Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu. La kwanza kabisa, nichukue fursa hii ya kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na sisi wote ni mashahidi. Kwa sababu hiyo najikumbusha mbali kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita lile 2010/2015 nilisimama Bungeni hapa na nikasema, kule kwetu mimi ni Mganga wa Kienyeji na nilitabiri kwamba CCM itaendelea kutawala miaka 200. Kwa dalili hizi ambazo naona, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kazi alizozifanya, kwa hiyo, utabiri wangu naona utakamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuongoza kwa miaka mingi. Kuongoza ni kufanya kazi nzuri ambayo wananchi wanaridhika na chama kile ambacho kiko madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo ushahidi wa kazi kubwa ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake; Mawaziri, kazi kubwa wanazozifanya katika nchi yetu, sisi wote ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jafo kwa kazi kubwa ambayo anaifanya nchi nzima. Sisi ni mashahidi, kila kona anazunguka kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushahidi kidogo tu. Kwenye Jimbo langu naishukuru Serikali nimepata fedha shilingi bilioni1.5 kwa ajili ya hospitali ya Wilaya; pia nimepata fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya. Kituo cha Afya hiki kiko Madindu, lakini nimepata fedha tena shilingi milioni 500 ya Kituo cha Afya cha Mlandizi. Haya yote ni mafanikio ya Serikali hii ya Awamu ya Tano. Ninajivunia, tumepata fedha karibu shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa soko pale Mlandizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha kwa ajili ya kujenga mabweni shilingi milioni 720. Sasa leo ukisema kwamba Serikali haifanyi kitu napata taabu kidogo. Vile vile tumepata gari la Kituo cha Afya Mlandizi pale, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi kubwa ambayo amefanya tumepata pale gari. Haya yote ni mafanikio makubwa sana katika Halmashauri yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo moja nataka kuzungumzia. Kuna ujenzi wa bandari kavu pale Kwala, nadhani na Mheshimiwa Jafo anafahamu, lakini liko tatizo moja kubwa pale. Tatizo la pale, tukipata barabara ile ya kutoka Vigwaza mpaka Kwala itatusaida sana kule kusukuma mambo kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameongelea sana suala la TARURA kuhusu kuongezewa bajeti, nami naunga mkono suala hili. Kwenye Jimbo langu kuna tatizo kubwa sana la TARURA kukosa vyombo vya usafiri ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Jafo, kama mambo yako sawasawa kule atuangalie Jimboni kwetu tupate gari liweze kutusaidia mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo moja tu la mwisho, kuna suala zima la Walimu. Pale Jimboni kwangu ni tatizo kubwa, Walimu wanalalamika kuhusu kupandishwa madaraja. Kwa hiyo, naomba sana upande huu nao tuweze kuangalia mambo yaende vizuri katika Jimbo pale kwa sababu kama walimu ndiyo wapiga kura wetu na sisi wote tunafahamu, lakini kuna malalamiko makubwa, kwa hiyo, tukiangalia Walimu hawa na yako maeneo mengine wanapandishwa madaraja, lakini sisi bado hatujapanda daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii ya kipekee tu kuipongeza Halmashauri yangu. Halmashauri yangu mwaka 2018 imekuwa ya kwanza Kitaifa katika ukusanyaji wa mapato. Nawapongeza Madiwani kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kuhakikisha kwamba Halmashauri yetu inaweza kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeze wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini na mimi mwenyewe kwa kazi kubwa ambazo tunazifanya kwenye Jimbo. Tumeweza kuleta container ya vitabu pale lenye thamani ya dola 250,000; juzi tumeshusha container moja la Vifaa vya Afya pale hospitali shilingi milioni 400; na tunaisaidia hospitali pale kujenga ukuta ule, karibuni milioni 200. Fedha hizo zote zinasaidiwa na nchi na Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)