Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ANDREW J. CHENGE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuhitimisha hoja yangu. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia hoja ya Kamati hii lakini baadhi yao hasa wale Wajumbe wa Kamati yenyewe; Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mheshimiwa Salome Makamba na wameelezea vizuri. Yupo Mheshimiwa Mnzava sikujua ni mwanasheria huyu, alielezea vizuri sana, namshukuru sana. Mheshimiwa Dkt. Kolimba na Mheshimiwa Mukasa, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nifanye sahihisho moja, limetumika neno Kamati ya Sheria Ndogo Ndogo, hii siyo Kamati ya Sheria Ndogo Ndogo ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. Tuelewane, hizi ni sheria za nchi wala siyo sheria ndogo ndogo, ni sheria kabisa zinazotokana na mamlaka ya Kikatiba ambapo Bunge linapoona inafaa kukasimu, linakasimu madaraka yake. Kupitia Kamati hii ndiyo linachungulia kudhibiti yale ambayo limekasimu kuona kama yamekaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumesema sheria hizi zinapotungwa na mamlaka inayokasimiwa zinaanza kutumika kabla ya kuwasilishwa humu Bungeni. Ndiyo maana busara ya Spika kwamba tuwahishe Kamati hii iwe inatoa taarifa zake mapema ili kusaidia kutoonea wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunakoelekea bado nashauri ni vyema tukaangalia utaratibu huu wa Sheria Ndogo kuanza kutumika zinapochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, hiyo ndiyo hoja na inazungumzika. Ndani ya nchi za Jumuiya ya Madola baadhi ya nchi zimebadilisha utaratibu ambao Tanzania tunautumia lakini nasema kwa sasa huo ndiyo utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa nichukue muda mrefu, matokeo ya uchambuzi wa kazi tuliyofanya kwa mwaka mzima mnayaona kwenye taarifa pamoja na lile jedwali. Tumeelezea changamoto ambazo zipo, ni kama tano, tunaiachia Serikali ione namna gani tunavyoweza kuzipunguza. Zipo zile za wazi kabisa, hii ya ku-copy tu Sheria Ndogo za Halmashauri fulani bila hata kuzamia, nadhani hapa ni suala la kutokuwa makini tu kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme moja, Ofisi ya Waziri Mkuu hasa kupitia Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama amekuwa mtu wa karibu sana katika kuunganisha shughuli za Kamati na Serikali, yeye kama daraja na wanayaona mapema na hasa zile ambazo zinahusu Ofisi ya TAMISEMI wanawapelekea haraka sana ili wafanye masahihisho na hatimaye kuzichapisha tena na kuletwa humu Bungeni. Tunamshukuru sana kwa kazi hiyo na tutaendelea kushirikiana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hii changamoto kubwa ya uandishi wa sheria, uchache wa wataalam hawa, hili sio la Tanzania tu. Nimekulia kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu naelewa kazi nzito walizonazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa upande wa Idara ya Uandishi. Kazi hii siyo ya kila mwanasheria, kazi hii unahitaji wanasheria wanaoipenda ile kazi, wenye weledi, wanaoifahamu sheria katika mapana yake sio katika eneo dogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowapata wanasheria kama hawa, changamoto kubwa ipo namna ya kuwatunza wabaki Serikalini au kwenye taasisi za Serikali. Ni utaalam wa kipekee huu, tunao wachache lakini naishauri Serikali iendelee kuwekeza kwenye eneo hili, bado hatujafanya vizuri. Tulifanya vizuri mpaka miaka ya 1980 sasa tumeanza kuwapoteza hawa ambao tulikuwa nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zetu, TAMISEMI wajitahidi kwa kadri inavyoweza kuwanoa wanasheria walionao. Mimi najua baadhi yao wanaweza wakapata mafunzo wakaongeza weledi wao wa namna ya kuzichambua na kuziandaa hizi sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili ndilo linakasimu mamlaka yake kwa mamlaka mbalimbali, nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge shughuli ya kukasimu itaendelea tu kwa sababu Bunge haliwezi likafanya kazi zote na kutunga sheria aspect zote zikawa kwenye sheria. Tunapokubali kama Bunge kukasimu nawaombeni sana tuwe makini kwamba ile misingi ambayo tunakasimu ikatungiwe kanuni lazima tuiweke katika lugha ambayo siyo pana sana na hii ndiyo kazi ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Ofisi ya Bunge, Katibu wa Bunge katika kuwajengea uwezo Wabunge wa kuchambua Miswada, naomba hili liendelee. Serikali nayo ione uwezekano huu wa kuwajengea uwezo Wabunge wa kuchambua Miswada, tusiachie wageni kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Kamati inachambua makaratasi na yanashuka kama mvua. Siyo kazi nyepesi na inafanywa na watu ambao siyo wanasheria, mimi nawapongeza sana lakini nazidi kuiomba Ofisi ya Katibu wa Bunge waangalieni kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo kuhusu shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2018 hadi Januari, 2019 pamoja na maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.