Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Supplementary Questions
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wilaya ya Rufiji ni Wilaya kongwe. Ni miongoni mwa Wilaya za awali, ina miaka zaidi ya 55 toka izaliwe lakini kutokana na mgawanyo wa Wilaya, Wilaya hii imebaki kuwa ni Wilaya pekee ambayo haina Mahakama ya Wilaya. Wananchi wangu wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za Mahakama ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kujenga Mahakama ya Wilaya kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji?
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya mshahara kati ya Hakimu na Jaji ni kubwa sana na kazi wanazofanya Mahakimu takribani ni kubwa kuliko wanazofanya Majaji. Nataka nifahamu Serikali inajipanga vipi kuboresha maslahi ya Mahakimu katika suala zima la mishahara, msaada wa nyumba (house allowance) pamoja na non-practicing allowance kwa Mahakimu nchi nzima?
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza Mheshimiwa Waziri atambue kwamba mimi siyo aina ya Wabunge ambao atawajibu rejareja nikamwachia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atambue kwamba mwaka 1955 Mwalimu Nyerere aliahidi ujenzi wa barabara hii akiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya TANU, Tarafa ya Mkongo. Pia tarehe 9/9/2015, Mama Samia Suluhu aliahidi ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami alipokuwa katika harakati za kampeni pamoja na Rais, Mheshimiwa Magufuli. Vilevile Rais wa Awamu ya Nne na Awamu ya Tatu wote waliahidi ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri ametudanganya hapa kwamba barabara hii inapitika kirahisi, naomba atuambie kwamba ahadi hizi za Marais hawa zilikuwa ni ahadi hewa? Hiyo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, terehe 5 Juni, 2016, Rais Magufuli akiwa Ubungo aliahidi ujenzi wa barabara ya Ubungo kwa kiwango cha lami ambapo suala hili wananchi wa Jimbo la Rufiji waliliona kwamba ni neema kwa kuwa Mheshimiwa Rais atakuja pia kuweka ahadi za namna hiyo katika Jimbo la Rufiji hususani barabara hii ya Nyamwage - Utete ambayo inategemewa na wananchi hususani akina mama. Naomba kufahamu kwamba Wizara hii ipo tayari kukiuka Ibara ya 13 ya mgawanyo sawa wa pato la taifa kwa kuwasaidia na kuhakikisha kwamba inawatendea haki maskini na wanyonge wa Jimbo langu la Rufiji? Ahsante
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru huku nyuma hatuonekani inatubidi tuanze kunywa maji ya kutosha.
Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Rufiji tunabeba asilimia 49.8 la eneo la hifadhi na misitu nikimaanisha square kilometer 6,300 ziko ndani ya hifadhi na misitu, na kati ya hizo square kilomita 13,000 ndiyo eneo kubwa la Jimbo langu la Rufiji. Wananchi wa Jimbo la Rufiji wana masikitiko makubwa katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambapo hatujaingiwa katika mgao wa madawati.

Waziri, umetumia kigezo gani kugawa madawati katika maeneo ambayo wanatunza hifadhi ya misitu yetu naomba kufahamu hilo kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Rufiji?
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza, lakini nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yamenipa faraja kuliko majibu ya juzi yaliyotolewa na Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza, katika kuwasaidia wakulima hao hao, bajeti ya Wizara hii ya Kilimo na Mifugo kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 imetenga maeneo ya kipaumbele na katika maeneo hayo ya kipaumbele Rufiji si maeneo ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. Kama Wizara hii ingeweza kutoa kipaumbele kwa Rufiji inamaanisha kwamba tatizo la sukari hapa nchini lingeweza kwisha kabisa kwa Serikali kuwekeza na kutengeneza viwanda vikubwa vya sukari. Nataka nifahamu hawa wataalam waliomsaidia Mheshimiwa Waziri kuandaa bajeti hii wana elimu gani, darasa la saba au ni form four? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali kupitia Wizara hii ya Kilimo ilituletea sera ya kutuletea RUBADA. RUBADAhii wamekuwa wabadhirifu wakubwa wa fedha za umma ambao pia ni madalali wa viwanja na mashamba, wamesababisha anguko kubwa la uchumi Rufiji kwa kushindwa kusaidia kuleta wawekezaji katika kilimo lakini pia kushindwa kusimamia Bonde la Mto Rufiji? Nataka nisikie kauli ya Mheshimiwa Waziri hapa ni lini ataifuta hii RUBADAna kutuletea mradi mkubwa wa kilimo kwa ajili ya Wanarufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona swali langu ni dogo tu ambalo linafanana na swali la msingi la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utamaduni uliokuwepo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka ya nyuma uliruhusu wananchi wanaoishi kando kando mwa maeneo ya hifadhi waliruhusiwa kuvua samaki kwenye mabwawa hususan wananchi wa Jimbo langu la Rufiji wa maeneo ya Luwingo na utaratibu huu ulienda sambamba na kata zote; kata ya Mwasenimloka, kata ya Ngolongo pamoja Kagira, naomba kufahamu Wizara ya Maliasili na Utalii inaweka utaratibu gani sasa ili kuweza kuwasaidia wananchi wa maeneo haya katika kuchimba mabwawa ya samaki ili wananchi hawa wawekeza kuuza samaki hizo kuwasaidia kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao shuleni? Ahsante.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya maji katika Jimbo langu la Rufiji ni makubwa na hatuwezi kuyafananisha na Morogoro. Eneo dogo la Rufiji ambalo linapata maji safi ni Tarafa ya Ikwiriri, lakini tumeharibikiwa motor pump huu sasa mwezi wa Nane. Tuliwasilisha maombi kwa Mheshimiwa Waziri lakini mpaka leo hii hatujapata motor pump hiyo au kupata fedha kwa ajili ya ununuzi wa motor pump ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Jimbo langu la Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa fedha hizi zitatoka kwa ajili ya ununuzi wa motor pump ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Jimbo langu la Rufiji hususan Tarafa ya Ikwiriri? Ahsante.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anasema kwamba msema kweli ndiyo mpenzi wa Mungu na mimi naomba niulize maswali ya kiukweli ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Rufiji ni takribani mwaka mmoja sasa tunapata umeme kwa saa nne tu kwa siku. Hali hii imesababisha vijana wa pale Ikwiriri kufunga viwanda vyao vidogo vya furniture kwa kuwa umeme wakati mwingine unakuja usiku. Naomba kufahamu kauli ya Serikali waliyoitoa kwamba nchi hii hakuna mgawo wa umeme, je, Rufiji siyo sehemu ya Tanzania? Hilo ni moja.
