Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Godfrey William Mgimwa

Supplementary Questions
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme hasa kwenye uunganishaji limekuwa ni tatizo kubwa hasa kwenye maeneo ya mita. Wananchi wengi na wateja wengi wamekuwa wakilalamika kwamba mita ambazo wanafungiwa zinaharibika baada ya muda mfupi. Ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba je, analifahamu hili na kama analifahamu, hatua gani zitachukuliwa, ili kuhakikisha kwamba, utaratibu huu mbovu unasitishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jimbo la Kalenga limekuwa lina changamoto kubwa katika masuala haya ya umeme na nina vijiji kadhaa ambavyo mpaka dakika hii viko gizani na vinahitaji umeme. Kijiji cha Lupalama katika Kata ya Nzii, Kijiji cha Kipera, Kijiji cha Itagutwa, Kijiji cha Magunga na Lyamgungwe; ningependa kusikia commitment ya Mheshimiwa Waziri, je, ana utaratibu gani na mpango gani kuhakikisha kwamba, vijiji hivi vinapata umeme? Na kama je, yuko tayari kuungana na mimi kwenda moja kwa moja Kalenga ili kuweza kuwapa hamasa wananchi wangu? Nashukuru.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuweka minara kwanza niipongeze sana Serikali kwamba imeendelea kupeleka minara katika Jimbo la Kalenga kwa kasi zaidi. Tatizo ninalolipata ni kwamba baada ya kusimikwa ile minara upatikanaji sasa au uanzaji wa kuanza kupata mawasiliano unatumia muda mrefu sana. Ningependa kujua Serikali ina mkakati gani ili mara baada ya kuwekwa ile minara mawasiliano yaanze kupatikana kwa muda unaostahili. (Makofi)
Swali langu la pili, narudi tu kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba amesema vijiji vilivyotamkwa hapa mwishoni vya Kaning‟ombe na Ikuvilo vitapita katika utaratibu wa kupitia UCSAF lakini katika tovuti ambayo nimekuwa nikiipitia ya UCSAF nitoe tu statistics kidogo inaonyesha kwamba kwa mwaka 2015 zilitangazwa zabuni175, Kata zilizopata wazabuni 116 hii kwa ni Tanzania nzima, idadi ya vijiji 156, miradi kuanza ilikuwa ni Mei, 2015. Lakini katika orodha hii yote hakuna vijiji ambavyo tayari vilishaanza kupatiwa mawasiliano ni zero, kupitia mradi ya UCSAF.
Ningependa kujua Serikali ina mikakati gani kuhakikisha kwamba inaipa pesa UCSAF ili kwamba miradi ambayo imeorodheshwa iweze kukamilika kwa wakati? Ahsante.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo ambalo lipo katika Jimbo la Mheshimiwa Mendrad Lutengano, ni sawasawa na tatizo ambalo liko katika Jimbo langu la Kalenga. Ningeomba kujua Miradi ya Maji ya Weru, Itengulinyi, Supilo, itakamilika lini kwa sababu wakandarasi wamekuwa wakipiga makelele na kudai pesa zao za malipo?
Ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Wakandarasi hawa watalipwa, ili kwamba, miradi iweze kuendelea na wananchi wangu waweze kupata maji? Ahsante.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, tatizo ambalo linaonekana la kuwanyanyasa wananchi ambalo linafanywa na Polisi linafanana sana na malalamiko mbalimbali ambayo yanatoka katika Idara ya Uhamiaji kwamba Idara ya Uhamiaji nao wanafanya unyanyasaji mkubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeomba kujua kwa sababu katika Idara hii kuna watumishi ambao hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi kirefu sana. Serikali inasema nini au ina tamko gani kuhusu watumishi hawa wa ajira mpya ambao hawajalipwa mishahara yao ili Serikali iweze kutoa majibu yanayoeleweka, kwamba watalipwa lini mishahara yao watumishi hao wa ajira mpya?
