Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Supplementary Questions
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa kuna umuhimu wa kuunganisha barabara za mikoa na wilaya na kwa kuwa barabara inayounganisha barabara ya Iringa na Morogoro inapitia kwenye milima Kitonga na kwa kuwa linapotokea tatizo katika milima hiyo inakulazimu upite Dodoma, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha kuunganisha barabara nyingine ambayo ni fupi inayoanzia Kidabaga – Idete – Itonya - Mhanga ambayo inaenda kutokea Mbingu kule Morogoro?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri. Niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kilichopelekea kuunda Tume hii mpaka kwenda Zurich ilikuwa ni swali ambalo liliulizwa hapa ndani na Mheshimiwa Hafidh Ali na imekuwaje Serikali imeshindwa kutoa jibu mapema mpaka leo baada ya kuuliza swali ndiyo majibu yamekuja?
Swali la pili, kwa kuwa kutotambuliwa kwa ZFA na FIFA kutapelekea bado kuwa na timu ya Taifa moja na kwa kuwa TFF na ZFA zinaposhiriki Kimataifa zinapata tatizo la ukosefu wa fedha na hivyo kupelekea timu zetu za Taifa kufanya vibaya, je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kuzichukua timu za Taifa wakati zinaposhiriki kwenye mashindano ya Kimataifa ili tusiendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jibu lako zuri, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa moja ya usumbufu mkubwa wanaopata wakulima ni suala la usambazaji wa pembejeo ambao haufiki kwa wakati. Lakini tatizo kubwa ambalo linasababisha hilo ni mawakala kutokufikisha kwa wakati na mawakala wamekuwa wakilalamika kwamba hawalipwi pesa za usambazaji. Mpaka leo ninavyozungumza kuna baadhi ya mawakala waliosambaza mwaka jana ambao walikuwa wanafanya kazi hiyo kwa niaba ya makampuni makubwa, kama TFC na MINJINGU, hawajalipwa. Sasa Serikali haioni kwamba tutaendelea na hili zoezi la kuwasaidia wananchi na kutowasaidia wengine wanaosambaza ni makosa?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri, kumekuwana kisingizio kikubwa cha sababu ya ucheleweshaji wa fedha kwa kutokukamilika kwa miradi mingi na kupelekea wakandarasi kudai kwamba wanalipwa kidogo kidogo. Kwa mfano, miradi ya maji ambayo iko katika Kijiji cha Ipalamwa, Kitoho, Ilamba na sehemu nyingine. Sasa Serikali inasemaje, nani wa kuchukuliwa hatua, ni Halmashauri husika au Mkandarasi ambaye ameshindwa kumaliza mradi kwa wakati na ubora?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa kiwango hicho ni kidogo ambacho kinapelekea hata nauli; kwa mfano, hata katika mabasi ya mwendo kasi ukipiga hesabu hayamtoshelezi huyu mfanyakazi; hawaoni sasa wafanyakazi hawatafanya kazi kwa moyo na tija kwa sababu ya mshahara mdogo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna wenzetu wawekeza wa nje hasa Wachina wameingia, wanafanya kazi ambazo Watanzania wanazifanya, tena kwa bei nafuu; sasa Serikali haioni ni wakati wa kuwabana kuhakikisha kwamba zile shughuli zinazoweza kufanywa na Watanzania zifanywe na Watanzania badala ya wawekezaji wanaouza mpaka vocha ambao wameshaingia nchini?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa barabara iliyotajwa ya kuunganisha Mbeya na Makete bado imechukua muda mrefu na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ana mpango wa kwenda Mkoa wa Njombe, haoni sasa kuna sababu kubwa ya kupita na kuangalia, kutokana na majibu aliyojibu kuona kama kweli itajengwa kwa wakati ambao ameahidi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hizi zipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ikiwemo hii ya kuunganisha Wilaya ya Kilolo na Iringa Mjini. Je, haoni sasa ni muda muafaka wa kufika na kutembelea barabara ambayo inaanzia Ipogolo – Ndiwili - Kilolo ambayo kwa miaka saba imejengwa kilometa saba na kilometa zilizobaki ni 28, haoni kwamba itachukua miaka 28 pia kumalizia hicho kipande kilichobaki?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi lilikuwa linahusu kuhusu kupandisha vituo vya afya; na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo toka ilipoanzishwa mwaka 2000 haijawahi kuwa na hospitali ya Wilaya, imekuwa na Kituo cha Afya cha Dabaga na hivyo imepelekea ili wananachi kufuata huduma za hospitali inabidi waende Ilula kilometa zaidi ya 120.
Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kupandisha hadhi kituo hicho cha Dabaga kuwa hospitali ya wilaya?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu zuri. Swali langu ni kwamba, kuna maeneo ya Wilaya ambayo hata Hospitali za Wilaya hakuna. Je, Serikali inasemaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kufika maeneo kama ya Kilolo, kuja kuona anafanyaje ili kuhakikisha angalau vile Vituo vya Afya na Zahanati ambazo zimeanzishwa na wananchi, kuzipa msukumo ili angalau wapate matibabu na wao wajue kwamba ilani yao wanaitekeleza vizuri?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa sasa hivi suala la michezo Tanzania ni sawasawa na mgonjwa na unapokuwa na mgonjwa aidha umpeleke kwenye maombi, hospitali au kwa mganga wa kienyeji.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri na anajua tatizo hilo na tatizo kubwa limekuwa ni kwamba Serikali imeshindwa kuwekeza kutoka chini kwa maana ya kwenye shule za msingi, UMISHUMTA, UMISETA na michezo mingine na kuifuta, sasa Serikali inasemaje kuhusu kufufua michezo hiyo kwa nguvu zote na kupanga bajeti ya kutosha? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa michezo ni ajira na Serikali ilikiri yenyewe kwamba itahakikisha inapeleka ajira kwa vijana kupitia michezo; na michezo inaleta pato la Taifa kwa mfano nchi kama Nigeria, Cameroon na Ghana imekuwa ni pato, sasa Serikali kwa nini imesahau kwamba hiyo itakuwa ni pato kubwa kwa nchi yetu na kuitelekeza michezo? Naomba jibu. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano ni Wizara ambazo zinashabihiana katika utekelezaji kwenye maeneo ya Wilaya yetu; na kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo hakuna barabara wala hakuna mawasiliano. Kwa mfano, Kata ya Mahenge katika Kijiji cha Ilindi Namagana, Kata ya Ruaha Mbuyuni katika Kijiji cha Ikula na Kata ya Nyanzwa katika Kijiji cha Nyanzwa hakuna mawasiliano, hakuna barabara, sasa Serikali inasemaje kuboresha maeneo hayo ili wale wananchi nao wahisi kwamba wapo Tanzania?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Kibondo ni Wilaya ambayo ilikaliwa na wakimbizi na kwa kuwa kuna majengo ambayo yamekaa kwa muda mrefu ya IOM ambayo Serikali ya Wilaya na Mkoa ilisharidhia kwamba yatumike kwa ajili ya chuo hicho. Je, Waziri haoni sasa ili kubana matumizi ya Serikali afike na kutoa ushauri ili yale majengo yatumike kwa ajili hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti swali la pili, kwa kuwa makampuni mengi ya ujenzi baada ya kujenga barabara yamekuwa yakiacha miundombinu ya majengo mazuri. Sasa haoni ni wakati muafaka wa kupunguza upungufu wa wauguzi zikiwepo Wilaya nyingi pamoja na Kilolo kwa kuweza kuyatumia yale majengo vizuri ili Serikali iweze kupata manufaa?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la ulinzi na usalama ni tatizo na sasa hivi ukichukulia kumetokea mauaji ya mara kwa mara nchi hii, na watu wamelalamika kwamba hawasikilizwi wanapokwenda kwenye vituo vya polisi na mahakama na kwa hivyo kujichukulia sheria mkononi. Serikali haioni sasa inabidi ifanyie kazi suala hili ili kupunguza haya mauaji ambayo yamekuwa ni kero na shida katika nchi hii?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo inafanana kabisa na matatizo ambayo yako hapo, na ni katika Majimbo makubwa, takriban lina kilometa za mraba takribani 21,000; na kwa kuzingatia hilo, Serikali iliamua kutoa Mji Mdogo wa Ilula, sasa ni muda mrefu.
Je, haioni sasa ni muda muafaka wa kupewa hadhi ya kuwa Halmashauri kamili?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa nafasi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu Wilaya zipo kisheria na zipo ndani ya Katiba, Serikali inasemaje kwa baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa vikiwapuuza, vikiwadharau na kutotii amri zao pale wanapotakiwa kufanya hivyo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningependa niulize swali langu moja.
