Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Selemani Moshi Kakoso

Supplementary Questions
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo lipo kwenye maeneo mengi katika nchi yetu ni miradi ya maji ambayo Serikali ilianzisha kushindwa kutekelezwa. Jimboni kwangu kuna miradi ya maji katika Kijiji cha Majalila na Igagala na imeanza kufanyiwa kazi na imefikia asilimia 70. Sasa hivi miundombinu ya miradi ile imeanza kuharibika kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ile miradi ambayo kimsingi ingewasaidia wananchi kwenye maeneo hayo?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ambayo Serikali imetoa ya hatua ya awali ya ujenzi wa hospitali ya Mkoa.
Swali langu la msingi nimeuliza kwa kuwa, hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ndiyo iliyobeba uzito wa kuhudumia takribani wagonjwa zaidi ya laki tano wanaotumia bajeti ya Halmashauti ya Wilaya ya Mpanda, ni lini Serikali itaharakisha mchakato wa ujenzi huo wa hospitali ya Mkoa ili kuepusha Halmashauri ya Mpanda inayotumia bajeti ya Halmashauri kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wengi kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuisaidia hospitali hii ili iweze kukidhi mahitaji kwa sasa?
Lakini swali la piliā€¦
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili naomba kuweka uzito, tunavyo vituo vya afya ambavyo kama vingeimarishwa vingesaidia sana uzito wa hii hospitali ambayo imeelemewa. Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vituo vya afya ambavyo vipo katika Mkoa wa Katavi, hususani vile vya Karema, Mwese na Mishamu, napenda kujua hayo.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya mpya ambayo ina Jimbo moja tu la Uchaguzi la Mpanda Vijijini. Eneo hili la kiutawala ni kubwa mno, lina uwezo wa kutoa mgawanyo wa halmashauri mbili, kwa maana ya Ukanda wa Ziwa, Halmashauri ya Karema na ukanda wa huku juu eneo la makazi mapya ya Mishamo. Je, ni lini Serikali itafikiria kutoa mamlaka ya kugawa maeneo haya, ili yaweze kuwasaidia wananchi wa Mpanda kwa ujumla?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mpanda Vijijini lina miradi miwili ya umwagiliaji. Mradi wa kwanza ni ule wa Karema ambao Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo lakini bado haujakamilika na mradi wa pili ni ule wa Mwamapuli ambao unamwagilia vijiji vya Kabage. Miradi yote hiyo haijaweza kukamilika kwa wakati. Je, ni lini Serikali inaweza kukamilisha miradi hiyo ili iweze kuwasaidia wananchi ili kutopata hasara kwa fedha za Serikali ambazo zimeshatumika?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali ilitumia fedha nyingi sana kujenga gati la Karema, fedha hizo ambazo zilipotea na kilichojengwa pale ni nyumba moja ambayo haijakamilika na kuna choo ndicho ambacho kilikamilka; lakini fedha zilizotolewa na Serikali ni nyingi sana:-
Je, wale walioisababishia Serikali hasara kubwa sana ya fedha nyingi, mmewachukulia hatua gani ambazo ni za kisheria?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, mradi wa ORIO ulikuwepo toka mradi wa umeme vijijini Phase II ambao ulihusisha vijiji vitano, vya Kabungu, Ifukutwa, Igalula na Majalila. Mradi huu ulikwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha, Serikali ilishindwa kuwekeza fedha ambazo zinge-support kampuni ya ORIO. Je, Serikali ina majibu yapi sahihi ambayo yatawezesha miradi hii iweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nilikuwa nataka kufahamu uwiano wa miradi hii ya umeme vijijini. Yapo maeneo mengine ambayo sasa hivi yana asilimia mpaka 80, yamepata miradi hii, maeneo mangine bado hayajakuwa na fedha zinazopelekwa kwenye maeneo husika kama Jimbo la Mpanda Vijijini. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya mgawanyo wa fedha zinazofadhili Mradi wa Umeme Vijijini?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi hasa ya WMA imekuwa ya muda mrefu katika nchi yetu. Jimboni kwangu vipo vijiji ambavyo vina migogoro ya WMA wakati vijiji hivyo ardhi hiyo ni mali yao, lakini kumekuwa na tatizo la wakulima kusumbuliwa, kufukuzwa, kuchomewa nyumba kwenye maeneo yao. Je, ni lini Serikali itakomesha tabia hii ya kuwachomea wananchi kwenye Vijiji husika vya Kabage, Sibwesa, Kapanga na eneo la Kagobole?