Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naunga mkono hoja Kamati zote mbili, Kamati ya Sheria Ndogo ambayo inaongozwa na Mtemi Chenge na Kamati ya Sheria ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Mchengerwa. Kuna hoja zimejitokeza hapa zinazohusiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kwanza ni ile ambayo Waheshimiwa wa Kamati ya Sheria Ndogo wamepitia na kweli kwamba kulikuwa na upungufu katika Halmashauri zetu umetajwa, sina sababu ya kuutaja hapa. Tunaomba tuseme kwamba tumepokea maoni yenu na mapendekezo yenu tutayafanyia kazi na kuboresha ili sheria ndogo kwenye Halmashauri zetu ziendane sawasawa na sheria mama pamoja na matumizi bora ya kuboresha utawala bora katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ambalo limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge hapa ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hili jambo bado lipo kwenye mchakato hatujachelewa. Kwa kawaida mambo ya kisheria na Wanasheria wanafahamu, Mheshimiwa Salome Makamba alikuwa anachangia hapa, ni kwamba jambo hili limeanza mchakato wa kuangalia uchaguzi uliopita, upungufu ambao ulijitokeza, malalamiko yaliyotolewa na wananchi na wagombea waliokuwa wanagombea nafasi mbalimbali, wakiwemo wagombea wa Uenyekiti wa Mtaa mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yamepokelewa na wataalam wetu katika Ofisi ya TAMISEMI yatarudishwa kwenye Halmashauri zetu, yatakuja kwenye vyama vya siasa, tutapokea maoni, kwa hiyo jambo hili mtashirikishwa vizuri. Tumeanza kufanyia maboresho maoni ya 2014 ambayo pia watu walitoa. Kwa hiyo ni jambo ambalo bado liko kwenye mikono salama, naomba mwendelee kutupa imani yenu, tutatoa ushirikiano hakuna tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu. Tumezungumza kodi ya majengo, hili jambo ni kweli wakati yametolewa maekelezo ya kukusanya kodi ya majengo, yamekuja maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani na Halmashauri na wadau mbalimbali na wananchi wenyewe na hasa wafanyabiashara ambao kimsingi wanalipa kodi kwa Watanzania jambo limechukuliwa na Serikali ambayo ni sikivu ya Chama cha Mapinduzi, limefanyika kwenye mchakato, yatakuja maboresho humu na Waheshimiwa Wabunge mtapata nafasi ya kutoa maoni yenu ili tufanye maboresho ya namna bora ya kusimamia kodi ya majengo bila kuleta kero na malalamiko kwa wananchi wetu. Hili jambo nilitaka niliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo limezungumzwa hapa, kuna Mbunge mmoja amezungumza anasema kuna mjumbe wa NEC alikuwa anasemwa huko mtaani kwamba sijui nilikwenda kwenye Mkutano fulani nikitaka watu wampinge Tundu Lissu. Naomba niseme kwamba, Tundu Lissu mke wake ni Mkurya anaitwa Robi, ameoa Nyarero pale nyumbani, kwa hiyo ni shemeji yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili, nataka niseme msimamo wangu ni kwamba, Tundu Lissu ana maumivu, alipatwa na tatizo na watu wote walimpa pole na sio kumwambia hadharani, lakini sasa baada ya kupata madhara hayo amegeuza machungu yake yawe machungu ya Watanzania, hatuwezi kukubali. Machungu ya mtu mmoja, hayawezi kugeuzwa machungu ya Taifa. Savimbi sio lazima awe na mandevu, unaweza ukawa Savimbi kwa matendo yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yanayofanyika duniani. Huyu ni Mtanzania, angerudi hapa Tanzania aeleze machungu yake, maumivu yake, tumsikilize, tumsaidie kulia. Ameamua kwenda ughaibuni, anamtukana Rais wa nchi, anasema Rais wetu ambaye ni Daktari, ni msomi wa hesabu kama mimi, wa hesabu na kemia, eti Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli hawezi kutunga hata sentensi moja ya Kiingereza, sio kweli this is very unfair, hizo haki mnazozungumza sijui mnatoa wapi? Hamwezi kuwa na haki ya kusema muonewe wenyewe huruma lakini haki ya kutukana wenzenu, kuwadhalilisha watu wazima na familia zao, hilo halikubaliki na haliwezi kuungwa mkono, ni very unfair. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika maelezo anasema, anapaka matope Taifa ili Serikali ianguke, amesema wakati anahojiwa Ai…International Study of Africa, nimemsikiliza, anasema yeye anapaka matope Taifa ili akirudi hapa asikilizwe, apate uongozi na Serikali ianguke, huyu atakuwa ni mhaini, anataka kuiangusha Serikali, anaipaka matope Tanzania, misaada ambayo inakuja hapa, Watanzania wa Singida, watu wa Mara, Wagogo, makabila yote, wanawake, wazee na vijana wananufaika, leo mnazungumza habari ya maji hapa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndio mambo ambayo hatuwezi kuyakubali yakafanyike. Tumeshasema kama kuna mtu ameonewa katika Taifa aseme, tutasimama upande wake kumtetea.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …lakini
sio anageuza mambo yake binafsi, mtu ambaye anatetea tumbo lake…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …halafu anageuza tena tuzungumze kama ya Taifa, haiwezekani…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Kwa mambo ambayo Mheshimiwa Tundu Lissu anayafanya Watanzania wasimame na watambue…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msigwa, kaa chini.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Watambue wazalendo ni wapi, wanafiki ni wapi, wasaliti ni wapi. Tanzania ni ya kwetu, una jambo lako rudi Tanzania, tukae pamoja, tujadiliane, tupange mipango yetu, uongozi wa nchi hii utatolewa na Watanzania, uongozi wa nchi hii hutakabidhiwa Ulaya, tutakupa sisi Watanzania kwa muda tutakaotaka. (Makofi/Vigelegele)