Kwa kuwa fedha ambazo zinatolewa kwa hawa akina mama lishe na kufanya biashara ni fedha za Serikali ambao walio wengi zinatoka TASAF, ni fedha za kuondo umasikini. Na kwa kuwa sasa Watendaji wengi sana wa Vijiji hawajaajiriwa kwa hiyo wanafanya zile kazi kama kukomoa. Je, sasa Serikali inasemaje kuhusu hilo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Simanjiro, naomba niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio chetu, lakini sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa swali la msingi lilikuwa linahusu ahadi za viongozi; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano alipopita kwenye maeneo mbalimbali alitoa ahadi kuhusu maji ikiwepo Wilaya ya Kilolo maeneo ya Ilula na aliahidi kwamba suala la maji litakuwa ni historia kwa Wilaya ile. Je, Serikali inasemaje na mwaka huu imetenga fedha kwa ajili ya wananchi wa Ilula?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo la maji linatatuliwa kwa ujenzi wa mabwawa na kwa kuwa kuna mabwawa yaliyojengwa sehemu za Nyanzwa, Ilindi, Ruaha Mbuyuni na Mahenge na wakati yanajengwa wananchi walikuwa wachache, sasa wameongezeka kwa hiyo maji yale hayatoshi. Serikali itakuwa tayari kuongeza fedha ili wananchi wale waweze kupata maji ya uhakika?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii imefanya sasa naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, kuna baadhi ya Vijiji vikiwemo Ng‟ang‟ange, Pomelini, Masege, Mwatasi, Kesamgagao, Masisilo, Ukumbi na vijiji vingine umeme tayari umeshafungwa na umefika, sasa tatizo ni kuwasha! Ni lini utawashwa ili wananchi sasa waendelee kuishi kwa matumaini na mategemeo makubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilolo ni majimbo yanayopakana. Kwa kuwa vijiji vingi ambavyo vinapakana na hifadhi huwa haviruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi lakini tembo wamekuwa kero kwenye vijiji hivyo, kwa mfano, Kata ya Ruaha Mbuyuni, Mahenge na Nyanzo hivi ninavyozungumza uharibifu mkubwa wa mazao umefanyika. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa tamko lolote leo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Pamoja na kufanya kazi nzuri ya kupatikana kwa wafanyakazi hewa ambao takribani wataokoa zaidi ya shilingi bilioni kumi na Serikali inapaswa ijazie hizo nafasi kutokana na watumishi wengine. Lakini walio wengi ni wale wanavyuo ambao sasa wanakwenda kuanza vyuo, lakini mpaka leo tunavyozungumza hawajapata mikopo wanahangaika. Je, kuendelea kutokuwapa mikopo hatuoni kwamba tunaweza tukazalisha hewa nyingine zaidi? Sasa Serikali iseme mpango mzima kwa nini mpaka leo mikopo ya wanafunzi baadhi hawajapata?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji pale Ilula, Wilaya ya Kilolo ni kubwa na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba anataka kuwatua akinamama ndoo kichwani, ni la muda mrefu. Je, Waziri anaweza akatoa majibu mazuri ambayo yatawafanya wananchi wa Ilula wapate moyo na kuacha sasa kuniita mimi Mwamaji badala ya Mwamoto?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa walengwa ni wakina mama ambao wengi wao bado wako Vijijini kama muuliza swali alivyosema. Lakini ukiangalia riba wanatozwa ni sawa sawa na wafanyabiashara wa kawaida na wao wanategemea kilimo. Sasa je, benki hii ili wafikie akina mama wakulima walipo maeneo tofauti na kule Kilolo inaonaje sasa ikiwapa mkopo uwe wa muda mrefu badala ya kuwapa kama wafanyabiashara ndogo ndogo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hali ya Wilaya ya Tarime kule Rorya inafahamika, kesi ni nyingi na zinachukua muda mrefu kuamuliwa na hivyo, kuwatia hasira watu wa Rorya, kama ambavyo tunajua.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuongeza watumishi wengi zaidi ili kesi ziende haraka? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyoko Rorya yanafanana kabisa na yaliyoko Kilolo na kwa kuwa Kilolo ni Wilaya ambayo imeanzishwa toka mwaka 2000, lakini haina Mahakama yoyote.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa kuanzisha Mahakama ya Wilaya kwa kuwa kesi nyingi za Wilaya ya Kilolo mnajua hasira zao huwa zinaishia wapi ili waanzishe haraka?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa fedha hizi ambazo zimekuwa zikipelekwa katika Halmashauri ni kidogo sana kiasi kwamba hata hazitoi msaada mkubwa kwa wale vijana. Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna ubaya gani kama vijana hawa ambao walio wengi hawana ajira hasa wale wanaotoka kwenye vyuo vikuu na sehemu nyingine wakaanzishiwa Benki ya Vijana ambayo itakuwa rahisi kui-control na kuwapata wale wahitaji ambao kwa kweli wanataka kutumia hizo fedha vizuri hasa sehemu kama za Kilolo na hasa hapa kwake Dodoma, je, atakuwa tayari?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo imeanza toka mwaka 2002 takribani sasa ni miaka 15, lakini kwa muda mrefu OCD amekuwa akikaa tarafa nyingine na makao makuu yako Tarafa nyingine na inabidi kuwasafirisha mahabusu kwani wako kule anakokaa OCD zaidi ya kilomita 100 kuwapeleka katika tarafa nyingine ya Kilolo. Kama Serikali yenyewe bado haijajiweka vizuri, kwa nini isitumie National Housing au NSSF kujenga nyumba pale Kilolo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali langu dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kilimo cha mvua ni kilimo ambacho hakitegemewi; sasa hivi kilimo cha uhakika ni umwagiliaji; na kwa kuwa, katika Wilaya ya Kilolo kuna maeneo ambayo tayari mabwawa yalishachimbwa kwa muda mrefu, lakini yanashindwa kusaidia wananchi kwa sababu ya ongezeko la watu; sehemu za Nyanzwa, Ruaha Mbuyuni na Mahenge. Je, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa, ni ahadi ya muda mrefu ya kuboresha mabwawa hayo, atakuwa tayari kufika na kuona ili katika bajeti hii aweze kutenga fedha ili kuboresha mabwawa hayo ili yaweze kulisha wananchi wengi wa Tanzania tuondokane na njaa?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa naamini kabisa wapo watu kutoka EPZ ambao walikuwa wanafuatilia jambo hili na kwa mara ya mwisho shamba hili lilifutwa miaka mitano iliyopita, kwa hiyo jambo hili lilikufa. Lakini kutokana na jitihada za Mkuu wetu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi limefufuliwa. Sasa Mheshimiwa huoni kuna haja sasa ya wewe mwenyewe kufika na kujionea; kwasababu, katika Mkoa wa Iringa sehemu pekee ambayo tumeitenga ni sehemu ambayo wananchi waliitoa au tulinyang‟anya mashamba kutoka kwa watu wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawayatumii. Sasa huoni kuna haja yaw ewe Mheshimiwa Waziri, na kwa kuwa, umesoma Tosa Maganga, ukafika ukaona hili jambo? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, kiashiria kimojawapo cha ujio wa viwanda ni pamoja na EPZ na mambo mengine, na ili viwanda viendelee, ili upate viwanda ambavyo unaimba kila siku na kuvizungumzia vizuri unahitaji uwe na miundombinu ya barabara, maji na umeme; na ukichukulia kwamba katika Mkoa wa Iringa sehemu pekee ni Kilolo ambayo ina sifa hizo, lakini haina miundombinu ya barabara, maji wala haina umeme wa kutosha. Sasa je, huoni kuna haja ya wewe na Mawaziri wenzio mkakaa mkaangalia uwezekano wa kuboresha miundombinu, hasa katika Wilaya ya Kilolo katika barabara za Rang‟ang‟ange, Kidabaga, Mwatasi na sehemu nyingine?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii inafanya, naomba niulize swali dogo tu la nyongeza. Niliwahi kuuliza hili swali kwamba kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ndiyo wilaya pekee ambayo maji mengi yanayojaza Kihansi yanatoka kule ambayo ndiyo yanasaidia kupelekea kuleta umeme nchi hii. Je, Kilolo inanufaikaje sasa? Naomba kwa nafasi hii atueleze hapa wananchi wa Kilolo watanufaika vipi ili kuhakikisha wanapata umeme.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa
Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nianze kwanza kwa kuishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha
watu wa Kilolo kwa ujenzi wa hospitali. Pamoja na hiyo, Mheshimiwa Waziri, itachukua muda mrefu hiyo hospitali kuweza kuisha. Lakini tatizo ambalo lipo ni kwamba Wagonjwa inabidi wapelekwe Kituo cha Afya Kidabaga ambacho hakijakamilika, hakina wodi ya watoto, wodi ya wazazi wala upasuaji, lakini inabidi sasa wasafirishwe waende
kwenye hospitali ambayo iko zaidi ya kilometa 120. Tatizo hakuna gari Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hiyo utatusaidiaje ilituweze either kukarabatiwa vizuri kituo cha Kidabaga au tupate gari?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyokiri Mheshimiwa Waziri, sheria hii ni ya muda mrefu lakini imekuwa ikikinzana
sana na baadhi ya mila, desturi za makabila na baadhi ya sheria za dini ambazo baadhi ya makabila na sheria za dini zinatambua mtoto wa kike hata akiwa na miaka kumi akishavunja ungo ni mtu mzima. Hivyo, haioni sasa hiyo pia ilikuwa ni kichocheo kikubwa cha watoto wadogo kuolewa kabla ya wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sheria hii ya ndoa imechelewa na kusababisha ongezeko kubwa
la ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto wa mitaani kuongezeka, sasa Serikali haioni kwa kuwa Katiba bado itachukua muda, sheria hiyo iletwe hapa ili tuifanyie marekebisho?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini swali langu hasa lilikuwa linahusu upande wa umeme. Naomba niulize maswali mawili madogo, kwa kuwa Waziri wa Nishati yuko hapa kama ataona anaweza kumsaidia basi anaweza akajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ambalonalielekeza Wizara ya Maji; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Kilolo kuna vyanzo vingi vya maji, lakini sasa hivi wakulima walio wengi walikuwa wanategemea sana vilimo vya mabondeni, kwa lugha ya kwetu tunaita vinyungu ambavyo ndiyo vimewapelekea kuwasomesha watoto zao na kuendesha maisha ya kila siku lakini sasa hivi wamezuiwa. Kwa kuwa Serikali ilipokuwa inazuia ukataji wa miti ilihamasisha watu watumie umeme na kupunguza bei ya gesi sasa Serikali imezuia watu wasilime kwenye vyanzo vya maji, Wizara imejipangaje ili kuhakikisha wale wananchi wanaendelea kupata fedha kwa kutumia kilimo cha vinyungu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nilitegemea ningejibiwa na watu wa umeme, kwamba kwa kuwa vyanzo vingi vimekwenda Kihansi na Kihansi ndiyo inatoa maji wananchi wa Kilolo wananufaika vipi kwa sababu wametumia muda mwingi kutunza vyanzo vile? Naomba maswali yangu yajibiwe.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa tatizo ambalo lipo kule Mufindi linafanana kabisa na kule Kilolo; barabara nyingi za Kilolo zimekuwa zikiahidiwa na hasa na Mheshimiwa Waziri. Sasa je, ni hatua gani ambazo inapaswa tuchukue endapo Mheshimiwa Waziri ameahidi kwa upande wa Serikali lakini utekelezaji haujafanyika?
MHE.VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nimpe pongezi kubwa kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia pale Kilolo kwa ujenzi wa hospitali, ni kilio cha muda mrefu. Pamoja na hayo, bado shida ipo, tuna tatizo kubwa sana la wagonjwa ambao inabidi waende kutibiwa kwenye Kituo cha Kidabaga lakini kituo kile kiko mbali na kata kama Idete, Masisiwe, Boma la Ng’ombe na Kata nyingine. Tatizo ni kwamba hakipo sawasawa kwa sababu hakuna daktari, hakuna chumba cha upasuaji, hakuna wodi ya akina mama wala hakuna ambulance. Sasa kwa wakati huu tunaposubiria ile hospitali, unasemaje?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali.
