Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Supplementary Questions
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na takwimu nzuri za Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu matukio ya uporaji kwa watu wanaotoka kuchukua fedha tasilimu benki, ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea hivi sasa na kwa kuwa kuna imani na minong‟ono miongoni mwa wananchi kwamba watumishi na wafanyakazi wa benki kwa namna fulani wanahusika na kuwezesha uhalifu huu. Serikali inatoa kauli gani kuhusu imani hiyo na minong‟ono ya Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya matukio ya uporaji wa pesa, watu wanavyotoka kuchukua pesa tasilimu benki yanahusisha matumizi ya pikipiki na kwa kuwa pikipiki zinatoa ajira halali kwa vijana wa bodaboda, lakini wachache wanatumia kuichafua na kuumiza Watanzania. Serikali inasema nini kuhusu kushindwa kwake kuwadhibiti hao wachache ambao wanatumia vibaya vyombo vya usafiri ambavyo vinatoa ajira na masilahi mengine kwa Watanzania katika kudhibiti hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yenye kuakisi nia ya Wizara na Serikali kushirikiana nasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la msingi, imeelezwa vizuri kabisa kwamba uvunjifu wa amani ni moja ya matokeo hasi ya kukosekana kwa fursa hizi za wananchi wa Mavota kushiriki kwenye uchumi uliowazunguka. Kwa sababu suala la uvunjifu wa amani si suala la kusuburi, ni la haraka, je, Serikali na Wizara iko tayari kutoa kauli inayothibitisha uharaka wao katika kuja kuzungumza na wananchi wa Mavota?
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wakandarasi wa REA wanalalamika hawajalipwa pesa mpaka juzi na hili linaweza kuathiri uanzaji wa Awamu ya III kwa sababu shughuli ya Awamu ya II haijakamilika, Serikali inatoa kauli gani?
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja; eneo la Karukwete lina wachimbaji wadogo na lipo jirani kabisa na Kijiji cha Busiri kinachazungumziwa kwenye swali la msingi. Waziri yupo tayari kulijumuisha kwenye mkakati wa kuwawezesha kielimu na uwezeshaji?
Swali la pili; naomba kujua orodha ya mambo ya kiuwezeshaji yatakayofanyika kwa wananchi wa Karukwete na Busiri na lini tutawenda kuzungumza nao kuwafahamisha? Nashukuru sana.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ipo ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati akiomba kura kwa wananchi wa Biharamuro ya kujenga barabara kilometa 4 - 5 kwa kiwango cha lami kwenye Mji wa Biharamuro. Naomba kufahamu kutoka Serikalini kwamba utekelezaji wa ahadi hiyo umefikia wapi? Ahsante
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa idadi ya karibu vifo 12,000 vilivyosababishwa na ajali za barabarani kwa miaka hiyo mitatu vinaweza kulinganishwa na mauaji ya kimbari, mauaji ya halaiki, na majeruhi 44,444 ni sawa na kiwanda cha kutengeneza Watanzania kupata ulemavu wa viungo mbalimbali. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kuja na suluhisho lenye mashiko na kutatua tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ajali za barabarani hasa za mabasi ya abiria zinashiriki sana kwenye kutengeneza vifo na majeruhi, tena kwa kiwango kikubwa kwa mara moja, Je, Serikali ina mkakati gani pia kudhibiti ajali za barabarani zinazohusisha mabasi ya abiria?
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inashiriki kwenye mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Taifa, lakini iko haja ya kutafuta namna ambavyo Wilaya na Halmashauri ambazo zinapakana na nchi jirani zinazoshiriki kwenye Jumuiya hii kuzitumia fursa ambazo wigo wake unaishia kwenye Wilaya zinazopakana na nchi hizo.
Kwa kuwa Biharamulo inapakana na Rwanda kijiografia na kimiundombinu; na kwa kuwa wananchi wa Biharamulo kwa kushirikiana na Mbunge wao wameshazitambua fursa lakini wanahitaji nguvu ya kidiplomasia ya ngazi ya kitaifa kuhakikisha tunazichukua; je, Waziri yuko tayari kuleta nguvu ya uchumi wa kidiplomasia Biharamulo kuzungumza nasi ili tuzitumie?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi akiwa pamoja na wataalamu wa diplomasia ya uchumi kutoka Wizara yake ili tukae na wataalam wa Biharamulo tuzitumie fursa hizo? Ahsante.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kazi ya kuboresha miundombinu ya maji kwenye Mji wa Biharamulo imefikia kwenye upembuzi yakinifu kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini hatua ya kupata fedha bado iko mbali; na kwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji ni dharura sasa hivi Biharamulo, wananchi wanapata maji kwa wiki moja katika wiki nne. Kwa hiyo wiki moja yanapatikana wiki tatu hayapatikani. Je, Naibu Waziri au Waziri wako tayari kuambatana na mimi twende kufanya tathmini ili kuona namna ya kutatua hali ya dharura wakati tunasubiri mradi mkubwa ufikie wakati wake?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kusikia pia kauli ya Serikali kuhusu pia wachimbaji wadogo wa Biharamulo wakiwemo wa Busiri, Kalukwete, Mavota, Kalenge na wale Nyanchimba Wilaya Chato kwa sababu nao wanapenda kusikia kauli ya kutengewa hekta kadhaa 500, 600 kama ilivyofanyika kwenye maeneo ya Geita.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ipo ahadi pia ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mji wa Biharamulo ya kuweka kilometa nne za lami wakati akituomba kura. Kwa kuwa sisi habari ya kilometa nne haina mambo makubwa yanayojumuisha mpaka habari ya vivuko kwenye Ziwa Victoria, Naibu Waziri anatuambia nini kuhusu utekelezaji wa haraka na wa siku za karibuni wa ujenzi huo wa ahadi ya Rais?
