Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. George Malima Lubeleje

Supplementary Questions
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza.
Kwa kuwa barabara ya barabara ya Mbande - Kongwa – Mpwapwa mpaka Kibakwe ni muhimu sana kwa maendeleo na uchumi wa Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa; na kwa kuwa barabara hii inaunganisha Majimbo matatu; Jimbo la Kongwa, Mpwapwa pamoja na Kibakwe; na kwa kuwa ni ahadi ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete na ahadi ya Mheshimiwa Rais John Magufuli ambaye ni Rais wetu sasa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya kukamilisha barabara hii kwa kujengwa kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa barabara ya kutoka Mpwapwa – Gulwe kwenda Berege – Mima mpaka Iwondo haipitiki, ni mbaya sana kwa sababu ya mvua zinazonyesha. Je, Mheshimiwa Waziri ana maelezo gani kuhusu wananchi wa Jimbo la Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa barabara hii ya kwenda Kondoa – Babati inafanana kabisa na ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Mstaafu na Rais huyu wa sasa, Mheshimiwa Magufuli, kwamba barabara ya kutoka Mbande – Kongwa – Mpwapwa mpaka Kibakwe itajengwa kwa kiwango cha lami; na ahadi hii ni ya miaka nane: sasa namwuliza Mheshimiwa Waziri, je, katika bajeti ya mwaka huu barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, nimeleta maombi yangu Wizarani kwa sababu Halmashauri ya Wilaya haina uwezo wa kukarabati barabara hii ya Gulwe - Berege - Chitemo - Mima - Sazima - Igoji Kaskazini - Fufu na Iwondo, sasa hivi haipitiki wananchi wanapata taabu hasa abiria kufika Makao Makuu ya Wilaya na ndiyo maana nimeleta. Tayari tulikuwa na kikao cha Bodi ya Barabara tarehe 29 mwezi wa Februari nilipeleka ombi hili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri muifikirie barabara hii kuipandisha hadhi ili TANROADS waweze kuitengeneza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kutoka Mbande - Kongwa kwa Mheshimiwa Spika, Mpwapwa na Kibakwe kwa Mheshimiwa Simbachawene Waziri wa TAMISEMI, hii barabara imeahidiwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami na ahadi hiyo ni ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Kikwete mwaka juzi na mwaka jana wakati wa kampeni za CCM Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wetu aliahidi kuitengeneza barabara hii ya Mbande - Kongwa - Mpwapwa mpaka Kibakwe kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri huoni kwamba kuna umuhimu wa kutengeneza barabara hii ambayo ni kiungo kikubwa cha Majimbo matatu Kongwa, Mpwapwa na Kibakwe?(
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nina swali dogo la nyongeza;
Kwa kuwa, wananchi wa Kijiji cha Majami, Kibolianana, Mlembule na Mgoma tayari wameshaonesha juhudi ya kujenga majengo ya zahanati, kilichobaki ni Serikali kusadia. Lakini Igodi Kusini, Isalanza jengo lipo tayari limekamilika pamoja na Igodi Kaskazini.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utakuwa tayari kuwapelekea watu wa Igoji Kaskazini na Kusini huduma ya madawa na kusaidia hawa ambao tayari wameonesha nguvu za kujenga zahanati?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ya Maji.
Kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa sana karibu nchi nzima na Majimbo matatu haya ya Kibakwe, Mpwapwa na Kongwa ni tatizo kubwa. Kuna visima ambavyo vilianzishwa kuchimbwa vya Benki ya Dunia mpaka sasa havijakamilika. Mpaka sasa hivi Mjini Kongwa, dumu moja la maji wananchi wananunua shilingi 1,000;
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kutembelea maeneo hayo kuhakikisha kwamba miradi hii ya Benki ya Dunia ambayo haijakamika sasa ikamilishwe?
Kwanza ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ni kweli mitambo imekarabatiwa, lakini bado huduma ya maji haiwafikii wananchi wa vijiji vya Ving‟awe namba 30, Mbuyuni, Ving‟awe Juu, Ilolo, Kwa Mshangu, Mahang‟u na Ising‟u; kwa hiyo nilikuwa nakupa taarifa tu kwamba maji hayafiki kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwamba kuna vijiji ambavyo hakuna uwezekano mwingine wa kupata chanzo cha maji ni kuchimba visima. Sasa naiomba Serikali, kwa vijiji nitakavyovitaja iwachimbie visima ili waweze kupata huduma ya maji. Kwanza Ngalamilo, Mgoma, Mzogole, Kisisi, Godegode, Mkanana, Chamanda, Lupeta, Makutupa, Nana, Simai, Isalaza, Nzonvu pamoja na Iwondo. Naomba sana wananchi hawa wana shida kubwa sana ya maji Serikali iwasaidie. Je, Waziri unasemaje kuhusu hilo.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize
maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza
napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya
Mpwapwa.
Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la
Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao
wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko
haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Chilonwa na Jimbo la Mpwapwa yanapakana, na kwa kuwa matatizo ya barabara ya Jimbo la Chilonwa ni sawa kabisa na matatizo ya Jimbo la Mpwapwa, Kibakwe na Kongwa.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utatusaidiaje wananchi wa Jimbo la Mpwapwa kuhusu barabara ya kutoka Lupeta - Bumila - Makutupa kwenda Mbori - Mang‟weta - Mlali mpaka Pandambili. Barabara hii iko chini ya TANROADS, lakini ni muda mrefu sasa haijatengenezwa, pamoja na barabara ya Mkanana – Majami pamoja na Nana. Nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri Serikali itoe tamko kuhusu barabara hii, ni lini itaanza kuzikarabati?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
25
Kwa kuwa Serikali ilikuwa imeniahidi kupandisha barabara ya Gulwe, Berege, Chitemo, Mima, Chazima, Igoji mpaka Seluka Ufufu. Barabara hii ni mbaya, Halmashauri haina uwezo. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini sasa mtapandisha hadhi barabara hii pamoja na kuweka lami barabara ya Mbande - Kongwa - Mpwapwa na Kibakwe?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali ya nyongeza. Kwa kuwa katika kipindi hiki cha mvua barabara nyingi sana zimeharibika, mfano, Wilaya ya Mpwapwa; Kata za Matomondo, Lembule, Mlima, Bereje, Mkanana, Londo, Chamanda, Majami mpaka Nana kule. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutenga fungu la kutosha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo kwa sababu zinapitika kwa shida?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, na mimi niulize swali moja dogo tu. Kwa kuwa vijiji vya Chipogolo, Mima, Pwaga, Kibakwe, Berege, Mbori na Chunyu vina idadi ya watu wengi sana, ni trading centers ambazo ni kubwa sana na kuna wafanyabiashara wengi.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, atakubaliana nami kwamba sasa ipo haja kwenda kufanya utafiti kuona kwamba vinaweza kupewa hadhi ya kuwa Miji Midogo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mpango wa REA umesaidia sana kusambaza umeme katika vijiji vyetu, je, SIDO haiwezi kuwasaidia vijana wetu vijijini kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kukamua karanga, ufuta ili tuweze kupata mafuta kwa ajili ya kuwauzia wananchi wetu likiwemo Jimbo la Mpwapwa
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi; na kwa kuwa Manispaa ya Dodoma imekamilisha vigezo vyote vya kupata hadhi ya kuwa Jiji; na kwa kuwa majengo ya Manispaa ya Dodoma yamejengwa kitaalam, yamefuata master plan, hakuna squatters. Ni lini Serikali sasa itatangaza Mji wa Dodoma kuwa Halmashauri ya Jiji? (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa Naibu Waziri umeshatembelea Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Mpwapwa kuna vijiji ambavyo vina matatizo makubwa sana ya maji; kwa mfano Kijiji cha Tibwetangula, Lupeta, Bumila, Makutupa, Nana, Chimai, Salaza, Iyoma, Ngalamilo, Chamanga na Majami.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utatembelea maeneo hayo, ili uone shida ya maji wanayopata wananchi wa Jimbo la Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, matatizo ya Jimbo la Tarime Vijijini yanafanana na matatizo ya Jimbo la Mpwapwa. Kwa kuwa barabara ya kutoka Mbande - Kongwa - Mpwawa - Kibakwe tayari ilishafanyiwa upembuzi yanikifu na detailed design na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya 2015 mpaka 2020 na ni ahadi ya Rais mstaafu pamoja na Rais wa sasa. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini sasa mtaanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali pili, unakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali langu nilitoa ombi kwamba barabara ya kutoka Gulwe, kwenda Berege, Chitemo, Mima, Chazima, Igoji mpaka Ihondo na Fufu kwamba barabara hii iko chini ya Halmashauri ya Wilaya, lakini Halmashauri ya Wilaya haina uwezo wa kutengeneza kwa sababu haina fedha na imeharibika sana, mvua zimeharibu sana. Je, Mheshimiwa Waziri anawaambia nini wananchi wa kata hizo kwa sababu barabara hiyo inapitika kwa shida sana? Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na kutenga shilingi milioni 15 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Mima na shilingi milioni 35 kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Mbori, je, Mheshimiwa Waziri haoni fedha hizi zilizotengwa ni kidogo kiasi kwamba vituo hivi vitachukua zaidi ya miaka mitano kukamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna majengo ya zahanati ya Kijiji cha Igoji Kaskazini na Igoji Kusini Salaze yamekamilika na kinachohitajika sasa ni huduma za dawa.
