Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza kabisa naomba nipongeze hotuba ya Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na naomba nichangie maeneo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Wizara yenyewe ya Katiba na Sheria. Wizara hii sasa imekuwa kubwa ina taasisi kama tano ndani yake ambazo zina uwezo wa kufanya kazi zake kwa kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Tume ya Kurekebisha Sheria. Tume hii inafanya kazi nyingi, inaleta marekebisho mengi ya Katiba na Sheria, lakini Tume hii inaonekana kazi zake hazifanyiwi kazi kwa wakati.
Naomba niende kwenye Sheria ya Vijiji kuhusu ardhi sheria ya mwaka 1999 Na. 5. Sheria hii ya Ardhi ilipitisha Hati za Kimila lakini kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika maeneo yetu, tunaomba sheria hii irekebishwe hata ikiwezekana Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wapewe nakala halisi kwa kufanya mikutano ya hadhara kuwaelimisha wananchi ili kuondoa mgongano kati ya Wenyeviti wa Vijiji na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi imetumika vibaya. Tangu Vijiji kugawiwa kwa wananchi, Operesheni Vijiji wananchi walipewa maeneo, lakini inavyoonekana hao wawekezaji, wahifadhi walikuja baada ya vijiji kugawiwa, leo hii inaonekana wananchi katika maeneo yale hawatakiwi kukaa pale wanaoneka wamevamia maeneo. tunajiuliza, nani alikuwa mkaaji wa kwanza katika hii ardhi kati ya mwekezaji na mwananchi. Tunaomba sheria hii irekebishwe ili kuondoa mgongano, wananchi wetu waishi kwa amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika eneo la tozo za kodi ya ardhi na nyumba. Kumekuwa na tabia mwananchi wa kawaida amejenga nyumba yake ya kawaida ya nyasi yuko kwenye Halmashauri ya Mji, hana elimu yoyote kuhusu kukuza Mji wala plan ya Mji, lakini mwananchi huyu pamoja na kuishi kwenye nyumba ya nyasi analipishwa shilingi 2,000 na kiwanja chake kama cha ardhi anakilipia, tunaomba hizi sheria zirekebishwe, zinatuletea matatizo, kumekuwa na manungā€˜uniko makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo la Mahakama. Mahakama nyingi za Mwanzo hazifanani na mahakama na hata wanaoingia humo hawafanani na majengo halisi. Miundombinu ya mahakama ni michafu, mahakama imekuwa ni mbovu, majengo yanataka kuanguka. Pia hata miundombinu ya vyoo, hakuna vyoo kabisa, maeneo mengi wanahifadhi mahabusu zaidi ya 60 wanatumia choo kimoja, jinsia ya kiume na ya kike, hapa tunahifadhi maradhi na sisi tunasema adui mkubwa ni maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende eneo la utawala. Kumekuwa na mgongano mkubwa sana hususani kwa Babati TC, mgongano huu unatokana na DC anaingilia mamlaka ya Kibunge, DC huyo amekuwa kero kwa Mbunge wa Babati Mjini. Tunaomba DC aelekezwe mipaka yake ya ki-DC.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Sheria ya Ndoa aliyozungumzia dada yangu Kiteto, lakini naomba niende kwenye magereza. Hali ya magereza yetu ni mbovu na ni mbaya. Kwanza kuna mrundikano wa mahabusu, pili hawapati lishe nzuri, hasa kwenye mahakama zenye vitengo vya watoto. Kumekuwa na vitendo vya kikatili wanafanyiwa wale watoto, tunaomba mahakama za watoto zitengewe eneo lake peke yake, sheria hii iwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la ajira; Kumekuwa na matatizo mengi katika eneo la ajira, vijana wengi hawaajiriwi, wanamaliza vyuo lakini kumekuwa na dana dana nyingi. Tunaomba hizi sheria zote zirekebishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende katika eneo la Sheria ya Walaji na Watumiaji. Kumekuwa na matatizo ya hapa na pale katika matumizi ya vyakula tunavyokula hasa vinavyotoka nje ya nchi. Hata hivyo kumekuwa na tabia ya TFDA kwenda kwenye maduka ya wale wanaouza bidhaa za vyakula. Unakuta bidhaa ina- expire mwaka 2016 mwezi wa sita, lakini hilo kontena limepita wapi? Utashangaa TFDA wanakuja kuvamia maduka ya watu wanatoa vyombo, wanachoma na wanatoza faini. Lakini tunajiuliza hili kontena limepita wapi? Sheria hii haiko sawa tunaomba hawa wa TFDA watueleze na Waziri mwenye dhamana ashughulike na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo la uvunjaji wa sheria na haki za binadamu. Mwaka jana tumetoka kwenye uchaguzi, tumefanya uchaguzi vizuri lakini tarehe 26 kulitokea na tukio kwa upande wa Upinzani. Vijana wetu walikamatwa, kompyuta zao zilichukuliwa kisa tu wanakusanya matokeo. Huu ni uvunjaji wa haki za binadamu, halafu bado tunasema hii haki tunaitumia. Haki hapa haijatumika! Vijana hawa wamebambikiwa kesi, bado tunalia tunasema haki imetendeka!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa kumalizia. Ni hatari sana kuanzisha familia ambayo uwezi kuitunza. Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, tumeona Bajeti ya Tume ya Haki za Binadamu, bajeti hii hairidhishi hata kwa mtu wa kawaida unaona ni jinsi gani hii Tume haihitajiki katika Serikali hii.
Mheshimiwa Waziri, Fungu namba 55 tunahaja ya kulishikilia, huwezi kubeba mzigo mzito ambao huwezi kuutekeleza! Tume hii inafanya kazi nyingi, Kazi nyingi zinaletwa kwenye Wizara husika lakini kazi hizi zinazimwa kwa sababu maalum. Sasa kwa nini hii Tume mmeiweka? Tume hii kwenye bajeti yake haina maeneo mengine zaidi ya OC, sasa kama ina OC na hawana jengo wanapangisha wana kazi gani ya kulipwa mishahara? Kwa kazi ipi wanayofanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema posho ya Wazee wa Mahakama. Wazee wa Mahakama wanalipwa shilingi 5,000; wanahudhuria mahakamani mwezi mzima halafu bado Serikali inawakopa! Tunaomba muwalipe hawa wazee na ikiwezekana wazee hawa wapandishiwe posho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia eneo linguine ni eneo la haki za wazee. Ahsante, siungi hoja mkono.