Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea na leo nitaongea kwa masikitiko makubwa sana. Masikitiko yangu ni kwamba katika Bunge hili wengine tulioingia kwa mara ya kwanza tulitegemea tujifunze sana tabia za wenzetu tuliowakuta lakini bahati mbaya tumekuta wengine ambao idhamu zao mimi mwenyewe sizifahamu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wananong’ona hapa kwamba umepita Jeshini, ni kweli. Nami nasema unapoishi katika dunia hii mambo yako yote ukiyafanya kwa nidhamu utafanikiwa lakini kama ukijihisi wewe ni mwamba katika dunia na kuwa unaamua jambo unalolitaka, siku zote utapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu tunayemzungumzia leo mimi mwenyewe nashuhudia hapa siyo mara ya kwanza hii, amekuwa na tabia hizo hizo na hataki kujirekebisha. Mimi naendelea kupata wasiwasi mmoja, mwenzetu kwa jinsia nayomfahamu hii, mwanamke, ndani ya Bunge kama hili la heshima yupo hivi, huko nje sijui yukoje? (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kuongea, haiwezekani.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MBUNGE FULANI: Ametumia lugha ya kudhalilisha.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi naomba mkae. Naomba ukae Mheshimiwa Lema nimeshakutaja mara mbili, naomba ukae. Mheshimiwa Masoud, endelea.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana watu wakichukia kwa kauli hii kwa sababu mimi nilivyolelewa na navyofahamu mama ni mlezi, ni mtu anayetakiwa kulea na awe na nidhamu, ili watoto anaowalea wawe na nidhamu lazima yeye kwanza awe na nidhamu. Leo nashangaa watu wanasikitika, mimi nasema usipokuwa na nidhamu huwezi kuheshimiwa na wewe kama utaishi hivyo unavyojiona katika dunia hii, maisha yote utapata matatizo na matatizo yanatokea kwa sababu mtu hajielewi.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ESTHER A. BULAYA: Mama Sitta yuko wapi?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, nimekataza taarifa na nadhani wewe ni shahidi, Mheshimiwa Masoud endelea.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema hili Bunge lina heshima yake iliyopewa na Taifa na sisi wenyewe tunatakiwa tujiheshimu, liwe na heshima na sisi lazima tujiheshimu.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Kuhusu utaratibu.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Tusipojiheshimu hatuwezi kuheshimiwa. Kama tunaambiwa dhaifu mtu mwingine anasimama anasema…

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, Kanuni iliyovunjwa?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 68(7) imevunjwa.

NAIBU SPIKA: Kanuni ya 68(7) inazungumzia mwongozo, umeomba kuhusu utaratibu, Mheshimiwa Masoud, endelea. (Makofi)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, bado…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbatia, Kanuni iliyovunjwa.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, natumia Kanuni ya 64(1)(f) na (g), naomba kuinukuu, inasema: “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge:-

(f) hatamsema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa Mbunge au mtu mwingine yeyote;

(g) hatatumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine”. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe tu Mbunge anayechangia aondoe yale maneno ambayo yalimdhalilisha wakati anachangia wanawake kwamba yanakuwaje, mambo ya ki-gender hapa hayapo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbatia amesimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(2) akizungumza kuhusu utaratibu. Anasema Kanuni ya 64 imevunjwa kwa sababu Mheshimiwa Kanali Masoud ametoa maneno ambayo yanaudhi ama kudhalilisha mtu mwingine.

Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Kanuni zetu hizi, maneno ambayo mimi nimeyasikia ambayo yameonyesha kuudhi baadhi ya watu nadhani ni maneno ya kuashiria tabia huko nje iko vipi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kanali Masoud maneno hayo uyafute ili yasiingie kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Na mimi nafuta maneno hayo lakini message sent. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Hata hayo ya message sent hayaingii kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyafuta na hayo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, tunamjua vizuri yule.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche umeruhusiwa na nani kuzungumza kwa kuwasha microphone? Mheshimiwa Masoud malizia mchango wako.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini narudia tu kusema kwamba kama mtu anafikiria kwamba kweli sisi tupo dhaifu basi ni yeye mwenyewe yupo dhaifu lakini siyo Bunge. Nakushukuru sana. (Makofi)