Kwa kuwa ukiangalia shule nyingi zilizoungua, chanzo kikuu huwa ni vibatari au mshumaa, hii ni kwa sababu ya kukosekana kwa umeme; kwa kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwamba kila sehemu yenye taasisi kama shule na sehemu nyingine muhimu umeme upite, lakini mpaka leo baadhi ya sehemu wamekosa haki hiyo ya kupelekewa umeme. Je, Serikali inasemaje?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji kwenye Wilaya ya Kilolo ni kubwa na kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ina utajiri mkubwa wa mito na vyanzo vya maji; na kwa kuwa tayari kuna utekelezaji mkubwa wa mradi wa maji ambao uliahidiwa na Mheshimiwa Rais ambao Wizara hii inafanya; je, kwa maeneo yale mengine ambayo tumekuwa tukipigia kelele kwa mfano Ruaha Mbunyuni, Wambingeto na sehemu nyingine, Waziri anasemaje? Ni pamoja na kuja kutembelea miradi hiyo ambacho ndicho kilio cha muda mrefu cha wananchi; Serikali inasemaje?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali ambalo nimeshawahi kuliuza leo ni mara ya tatu, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nilishawahi kuishauri Serikali kwamba moja ya sababu kubwa ambayo inasababisha timu yetu ya Taifa kutokufanya vizuri ni utitiri wa wachezaji wa kigeni kwenye nchi yetu na tulipoanza kwanza walikuwa wanaruhusiwa wachezaji watatu, baadae wakaongeza wakwa watano, leo ni saba. Sasa tunategemea Taifa Stars itafanya vizuri? Ningeshauri Serikali wapunguze idadi ya wachezaji wa kigeni abaki moja au wawili kwa sababu sisi tuna wachezaji wetu. (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Bunge lilishawahi kutunga sheria ya kutenga fedha kutoka kwenye michezo ya kubahatisha kwenda kusaidia michezo ni kwa nini basi hizo fedha zimekuwa hazipelekwi ili kusaidia michezo maana sasa hivi ni sawasawa unakwenda benki kuchukua fedha wakati hujaweka pesa, usitegemee kama utapata. Naomba majibu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu wa Rufiji na sehemu nyingine ambapo gesi hiyo itapita ni watu ambao wanasubiria kwa hamu jambo hilo. Bado hawajapata elimu ya kutosha kujua umuhimu wa jambo hilo kwenye maeneo yao. Sasa Serikali itakuwa tayari kupita kutoa elimu ya kutosha, hasa mashuleni, ili wananchi kazi hiyo itakapoanza ya kupitisha gesi waone kwamba ile ni rasilimali yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi sasa walio wengi wanategemea gesi ikianza kutoka kwa wingi na tumepewa taarifa kwamba, kuna gesi ambayo inaweza ikatumika kwenye magari. Anatuambiaje Mheshimiwa tujue kwamba unafuu wa kutumia gesi ama petroli kutakuwa kuna tofauti kubwa?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa REA III tayari umeanza na vijiji vingi vimepimwa, lakini sasa hivi kuna baadhi ya vijiji ambavyo vilisahaulika na baadaye tukaleta kuomba tena viingizwe.
Sasa Serikali inatuambiaje hasa katika Wilaya ya Kilolo, je, vijiji ambavyo vilisahaulika vitaongezwa?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ambayo yanatofautiana na swali langu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimkumbushe kidogo Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Milima ya Uluguru wanakaa Waluguru, Milima ya Usambaa wanakaa Wasambaa wanaotoka Tanga na Milima ya Udzungwa wanakaa Wadzungwa na Udzungwa iko Wilaya ya Kilolo kwa asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu nililopewa hapa, inaonekana kwamba Kilolo wanapewa kama hisani, siyo haki yao. Kwa hiyo, ninachoomba kwa kuwa tayari yalikuwepo makubaliano ya kuhamisha Makao Makuu ya Udzungwa kwenye Kilolo Udekwa, lifanyike ili wananchi wale wanufaike kwamba ile Udzungwa ni ya Wadzungwa siyo ya Waluguru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mara nyingi yamekuwa yakitokea maafa, kwa mfano vijiji vya Msosa, Ikula, Ruaha Mbuyuni, Mahenge na Mtandika wananchi wanauawa na tembo bila kulipwa fidia; na fidia ambayo wanalipwa ni fedha ndogo sana, ni pamoja na uharibufu wa mazao yao.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutunga au kuja kuleta hapa tubadilishe sheria ili wananchi hawa wawe na thamani zaidi ya wanyama ambao ndiyo wanawaua? (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ambayo ina matatizo makubwa sana ya miundombinu na kupelekea usafiri wa magari usiwepo, kwa hiyo, mawasiliano pekee tuliyokuwa tunategemea, ni simu.