Je, yuko tayari sasa majengo haya yakaanza kutumika kwa ajili ya huduma za dawa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, vilevile katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna matatizo makubwa sana ya maji katika Vijiji vya Mima, Chitemo, Berega, Nzase, Lupeta, Bumila na Makutupa na kulikuwa na mradi mkubwa sana wa maji na mpaka sasa umechakaa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuusaidia ule mradi uanze kuhudumia wananchi wa vijiji hivyo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa niliwahi kumlalamikia Mheshimiwa Naibu Waziri wakati tunakwenda Mpwapwa kwamba kuna vituo viwili vya afya ambavyo havijakamilika sasa ni miaka 10, Kituo cha Afya cha Mima na Kituo cha Afya cha Mbori na bajeti haijatengwa zaidi ya miaka 10. Je, unawaeleza nini wananchi wa maeneo hayo ya Mima na Mbori na kwamba vituo hivyo vitakamilika lini?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni muda mrefu Wabunge tumekuwa tukiishauri Serikali kuwalipa wazee kiinua mgongo. Mimi tangu nimeanza Ubunge zaidi ya miaka 20 nadai hivyo na leo Serikali inasema wapo katika mipango, sasa mipango hii ni lini itaisha? Sisi tunaomba kama inawezekana katika bajeti hii wazee waanze kulipwa kiinua mgongo
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapa na Kongwa kuna mabonde mazuri sana ya maji na yanatiririsha maji mwaka mzima. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga scheme ya umwagiliaji katika vijiji vya Godegode, Nzovu, Bori, Msagali, Tambi, Mang’weta, Chamkoroma, Mseta na maeneo mengine ili scheme hii iweze kusaidia kilimo cha umwagiliaji na kusaidia kuondoa tatizo la njaa, katika maeneo hayo?(Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa maeneo ambayo ameyataja, kwa mfano Iyoma, Mzase na Bumila kwamba kazi inaendelea. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kufuatana na mimi kuona kama kazi hiyo imeanza? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Mpwapwa ni mji wa zamani sana, una zaidi ya miaka 100 sasa tangu mwaka 1905 lakini vyanzo vya maji ni vilevile, kuna maji baridi na kuna maji ya chumvi, na kuna maeneo ambayo wanaweza wakachimba visima vya maji tukapata maji baridi ili wananchi wa Mpwapwa waweze kupata maji baridi. Je, Serikali iko tayari kutuma watafiti waende waanze kufanya utafiti ili kuongezea visima vya maji kwa Mji wa Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa REA inafanya kazi nzuri sana na imesambaza umeme karibu nchi nzima na Mpwapwa kuna vijiji ambavyo havijapata umeme, kijiji cha Kibojani, Mgoma, Mzogole, Viberewele, Sazima, Mkanana, Igoji Kaskazini na Igoji Kusini pamoja na Iwondo.
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kupeleka umeme katika vijiji hivi kwa sababu umeme ndio uchumi wetu na ndio maendeleo yetu katika nchi yetu?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali, naomba niwape pole wananchi wa Kitongoji cha Chinyika na Kwamshango kwa maafa waliyopata ambapo watu watano wamefariki kwa kusombwa na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize swali. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa na anajua vijana wengi sana katika Wilaya ya Mpwapwa hawana ajira na hizo fedha zinazotolewa ni kidogo sana. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongeza fungu la fedha hizo ili vijana wengi waweze kupata ajira pamoja na wa Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru
sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali hayo. Sasa nina maswali
mawili.
