tayari
kuhakikisha kwamba miradi hii miwili katika Halmashauri hizi mbili katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 wanatenga fedha kwa ajili ya kuifufua miradi hii ili wananchi wa maeneo hayo waweze kufaidika?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba mwaka 2010 wananchi wa Jimbo la Nzega waliahidiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kilometa 10 za lami ndani ya Mji wa Nzega. Mwaka 2014, Waziri wa Ujenzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa aliwaahidi tena mbele ya Rais Kikwete ahadi hiyo hiyo. Mwaka 2015 Rais wa sasa, Rais John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Nzega ujenzi wa Daraja la Nhobola na kilometa kumi za lami ndani ya Mji wa Nzega. Waziri wa TAMISEMI ndani ya Bunge hili mwaka 2016 akijibu swali langu la msingi alisema Serikali inashughulikia ujenzi wa Daraja la Nhobola katika bajeti ya 2016/2017 na Naibu Waziri Ngonyani katika Bunge lililopita aliahidi daraja hili litajengwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Naibu Waziri anijibu ni lini ahadi ya daraja hili itatimizwa katika Halmashauri ya Mji wa Nzega? Ahsante.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninauliza swali moja la nyongeza.
Kutokana na ripoti ya BOT latest ya mwezi Juni, inaonesha kwamba export volume yetu imeshuka kutoka dola milioni 4.5 mpaka dola milioni 3.8 wakati huo huo prices za commodities kwenye soko la dunia imeendelea kushuka na import volume yetu ya capital goods imeendelea kushuka.
Je, Serikali ina mpango gani kutokana na variables hizi zote nilizozitaja kuhakikisha kwamba, miezi mitatu mpaka sita ijayo stability ya shilingi yetu inaendelea kuwa imara kwa sababu indications zote zinaonesha kwamba, shilingi yetu inaendelea kushuka kila siku kutokana na hali ya uchumi na uzalishaji?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri au niombe tamko la Serikali, kwenye bajeti mwaka huu tulitaka Halmashauri zote ambazo ni class three ambazo zina madeni Serikali Kuu kupitia funds zinazokusanywa na EWURA zipelekwe Wizara ya Maji ili madeni hayo walipwe. Leo ni wiki ya pili Halmashauri ya Mji wa Nzega imezimiwa umeme na TANESCO kwa sababu ya madeni yaliyotokana na Serikali Kuu kutokupeleka fedha za utilities kwenye Halmashauri kwa miaka mingi.
Je Serikali iko tayari leo kuitaka TANESCO iweze kuruhusu watu wa Nzega waweze kupata maji?
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mwaka 2010 na mwaka 2015 kwa maana ya uchaguzi wa mwisho wa kumchagua Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wananchi wa Jimbo la Nzega waliahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete, vilevile ahadi hiyo imekuja kutolewa na Mheshimiwa Rais Magufuli, ya ujenzi wa daraja la Nhobola. Mwaka wa jana Desemba Mheshimiwa Rais aliwahakikishia wananchi wa Jimbo la Nzega kuwa daraja hilo linajengwa kwa commitment iliyotolewa na Wiziri wa Ujenzi. Je, ni lini daraja hilo litajengwa. Nashukuru.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo. Tatizo la maji katika Halmashauri ya Mji wa Nzega ni kutokana na uchakavu wa miundombinu iliyokuwepo toka miaka ya 70 na mwaka jana Desemba tulipata ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kutatua tatizo hili. Tukapokea millioni 200. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wananchi wa Mji wa Nzega juu ya utekelezaji wa milioni 200 ambayo tumekuwa tukiisubiri toka mwezi wa Nne mwaka huu? Nashukuru.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's