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Vituo vya Afya vya Mwese, Karema na Mishamo ni vituo ambavyo vinahudumia wananchi wengi kwenye Jimbo la Mpanda Vijijini. Vituo hivi havina huduma ya kimsingi ya wataalam na hasa suala zima la ambulance. Naomba kujua, Mheshimiwa Naibu Waziri atavisaidia vipi hivi vituo vya afya ambavyo vinahitaji huduma ya Serikali ili kuokoa maisha ya wananchi kwenye Jimbo hilo?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mpanda Vijijini ni jimbo ambalo lina kata 16, kati ya hizo tatu tu ndizo ambazo zina vituo vya afya. Napenda kumuuliza swali Naibu Waziri, ni lini itajenga vituo vya afya katika Kata ya Mnyagala, Kasekese, Mpanda Ndogo, Tongwe, Bulamata, Ilangu, Ipwaga na Katuma?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua barabara ya kutoka Mpanda kwenda Mkoa wa Kigoma ni barabara ambayo imeahidiwa na Serikali kujengwa kwa kiwango cha lami na tayari kuna kilomita 30 kutoka Mpanda Mjini mpaka eneo la Usimbili Vikonge, limeshafanyiwa upembuzi yakinifu. Swali kwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itaanza mchakato wa kuijenga barabara hii?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema ni kituo ambacho kimekamilishwa ujenzi na Serikali lakini tatizo kituo hicho hakina umeme ili kiweze kufanya kazi. Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kukamilisha kituo hicho ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Tarafa ya Karema?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kuhudumia miradi ya maendeleo ya maji katika Kijiji cha Igagala na Kijiji cha Majalila ambacho ni Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Tanganyika. Serikali ilipotoa hizo fedha usimamizi wa mradi huu haukwenda sahihi. Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia miradi ambayo tayari fedha ilikuwa imetengwa na wafanyakazi ambao ni wasimamizi wamesababisha hasara ya kutokukamilika kwa mradi?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Namuuliza swali Naibu Waziri, alipokuja Mpanda alituhakikishia wananchi wanaoishi vijiji vya Kabungu, Mchakamchaka, Ifukutwa na Majalila ambako ni Makao Makuu ya Wilaya kwamba ataleta umeme ifikapo mwezi wa tisa. Je, ni lini Serikali itathibitisha kauli yake ambayo aliitoa yeye mwenyewe alipofika huko?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali na kwa kiwango kidogo kitakachozalishwa mwaka huu:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la ukosefu wa classifiers ambao wanafanya msimu wa zao kuwa mrefu sana? Ni lini Serikali itakuja na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuajiri classifiers ambao watasaidia kutatua tatizo la tumbaku?
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wakati Jumuiya inaanzishwa maeneo haya yalikuwa na kijiji kimoja tu cha Sibwesa, lakini leo hii kuna vijiji zaidi ya sita na kata mbili zimeanzishwa kwenye maeneo hayo na Serikali inatambua maeneo hayo ya kiutawala. Je, ni lini Serikali kupitia Wizara wataenda ku-review mipaka hiyo ambayo ipo inayoleta migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo hayo ili kuondoa shida inayosababisha wananchi kupigwa mara kwa mara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati Jumuiya inaanzishwa ilikuwa na malengo mazuri ya kiuchumi ambayo kwa sasa hayapo na wananchi hawajanufaika na mradi wowote ule ulioanzisha Jumuiya hiyo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaachia hayo maeneo ili yaendelezwe na vijiji vyenyewe husika?
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya maji ya Tabora ni sawa sawa na matatizo ya maji ya Mkoa wa Kagera hasa Bukoba Mjini. Kwa sasa hivi ukame umechukua muda mrefu mito mingi imekauka. Je, ni lini Serikali itatuweka kwenye Mpango wa Ziwa Victoria angalau hizi kata zilizoko karibu na Bukoba Mjini zipate maji?

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Dr. Thomas D. Kashililah

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's