Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Ally Mohamed Keissy

Supplementary Questions
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwambao wa Ziwa Tanganyika wavuvi wengi wanatoka DRC-Congo. Cha ajabu wanakata leseni kwa bei kama mvuvi mwenyeji wa Ziwa Tanganyika. Je, ni lini Serikali itachukua hatua ili wavuvi kutoka nchi za jirani walipie leseni kama inavyotakiwa?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimwia Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kigoma pamoja na Wilaya zake zinaingiza gharama kubwa sana katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia majenereta, zaidi ya bilioni 160 kwa mwezi, kwa nini Serikali pamoja na Wizara ya Nishati na Madini isifanye haraka mradi huu ili kuokoa pesa kwa Mkoa wa Kigoma?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jiografia ya Wilaya ya Nkansi, naomba hilo swali labda angesaidia kujibu Mheshimiwa Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Elimu, Teknolojia na Elimu ya Juu. Inaonekana hilo swali halikujibiwa jinsi inavyotakiwa na aliyeandika hilo jibu, hajui Wilaya ya Nkasi ilivyo; Kipili iko wapi, Namanyere iko wapi, Kala iko wapi, Itindi iko wapi, Kabwe iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majambazi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hilo gari haliwezi kuhudumia vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, lini Serikali, itawapatia mgawo wa mafuta wa kutosha Wilaya ya Nkasi?
Mheshimiwa Naibu Spika, gari lenyewe liko Wilaya ya Nkasi, hata mafuta halina! Lini itaongeza mgao wa mafuta katika Wilaya ya Nkasi? Lini itawapatia pikipiki vijana wa Marine Kipili, ili kuondoa tatizo la usafiri ambako unatokea ujambazi katika vijiji vilivyopo jirani jirani na mwambao wa Ziwa Tanganyika ili kupunguza uharamia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kituo cha afya cha Kirando kilianzishwa miaka 42 iliyopita wakati Kirando ikiwa ni Kijiji, leo kina wakazi mara 50 zaidi kutoka miaka 42, aliyekuwa Waziri wa Afya Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid alifika pale Kirando na akaniahidi kwamba hiki kituo kweli kimezidiwa na ninafanya mpango wa kuwa hospitali kamili.
Lini Serikali yako itaipa hadhi kituo cha afya Kirando kuwa hospitali kamili kwa kuwa kimezidiwa na wagonjwa?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Nkasi, kuna Ranchi ya Kalambo ambayo iligawiwa kwa wafugaji block kama kumi, kila block heka 3000 mpaka 2500 kila mfugaji, block kumi. Lakini hizo block kumi hakuna ng‟ombe zilizopelekwa baadhi ya blocks na baadhi ya waliochukua hizo block ni wajanja hawana mfugo hata mmoja wanakaa wanakodishia wafugaji.
Je, Serikali iko tayari kupitia upya Ranchi ya Kalambo ili kugawa upya kwa wafugaji ili kuondoa matatizo ya wafugaji na wakulima nchini?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi leo ina miaka 40 tangu ilipoanzishwa, lakini haina hospitali ya Wilaya, wala Serikali haina mpango wa kujenga hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali yetu itakuwa na azimio la kujenga hospitali ya Wilaya hasa katika Makao Makuu ya Wilaya katika Mji wetu wa Namanyere?
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Waziri ametembelea mpaka Wilayani kwangu Nkasi kule na kujionea mwenyewe jinsi matatizo ya mawasiliano ya Redio TBC hayafiki kule kwetu. Ni lini sasa bataweka mkazo ili watu wanaokaa mwambao mwa Ziwa Tanganyika waache kutegemea matangazo kutoka DRC Congo?
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali lake la kwanza alisema kwamba ana ziara ya Iringa, Mbeya na Songwe. Je, yuko tayari sasa katika hiyo ziara kuunganisha mpaka Wilaya ya Nkasi akajionee mwenyewe matatizo ya Afya, Elimu na Barabara katika Wilaya yetu ya Nkasi?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hii Awamu ya Tano, kila siku namsikia Mheshimiwa Rais anazungumza haya mambo, kwamba ukinunua kitu dukani omba risiti; ukienda hotelini, omba risiti, je, Serikali imejipangaje kuhusu hawa wauza mitumba na wanaotembeza mali (machinga) na mama ntilie kwa ajili ya kutoa risiti ili tupate kodi ya Serikali yetu? Serikali imejipangaje hapo?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kijiji cha Kipili, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa, tulikuwa na Chuo cha Uvuvi, na kulikuwa na generator na cold room, lakini bahati mbaya awamu zilizokuja ikageuzwa ikawa secondary school na uvuvi ukaisha, na sisi watu wa mwambao tunategemea sana uvuvi, hasa mwambao wa Ziwa Tanganyika, na hakuna Chuo:-
Je, ni lini Serikali itakirudisha Chuo cha Uvuvi cha Kipili ili kusaidia wavuvi wetu wa mwambao wa Ziwa Tanganyika?