Kwa kuwa, MSD imetengewa fedha shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kununua
madawa, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa sana wa madawa katika hospitali
zetu wagonjwa wakienda hospitalini wanaandikiwa vyeti na Madaktari
wanawaambiwa mkanunue dawa maduka binafsi. Je, kwa nini hizo fedha bilioni
251 zisipelekwe moja kwa moja MSD badala ya kukaa Hazina na wanapelekewa
kidogo kidogo?
Swali la pili, kwa kuwa, katika Jimbo langu la Mpwapwa kuna Vituo vya
Afya, vya Mima, Mbori, Berege, Mkanana pamoja na Zahanati za Chamanda,
Igoji Kusini, Kibojane Lupeta, Makutupa, Majami, Nana, Mgoma havijakamilika
hadi sasa na ujenzi huu sasa umechukua zaidi ya miaka kumi. Je, Serikali ina
maelezo gani kwa wanachi wa vijiji hivyo, kwa sababu wananchi wa vijiji hivyo
hufuata tiba zaidi ya kilomita 15?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ina upungufu mkubwa sana wa chakula pamoja na Wilaya za Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida; na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna Halmashauri za Wilaya 55 ambazo zina upungufu mkubwa sana wa chakula na Serikali ina chakula cha kutosha kwenye maghala. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu kwasababu hivi sasa debe la mahindi ni shilingi 20,000 na mfuko wa sembe ni shilingi 40,000 ni lini Serikali itaanza kusambaza chakula cha bei nafuu Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa pamoja na hizi Halmashauri 55?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kila Halmashauri ya Wilaya ina Mratibu wa TASAF na waratibu ndiyo wameandikisha kaya
maskini, walijua kabisa kwamba kaya hii ni maskini. Hivi
karibuni kuna kaya ambazo zimeondolewa kwamba hazina sifa na wanaambiwa warejeshe fedha, wengine ni wazee kabisa. Mheshimiwa Waziri nani mwenye makosa, ni mratibu aliyeorodhesha au ni yule ambaye ameambiwa kwamba alipe hizo fedha?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuchimba visima vya maji katika kijiji cha Bumila, Iyoma na Mima. Hata hivyo, sasa ni miezi nane tangu visima vimechimbwa, hakuna pampu zilizowekwa, hakuna mabomba ya kusambaza maji wala matenki. Je, Serikali inasemaje kwa wananchi wa vijiji hivi ambao wana shida kubwa sana ya maji?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Meneja wa TANROADS wa Mkoa ameshaikagua barabara ya kutoka Gulwe – Berege –Chitemo – Mima – Chazima - Igodi Moja – Igodi Mbili mpaka Seluka; na kinachosubiri sasa hivi ni barabara hii ipandishwe hadhi ili iwe barabara ya Mkoa.
Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje na kwa ombi hilo Serikali inawaambiaje wananchi wa maeneo hayo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kuna miradi imeshaanza kutekelezwa, kwa mfano, Wilaya ya Mpwapwa tulikuwa na matarajio ya kujenga barabara za lami, Mpwapwa Mjini kilometa 10; na kwa kuwa fedha iliyoletwa ni kidogo sana na ni karibu Majimbo yote kuna viporo; je, fedha iliyobaki Serikali italeta fedha zote kwa Wilaya zote? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya Mima na Mbori ni kidogo sana na ndiyo maana havijakamilika sasa zaidi ya miaka kumi; je, Serikali itaongeza fedha ili tukamilishe vituo hivyo?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijiji vya Makutupa, Mlembule, Tambi, Bolisazima na Mgoma tayari nyaya na nguzo zimeshawekwa bado transfoma. Sasa namuuliza Naibu Waziri, vijiji hivi vitapata lini transfoma ili waweze kuanza kupata huduma ya umeme?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wazabuni wanaohudumia chakula Mpwapwa High School, Mazai Girls’ School pamoja na Berege Secondary School form five na six sasa ni zaidi ya miaka miwili hawajalipwa na bado wanahudumia na wamekopa benki. Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Mpwapwa sekondari na ameona hali ilivyo na wanataka kukamatiwa nyumba, je, hawa wazabuni watalipwa lini?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa magari ya kunyonya maji machafu na kuzoa taka siyo lazima tu iwe kwenye Manispaa au Majiji, hata Wilaya zetu tunahitaji magari ya kunyonya maji machafu na magari ya kuzoa taka. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka gari la kunyonya maji machafu pamoja na kuzoa taka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza napenda niipongeze sana Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kuanza kujenga barabara ya lami kuanzia Mbande kwenda Kongwa - Mpwapwa mpaka Kibakwe. Sasa swali langu ni hivi, je, hii barabara ikishafika Njia Panda ya Kongwa inaendelea moja kwa moja mpaka Mpwapwa? Hilo ndiyo swali langu. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, nilishamwomba Mheshimiwa Waziri kwamba, wataalam wa utafiti wa visima vya maji, visima ambavyo vitatoa maji baridi wafike na kufanya utafiti wa visima hivyo. Kwa sasa wananchi wa Mji wa Mpwapwa wanatumia maji ya chumvi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu ombi langu hilo la kutafiti visima vingine vya maji baridi, ni lini atalitekeleza?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza utaratibu wote umeshafuatwa, vijijji vimekaa, Kamati ya Maendeleo ya Kata imekaa, Full Council imekaa na mpaka kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa na ni ombi la muda mrefu sana. Wananchi wa Mkanana wanapata shida, kwanza hakuna mawasiliano ya barabara kabisa na ninakuomba tukimaliza Bunge tuende kule upite ile njia uone kama inapitika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, kwa kuwa kwenye swali langu limetaja kuna umbali kutoka Mkanana, Chibwegele mpaka Chitemo ni kilometa 45 ndipo wananchi wanafuata usafiri. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, utakuwa tayari kukubali ombi langu tufuatane na wewe sasa baada ya Bunge hili, ukawaone watu wa Mkanana, Chibwegele, wanavyopata shida?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri, niipongeze sana TASAF kwa kazi nzuri, sasa nina maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba kazi hii kweli imeanza Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado haijakamilika katika vijiji ulivyotaja. Ni lini kazi hii itakamilika ili maeneo haya yaweze kupata huduma ya maji kwa sababu kuna shida kubwa sana ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vijiji katika mpango wa kuchimbiwa mabwawa, katika vijiji vya Kisisi, Ngalamilo, Iwondo pamoja na Nana kwa sababu hawa nao wana matatizo makubwa sana ya maji. Ni lini wataanza shughuli hizi? (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mwaka 2015 wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais alituahidi kilomita10 Mpwapwa Mjini na kwa kuwa bajeti iliyopita tumepewa kilomita moja tu, hata Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo analifahau hilo. Je, Mheshimiwa Waziri ataahidi wananchi wa Mji wa Mpwapwa kwamba hizo kilomita 10 zitakamilika?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lengo la Serikali kuchukua vyanzo vingi vya Halmashauri za Wilaya ilikuwa ni kusaidia ruzuku ya kutosha kwenye Halmashauri hizi. Lakini kwa kuwa ruzuku inayotolewa haitoshelezi kabisa kwa Halmashauri hizi kujiendesha.
Sasa swali langu, naishauri Serikali kwamba je, Serikali inaweza kurudisha baadhi ya vyanzo vya mapato kwa Halmashauri ili nazo ziweze kujiendesha badala ya kusubiri ruzuku na ruzuku yenyewe inachelewa sana?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, nina maswali mawili.
Swali la kwanza, kwa kuwa MKURABITA katika Wilaya ya Mpwapwa walichagua vijiji viwili; Kijiji cha Inzomvu na Kijiji cha Pwaga, lakini kwa upande wa Kijiji cha Pwaga mambo ni mazuri, mradi ulitekelezwa, masijala ilijengwa na wananchi walipewa Hati za Kimila. Lakini katika Kijiji cha Inzomvu hakuna kilichofanyika, baada ya kupima mashamba wananchi walipewa mafaili tu wakaenda nayo majumbani, hakuna chochote na ofisi ya masijala haipo.
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kwamba ipo haja sasa ya Serikali kuleta muswada hapa ili tubadilishe chombo hiki MKURABITA ambao unategemea zaidi fedha za mfadhili na fedha za Serikali ni kidogo sana ili tubadilishe uwe mfuko wa urasimishaji ili wadau wengi waweze kuchangia na chombo hiki kiwe na fedha za kutosha ili wananchi wengi waweze kunufaika?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Swali langu ni kwamba, kwa kuwa kuna waajiri ambao wanakata mshahara lakini hawapeleki fedha hizi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Je, Serikali inawachukulia hatua gani?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa mgao wa Road Fund Serikali Kuu wanachukua asilimia 70 na Serikali za Mitaa asilimia 30 na kwa kuwa Serikali imeunda chombo cha TARURA na kama mgao utakuwa asilimia 30 zile zile na barabara zetu ni mbaya sana vijijini kule hasa Wilaya ya Mpwapwa.
