Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Innocent Sebba Bilakwate

Supplementary Questions
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri lakini sijaridhika na majibu yake. Niliuliza ni lini masoko haya yatafufuliwa kwa sababu haya masoko ni muhimu kwa ajili ya wananchi wa Kyerwa na Waziri mwenyewe anajua wananchi wa Kyerwa wanapata shida hawana mahali pa kupeleka mazao yao. Naomba anieleze ni lini masoko haya yatafufuliwa yaanze kujengwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba Naibu Waziri awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa na Watanzania ambao wananufaika na masoko haya, je, Serikali imetenga pesa kwenye Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya masoko haya kukamilika?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati yupo kwenye kampeni aliahidi kuondoa tozo mbalimbali ambazo zinamdidimiza mkulima wa kahawa. Mpaka sasa Serikali bado haijaondoa hizo tozo. Je, Serikali ipo tayari kuwaruhusu wananchi wale wanaolima kahawa waweze kuuza kahawa sehemu nyingine ambapo watapata bei nzuri?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hizi pesa ni za wananchi ambao ni maskini na zimekaa muda mrefu bila kupata hiyo mikopo. Je, Serikali iko tayari kurejesha hizo pesa au kuongeza riba kwa sababu hizi pesa zimekaa muda mrefu na hawa wananchi hawajapata jibu na hili tatizo limekuwepo Karagwe pamoja na Kyerwa. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza sijaridhika na majibu ambayo amenipa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu kusema hii barabara inapitika kila wakati si kweli! Barabara hii mwaka wa jana mzima ilikuwa ni barabara mbovu imejaa mashimo, magari yote yanayopita barabara ile yanaharibika sana. Kwa hiyo, kuna taarifa ambazo wamekuwa wakiletewa ambazo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza; je, yuko tayari yeye mwenyewe binafsi kwenda kuitembelea barabara ile na kuiona ili aone umuhimu wake kwa sababu taarifa ambazo wamekuwa wanaletewa sio za kweli?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Rais akiwa pale Nkwenda kwenye kampeni aliiona barabara ile ikiwa na umuhimu kwa kuwa barabara hii inapita katikati ya Wilaya. Aliahidi kutupa kilometa 20 akiingia tu madarakani. Hizo kilometa 20 zinaanza kujengwa lini? Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mheshimiwa Waziri naomba nikuulize swali; barabara ya Mgakolongo kwenda Kigarama mpaka Mlongo upembuzi ulishafanyika muda mrefu na wananchi wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwasababu walishawekewa “X”. Barabara hii ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la maji katika Jimbo la Kyerwa ni kubwa sana na wananchi wake hawapati maji, hata asilimia 20 haifiki: Je, Serikali inawaahidi wananchi wa Jimbo la Kyerwa kama alivyojibu, “upembuzi yakinifu unaoendelea utakapokamilika mwaka 2017/2018;” Serikali inaahidi kutenga pesa ya kutosha kwa ajili ya kukamilisha mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ili miradi hii iweze kusimamiwa vizuri, ni vizuri tukawa na wataalam. Wilaya yangu ya Kyerwa hatuna wataalam wa kutosha, lakini wataalam wenyewe hao waliopo hawana vitendea kazi kama gari na vifaa vingine. Je, Serikali ipo tayari kutuletea wataalam wa kutosha na vitendea kazi ili kazi isimamiwe vizuri?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lilivyo swali la msingi, kwa zao la kahawa na migomba kuna ugonjwa uitwao mnyauko kwa jina lingine unaitwa ugonjwa wa manjano. Ugonjwa huu umeshambulia migomba pamoja na kahawa. Je, Serikali imefanya utafiti upi ili kulipatia ufumbuzi zao hili lisije likapotea?