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Ziwa Tanganyika tuna Halmashauri tano na kila Halmashauri ina licence yake na mvuvi anakata licence, lakini anapotaka kuhama kwenda Halmashauri nyingine hata kama licence yake haijakwisha muda lazima alipie licence upya kwenye Halmashauri anayokwenda. Je, ni lini Serikali itaondoa kero hii kwa wavuvi?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, Asante sana. Pamoja
na jibu zuri la Naibu Waziri. Sasa lini Serikali itatoa kero kwa hizi kodi ndogo
ndogo za akina mama hasa wakinamama wauza vitumbua, wauza mchicha,
wauza dagaa, wauza nyanya ili kutoa kero kwa wananchi wetu wasiendelee
kudhulumiwa na kuteswa na hawa wakusanya kodi na hawa Wanamgambo,
imekuwa kero na Serikali kila mara ilitangaza hapa kwamba kodi ndogondogo
hizi ni kero lini Serikali itatangaza Halmashauri zote ziache mara moja kutoza
akina mama kwenye masoko madogo madogo?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Swali; je, wale Wakandarasi au Halmashauri zilizolipa pesa kwa Wakandarasi hewa, mtachukua hatua gani? Kuna miradi kadhaa katika Wilaya ya Nkasi ambayo pesa zililipwa lakini hakuna kilichofanyika.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kama Serikali ipo tayari kupeleke pesa hizo, lakini nataka kujua ni shilingi ngapi zitapelekwa kwa ajili ya kumalizia huo mradi wa Skimu ya Lwafi? Nataka kujua kiasi cha pesa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vituo vya Kirando na Kabwe ni majengo ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani ilinunua kwa wananchi wa kawaida. Ni majengo yaliyojengwa kwa tofali mbichi na hata leo akienda kuyaona hayana milango, saruji na yanabomoka na baadhi ya nyumba za uani wanazolala polisi hazina milango kabisa. Je, katika hizo nyumba 4,136 vituo vya Kirando ni miongoni mwa vituo vitakavyokarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara katika Wilaya ya Nkasi kuvitembelea Vituo vya Polisi Kirando na Kabwe na vituo vya Uhamiaji vya Mwambao wa Ziwa Tanganyika ambavyo viko katika hali mbaya sana, havistahili Polisi kuishi wala kufanyia kazi?
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa mara ya kwanza Serikali kutoa jibu zuri la kuridhisha kwa wananchi wa Nkasi.
Kwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliniahidi mimi humu Bungeni kwamba mara baada ya kukamilika ile barabara yuko tayari kutoa yale majengo kwa Chuo cha Ufundi VETA. Na sasa barabara yetu inakwenda speed ya ajabu, imebaki kilometa 10 au 12 na wakandarasi wameniahidi Januari au Disemba kipande cha barabara hiyo kitakamilika.
Je, lini sasa mazungumzo kati ya Wizara ya Elimu na Wizara ya Ujenzi yataanza haraka iwezekanavyo wananchi wapate kile chuo?
