Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Kasuku Samson Bilago

Supplementary Questions
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Waziri mwenyewe amekiri katika majibu yake ya swali la msingi kwamba ajira ya walimu imekasimiwa kwenye mamlaka zingine, na mamlaka zilizokasimiwa ajira za walimu ndizo zimesababisha matatizo makubwa ya walimu, walimu kutopanda madaraja kwa wakati, walimu kutolipwa mishahara mizuri na walimu kutolipwa madai yao kwa muda mrefu sana.
Je, Waziri yuko tayari hii Tume iliyoundwa namba 25 ya mwaka 2015 iwe na mamlaka kamili ya kuwaajiri na kulipa mishahara bila kukasimiwa kwenye mlolongo wa vyombo vingine?
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyosababishwa ya walimu nchini yametokana na mfumo kwa kukasimu mamlaka ya ajira ya walimu kwa vyombo vingine vingi kuanzia Katibu Kata, Mratibu, TSD, Utumishi, Hazina na kadhalika, vyote vinavyoleta usumbufu kwa ajira ya mwalimu na maslahi yake kupotea.
Je, Serikali iko tayari kuwahudumia walimu kwa dharura kabisa kulipa madai yao yanazidi shilingi bilioni 20 kwa dharura ya haraka ili walimu hao waweze kufanyakazi kwa moyo? Asante
MHE. KASUKU S. BILAGO: Hii nafasi ni ya Mwalimu.
Mheshimiwa Spika, nina swali dogo kuhusiana na fedha hizi zinazotarajiwa kutolewa vijijini za Sh. 50,000,000 kwa kila kijiji. Sasa hivi imeanza mizengwe kwamba fedha hizi zitatolewa kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi. Naomba Serikali itoe kauli fedha hizi zitatolewa kwa utaratibu gani ili kuepuka kwenda kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi peke yao?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu yaliyotolewa na Wizara ambayo hayakidhi viwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wastaafu zaidi ya idadi iliyotolewa na hasa walimu, hata Jimboni kwangu Buyungu idadi kubwa ya walimu waliostaafu inaweza ikaakisi idadi ya watumishi walistaafu katika nchi hii. Sababu zilizotolewa za wastaafu hao kutolipwa moja kubwa ni kukosa fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo Serikali haijataja.
Swali la kwanza, naomba Serikali ikiri ni lini italipa wastaafu wote kwa kupeleka fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wasiendelee kuteseka sambamba na kuwarudisha nyumbani kwao mara baada ya kustaafu? (Makofi)
Swali la pili, wapo wastaafu wa aina mbili, wapo wanaolipwa pensheni na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na wapo wanaolipwa pensheni na Hazina. Wale wa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii wanapata monthly pension wale wahazina wanalipwa kwa miezi mitatu (quaterly pension) hali hii inawasumbua na kuwatesa wastaafu wetu. Naomba wastaafu wote walipwe monthly pension kama ilivyo kwenye mkataba wa kazi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naomba uulize swali, naona unaleta ombi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Swali la pili dogo, ni lini Serikali itaanza kuwalipa wastaafu wote pensheni ya kila mwezi badala ya miezi mitatu? Ahsante!
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali fupi. Kwa kuwa, suala la Katavi linafanana sana na la Mkoa wa Kigoma ambao hatuna kiwanda hata kimoja na rasilimali ziko za kutosha, hususan katika Jimbo la Buyungu ambako kuna rasilimali kama mihogo, mpunga na kadhalika. Je, Waziri yuko tayari kuja kujenga viwanda katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.
Kwa kuwa, hili suala la Geita linafanana sana na tatizo lililoko Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu kutokuwa na sekondari kabisa ya A-level na tunayo shule moja ya sekondari Kakonko ambayo ikiwekewa miundombinu mizuri yafaa kuwa na A-level.