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya kupeleka mawasiliano katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, swali hili nimeuliza mwaka 2014 nikajibiwa kwamba 2015 nitapata majibu ya uhakika, sikupata majibu. 2015 nikapata nafasi ya kuuliza nikaambiwa 2016, leo hii ni 2017 naambiwa ni 2018. Naomba niweze kupata majibu ya uhakika leo kwamba ni lini sasa vijiji hivi vilivyoorodheshwa vitapata minara ya simu na wananchi wangu waweze kupata mawasiliano hayo ya simu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika minara ya simu ambayo inajengwa katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Kalenga service levy hailipwi moja kwa moja kwenye Halmashauri, inaenda kulipwa kwenye makampuni yenyewe ambayo mengi yapo Dar es Salaam. Wananchi katika Jimbo langu wanakosa mapato ya ndani kutokana na minara hiyo ya simu. Ningependa kujua kutoka Wizarani, je, ni namna gani sasa wanaweza kuwapelekea fedha hizi wananchi ambao nao wanatakiwa kwa namna moja au nyingine waweze kupata faida kutokana na minara hii ya simu, kwa sababu inayotumika pale ni ardhi?
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba fedha ambazo yanapata makampuni haya au faida ambazo zinapata kampuni hizi zinakwenda pia kuwasaidia wananchi katika maeneo husika? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nitakuwa na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri nyingi zimekuwa hazitengi fedha hizi kwa ajili ya vijana na akina mama; lakini vile vile tuna tatizo sasa hivi ambalo tungekuwa makini zaidi kuliangalia suala la ndugu zetu walemavu, kwamba kuweze kuwa na uwezekano sasa wa kuzitenga fedha kutoka katika hizi asilimia 10 kwa ajili ya walemavu, vijana na akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu majibu ya msingi yameshatolewa ningependa kufahamu kwa hizi Halmashauri ambazo kwa ujumla zimeshindwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya vijana kama mimi akina mama; na kama tulivyoongea kuhusu walemavu ningependa kufahamu sasa.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inazibana halmashauri hizi ili ziweze kupata mapato ya ndani kwa uhakika na kuhakikisha kwamba inatenga fedha hizi kwa ajili ya makundi haya? Nakushukuru.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niishukuru Serikali kwa kupeleka fedha kwa ajili ya miradi hii ambayo imeorodheshwa, lakini kwa uhalisia ni kwamba miradi hii haijakamilika kwa asilimia mia, miradi miwili mradi wa Mfyome na Mradi wa Magunga – Isupilo kuelekea Lumuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii kwa sababu imekaa kwa muda wa miaka miwili haijakamilika na Halmashauri imeshapelekwa Mahakamani kwa ajili ya kufanyiwa arbitration, napenda sasa kupata commitment ya Serikali ikiwa kama arbitration itaenda kinyume na matakwa ya Serikali, yaani Serikali ilipe fedha hizi kwa mkandarasi, itatumia mida gani kukamilisha malipo haya kwa wakandarasi ili wananchi wangu waweze kupata maji katika miradi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika utaratibu wa kutafuta wakandarasi, Serikali inawaagiza wakandarasi kununua vifaa na hivyo katika ununuzi wa vifaa wakandarasi hawa wanatozwa kodi ya VAT, lakini wakati wa malipo baada ya kupeleka zile certificates Wizarani, Serikali hailipi zile fedha ambazo wakandarasi wameingia kwa maana ya VAT na hivyo basi miradi inaendelea kusimama…

MHE. GODFREY W. MGIMWA: ...miradi inaendelea kusimama kwa sababu ya kutofanyika kwa malipo haya. Napenda kujua, je, Serikali ina mtazamo gani sasa kuhakikisha kwamba VAT inalipwa kama fidia kwa hawa Wakandarasi ambao wako katika miradi hii? Nashukuru. (Makofi)
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na nitakuwa na maswali mawili.
Mheshimiwa naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba inapeleka miundombinu kwenye vijiji na miji midogo. Hata hivyo, bado hakujakuwa na mbinu mbadala ambayo inaweza ikasababisha mabenki haya yakaenda kuanzisha benki katika vijiji. Napenda kufahamu, ingawa hakuna sera, sasa Serikali kwa sababu imeshafanya haya yote, ina utaratibu gani sasa kuhakikisha kwamba Benki zinapeleka huduma zao kule vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba mabenki mengi hasa Benki za Kilimo na Benki ya Wanawake bado hazijapata fursa ya kupeleka huduma vijijini. Mwezi huu na miezi inayofuata benki hizi zitakwenda kufungua matawi Dodoma na Mwanza, lakini bado hazijagusa katika vijiji husika ambako kuna asilimia kubwa ya wakulima na wananchi wetu wapo kule ambao wanategemea sana shughuli za kibenki.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kufahamu; je, kwa nini sasa Serikali inaendelea kuruhusu mabenki haya kuanzishwa au kufunguliwa katika miji mikubwa na siyo vijijini ambako ndiko kwenye tija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kukushukuru, ahsante. (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's