Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii iliyoko mezani inayomhusu Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Godbless Lema.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge ipo kisheria ndani ya Bunge na ipo kikanuni. Kabla ya kuanza kazi ya Kamati hii tulipewa instruments; tulipewa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2016, tulipewa Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge, lakini pia tulipewa Katiba ya nchi hii ili Kamati hii itende haki.

Mheshimiwa Spika, Kamati hii inafanya kazi kwa kanuni ya Nyongeza ya Nane, kanuni ya 4 inayotaka; na naomba kwa faida ya Bunge hili ninukuu, inasema: “Kamati ya Haki na Maadili ya Madaraka ya Bunge itatekeleza majukumu yafuatayo:-

(a) Kuchunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala yote ya haki, kinga na Madaraka ya Bunge, yatakayopelekwa kwake kwenye Kamati hii na Spika.

(b) Kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya Wabunge yatakayopelekwa na Spika.”

Mheshimiwa Spika, suala la Mheshimiwa Godbless Lema chimbuko lake lilitokana na kesi ya Mheshimiwa Profesa Assad aliyetamka maneno kuhusu dharau na kuliteremsha hadhi Bunge, akisema Bunge hili ni dhaifu. Suala hilo lilishadidiwa na Mheshimiwa Halima Mdee aliyasema pia yeye ni Mbunge mzoefu na ana hakika Bunge hili ni dhaifu. Mheshimiwa Godbless Lema alishadidia zaidi naye akasema kwamba yeye ni Mbunge mwenye vipindi viwili, naye anashadidia kwamba Bunge hii ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, kisheria Mheshimiwa Godbless Lema aliunganishwa na kesi ambayo aliikuta. Kwa hiyo, akathibitisha kwamba naye pia anafanya kosa hilo hilo kwa ushahidi alionao yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, ulimleta Mheshimiwa Godbless Lema aje athibitishe kwenye Kamati kwamba anao ushahidi wa kutosha kwamba Bunge hili ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, neno “shahidi” linatumika kwa ajili ya Wabunge wanaokuja kwenye Kamati. Shahidi huyu alipofika kwetu alithibitisha kwamba naye bado anaamini kwamba Bunge ni dhaifu. Kwa hiyo, anakiri kwamba alifanya kosa hilo na alithibitisha na bado aling’ang’ania kwamba ni kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, msemaji aliyetangulia hapa, ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika, ame-quote kifungu cha sheria ambacho hajui kwamba tulikitumia au hatukukitumia. Tunatumia sheria mara nyingi kwa watu ambao hawahusiki. Ali-quote kifungu cha 33 na ange-quote na cha 26 pia cha Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge, lakini sisi tunatumia sana kanuni hizi kwa ajili ya Wabunge ambao ni wanachama wa Bunge hili na angekwenda kwenye kifungu cha 74 kingemsaidia zaidi kupata majibu, kwa nini Mheshimiwa Lema amechukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nami kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wengine, ningependa kusoma kanuni ya 74 (4) wale wenye kanuni za Kudumu za Bunge, inasema hivi: “Bunge linaweza kuzingatia ushauri mwingine wowote utakaotolewa na Kamati ya Haki Maadili ya Madaraka ya Bunge kuhusu adhabu anayostahili kupewa Mbunge aliyekiuka masharti ya kanuni hii.

Mheshimiwa Spika, vile vile kanuni ya 74 kifungu kidogo cha (5) inasema: “bila ya kujali masharti ya fasili ya (4) ya kanuni hii, Bunge linaweza kumchukulia hatua nyingine za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi Mbunge yeyote atakayetenda kosa chini ya kanuni hii.” Kwa hiyo, kanuni aliyojielekeza Mheshimiwa Mnyika sidhani kama aliamini kwamba tuliitumia sisi.

Mheshimiwa Spika, nini maana ya kazi ya Kamati hii? Sisi katika Kamati ya Maadili, tuko pale kwa ajili ya kutumia Kanuni, kusahihishana Wabunge, kwa Wabunge ambao umewaleta wewe kwenye Kamati yetu. Hata hivyo, huyu Mheshimiwa Lema ambaye ni shahidi wa mwisho kwa suala hili, alipokuja kwetu hakuonesha hata kidogo kujutia kosa alilolifanya alithibitisha kwamba amelifanya na tulipompa nafasi ya mwisho aseme, akasema moja nawaombeni kabisa kabisa msinihurumie. Narudia, tulipompa ruhusa aseme chochote kwamba sisi tunataka kumtia katika hatia kwa sababu amevunja kanuni kwa kulidhalilisha Bunge kwamba Bunge hili ni dhaifu, akasema, naiomba Kamati hii isinionee huruma na wala isinipe msamaha. Sasa sisi tulibaki na jambo la kushangaa sana Mheshimiwa Lema tulipotaka, unamwambia Hakimu wewe Hakimu usinihurumie mimi na wala usinisamehe, wewe hukumu.

Mheshimiwa Spika, imetupa tabu sana, tukafikiria makosa ya nyuma ya Mheshimiwa Lema. Mheshimiwa Lema huyu alipoitwa mara ya kwanza kwa kudharau Bunge kule Dar es Salaam alisema naomba nikatafute Wakili na alipopewa fursa hiyo hakurudi tena. Kwa hiyo jana alipokuja alikuwa na wazo hilo kwamba naomba mnisamehe nikatafute Wakili, lakini tulipomwambia wewe unaweza kujitetea, akaongea mambo mengi sana ya kujitetea, lakini sio kujitetea ili asamehewe, ya kusema mambo mabaya kuhusu Bunge ili Bunge halina uwezo na uwezo wa Spika si, alisema maneno mengi kwenye Kamati ile na akatuma salamu tukwambie Mheshimiwa Spika kwamba unavyoendesha Bunge sio vizuri na tulivyomwambia aeleze hasemi lolote la maana akijaribu kusema kwamba mimi nathibitisha kwamba Bunge hili ni dhaifu.

Mheshimiwa Spika, Kamati ilimtia hatiani kwa adhabu ambayo azimio limeomba na mimi naunga mkono adhabu hii ya mikutano mitatu na kwa kweli Kamati ingeomba zaidi mikutano zaidi ya mitatu iliyoombwa sababu kubwa ya kumpa mikutano mitatu ni kwamba Bunge linakaribia mwisho, tumetaka awepo kwenye Mkutano wa mwisho wa Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)