Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Supplementary Questions
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Bukene linafanana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Kata ya Kizara. Mwaka 2012 tulimchukua Naibu Waziri hapa alikwenda mpaka kule akawaahidi wananchi wa Kizara kwamba mwishoni mwa mwaka 2012 mnara utapatikana. Cha kushangaza mpaka leo hii hakuna cha mnara wala namna ya kupata mnara. Je, ni lini sasa Serikali itawapelekea wananchi wa Kizara mnara?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye maana. Mwaka jana mwezi wa Sita niliomba Serikali iende mpaka Korogwe ikaangalie maeneo ambayo hayaendelezwi na Serikali iliniahidi kwamba ingekwenda kule na kukagua mashamba ambayo hayaendelezwi ili ufanywe utafiti wa kuwagawia wananchi, hadi leo hii na mimi nilienda kwenye mikutano ya hadhara na kuwaambia wananchi kwamba Naibu Waziri atakuja kuangalia mashamba ambayo hayaendelezwi na watu wakakipa sana kura Chama cha Mapinduzi kwa kujua kwamba viongozi wanafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hawajafika na badala yake nasikitika sana baadhi ya Watumishi wa Halmashauri wanaleta habari ambazo siyo njema, zisizoweza kumsaidia mtu wa aina yeyote. Naomba Waziri, ni lini mimi na wewe tutakwenda mpaka Korogwe Vijijini ukaone huku kudanganywa kwamba ni shamba moja katika mashamba 17 yanayozunguka Jimbo langu hayajapatiwa ufumbuzi.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Karatu linalingana kabisa na tatizo la Korogwe Vijijini hasa kwenye barabara inayotokea Korogwe - Kwashemshi - Bumbuli - Soni imekatika na barabara hii iliamuliwa na Serikali kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na sasa hivi mawasiliano hakuna. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuitengeneza barabara hii haraka haraka ikarudisha mawasiliano ya dharura ambayo yalikuwa yameshakatika kwa muda mrefu?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti,ahsante, kwa kuwa tatizo la Tunduru huko linalingana kabisa na Korogwe Mjini. Ni lini Serikali itaifanya Hospitali ya Magunga iwe Hospitali Teule?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza nikupongeze kwa kuzaliwa juzi Muhimbili na Mama Ulega, Mungu akubariki sana.
Swali langu ni kwamba, kwa kuwa baraza la ardhi la Wilaya ya Korogwe linafanya kazi katika mazingira magumu. Kuna kesi nyingi za kutoka mwaka 2009 mpaka leo hazijamalizika.
Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi pale ili kesi zile ambazo zimekaa kwa muda mrefu katika Baraza la Ardhi la Korogwe ziwe zimepata ufumbuzi wa haraka ili wananchi waone umuhimu wa Serikali yao?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini kulitokea kampuni ambayo sio mali ya Serikali, UNDP, ilinipa milioni 243 nikachimba visima tisa. Baada ya kuchimba visima hivyo walikuja wataalamu wa Serikali wakasema sehemu hizi tukichimba tutapata maji safi, lakini cha kusikitisha baada ya kuchimbwa maji yale yalivyokwenda Serikalini kuleta majibu nikaambiwa maji yale hayafai kutumika kwa binadamu na hela tayari zimeshatumika shilingi milioni 243.
Je, hii hasara ambayo wameipata wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini italipwa na nani?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshuruku Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini kwa wananchi wa Mombo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu sasa hivi una muda mrefu na tatizo la maji la Mombo ni la muda mrefu na wananchi wameanza kukata tamaa; na kwa kuwa halmashauri mbili zilishakubaliana, ya Bumbuli na Korogwe kwamba maji yale yapitie katika vile vijiji vinavyolinda chanzo cha maji, ni wakati gani wananchi wale wa Korogwe Vijijini na Bumbuli wataanza kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi Serikali imetutengea shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mradi wa maji wa Korogwe Vijijini; kuna mradi wa maji wa Bungu, mradi huu hatukuwa tunatumia hela za Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yalitumia hela zao kukamilisha mradi huu ambao ulikuwa ni kwa ajili ya vijiji saba. Kati ya vijiji hivyo saba vijiji vinne tu ndivyo vimepata maji. Serikali iliombwa shilingi milioni 410 ili mradi huu ukamilike lakini mpaka sasa hivi hela hiyo haijapatikana. Vijiji ambavyo vimekosa ni Mlungui, Kwemshai na Ngulwi. Naomba sasa Serikali mtenge hela za dharura ili tukakamilishe mradi huo ambao haukutumia hela za Serikali, ni mashirika binafsi yaliamua kujenga mradi huo. Ahsante sana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tanzania nzima ili iwe barabara ni lazima kuwepo na madaraja. Katika Wilaya yangu ya Korogwe Vijijini wakati wa mvua barabara za Mkoa zote zimevunjika madaraja na hakuna magari yanayoweza kupita katika barabara ya Mkoa kutoka Korogwe kwenda Mnyuzi kwa kupitia Muheza; na barabara ya kutoka Korogwe kwenda Magoma kwa kupitia Maramba hadi Daruni.
