Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa nafasi hii nami kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze kwa kunukuu maneno ya Mheshimiwa Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwahi kusema kwamba, “uhuru bila nidhamu ni wazimu.” Nadhani hata kaka yangu Mheshimiwa Mbowe analifahamu hilo kwamba tuna uhuru lakini lazima uhuru uwe na mipaka. Ndiyo maana hata wakati ule akina Mheshimiwa Kubenea walipoona kwamba wana uhuru usio na nidhamu na kuanza kuikosoa Kamati Kuu ya CHADEMA, waliitwa kwenye Kamati Kuu na wakapewa onyo kali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, japo taarifa ya CHADEMA ilionesha kwamba…

WABUNGE FULANI: Walisamehewa.

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Taarifa ya CHADEMA ilionesha kwamba walikiri kosa...

WABUNGE FULANI: Walisamehewa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vuma naomba utoke kwenye kiti chako uende upande huu, tafuta kiti pale sehemu ya kukaa, ili upate nafasi ya kuchangia vizuri kwa sababu kuna watu humu ndani huwa wanaamua kufanya fujo kama wao jambo lao haliendi sawasawa. Mheshimiwa Vuma. (Makofi)

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze upya. Nasema, nimeanza kwa kunukuu kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Aliwahi kusema, “uhuru bila nidhamu ni wazimu.” Maana yake ni kwamba hakuna uhuru usio na mipaka. Nikaenda mbele kwa kusema, hata kaka yangu Mheshimiwa Mbowe analifahamu hilo, ndiyo maana wakati ule ambapo akina Mheshimiwa Kubenea na Mheshimiwa Mzee Komu walipodhani wana uhuru usio na mipaka wakakaa kuikosoa Kamati Kuu ya CHADEMA Kamati Kuu iliwaita na kuwapa onyo kali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa iliyotoka kwa Umma ya CHADEMA ilionesha wale watu walikuwa waungwana wakakiri makosa, lakini bado walipewa jukumu la kwenda mbele ya jamii na kuomba radhi wana-CHADEMA wote. Sasa kama CAG angekuja hapa akakiri kosa akaomba radhi, labda tungefikiria. Hajawa muungwana kama walivyokuwa akina Mheshimiwa Kubenea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme, kazi ya Bunge mnavyofahamu na Waheshimiwa Wabunge tukubaliane jambo moja, tunao wajibu wa kulinda madaraka ya Bunge kwa wivu. Haiwezekani Bunge lije lichafuliwe, halafu wewe Mheshimiwa Mbunge ubaki uko salama. (Makofi)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najua kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kuisimamia Serikali na kuwakilisha wananchi. Kwenye kutunga sheria tumeona Bunge hili linatunga sheria nzuri kwa ajili ya wananchi. Mwaka 2018 tumetunga sheria ya kurekebisha Sheria ya Madini ambayo tumeona imeongeza mapato kwa Taifa letu; Bunge hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, kwenye kusimamia Serikali, mimi niko Kamati ya PIC, tunasimamia mashirika ya Umma zaidi ya mashirika 200 na tumeona mwaka 2018 kwa sababu tumekuwa tukiwapa maelekezo mazito kwa mara ya kwanza mashirika ya Umma yameanza kutoa gawio kubwa. Mwaka 2018 walitoa zaidi ya shilingi bilioni 700 na tunategemea mwaka huu watatoa zaidi ya shilingi trilioni moja. Hiyo ni kazi ya Bunge kusimamia Serikali kufanya kazi. Tunawakilisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hizo hizo na miongozo ambayo Bunge inatunga na kutoa kwa Serikali ndio imesababisha nchi inatawalika, nchi hii imekuwa nzuri. Juzi kumetoka report ya Global Peace Index ambayo inaonesha Tanzania kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni nchi ya kwanza kwa kuwa na amani, lakini ni ya saba Afrika na ya 51 duniani. Sasa anatoka mtu anakuja anasema Bunge ni dhaifu, anapata wapi mamlaka hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja. CAG ametukosea adabu, ametukosea heshima, nami naunga mkono hoja ya Kamati kwamba hatuko tayari kufanya naye kazi. Tunahitaji mtu mwingine ambaye tutakuwa tunaongea mamoja, twende pamoja kusaidia Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)