Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kupata nafasi ya kuchangia mafungu mbalimbali katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mzee wangu Mheshimiwa Balozi Mahiga kwa uteuzi wake wa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Naamini kwamba uzoefu wake katika Mambo ya Nje utaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kazi kubwa iliyoko katika Wizara hii. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mahiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitoe shukrani za dhati kwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha ufunguzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma. Mahakama hiyo itaweza kutusaidia sana watu wa Kigoma kuweza kupunguza mwendo wa kwenda Tabora kwa ajili ya kufuatilia kesi mbalimbali. Kwa hiyo, naomba salamu zangu kwa Jaji Mkuu ziweze kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili tu ambayo ningependa kuya-address. Jambo la kwanza linahusiana na mashauri mbalimbali ambayo Serikali yetu inakabiliwa nayo katika Mahakama mbalimbali za Kimataifa na namna gani bora ya kuweza kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa kwa maana ya public interest yanazingatiwa katika kukamilisha mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa siku za nyuma nimekuwa nikishauriana kwanza Waziri, Mheshimiwa Kabudi na baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba kuna baadhi ya kesi ambazo sisi tumeshtakiwa lakini tuna vithibitisho vya kuhakikisha kwamba sisi tusishitakiwe katika kesi kama zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi mojawapo ni ambayo inafanyika sasa na imeshaamuliwa kati ya Tanzania na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong ambayo mwaka jana ilikuwa ni audit query kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na mwaka huu nimeona Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameweka Jedwali la Utekelezaji na ameeleza kwamba TANESCO kwa kushirikiana na Serikali iko katika mchakato wa kutekeleza Deed of Indemnity iliyotumiwa na Bwana Harbinder Singh Sethi kwa niaba ya IPTL na Benki ya Tanzania kwa ajili ya Serikali ya Tanzania kutatua madai yanayotarajiwa na Standard Chartered Bank - Hong Kong ikiwa TANESCO itashindwa. Hii ni kesi ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 148.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala ambalo napenda Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Serikali nzima iweze kulieleza kwamba public interest yetu hapa ni fedha ambazo zilichotwa kutoka Benki Kuu kurejeshwa. Ndiyo public interest yetu hapa, public interest siyo kuwaweka watu ndani na fedha zile zikosekane. Sasa kwa sababu tuna Deed of Indemnity na tayari mazungumzo yanaendelea, Serikali inaweza kulifahamisha Bunge ni hatua gani inazichukua ili watu ambao wamewaweka ndani waweze kushirikiana na Serikali, Deed of Indemnity ifanye kazi tuondokane na haya madai ambayo sisi tunadaiwa. Kwa hiyo, naomba hili Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake waweze kutupatia majibu kwa sababu ni jambo ambalo linaweza kuokoa mabilioni ya fedha iwapo tutalifanya kwa maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kesi ambayo sitaki kuizungumzia kwa undani, ya Standard Bank ya Mzee Kitilya ya zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 6. Wote tunafahamu kwamba kuna Benki ya Kimataifa ambayo iwapo raia wetu wangetumika kama mashahidi nchi yetu tungeweza kukwepa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 600 ambao sisi tunaamini kwamba ulipatikana kwa njia za rushwa. Hata hivyo, Serikali yetu badala ya kufanya kazi na raia wake inawaweka ndani raia wake, inarefusha kesi wakati kuna deni hapa ambalo kila mwaka tunalipa riba na thamani ya shilingi inaporomoka na gharama ya deni inaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kuelewa Serikali hapa hekima yake ni ipi? Hekima yake ni kuhangaika na Dola milioni 6 na kuwaweka watu ndani au hekima ni kuokoa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 600 ambao kama tuki- prove kwamba ulipatikana kwa rushwa mkopo ule nchi yetu haitaweza kuulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nipate maelezo ya Serikali inatumia hekima gani katika hili? Au inaona raha tu kumweka Kitilya ndani au inataka kumkomoa Kitilya na wenzake? Kwa nini hatufanyi maamuzi ambayo public interest ni kubwa zaidi kuliko kuumiza watu kama ambavyo tunafanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni jambo ambalo nililizungumza kwenye bajeti ya mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika, suala la Ofisi ya DPP. Majibu ambayo Mheshimiwa Mkuchika aliyatoa pamoja na kwamba aliongea kwa busara sana lakini sikuridhika nayo kwa sababu mateso ambayo wananchi wanapata kutokana na ubambikiwaji wa kesi na majadiliano ya pembeni ambayo hayafuati sheria kwa sababu hatuna sheria ya pre-bargain tunawaonea raia wetu sana. Naomba Serikali iweze kutazama na ni jambo rahisi sana.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachokiona ni kwamba mfumo wetu wa jinai (criminal justice system) ni mfumo ambao umejaa uonevu, unaweka mazingira ambapo tunawatesa raia wetu na unapaswa kufumuliwa. Ili mfumo huu ufumuliwe sawasawa lazima tuanze na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachokiomba na nitatumia Kanuni ya 120(2)(a) ya Kanuni za Bunge kwamba mara baada ya mjadala huu kukamilika, nitatoa taarifa kwamba Bunge liunde Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza, kufanya probe ya makubaliano ambayo Ofisi ya DPP inafanya na watu ambao walikuwa watuhumiwa na kutoa fedha, kwa sababu fedha zingine zinatolewa pembeni, wanazungumza unaambiwa mpelekee mtu fulani, malalamiko mtaani ni makubwa sana. Ukiyasikia malalamiko hayo unaumia, mtu yoyote anayependa justice anaumia. Haiwezekani mfumo wetu wa mashtaka ndiyo ukawa mfumo wa kukomoa watu, ikawa kama ni Kangaroo Court ikawa watu wanaonewa, unakamatwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)