Swali la pili, wananchi hawa wa Rufiji hawana barabara hata robo kilometa, hawana maji, hawana hospitali hata X-ray machine hawana japokuwa wilaya hii ni ya zamani sana. Mchango wa Rufiji kwa Pato la Taifa ni asilimia 19 kutokana na hifadhi ya Taifa pamoja na misitu. Naomba kufahamu kwa nini Serikali inawachonganisha wananchi wa Jimbo la Rufiji na Chama chao cha Mapinduzi?
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi waliokuwa na umri wa kuelewa mambo, mwaka 1956 Mwalimu Nyerere aliahidi ujenzi wa Bwawa la Stiegler‟s Gorge ili kuweza kutatua tatizo la umeme. Bwawa hili lingejengwa pale katika Kata ya Mwaseni. Ahadi hii ina miaka 61.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu kama ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri aliyotuahidi hapa ujenzi wa mabwawa katika Kata za Mwaseni, Kipugira, Kilimani pamoja na Mkongo itachukua pia miaka 61 au itakuwa muda mfupi kidogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Wizara ya Maliasili na Utalii inachangia pato la Taifa asilimia 19 na Rufiji yetu iko ndani ya hifadhi kwa zaidi ya nusu ya Rufiji, yaani square kilometer 6,500 ipo ndani ya hifadhi ya Maliasili na Utalii. Naomba kufahamu, mchakato wa ujenzi wa vyoo katika eneo la Selous pale Rufiji, leo hii watalii wanajisaidia katika maeneo ya hifadhi bila kuwa na vyoo. Naomba kufahamu, hili pato la Taifa mgawanyo wake ukoje katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ili kuweza kusaidia wanyama hawa ambao wapo ndani ya hifadhi ikizingatia kwamba watalii wetu leo hii wanajisaidia sehemu ambazo ni za wazi bila kujisaidia eneo la vyoo.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sekunde moja naomba niendelee kutoa pole kwa wananchi wangu wa Rufiji hususan tukio la jana ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambuju alitaka kuuawa lakini alisalimika baada ya kukimbia kugundua majambazi wale wameshaingia nyumbani kwake,
taarifa ambazo nimezipokea muda huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili tu ya nyongeza; la kwanza nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri migogoro baina ya wananchi na wahifadhi imechangiwa na kuondolewa kwa mipaka ya awali iliyokuwepo hususan katika Kata ya Mwaseni na wananchi kuzuiliwa kuvua samaki
wale ambao wapo katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Naomba kufahamu Serikali ina mpango gani sasa ili yale mabwawa matano niliyoyaomba kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii yaweze kuchimbwa haraka katika Kata ya Mwaseni, Kata ya Kipugira hususan maeneo ya Nyaminywili, Kipo na Kipugila pia katika Kata ya Ngorongo? Naomba kufahamu Serikali inaharakisha vipi
mchakato wa uchimbwaji wa mabwawa ya samaki kwa wananchi wangu wa maeneo hayo?
Mheshimiwa naibu Spika, lakini pili……
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafuta hilo swali la samaki, naomba la mgogoro wa mipaka libaki. Swali la pili, watumishi wa hifadhi wamekuwa
wakiweka beacons na alama kadhaa katika baadhi ya nyumba hususani katika maeneo ya Kipugila maeneo ya Nyaminywili na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa uwekaji wa beacons unakiuka Ibara ya 13 ya Katiba, pia unakiuka Ibara ya 16 ya Katiba ambayo inazungumzia haki za msingi za wananchi ubinafsi wao, ufamilia wao pamoja na uhifadhi wa maskani zao. Ninaomba kufahamu je, Wizara hii ya Maliasili na Utalii imedhamiria kabisa kukiuka Katiba ya haki za msingi ya Ibara ya 13 na Ibara ya 16, katika kuweka beacons na kusababisha uhuru wa wananchi wa mnaeneo husika kukosa haki zao za msingi?
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kilio kikubwa sana cha mahitaji ya umeme Kata ya Mkange pale Chalinze ukizingatia kuwa sehemu hii inachangia kwenye uchumi wetu wa Taifa hususan katika Wilaya ya Bagamoyo, pia na Halmashauri ya Chalinze na Tanzania kwa ujumla hususan katika viwanda pamoja na utalii.
Je, Serikali inajipangaje kusaidia wananchi pamoja na wawekezaji wa viwanda umeme ili kupunguza ukali wa maisha wa eneo hili la Kata ya Mkange? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa Stiglers Gorge unadhamiria kuikomboa nchi yetu katika umeme hususan katika viwanda vinavyojengwa pamoja na treni hii ya umeme.
Je, Serikali inawaachaje wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wametunza bwawa hili pamoja na Mto Rufiji kwa miaka mingi sana hususan wakazi wa Kata ya Mwaseni, Kipugira, Ngorongo na Mkongwa? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's