Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ambayo iko mbele yetu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wa taarifa yake ya utekelezaji kwa kipindi hiki cha 2019/2020, hotuba ambayo imesheheni mambo mbalimbali ambayo yametekelezwa lakini na mwelekeo wa Serikali katika kukuza uchumi wetu na katika kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano ambao tutaumalizia mwaka kesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo anajitoa na namna ambavyo anatumikia Serikali hii lakini kwa namna ambavyo anawajali wananchi wake wa Wilaya ya Ruangwa kule Jimboni kwake. Pamoja na kwamba ana majukumu makubwa ya kitaifa lakini anapopata fursa hata ya siku moja, mbili anakimbia na kwenda kuungana na wananchi wake katika Jimbo lake la Ruangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Makamu wake wa Rais kwa namna ambavyo wanasimamia utekelezaji wa miradi mikubwa na kuona ni namna gani wanaendelea kukuza fursa za uchumi katika nchi yetu lakini kuendelea kukuza uwekezaji kwa kutekeleza hii miradi mikubwa. Tumeona namna ambavyo ujenzi na upanuzi wa barabara pamoja na madaraja makubwa ambayo yanajengwa katika kuhakikisha kwamba Watanzania tunasafiri bila matatizo yoyote kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Lindi tumebahatika kipindi kilichopita tulitenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara inayotoka Nanganga – Luchelegwa – Nachingwea - Masasi. Wananchi wa Wilaya hizi tumefarijika sana kuona kwamba tulitengewa fedha. Mpaka sasa ujenzi haujaanza napenda kujua wamekwama wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba Serikali imeendelea na ujenzi wa reli ya Standard Gauge ambayo inaendelea vizuri. Kwa speed inayokwenda nayo nina hakika kabla hatujamaliza Bunge hili na sisi tutakuwa tumeshuhudia namna ambavyo reli hizi za kisasa zinafanya kazi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pia upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam kule Tanga na Mtwara. Upanuzi huu wa bandari umetoa fursa kubwa kwa wananchi wa Mikoa hii ya Kusini kwa sababu sasa nafasi za ajira kwa vijana wetu zinaongezeka kwa kutumia bandari ya Mtwara. Si hivyo tu hata wafanyabiashara wanaouza mafuta sasa wanapata urahisi wa kupokea mafuta kutoka Mkoa huu wa Mtwara kwa sababu ya upanuzi wa bandari ile ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru pia Serikali imeendelea kuboresha kwa kujenga vituo vya afya na hospitali na kuboresha zahanati katika maeneo mbalimbali. Sisi katika Mkoa wa Lindi tumebahatika katika Majimbo yote tumepata vituo viwili viwili katika kila Jimbo na viko kwenye hatua nzuri sana na vingine viko tayari kwa ajili ya ufunguzi. Nachoiomba Serikali kufanya maandalizi sasa ya watumishi pindi vituo hivi vya afya vitakapokamilika basi tuwe na watumishi wa kutosha wa kusimamia vituo vyetu vya afya ili kuendelea kuboresha afya kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia mradi wetu wa Stigler’s Gorge. Nimebahatika kutembelea eneo la mradi wa huu, kwa fedha iliyotoka kwa hakika mradi unekwenda vizuri sana. Naomba Mheshimiwa Rais wetu asirudi nyuma katika kuhakikisha kwamba mradi huu unafanikiwa na hatimaye tuweze kuwa na umeme wa kutosha kwa sababu uwekezaji unategemea sana uwepo wa umeme katika nchi yetu. Kwa hiyo, umeme huu utakuwa ni mkombozi mkubwa sana na uwekezaji utakuwa ni mkubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kuipongeza Serikali, kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa ujasiri ambao ameuonesha katika ununuzi wa ndege, maana sasa tunapata heshima kubwa katika nchi yetu kumiliki ndege zetu wenyewe. Hilo ni jambo la faraja sana, ni jambo jema katika kukuza uchumi na kuendelea kuimarisha uwekezaji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie katika Mkoa wetu wa Lindi. Katika Mkoa wetu wa Lindi sasa tumefungua fursa za uwekezaji. Kwa hiyo, ninaomba sana ushirikiano na Serikali kuhakikisha kwamba eneo hili la uwekezaji katika Mkoa wetu wa Lindi tunafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mbalimbali kwa kila Wilaya, kuna fursa mbalimbali za uwekezaji, nami nitumie nafasi hii kuwaalika Waheshimiwa Wabunge mbalimbali, karibuni kwetu Lindi, mje kujionea, yawezekana nanyi mkabahatika au mkapenda kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali ilimradi katika Mkoa wetu wa Lindi tuendelee kukuza uchumi wetu, lakini tuweze kutengeneza ajira mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Lindi tuna viwanda vidogo vidogo na nina hakika kwa nafasi hii tumekuwa tukiongoza kwa kuwa na viwanda vingi vidogo vidogo vinavyofikia karibu 400 na zaidi. Viwanda hivi vyenye ajira kuanzia mtu mmoja, wawili, watatu; kwa hiyo, SIDO Lindi wamefanya kazi nzuri maana viwanda hivi vimetokana na mafunzo ambayo SIDO wameweza kuyasimamia katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Lindi wanaweza kupata ajira kwa kujiajiri wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali kuhakikisha kwamba tuendelee kuwasaidia SIDO Lindi ili waendelee kufanya kazi zao za kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba wananchi wa Lindi wanaendelea kuingia katika eneo hili la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali katika kukuza utalii katika Mkoa wa Lindi kwamba tunao mji mkongwe wa Kilwa, mji ambao ulianza kutumia sarafu yake wenyewe katika eneo hili la Afrika Mashariki. Kwa hiyo, yako mambo mbalimbali ambayo tukiyasimamia yanaweza yakatuletea fedha nyingi za kigeni na kuwavutia watu mbalimbali kuja kutembelea katika eneo hili la Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba Vita vya Maji Maji vilianzia pale Kilwa katika Kata ya Kipatimu. Eneo lile lina historia yake kwa sababu, ndugu zetu Wakoloni walikuwa wanashangaa namna ambavyo Kinjikitile Ngwale aliweza kutengeneza jambo ambalo lilifanya Wakoloni watupige risasi za moto maana yake zinabadilika na kuwa maji. Kwa hiyo, ni historia kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kila namna ya kuukuza utalii katika eneo hili, kwa sababu ndugu zetu Wakoloni waliweza kukata kichwa cha Kinjikitile Ngwale na kupeleka kwao kwenda kuchunguza kwamba mtu huyu, utaalamu huu amewezaje kubadilisha risasi ya moto na kuwa maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna kila namna ya kukuza utalii katika eneo hili. Maana ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Muda wako umekwisha. Ahsante sana.

MHE. MAIDA H. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.