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika utendaji wao wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Lwakajunju, imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana zaidi ya miaka 15. Kwa maana hiyo tumewaahidi sana akina mama wa Karagwe na wananchi kuwatua ndoo kichwani kwa muda mrefu sana. Kama unavyojua akina mama ule muda ambao wanautumia kwenda kuchota maji umbali mrefu ndio muda huo huo ungeutumia kufanya kazi za maendeleo. Sasa swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri naomba unipe comfort, je,huu mradi wa Lwakajunju utatekelezwa lini? Ni lini wananchi wa Karagwe watapata hii huduma ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za kibajeti za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, je, Wizara ipo tayari kushirikianan na Halmashauri kuhakikisha fedha ambapo tunahitaji kwa ajili ya kuchimba mabwawa katika Kata za Kanoni, Igulwa Ihanda, Chonyonyo na Nyakahanga zinapatikana ili wananchi wapate huduma ya maji?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kweli nasikitika sana kuona majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri. Hii ni mara yangu ya pili namwuliza hili swali. Mara ya kwanza alinijibu hapahapa Bungeni, akasema kabla ya mwezi wa Sita barabara hii itakuwa imeanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, anapotujibu siyo kuwajibu Wabunge kuwafurahisha, haya ni majibu ambayo tunakuja kuuliza kwa ajili ya wananchi wetu. Naomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu ambayo ni ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; ni lini barabara hii ujenzi utaanza? Kwa sababu hii barabara ni ya muda mrefu tangu kipindi cha Mheshimiwa Rais Mkapa amestaafu; amekuja Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, sasa anakuja Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, je, imetengwa pesa kwa ajili ya ujenzi huu kuanza na wananchi wapewe fidia?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ya mwaka huu hakutupatia pesa kwa ajili ya mradi mkubwa ambao uko kwenye usanifu. Naomba awaeleze wananchi wa Jimbo la Kyerwa, mradi huu utakapokuwa umekamilika kwa ajili ya usanifu.
Je, yuko tayari kuhakikisha anawapatia wananchi wa Jimbo la Kyerwa maji safi na salama kwa sababu maji ni tatizo Wilaya ya Kyerwa?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwa Redio ya Taifa haisikiki katika Wilaya ya Kyerwa na wananchi hao wanapofungua redio wanapata Redio ya Rwanda na Uganda kitu ambacho kimewafanya wananchi hawa kuonekana kama wametengwa kwa sababu hawawezi kupata taarifa ambazo ni muhimu zinazohusu Taifa lao.
Je Serikali haioni kuwa wananchi hawa wamekosa haki yao ya msingi ya kupata habari za Serikali hasa hasa kutoka kwa viongozi wao kama Mheshimiwa Rais anapokuwa anaongea na viongozi wengine? Hata mimi Mheshimiwa Mbunge ninapokuwa Bungeni nawawakilisha, hawa wananchi hawapati taarifa yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za dharura ili wananchi hawa waweze kupata taarifa ya Redio ya Taifa kwa sababu wanakosa hii haki ya msingi? Laini hata Televisheni ya Taifa haisikiki wala haionekani vizuri. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu miradi hii ni ya muda mrefu na miundombinu yake inazidi kuharibika kama vile vifaa ambayo viko pale kuna kama nondo na vifaa vingine vinazidi kuharibika, kwa sababu Serikali imeshatenga pesa kwenye bajeti ya 2017/2018, kwa nini Serikali isichukue hatua za dharura kupeleka pesa hii ili iweze kukamilisha miradi hii kwa sababu ya umuhimu wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale kwenye miradi ile kuna walinzi ambao walikuwa wamewekwa pale, walinzi hao wametelekezwa muda mrefu na imefikia wakati hao walinzi wameondoka, pale hakuna walinzi. Serikali haioni pasipokuwa na walinzi inaweza ikasababisha vifaa vingine kuibiwa na kuharibu miundombinu ya mahali pale?
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kama lilivyo swali la msingi, kwenye Jimbo langu la Kyerwa, wananchi wameanzisha vituo ambavyo wameshaanza ujenzi, wamefika kwenye kumalizia boma. Kwa mfano, kama Kata yangu ya Kimuri, kuna wananchi ambao wamejenga boma limefikia kwenye lenta na wameweza kujenga maboma zaidi ya kumi. Maboma haya yamekaa karibu miaka saba. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha maboma haya? (Makofi)

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's