Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika na Bunge lako Tukufu, nishukuru kupata tena nafasi hii kuweza kuhitimisha hoja hii ambayo imeleta sijui niite malumbano au utata mkubwa sana au mjadala mkubwa ndiyo Kiswahili hicho, mimi Mpare kwa hiyo Kiswahili wakati mwingine inakuwa shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, muhtasari wa kuhitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Kamati, jumla yao walikuwa Wabunge kama 11 waliochangia kwa kuzungumza hapa ndani ya Bunge. Sijapata michango yoyote kwa maandishi na nadhani labda haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na wajumbe ambazo kwa ujumla wake zote zimelenga kuboresha usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Mashirika ya Umma. Nikianza na wenzangu tuliokuwa nao kwenye Kamati na kutengeneza ripoti hii Mheshimiwa Kiswaga amezungumzia kuhusu miradi ya NSSF na viashiria vya ubadhirifu katika miradi hiyo. Nakubaliana naye ni muhimu kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina kwa watu wote waliohusika na manunuzi haya ya ardhi na kuchukua hatua stahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kiula ameongelea suala la tofauti ya shilingi trilioni 1.5 na kubainisha kuwa ni kweli kulikuwa na changamoto za takwimu katika suala hilo wakati ukaguzi unakamilika. Kama mapendekezo ya Kamati yalivyofafanua, tumependekeza kuongeza nguvu zaidi katika utunzaji wa kumbukumbu na wafanyakazi wenye weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ameongelea suala la mikopo ya matrekta ya SUMA JKT. Kamati inasisitiza kuwa madeni haya yalipwe na viongozi wa Serikali waliokopa matrekta hayo waonyeshe mfano kwa kulipa madeni hayo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ali Salim ameongelea kuhusu kuboreshwa kwa mfumo wa Hazina wa utunzaji wa taarifa za hesabu. Amesisitiza kuwa uhamisho wa fedha ufanyike kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Stanslaus Mabula ameongelea kuhusu suala la uwezo wa kibajeti wa CAG. Ni kweli kwa mwaka huu CAG amefanikiwa kukamilisha kazi ya ukaguzi wa wakati. Aidha, amesisitiza kuwa watuhumiwa wa suala la malipo ya ration kwa watu wasiokuwa askari ni lazima wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe aliongelea kuhusu suala la over released funds from the Consolidated Fund to some votes. Naomba kufafanua tu suala hilo kwa ufupi, kufuatia mabadiliko ya mzunguko wa bajeti hapo awali, uhamisho wa bajeti uliandaliwa baada ya kufungwa mwaka wa fedha na kuletwa Bungeni wakati Bunge likiendelea hadi mwezi Agosti. Baada ya mzunguko wa bajeti kubadilika, taarifa za uhamisho wa bajeti zimekuwa zikiandaliwa mapema ili kuwasilishwa kabla ya mkutano wa bajeti kukamilika tarehe 30 Juni kila mwaka. Hivyo Hazina imekuwa ikisitisha maombi ya uhamisho wa fedha kila ifikapo tarehe 15 Juni ya kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, panapokuwa na mahitaji maalum baada ya tarehe hiyo, maombi hayo hupokelewa na taarifa yake hutolewa katika taarifa ya mwisho wa mwaka. Kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 na mzunguko mpana wa bajeti, taarifa za uhamisho wa fedha hutolewa kila baada ya utekelezaji wa bajeti wa kipindi cha nusu mwaka. Kutokana na majibu hayo, baada ya uhakiki wa CAG kukamilika, hapakuwa na fedha zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa kwenye mafungu husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Felister Bura amesisitiza kuhusu tofauti iliyokuwa imejitokeza hapo awali kwenye tofauti ya makusanyo na fedha zilizotolewa. Nakubaliana naye kuwa ni muhimu Serikali ikaendelea kuchukua hatua kwa watu ambao wanahusika na miradi isiyokuwa na tija. Ametolea mfano hatua zilizochukuliwa NSSF kwa Wakurugenzi waliokuwepo hapo awali. Kamati inaendelea kusisitiza kuwa ni muhimu hatua zaidi zikachukuliwa NSSF hasa