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwanza ni amani yangu kwamba wataalamu waliopelekwa kutoa ushauri wa kupelekwa Wilayani Chato ila wamepeleka Wilayani Biharamulo.
Pili maelezo kidogo tatizo hili limekuwepo kwa miaka mingi na tumekuwa tunapata majibu mara nyingi kutoka Serikalini ambayo kwa kweli hayajaweza kukidhi kulingana na ukubwa wa tatizo. Tulisikia swali la kisera kuelekea kwa Waziri Mkuu mwezi wa saba likapelekea kiti chako Mheshimiwa Naibu Spika kutoa maelekezo kwamba Serikali ichukue hatua na ilete majibu hapa.
Sasa swali langu kwa sababu hali halisi inaonesha kabisa kwamba tatizo hili ili likabiliwe kuna mambo matatu lazima yafanyike la kwanza utafiti ili kuja tatizo ni nini ambalo tayari...
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kufanya kikao maalum na Wabunge wa Mkoa wa Kagera ili tuone namna gani tunaweka mikakati ya kutafuta utashi wa kisiasa wa kukabili tatizo hili, lakini namna ya kutafuta na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi na hata private sector ndani ya Tanzania ili tukabiliane na tatizo hili? Kama uko tayari, upo tayari kwa muda wa karibuni, muda wa kati au muda wa mbali?
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Upo ushahidi wa matumizi yasiyo sahihi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa viongozi wa Serikali na miongoni mwetu Wabunge. Kwa sababu Bunge na viongozi wa Serikali ni miongoni mwa makundi ya jamii na taasisi zenye wajibu wa juu kabisa wa kulinda lugha hii na kwamba inaashiria tatizo hili haliko kwenye vyombo vya habari tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inasema nini kuhusu upana wa tatizo hili hasa kwa wakati huu ambapo inatengeneza sera hiyo?
Pili, kwa sababu matumizi, kwa mfano ya neno “hichi” badala ya “hiki,” “nyimbo hii” badala ya “wimbo huu,” uchanganyaji wa lugha ya Kiingereza kwa kiwango kilichokithiri kwenye sentensi za Kiswahili, vinakera. Tunaomba kujua ni lini sera hii inakuja kudhibiti hali hii inayoendelea? Nakushukuru.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa mujibu wa takwimu tulizopewa kwenye majibu na Mheshimiwa Waziri, asilimia 80 ya waendesha bodaboda hawana leseni, jambo ambalo linawafanya waishi kwenye mzunguko wa kukimbizana na polisi badala ya kuzalisha mali kwa ajili kujenga uchumi wao na uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari kuwasaidia kwa kuwawekea ruzuku ya kupunguza walau kwa mara moja kodi ya kulipia leseni angalau kwa nusu ili waweze kupata leseni kama hatua ya kwanza ya kuwasaidia ili tuweze kushirikiana nao kuongelea habari ya kuwahamisha kuwapeleka kwenye ushirika wa SACCOS na mambo mengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi twende Biharamulo kuziona fursa nyingine zaidi ya kuwaomba tu wajiunge kwenye SACCOS ambazo Serikali Kuu ikishirikiana na sisi tunaweza kuzitumia kuwatoa kwenye yale waliyonayo ili Biharamulo iwe mfano wa kusambaza hatua kama hiyo maeneo mengine ili kundi kubwa la bodaboda nchini tulisaidie liwe la ujasiriamali kweli kweli? Ahsante.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba kufahamu kwamba kwa maelekezo hayo ambayo Serikali imeyatoa kwa waajiri kutekeleza upandishwaji wa madaraja hayo.
Je, Serikali iko tayari sasa kuratibu suala hilo ili kuhakikisha kwamba tunafanya uhakiki wa walimu wote wenye malalamiko haya ili yapatiwe utatuzi.
Swali la pili, kwa sababu pia yako malalamiko kutoka kwenye Halmashauri zetu kwamba Walimu wanapokwenda kujiendeleza unatokea upungufu wa Walimu kwenye shule wanazotoka.
Je, Serikali iko tayari kutumia vizuri fursa ya Chuo Kikuu Huria ili yenyewe kwa ngazi ya Serikali Kuu iratibu namna ya kuwasaidia Walimu wajiendeleze kwa kupitia Chuo Kikuu Huria bila kuathiri uwepo wao kwenye shule zao? Ninakushukuru.
HE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naishukuru Serikali kwa majibu yake, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja natambua jitihada za Serikali za kuweka mfumo kwa ajili ya kuwafikia walemavu, lakini suala la mfumo ni moja na suala la kufikisha huduma wanazohitaji kwa maana ya kuwafanyia upendeleo chanya (positive discrimination) ni lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kwa namna gani Serikali sasa imeweza kuwafikishia rasilimali fedha na rasilimali mafunzo watu wenye ulemavu kwenye vikundi vyao, tofauti na kuwajumuisha kwenye vikundi vingine ambapo mahitaji yao mahususi hayawezi kutimizwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa namna gani na kwa kiwango gani Serikali inadhani inaweza kuwapatia nafuu kwenye yale mambo ya msingi kwa mfano Bima ya Afya. Tuchukulie mfano mlemavu wa ngozi akipata ruzuku kwenye bima ya afya una uhakika wa kuhakikisha anakingwa kwa bima, kitu ambacho anakihitaji kama Watanzania wengine lakini yeye anakihitaji zaidi? Nakushukuru sana.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's