Je, Serikali hamna mpango wa dharura kutusaidia madaraja haya ambayo wananchi wamepata taabu kwa muda mrefu?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga barabara ya lami kilometa 1.5 katika Mji wa Mombo na Rais wa Awamu ya Tano ameahidi vilevile kujenga barabara hiyo kilometa moja, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hela hazijaingia katika Mfuko wa Mkoa. Je, ile barabara ambayo imeahidiwa na Marais wawili itajengwa lini kwa kiwango cha lami kule Mombo?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kuishukuru Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kuupendelea Mkoa wa Tanga, Wizara ya Ardhi ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuangalia mashamba ambayo hayaendelezwi lakini fedha ziko mikononi mwa mtu na Korogwe hawajafika na hawajafanya utafiti wowote na badala yake wanakwenda pale kwa ajili ya kumdanganya danganya tu Waziri wa Ardhi. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari twende wote mpaka Korogwe tukaangalie yale maeneo ambayo hawajapewa wananchi na yameachwa kama misitu ili atusaidie kutatua tatizo la wananchi wa Korogwe?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, nina maswali mawili ya nyongeza:-
Kwa kuwa wananchi wa Mwanza na Ukelewe wamepata usumbufu zaidi ya miaka mitano kwa kukosa usafiri; na kwa kuwa ni sehemu muhimu sana kwa wavuvi; ni lini sasa Serikali itawapa usafiri wa dharura wananchi wale ili waone umuhimu wa Serikali yao inavyowasaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tatizo la Ukerewe linalingana kabisa na Tanga, wananchi wa Tanga, Pemba, Unguja pamoja na Bagamoyo wanahitaji meli kama hiyo ili iwasaidie; je, Serikali ina mpango gani wa kuwahakikishia wananchi wa Ziwa, umetaja Ziwa Nyasa, umetaja Ziwa Victoria, umetaja Ziwa Tanganyika; lakini je, katika Bahari ya Hindi wananchi wa Tanga, Pemba, Unguja na Bagamoyo ni lini na wao watapata meli ili na wao waepukane na kile kimbunga cha kila siku kufariki kwenye meli? Ahsante sana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Tatizo la Maswa Mashariki linalingana kabisa na tatizo la Mji wa Mombo, katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini. Rais wa Awamu ya Nne aliaahidi kwamba atajenga kiwango cha lami barabara kilometa 1.5 na Rais wa Awamu ya Tano alivyokuja vilevile alitoa ahadi hiyo kwamba atatekeleza ahadi ya ambayo imeachwa na Rais Mstaafu. Lakini mpaka leo hii hakujafanyika kitu cha aina yoyote, je, Serikali inasemaje kuhusiana na Mji wa Mombo ambao wananchi wake wanategemea sana mpaka sasa hivi kungekuwa na barabara ya lami lakini hakuna kinachoendelea
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa maneno mazuri ndani ya Bunge hili ila nilikuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa suala la utalii ni suala muhimu sana kwa Watanzania na kwa kuwa Zanzibar na Pemba na Tanga watalii wengi walikuwa wanakwenda kwa ajili ya kuogelea ndani ya bahari. Pia kwa kuwa tatizo hili limewaathiri kwa kiwango kikubwa sana watalii wanaotoka nje kwa ajili ya kuja kufanya utalii katika eneo la pembezoni mwa bahari. Je, Serikali inaweka hatua gani ya dharura kwa kuhakikisha suala hili linachukuliwa maamuzi ya haraka ili watalii waendelee kuwepo katika eneo la bahari?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudi zake kubwa mnazofanya za kusambaza mawasiliano nchi nzima.