Je, sasa mgao utaongezeka iwe asilimia 50 kwa 50?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika mipango yote ya kujenga shule za sekondari, shule za msingi, zahanati, vituo vya afya tunasahau sana huduma za maji, umeme pamoja na afya. Sasa nataka niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri na bahati nzuri sana Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI Mpwapwa anaifahamu vizuri sana. Katika bajeti ya mwaka 2018/2019; je, Serikali itakuwa tayari kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo vya afya, zahanati, shule za msingi, sekondari zote Jimbo la Mpwapwa zinapata huduma ya maji, umeme na afya?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Kadutu la Ulyankulu linafanana kabisa na Tarafa ya Mima ambayo imeshatangazwa kwamba imeanzishwa kuwa Tarafa ya Mima, lakini mpaka sasa hakuna majengo, hakuna watumishi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini mtajenga majengo, mtaleta watumishi ili kweli ile Tarafa ya Mima ianze kufanya kazi mara moja maana sasa inatamkwa tu Tarafa ya Mima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kata za Matomondo pamoja na Mlembule ni kata kubwa sana na zina vigezo vyote kuwa tarafa, je, Mheshimiwa Naibu Waziri, unasemaje kuhusu hili? Ni lini mtaanzisha Tarafa hizi Kata mbili, Mlembule na Matomonda?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 1998/1999, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Katiba ya Sheria na Utawala, Serikali iliamua TRA ijaribu kukusanya kodi ya majengo na walianzia na Halmashauri za Manispaa tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni. Baadaye walishindwa, Serikali ikarudisha tena kodi hizo zikusanywe na Manispaa hizo. Sasa ni sababu gani za msingi tena Serikali imeamua kodi ya majengo ikusanywe na TRA na siyo Halmashauri zenyewe? (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nina swali moja tu; kwa kuwa Serikali imerejesha Kambi ya JKT Mpwapwa na kwa kuwa vijana wengi wa Wilaya ya Mpwapwa wanataka kujiunga na JKT Mpwapwa, je, ni taratibu gani watumie ili waweze kujiunga na ile kambi?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa magari ya kunyonya maji machafu na kuzoa taka siyo lazima tu iwe kwenye Manispaa au Majiji, hata Wilaya zetu tunahitaji magari ya kunyonya maji machafu na magari ya kuzoa taka. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka gari la kunyonya maji machafu pamoja na kuzoa taka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja dogo. Bahati nzuri mimi nimekuwa Diwani kwa miaka kumi na tano na Mwenyekiti wa Halmashauri. Kazi ya Udiwani zamani ilikuwa mikutano tu, unakuja kuitwa kwenye kikao unarudi nyumbani; lakini kwa kuwa sasa hivi Udiwani ni kusimamia miradi, ikianza kujengwa darasa mpaka jioni uko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba mtekeleze yale maagizo au maelekezo ya Tume ya Lubeleje ya kushughulikia maslahi ya Madiwani, muwalipe Madiwani posho ya kutosha ili nao waweze kumudu maisha kwa sababu wanashinda kwenye miradi mpaka jioni?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali hili linafanana kabisa na vituo vya afya vya Mima na Mbori ambavyo havijakamilika sasa ni zaidi ya miaka 10 lakini naishukuru Serikali kwamba mmetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo. Sasa Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kutembelea kuona ujenzi wa kituo cha afya - Mima na kituo cha afya cha Mbori?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kuna mpango wa kujenga kituo cha afya Chunyu na eneo la Chunyu lina idadi ya watu wengi, je, mpango huu umefikia wapi? Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Katika Wilaya ya Mpwapwa, Vijiji vya Bumila, Mima na Iyoma vilichimbwa visima vya maji na maji yalipatikana, sasa ni miezi nane hakuna cha bomba, hakuna cha pampu. Sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri vile visima vilichimbwa kwa ajili ya mapambo kuonyesha wananchi tu au ni lini wataweka pampu na mabomba wananchi wanapata tabu?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's