kwenye suala la miradi ya ununuzi ya ardhi ambayo imeonyesha kutokuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Khadija Nassir amezungumza kuhusu ushauri ambao umekuwa ukitolewa na Kamati. Katika hili nipenda kuishauri Serikali kutekeleza ushauri wa Kamati na Maazimio ya Bunge kwa wakati. Haipendezi Maazimio ya Bunge kutolewa kwa zaidi ya mwaka mmoja bila ya kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Anatropia ameongelea suala la uweledi wa watumishi katika Wizara ya Fedha na Mipango. Jambo hili tumelilisitiza kuwa ni muhimu likaangaliwa kwa makini, ni sahihi kuwa maboresho ya mifumo iliyopo Hazina ni lazima iendane na kuongeza weledi wa watumishi ili kumbukumbu za Mfuko Mkuu ziwe sahihi na Mheshimiwa Omari Kigua amejaribu tu kufafanua kwamba kumekuwa na mikanganyo ya kutumia MS Excel pamoja mifumo mingine. Hata hivyo ni kweli CAG aligusia kwamba kuna taarifa ambazo zilitengenezwa kwa kutumia excel na kwa ajili hiyo ndiyo maana hata kwenye Kamati kulikuwa na hoja kwamba je hizi taarifa nyingine ambazo zilitumika kwa kutumia excel ni za kuaminika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine tena namshukuru Mheshimiwa Spika kwa uongozi wake dhabiti nakushukuru pia wewe binafsi kwa uongozi wa Bunge letu, nawashukuru wajumbe wenzangu wa Kamati kwa ushirikiano wao mkubwa hadi kukamilika kwa taarifa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu kuwa Serikali itazingatia kwa ukamilifu uchambuzi wa Kamati na kutekeleza mapendekezo ya Kamati. Nipende kuchukua nafasi hii kusema kwamba Bunge lako limeshuhudia mapendekezo yalitolewa mara ya mwisho mwaka jana kipindi kama hiki manne yote ambayo ni muhimu sana hayajafanyiwa kazi. Sasa hapo ni wazi kwamba wale wahusika wote ni kama wamedharau Bunge, maana wasingekuwa wamelidharau Bunge wangeweza kuleta angalau taaarifa ya kuonyesha kwamba wamefikia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipende kusema kwamba hapa kumetokea majadiliano mazito kutokana na fedha hii ya trilioni 1.5, kwa mtu aliyeko nje ni rahisi aone kwamba kuna kitu kinafichwa katika hela hii. Pamoja na kwamba tumesikia pande zote zinazosema kuna tatizo na zile zinazosema hazina tatizo, nipende kusema kwa kipindi kinachokuja wakati CAG atakapofanya ukaguzi ni vyema akapitia kwa undani suala hili pamoja na matatizo mengine ambayo yametokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili kwa nini? Ni kwa sababu kwanza hii halikuja kama hoja haikuwa imekuja kama hoja kwa hiyo hata sisi kwenye Kamati tulipata shida sana kwamba tunalibebaje wakati halikujaa kama hoja. Lakini sasa tunaona muda mwingi Bunge limechukua katika kuzungumzia hili trilioni 1.5 kwa maana hiyo ni kwamba hata Mheshimiwa Rais unakumbuka mwaka jana alimuuliza CAG kwamba je, hii hela imeibiwa? Na akaendelea kusema kama ingekuwa imeibiwa ningechukua hatua kali sana kwa wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naamini Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli huko aliko akisikia hii mijadala lazima aingie na mashaka kwamba kulikoni nitaangalia vile vifungu vyote vya taarifa yetu ambavyo vimeonesha kwamba Hazina walikubali kwamba kuna sehemu ambayo wamekosea wakakiri. Kwa maana hiyo ni kwamba kuna maeneo ambayo hayajatendewa haki. (Makofi)