Je, Waziri yuko tayari kuweka kipaumbele katika shule ya sekondari Kakonko ili ipewe hadhi ya kuwa na A-level itakayokuwa ya kwanza katika Wilaya ya Kakonko?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii adimu. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri, ipo nguvu kazi nzuri sana katika nchi hii iliyotafuta ajira binafsi; vijana wa bodaboda. Hawa vijana wa bodaboda tunawatumia vizuri wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi, wanapata misukosuko ya kufa mtu. Wanasumbuliwa na Polisi. Bodaboda wangu waliopo Kakonko na nchi nzima, hawa bodaboda tunawalindaje katika ajira zao hizi? Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mgogoro uliopo Kasulu - Kagera Nkanda unafanana kabisa na mgogoro ambao upo Wilaya ya Kakonko ambako tunayo mbuga ya wanayama ya Moyowosi na Kigosi inayozungumzwa. Vijiji vya Mganza, Itumbiko, Kabingo na Kanyonza vinapakana na maeneo hayo na; kwa hiyo vimekosa ardhi kabisa ya kutumia kwasababu ya ongezeko la watu. Kwa hiyo, nauliza swali; ni lini mchakato huo wa Wizara ya Maliasili na Utalii itaiona hoja ya wananchi kuongezewa ardhi kutoka kwenye hifadhi badala ya hifadhi kuwa na ardhi kubwa kuliko wananchi? Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Kwa kuwa suala la wakimbizi ambalo linaathiri Wilaya ya Kibondo, vilevile limeathiri Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu.
Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuwashauri watu wa UNHCR kutoa huduma za afya katika Kituo cha Afya Wilaya ya Kakonko?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na tatizo la Serikali kuwatishia Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zitapata janga la njaa, kwamba watapoteza Ukuu wa Wilaya na hivyo kusababisha wasitoe takwimu halisi za upungufu wa chakula uliopo katika Wilaya zao. Wananchi wengi wamekuwa wakifa kutokana na njaa kwa kuficha wasijulikane kama kuna njaa wilayani kwao. Je, ni kwa nini chakula kinakuwepo wilaya nyingine au mikoa mingine kingi na wilaya nyingine hakipo, watu wanakufa njaa ndani ya nchi hii moja?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Pamoja na maelezo mazuri ya Naibu Waziri juu ya Workers Compensation na sheria inayohusika, kuna tatizo moja kutoka chombo kilichokuwa kinashughulikia compensation ambacho kimekwisha na kikachukuliwa hiki cha sasa ambacho ni Compensation Act ambayo imeanza Julai, 2016. Naomba anihakikishie kwamba wale wafanyakazi walioumia kwa sheria ya zamani ambayo ilikuwa inalipa viwango vidogo kama sh. 100,000/= watachukuliwa walipwe na Mfuko huu mpya kwa malipo ya Mfuko huu wa sasa? Ahsante.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Suala la ufaulu wa watoto wa kike elimu ya juu inategemea na ufaulu wa watoto haohao wa kike kwenye shule za chini (O-Level na A-level), sasa kumekuwa na tatizo la watoto wa kike wanaobeba mimba wakiwa shuleni kuachishwa masomo, na hili tumekuwa tukilizungumza muda mrefu; ni lini Serikai italeta utaratibu hapa Bungeni, sheria itungwe ili watoto wa kike wanaobeba mimba shuleni wakishajifungua waruhusiwe kuendelea na shule?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika majibu ya swali la msingi, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba mifuko hii iko imara. Kama kweli mifuko iko imara, kuna Walimu waliostaafu zaidi ya 6,000 hawajalipwa mafao yao zaidi ya shilingi bilioni 550. Walimu hawa wanateseka wakiwemo Walimu wangu wa Jimbo la Buyungu ambao kila wakati nahangaika kufuatilia mafao yao ya kustaafu. Ni kwa nini anayestaafu halipwi mafao yake kwa mujibu wa mkataba ndani ya miezi miwili baada ya kustaafu?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's