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jiji la Dar es Salaam linashangaza kwani wamechukua kampuni ya kutoka Kenya ili kukusanya fedha za maegesho ya magari Dar es Salaam. Vilevile hawatumii mashine za EFD kukusanya pesa na kupandisha kutoka Sh.300 kwenda Sh.500. Hivi kweli nchi nzima ya watu milioni 50 wamekosa kampuni yoyote katika nchi yetu mpaka kuchukua Kampuni ya Kenya?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika kijiji cha Kirando mwambao wa Ziwa Tanganyika, TPA wameweka mtu wao kutoza ushuru mzigo wowote unaotoka pale katika kijiji cha Kirando wakati TPA hawajaweka huduma yoyote. Hamna kibanda, hamna hata
choo, hamna chochote walichoweka lakini kila mwananchi anayesafirisha mzigo kwenda Kabwe, kwenda Mwandakerenge, kwenda Mvuna anatozwa ushuru na watu wa TPA.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna Halmashauri nyingi zilianzishwa kwa misingi ya kisiasa na kuacha Halmashauri ambazo zina hadhi kabisa ya Halmashauri. Vipi Serikali inaonaje kuzifuta mara
moja Halmashauri ambazo zilianzishwa hazina vigezo na kuzipa Halmashauri zenye vigezo?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushuku sana. Kwanza naishukuru Serikali kusema kweli kutenga pesa za daraja kiungo muhimu sana kuhusu barabara. Hii barabara ni muhimu inaunganisha mikoa mitatu; Katavi, Rukwa na Songwe, ni muhimu kwa ajili ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka jibu sahihi, ni lini Serikali itakuwa tayari kujenga barabara ya lami katika mwambao wa Ziwa la Rukwa ili wananchi wafaidike? Atoe tarehe maalum, ni lini na mwaka gani? Maana hili daraja litajengwa, barabara inaweza ikaendelea hivyo hivyo kuwa tope wananchi wakateseka. Mwambao kule wanalima sana mazao muhimu sana. Kwa kuwa hii nchi ina njaa kila sehemu, tutakuwa tunakomboa sana wananchi wengine kutokana na mwambao wa Ziwa Rukwa kuwa na ardhi nzuri sana…
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, hii
barabara inaanzia Mkoa wa Katavi, Kibaoni inakwenda mpaka Songwe kupitia Mwambao wa Ziwa Rukwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana Mwenge ulizimwa Simiyu, Mtukufu Rais John Pombe Magufuli alizuia misafara ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Wakurugenzi na kuokoa kiasi cha pesa sijui zaidi ya shilingi bilioni sita.
Nataka kujua kwa mwaka mzima kukimbiza Mwenge wa Uhuru kunagharimu Taifa hili shilingi ngapi? (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza Mbunge aliyeuliza swali kwamba Wabunge wanatumia zile pesa, namshukuru sana Naibu Waziri alivyoeleza kuhusu zile pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa Wabunge hawashiki, pesa zinakwenda kwa Mkurugenzi, Mwenyekiti yeye ni Mwenyekiti tu. Kuna Afisa Mipango, kuna Madiwani wawili, kuna watendaji wawili ndipo utagawa zile pesa, hatugusi hata senti tano moja sisi kuweka kwenye mafuta.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mfuko wa Jimbo nimezungumza tangu mara ya kwanza una matatizo. Kuna majimbo mengine na tujimbo twingine.
Huu mfuko hauwezi kufutwa kwa sababu kuna Wabunge wengine kama Viti Maalum, mzee wangu anasema Majimbo, Majimbo mengine yana watu 30, watu 40, mengine kata 10 Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kama nilivyosema mara ya kwanza usimamishwe, wafanye tathmini upya, wagawe upya kutokana na idadi ya watu na ukubwa wa majimbo. Haiwezekani kuna majimbo mengine ni madogo wanapewa sawa na Jimbo kubwa haiwezekani. Ifanywe tathmini upya ili hela ziende kwa usawa bila ubaguzi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majimbo ambayo hayana vigezo, hayastahili kuapata mfuko wa Jimbo mkubwa, haiwezekani. Jimbo lako la Ilala kubwa lipate sawa na Jimbo...
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuende na takwimu sahihi, haiwezekani.