Kama ukiongelea masuala yaliyoleta utata limetokana na mfumo swali ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanaweza kujiuliza wa pande zote mbili kama mfumo una matatizo je, taarifa zilizokuja inawezekana zisiwe na matatizo? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unapoongelea mfumo unaongelea kwamba huo mfumo na CAG amesisitiza hata sisi kwenye Kamati tumezungumzia mifumo unaweza ukatupa taarifa zisizo sahihi, ndiyo maana nasema CAG atakapofanya ukaguzi kipindi kinachokuja na kwa vile Hazina wamesema wanaweka mfumo bora basi atuletee taarifa maalum ya kuonesha kwamba mifumo imekaaje na je, mfumo wa awali umetuleta taarifa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu weledi wa CAG amezungumza kwa urefu sana jinsi ambavyo alipata taarifa kwa shida ukiangalia taarifa inaonyesha akitaka taarifa hii inachukua muda sansa kupata majibu, wale wafanyakazi watakwenda huko watakaa muda mrefu bila kuleta taarifa kwa wakati, kwa maana hiyo hii ina maana gani ni kwamba Hazina haijawa-well organized, ama wafanyakazi lingine wanaloweza kufanya pia by profession ni administrator ni kwamba kunawezekana kuna wafanyakazi wengi wapya ambao hawakufanyiwa mafunzo ya kuweza kuweka taarifa vizuri kiasi kwamba ukitafuta taarifa huipati. (Makofi)

Kwa hiyo ndiyo maana pamoja na kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kweli kuna wabobezi kwenye mahesabu, lakini pia ikubalike kwamba kama hakuna utaratibu mzuri wa kuweka taarifa haiwezi kuleta tija katika sehemu kubwa au katika jicho la nchi ya Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo ndiyo tulisema hata wakati itakapofanyiwa ukaguzi tutahitaji CAG atueleze kuhusu utata huu wa kutopata taarifa kwa wakati aliohuitaji kwamba alichukua muda mrefu katika hii verification kupata documents imetokana na nini? Je, ni uzembe ule ule wa kimfumo? Je, ni uzembe wa wafanyakazi? Je, ni kwamba hapakuwa na mafunzo ya kuelimisha wale wapya walioingia jinsi ya kuweka taarifa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo twende kusema kwamba hapa wote tukubali maana siye tunaongea kama Bunge na wananchi wanatusikiliza sana na hatupo katika ushabiki wa vyama, na mimi kama Mwenyekiti wa PAC nipende kusema tunapenda popote walipo wananchi wetu waelewe kwamba Bunge liko serious kutokana na haya ambayo yanateandeka au ambayo yameonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo tusichukulie kisiasa tukazungumzia juu juu kwamba suala hili limefungwa lazima tunapoona suala limeleta utata mkubwa tuangalie kwanza aulize kwa nini hapakuwa na hoja ya CAG ili verification hii ambayo imefanywa na mfumo au mifumo ambayo ina utata je imeleta taarifa sahihi? Kwa hiyo nipende kusema kwamba naomba Bunge lako likubali kwamba wakati CAG atakapofanya ukaguzi unaokuja atuangalizie haya masuala ambayo yamefikisha Bunge lako kuwa na discussion kubwa kwenye trilioni 1.5 ambayo kwanza haikuwa hoja, lakini mfumo na weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona matatizo mengi ya fedha ambayo yamechukuliwa kwenye mashirika ambayo tungechukua muda mwingi pia kuangalia hao wote waliochukua fedha nyingi hivyo na bado wapo wengine kwenye kazi, hao waliochukua mikopo ambao bado wapo Serikalini na ambao wamestaafu. Imekuwaje kuwe na kigugumizi cha kuchukua hatua stahiki, kwa nini Benki ambazo zinatumia fedha za umma waoe kigugumizi kuchukulia watu hatua ambao ni wadaiwa sugu wakati benki zetu nyingine za biashara hawatoi mwanya kama huo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nategemea Bunge lako lizamie katika sehemu hii ambapo kuna pesa nyingi inapotea na ujue kwamba hii ripoti iliyokuja ni ndogo tu ya sehemu kubwa ya tatizo kubwa ambalo tungekwenda maradi hadi mradi kuanzia NSSF na mashirika yote mngeona matrilion ambayo yamepotea. Kwa hiyo, tusingezungumzia tena trilioni 1.5 kwa uzito huo ukilinganilisha na hizi zinazopotea katika miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe kwamba Bunge lako lijalo kama ni semina tupatiwe semina ya kwamba hizi taarifa tunazichambuaje kwa uweledi tutakapokwenda kivyama tutapoteza mwelekeo na utashi wa Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwamba baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja sasa kwamba Bunge likubali mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali PAC ili yawe Maazimio ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.