Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi kidogo nataka nianze kwa historia. Katika ukuaji wa lugha matendo huzaa nomino. Enzi hizo wakati mimi niko mdogo kulikuwa kuna Mwanamuziki mmoja anaitwa Mbaraka Mwishehe na mwingine alikuwa anaitwa Juma Kilaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Juma Kilaza alikuwa ni mtu mwenye majigambo sana, yaani yeye kila kitu anajua, anajifanya anajua kuimba muziki. Sasa wakasema tukate mzizi wa fitna, wakaweka pambano. Baada ya kuweka pambano la muziki, Mbaraka Mwishehe akaonesha shamra shamra zake, Juma Kilaza akaonyesha udhaifu wake. Kuanzia siku hiyo, mtu yeyote ambaye alikuwa hajui akawa anaitwa Kilaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo miaka ya nyuma wakati niko mdogo Ubunge Jimbo la Temeke kuna mtu mmoja Lamwai na mwingine alikuwa anaitwa Kihiyo. Wakagombea, baada ya kugombea Mheshimiwa Kihiyo aliweka vyeti feki, Lamwai akaenda Mahakamani kuweka pingamizi. Baada ya kuthibitisha yule mtu kuwa vile vyeti alifoji akang’olewa Ubunge, kwa hiyo tangu siku hiyo mtu ambaye hajasoma alikuwa anaitwa Kihiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudi sasa hivi. Rais wa TFF juzi alisema kwa sababu katika nchi ameshaonekana mtu mbishi sana ambaye anajifanya anajua sana lakini hajui, hakubali chochote, akatoa mfano wa Mheshimiwa Tundu Lissu akasema kuwa msilete Utundulisu kwa sababu ya matendo yake huo ndio ukuaji wa lugha haizuiliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa, jana ilizuka mijadala miwili humu ndani, mwisho alimalizia Mheshimiwa Joseph Selasini kwa kuomba Mheshimiwa Rais aingilie kati suala la Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Ester Matiko. Nataka nimwambie Rais wangu mimi bado kijana mdogo sana, asije akaingia kwenye huu mtego hata wakimfuata kwa kuburuza magoti. CHADEMA ndio wamekuwa wakizunguka dunia nzima kusema Rais hafuati Katiba..

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Hansard yako ya jana isomwe, nataka nimpe taarifa sijawahi mimi kusimama katika Bunge hili kumwomba Mheshimiwa Rais aingilie kati suala la Mheshimiwa Mbowe na Matiko. Kwa hiyo, naomba mzungumzaji aweke kumbukumbu zake sahihi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga futa jina la Selasini, endelea.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kujua kama wanawajali au hawawajali. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitamkwa humu Bungeni, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Rais hawa ndio wanaozunguka dunia nzima…(Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mlinga wewe sema tu nafuta jina la Mheshimiwa Selasini ili tuendelee.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Basi ili aridhike nalifuta hilo jina la Mheshimiwa Selasini, lakini message imefika. Kwa hiyo namuomba Mheshimiwa Rais aje akaingia kwenye huo mtego, kwa sababu hawa ndio wanazunguka dunia nzima kusema Rais wetu hafuati Katiba, hafuati sheria, hafuati kanuni za nchi hii, hafuati taratibu, yeye ni dikteta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nataka nizungumze kuna kitu sasa hivi watu wanazunguka duniani wanasema Tanzania hakuna freedom of expression. Wote ni shahidi, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vyombo vingi vya habari katika Bara la Afrika. Tanzania ina magazeti 216 yakiwemo ya CHADEMA. Nchi yetu ina Redio 158, nchi yetu ina TV 34 na hazijawekewa mazuio ya kuandika. Tuna Online TV 224, tuna blogs zaidi ya 60. Hivi vyote vinafanya kazi bila ya kufuatiliwa. Kwa kuthibitisha hilo tuambiwe ni Mwandishi wa Habari gani sasa hivi yuko jela, kama hakuna freedom of expression.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchora katuni mmoja anaitwa Masoud, kwa katuni anazomchora Mheshimwa Rais, ningekuwa mimi nisingemwacha, lakini yote haya yameruhusiwa watu wanafanya lakini watu wengine wanazunguka dunia nzima wanasema Tanzania hakuna freedom expression.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi anayoitolea mfano, kwa mfano mwenzetu mmoja yuko Marekani, hiyo nchi ya Marekani kuna uhuru lakini wanaweka mipaka, hata hiyo freedom of expression. Marekani freedom of expression ipo lakini usije ukaongopa, usije ukadhalilisha mtu, usije ukamsingizia mtu kitu, usije ukavuruga usalama wa nchi na kwa kuthibisha hilo kuna mtu mmoja anaitwa Edward Snowden, waulize kwa nini Marekani wanamtafuta yule pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa upande wa Mahakama. Najiuliza Mahakimu wanafanya kazi kubwa kwelikweli, wanafanya maamuzi magumu, hivi kwa nini Hakimu hapewi ulinzi, OCD anapewa ulinzi. OCD ambaye kazi yake kukamata tu mtu, lakini Hakimu kazi yake kumuhumu mtu aozee jela au anyongwe, kwa nini hapewi ulinzi. Naomba Mahakimuwapewe ulinzi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, leo kumezuka mjadala wa mwisho humu. Watu wanataka wafungwa waruhusiwe kufanya matendo ya ndoa na wake zao. Wafungwa wana haki nyingi sana na ndio maana wameitwa wafungwa. Lakini sasa tukianza kuwawekea huru, maana yake tendo la ndoa ndio tendo zito kuliko yote duniani.

Mheshimwa Mwenyekiti, wanaume sisi tunakuwa majambazi, tunaenda kuiba hela tunapokea rushwa ili tufanikiwe kupata hilo tendo kirahisi. Leo hii mfungwa ambaye amefungiwa gerezani anaambiwa aruhusiwe kufanya tendo la ndoa na mke wake au na mume wake. Hilo suala halikubaliki sisi ndio tutakuwa wa kwanza katika nchi zenye demokrasia duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.