Swali, Wabunge Viti Maalum hawaruhusiwi kupata Mfuko wa Jimbo na wasitegemee kuzipata, kwa sababu Mbunge wa Jimbo ndiyo anastahili kupata ule Mfuko wa Jimbo na ikiwezekana Wabunge wale wengine wachunguzwe walikotoka. Haiwezekani wewe uliyekuja kuzungumza hapa wakati ulikotoka wewe hauna hata wa...(Kicheko)
MHE. ALLY K. MOHAMED:Ahsante sana Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi bima za afya baadhi ya maduka na hospitali zinatumika vibaya, kuzidisha double allocation mtu anaenda kutibiwa anaweza akaandikwa double akaiga saini ya mteja au na zingine zinazidisha bei mara mbili, je, nani anazikagua bima ya afya kabla ya malipo, kwa kuwa zinaendesha wizi wa hali ya juu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, kwa mara ya kwanza wananchi wa Kazovu, Isaba, Chongo na Katete wataona hata bajaji na gari. Nilipoingia Bungeni mwaka 2010 kilio changu cha kwanza ilikuwa ni barabara lakini awamu ya sasa ni awamu ya chapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo, Mheshimiwa Naibu Waziri juzi umetuma wakandarasi wako kuangalia kipande kilichosalia cha kutoka Kazovu kwenda Korongwe, lini sasa Serikali yako itasaidia kipande hicho kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi haina fedha?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko mengi sana, hii inaitwa road licence kama anavyosema, gari yangu mfano imekaa jikoni, uani, garage miaka mitatu, sina pesa za kutengeneza lakini nikadaiwa hiyo road licence na faini juu. Kwa nini Serikali isione kwa sasa kwamba kwa nini wasiingize kwenye mafuta ili gari yangu ikitembea mimi nilipie kodi moja kwa moja kuliko kumtesa mtu gari yake imekaa jikoni miaka mitatu aendelee kulipa kodi wakati hana uwezo hata kununua spare. Gari yake kama anavyosema imepata ajali, lakini gari inaweza kukaa miaka mitatu, asiyekuwa na uwezo wa kutafuta pesa, lakini itaendelea kudaiwa road licence na inapigwa na faini juu, hii ni halali kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini msichukue kigezo cha kuweka kwenye mafuta, pesa kwenye mafuta, ili ninapotembeza ile gari yangu nalipia moja kwa moja road licence?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na jibu zuri la kuridhisha la Serikali nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mto Lukuga kupoteza maji katika Ziwa Tanganyika, je, Serikali iko tayari kuwahamasisha wananchi wanaokata miti katika milima yote inayozunguka Ziwa Tanganyika, ili wakati wa masika maporomoko yote yanayoleta tope, mchanga, kupunguza kina cha maji ya Ziwa Tanganyika, kuacha shughuli hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, je, Serikali iko tayari kuwaelimisha wananchi waache kukata miti hovyo na kuwachukulia hatua wote wanaofanya kandokando ya Ziwa Tanganyika kufanya shughuli ambazo Serikali hairidhishwi, kama kujenga karibu na ziwa na kuharibu vyanzo vya maji vinavyoporomosha maji katika Ziwa Tanganyika?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ingawa Serikali ina mpango sana wa kufungua mabenki ya wakulima, je, Serikali haioni kama tatizo hiyo benki inafilisika kwa kuwa wakati wa msimu mkulima analazimishwa asiuze mazao bei anayotaka? Kwa mfano, mahindi kule kwetu yanashuka bei, mengi hakuna mahali pa kupeleka.
Je, Serikali haioni kwamba iweke sheria mtumishi abanwe mshahara wake ili asiutumie hovyo ili wakati wa matatizo awasaidie majirani zake kama vile wakulima wanavyofanywa ili wasiuze mazao wasaidie sehemu zenye njaa?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachukulia mfano wa mabasi, kuna utingo, kuna dereva, kuna konda, mwenye licence ya kuendesha chombo pale ni mmoja tu ambaye ni dereva, utingo hana licence wala konda. Cha ajabu katika Ziwa Tanganyika mwenye chombo anakuwa na wavuvi wake kama kumi au kumi na tano na wote wanalazimika kuwa na leseni. Je, Serikali haioni kama ni kero?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante leo ni karibu siku tatu BBC inatangaza kuhusu Ziwa Tanganyika kuathiriwa na kukata miti, na kutoweka samaki. Je, Serikali ina mpango gani kuzuia na kusaidia kuzungumza na nchi ya DRC Kongo, Burundi na Zambia ili kujenga kibanio katika mto Luguga ili maji yasiishe katika Ziwa Tanganyika?
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inasema mwambao wa Ziwa Tanganyika ni mita 60, lakini kuna upendeleo wa hali ya juu hasa kwenye Kijiji cha Kilando, wanavunjiwa watu na baadhi hawavunjiwi ambao wako chini ya hiyo kiwango cha mita 60. Je, Mheshimiwa Waziri anatoa tamko gani kuhusu wananchi wanaokaa mwambao mwa Ziwa Tanganyika kuacha upendeleo, kuvunjiwa baadhi ya watu na wengine kuachwa? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's