Kwa kuwa tatizo la mawasiliano katika Jimbo la Korogwe Vijijini ilikuwa ni Kata nyingi hazina mawasiliano; na kwa kuwa Serikali hii ni sikivu; kuna Kata ambazo hazina mawasiliano kabisa, kwa mfano, Kata ya Dindira katika Kijiji cha Kwefingo, Kata ya Chekelee katika Kijiji cha Bagai, Kata ya Mkalamo katika Vijiji vya Kweisewa na Toronto, Bungani na Kata ya Kerenge katika Kijiji cha Makumba:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini vijiji hivi navyo vitajengewa minara ili nao wanufaike na Serikali hii ya Awamu ya Tano?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Tatizo la Lushoto linalingana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Mji Mdogo wa Mombo. Serikali kwa kupitia Benki ya Dunia ilitenga milioni 900 kwa mradi wa maji ambao unakwenda kutoka Vuga mpaka Mombo kwa kupitia Mombo kwenda Mlembule. Mradi huu umekamilika kwa asilimia 80, tatizo ni kwamba, wananchi wanaolinda chanzo cha maji katika Wilaya ya Bumbuli au katika Mji wa Bumbuli ambao wanatoka Vuga walikuwa wanaomba wapatiwe maji na sasa hivi Serikali iliahidi kwamba, wale wananchi wanaolinda chanzo cha maji watapatiwa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini mradi huu wa Mombo ambao Serikali imetumia gharama zaidi ya milioni 900, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini, pia nimpongeze kwa safari alizofanya katika Jimbo langu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Naibu Waziri umefika na kuliona shamba hili ambalo limetelekezwa zaidi ya miaka 22, ni kwa nini sasa Serikali isiwakabidhi wananchi wakalitumia kwa shughuli zao mbadala? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa mashamba mengi yamechukuliwa mikopo kwenye mabenki na sasa hivi yametelekezwa, nini kauli ya Serikali kwa yale mashamba ambayo yalichukuliwa mikopo, hayaendelezwi na yametelekezwa mpaka muda huu?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la Busokelo linalingana kabisa na Korogwe Vijijini. Kwanza nianze kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayonifanyia kule Korogwe kwa kujenga daraja la Magoma. Barabara ya kutoka Old Korogwe kwenda Maguzoni ni barabara ya Mkoa, lakini daraja lake lilibomoka toka mwanzo wa mwaka huu.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kujenga daraja hili ili wananchi waliokuwa wapo kwenye kisiwa waitumie barabara yao?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mradi huu unagusa hasa sehemu za tambarare peke yake, ni lini sehemu za milimani kama vile Suji, Mkomazi, Manga Mtindilo, Mikocheni na Bwiko mradi huu nao utatekelezwa huko kwa sababu wakati wa mwanzo tuliambiwa hela zipo na mradi unaanza? Naomba kujua ni lini sehemu zile za milimani na zenyewe zitapata maji?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo. Nilikuwa na swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao la mkonge ni moja ya mazao yanayoiingizia nchi yetu kipato, na kwa kuwa wakulima wa mkonge katika Jimbo la Korogwe Vijijini na hasa Mkoa wa Tanga wamekuwa wanajitahidi sana kulima mkonge ili wajinufaishe wao na familia zao na kuwasomesha watoto wao, je, Serikali itawasaidiaje ili wapate kulipwa haraka fedha walizokuwa wanadai kwenye Mamlaka ya Mkonge au Katani Limited ili ziweze kuwasaidia kuendesha na kustawisha zao la mkonge hapa nchini?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nampongeza ndugu yangu Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na hasa ya kushughulikia matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tatizo la kule Mbulu hasa kule Haydom, inalingana kabisa na Korogwe Vijijini
katika Mji Mdogo wa Hale na wewe mwenyewe umeshafika pale; je, Serikali Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Kijiji cha Hale kuwa Mji mdogo kule Korogwe Vijijini?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Mimi nilikuwa nataka kujua ule Mradi wa Vuga - Mlembule - Mombo ambao yeye ameutembelea kwa muda mrefu sana na kuona matatizo yake na kuwaahidi wananchi wa Mombo kwamba ikifika mwezi wa sita watapata maji. Ni lini Mradi huu utakuwa umekamilika na wananchi wale wafurahie mradi ule mkubwa wa maji ambao unagharimu zaidi ya shilingi 900,000,000?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza kufuatana na Wizara hii kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, REA ya Awamu ya Pili ilikuwa ina sehemu ambayo imepima lakini sehemu hizo mpaka leo hii bado hazijapata umeme. Mfano ni katika kata ya Magoma katika kijiji cha Makangala na Mwanahauya na Pemba na katika kata ya Kerenge katika vitongoji vya Ntakae, Mianzini, Kwaduli, Migombani, Mfunte na Kiangaangazi. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba vijiji hivi na ile vya Kata mpya ya Mpale vinapata umeme kwa haraka?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwanza niipongeze Serikali kwa mpango mzuri wa kunipatia fedha shilingi milioni 18. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ukiacha fedha ambayo napewa na Serikali milioni 18 Serikali iliniahidi kunipatia fedha zaidi ya milioni 60 na ikatoa milioni 20 toka 2012 hadi leo hii milioni 40 hawajanipatia. Ni lini ahadi ya Serikali ya milioni 40 ambazo waliniahidi kunipatia ili nimalizie sehemu ya vijiji ambavyo vimebakia vya Kwemshai na Mnungui itatimia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Shirika Lisilokuwa la Kiserikali liliamua kunipatia fedha na kuchimba visima tisa katika Jimbo langu la Korogwe Vijijini na baadhi ya sehemu Serikali iliamua kuchukua dhamana ya kufunga pampu na kusambaza maji. Katika sehemu hizo Serikali iliamua kwamba katika Kijiji cha Lusanga Mnyuzi, Makuyuni, Kwikwazu pamoja na Kerenge kibaoni kwamba watafunga maji hayo na kuyasambaza. Je, ni lini maji haya yatapelekwa katika vijiji ambavyo Serikali iliamua kwamba watawapelekea maji?
MHE. STEPHEN HILARY NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza kwa ruksa yako naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kunipa shilingi bilioni moja kwa ajili ya vituo viwili vya Afya, Kata ya Mkumbala na Kituo cha Afya Bungu, Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwaka 2012 Mahakama hii iliahidiwa kwamba itajengwa, mwaka 2014 iliahidiwa itajengwa, mwaka 2015 iliahidiwa itajengwa, sasa nataka tamko la Serikali mwaka 2020 ni kweli kituo hiki au Mahakama hii ya Mwanzo itajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ilijenga Mahakama ya Mwanzo ya kisasa zaidi pale Magoma katika Tarafa ya Magoma, na nikajitahidi nikakarabati Mahakama moja katika Tarafa ya Bungu, lakini Mahakama hizi mpaka zaidi ya miaka saba hazijafunguliwa.
Sasa naomba Serikali iniambie ni nini sababu zinazuia Mahakama hizi zisifunguliwe wakati wananchi wanapata shida sana kutolewa umbali wa kilometa 30 kwenda kufuata Mahakama sehemu nyingine? Ahsante sana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Profesa mwenzangu kwa majibu mazuri na yenye msimamo. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mahakimu wengi wa Mahakama za Mwanzo wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanapokwenda kwenye Mahakama za vijijini huwa wanatumia usafiri wa mabasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia usafiri kwa ajili ya usalama wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mahakimu wengi wanakaa katika nyumba za mtaani za kupangisha. Katika nyumba hizo huwa baadhi yao kuna watuhumiwa wanaowajua sehemu walipo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mahakimu hao wanapata nyumba maalum kwa ajili ya usalama wao? Ahsante sana.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Mto wa Mbu lina linalingana kabisa na tatizo la Mji wa Mombo. Mji wa Mombo toka Awamu ya Nne ulihaidiwa na Serikali kwamba utajengwa kiwango cha lami kilometa moja na nusu, na wataalam walienda pale wakapima na wakachukua sample ya udongo, lakini cha kushangaza mpaka leo hii barabara hile ya Mji Mdogo wa Mombo haijafanyiwa utafiti wala haijafanyiwa chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tamko la Serikali kuhusiana na Mji Mdogo wa Mombo?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Waziri wa maji kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri mradi wa maji wa Mombo - Mlembule ulikuwa wa Serikali imetenga shilingi milioni 900 lakini cha kushangaza sasa hivi mradi huo umekuwa wa shilingi bilioni nne. Nini tamko la Serikali kuhusiana na mradi wa shilingi milioni 900 mpaka ukafika shilingi bilioni nne? Hizo shilingi bilioni nne ni kwa ajili ya mradi gani mwingine?
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Kambi Mbadala, kwanza niwapongeze Wizara hii ya Maji kwa kufanya kazi vizuri hasa mdogo wangu kwa kubeba ndoo kichwani. Kule Mnyuzi katika Kijiji cha Lusanga kuna mradi mkubwa wa maji ambao upembuzi yakinifu umeshafanyika na maji hayo yangeweza kufika mpaka Shamba Kapori; je, mradi huu mpaka sasa hivi umefikia wapi?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's