Sasa kuna vijiji ambavyo havina kabisa mawasiliano na hivyo kupelekea watu kupata shida na hata kupoteza maisha. Kwa mfano, Masisiwe, Ilambo, Magana, Mdaila, Kising’a, Masege na Uruti, hakuna kabisa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu unawaambiaje watu wa Kilolo?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza nianze kuwapa pole wananchi wa Kilolo ambao wameunguliwa na shule ya wazazi kule Ukumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize swali langu moja, kwa kuwa wananchi wa Kilolo moja ya zao kubwa wanalolitegemea ni misitu, tumehamasisha na inasaidia kutunza mazingira. Pia kwa njia ya misitu wanapata mbao ambazo zimesaidia kwa kiwango kikubwa sana kujenga majengo ambayo yamesababisha ofisi nyingi kuhamia Dodoma haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo lipo sasa ni kwamba wale wananchi wameanza kunyanyasika kusafirisha mbao, watu wa TFS (Wakala wa Misitu) wanawasumbua, TRA wanawasumbua kiasi kwamba wananchi sasa wako tayari kuacha kupasua mbao. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kwenda kukaa na watu wa TRA kule ili tatizo hili liishe na wananchi wa Kilolo waendelee kufanya biashara zao?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali. Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa askari katika baadhi ya sehemu na askari wengi sana kwa maana ya traffic wako barabaran, je, Serikali sasa haioni imefikia wakati wa kuweza kupata kamera au teknolojia nyingine badala ya kutumia askari ambao kwa kweli utendaji wao hauna tija. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda naomba usikilize vizuri kwa sababu ni kiwanda hicho. Kwa kuwa ligi bora duniani ni Uingereza na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa kigeni kuliko ligi nyingine lakini timu ya Taifa ya Uingereza ni moja ya timu mbovu ambazo zinashindwa kufanya vizuri kwa kuwa ina wageni wengi. Ligi bora katika Afrika Mashariki ni Tanzania, lakini kwa kuwa inawachezaji wengi wa kigeni timu ya Taifa imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Kwa kuwa mwaka 2000 wakati tukiwa hatuna wachezaji wengi wa kigeni timu yetu ilifikia rank ya kimataifa ya 65 na leo tumeongeza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni tumefikia kwenye rank ya 139. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuendelea kuruhusu wachezaji wengi wa kigeni ni kuua timu yetu ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanuni za TTF ziko wazi ili timu ishiriki Ligi Kuu lazima iwe na kiwanja, ikate bima kwa ajili ya wachezaji wake na iwe na timu ya under 20 vyote hivyo vinakiukwa. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nia kubwa ya kugawa maeneo ni kusogeza huduma kwa wananchi na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri baada ya sisi wananchi wa Kilolo kupige kelele kutokana na ukubwa wa Wilaya yetu, uliridhia na kutupa Halmashauri ya Mji Mdogo sasa ni muda mrefu na ulifika na kuona kwamba sasa tunastahili kupata Halmashauri kamili. Je, ni lini sasa Mheshimiwa? Hebu tupe jibu ili wananchi wakusikie.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa katika kuhimiza ujenzi wa Vituo vya Afya, kumetokea tatizo kubwa sasa hivi ambalo linakabili vituo ambavyo vimekwisha; ni upungufu wa watoa dawa za usingizi. Kwa hiyo, nataka nijue tu, kwa kuwa Vituo vya Afya vingi vitajengwa katika nchi yetu, Serikali
imejipangaje?
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji katika Wilaya ya Kilolo hasa sehemu za Ilula Mheshimiwa Waziri analifahamu na ameahidi mara nyingi kufika pale, sasa hivi mradi umeanza kwa sababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Je, atuambie leo ni lini atakwenda pale kuona ule mradi ambao ni ahadi ya Mheshimiwa Rais unaendelea vizuri na unakwisha? (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa naomba niulize swali moja. Kwa kuwa, miradi ya maji imekuwa ikisumbua sehemu nyingi hata Wilaya ya Kilolo imekuwa haiishi vizuri na kwa kuwa kuna watu wanaitwa Wakandarasi Washauri wamekuwa wakilipwa pesa kwa ajiili ya kushauri miradi yetu ili iende vizuri pale inapokuwa imeharibika wanachukuliwa hatua gani hawa Wakandarasi Washauri?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

View All MP's