Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunijalia uzima na leo nasimama kuchangia maoni yangu kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ni Wizara muhimu sana kwa ustawi wa jamii yetu ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia kwanza kabisa kuhusu Vitambulisho vya Taifa, maana yake leo asubuhi iliongelewa sana hapa Bungeni. Majibu ambayo Serikali imetoa asubuhi Bungeni ni majibu ambayo ni mepesi sana kwa Watanzania kuyasikia na hayana uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa kwamba Serikali inadaiwa zaidi ya dola 30,000 za Kimarekani na Mkandarasi Alice ambaye amesitisha production ya hivi vitambulisho kuanzia Januari, 2019. Sasa haya mambo ambayo wamekuja hapa asubuhi wanaeleza ooh, watakwenda kutambuliwa kwa sababu ya usajili wa simu kwa kutumia namba, tutambue kwamba Watanzania wanahitaji vitambulisho vya Taifa, siyo kwa usajili wa simu tu. Kuna sehemu nyingi Watanzania wakienda wanaombwa vitambulisho vya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ituambie Bunge hili, ni lini itaenda kumlipa Mkandarasi huyu hizi takribani shilingi bilioni 69 ili Mkandarasi aendelee na production, aendelee kuandikisha Watanzania na wapate hivyo vitambulisho ambavyo ni muhimu? Mtueleze ni lini mtamlipa Mkandarasi huyu hizi shilingi bilioni 69. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ndiyo maana tukikaa tunasema lazima Serikali iwe na vipaumbele. Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa, mlikuwa na target ya kuandikisha Watanzania milioni 25, leo waliopata ni milioni nne tu. Mkandarasi amesitisha uzalishaji, Kisa, hamjalipa fedha; lakini fedha nyingine mnapeleka kwenye sehemu ambazo hata hazina tija kwa maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nitaenda kuzungumzia Jeshi la Polisi; na hapa tukizungumzia Polisi, tunazungumzia wale ambao wanakiuka miiko na maadili ya kazi zao. Maana yake Wabunge wa CCM mkisimama huko mna generalize sijui mnafikiri nini. Tuko hapa kulisimamia Taifa, kulisimamia Jeshi la Polisi likienda kinyume. Nao wanatambua sisi ndiyo tunapigania maslahi yao hapa, lakini hatuwezi kuacha kuwasema wakienda kinyume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unyanyasaji wa raia wanapokamatwa na Jeshi la Polisi; tumeshuhudia raia wanapigwa, wengine wanafariki. Juzi nimesikia Mwanga kuna kijana amefariki kwenye kituo cha Polisi. Yaani haiwezi kupita mwezi, miezi minne hatujasikia kuna raia amepigwa na Polisi, amefia Kituo cha Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, nilipokuwa Segerea kuna mabinti walikuja wamekamatwa kwenye Vituo vya Polisi, wamebakwa, wameingiliwa kinyume na maumbile, wengine wameambukizwa magonjwa ya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumza hapa, tunataka Jeshi la Polisi liwawajibishe hawa Askari. Majina ya Maaskari nawajua na nilitaja kwamba Kituo cha Sitaki Shari, Kituo cha Kawe na Kituo cha Mabatini. Wanakaa na mabinti hawa zaidi ya mwezi, wiki tatu, miezi miwili wanawafanya kinyume na maumbile. Binti amekuja pale ameoza huku nyuma. Halafu tukizungumza, mnasema kwamba tuna…, come on! Lazima tusimamie hawa Polisi wasiende kinyume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, kubambika kesi raia. Unamkamata raia kwa uzururaji, unampa amri robbery. Asipokuwa na fedha ya kukupa kitu kidogo, unambambika. Lazima tukemee hili ili Jeshi la Polisi, wananchi ambao ni walipa kodi ndiyo wanawalipa kuwepo; wanatakiwa wawalinde raia na usalama wao na siyo kuwageuza vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kabla sijaendelea hapo hapa katika kuwanyanyasa raia; tumekuwa tukisia matamko kwa kweli ambayo hata hayakemewi. RPC wa Dodoma, mwaka 2018 wakati nachangia nilimsema. Mwaka 2018 alisema kipigo cha mbwa koko; mwaka huu wakati ACT Wazalendo wanasema wataandamana, ambapo ni haki yao Kikatiba, akatoka kabisa confidently anaongea atawapiga mpaka wachakae. Kweli mnawachakaza Watanzania, maana yake mmewachakaza mpaka mnawaua. Kama hamkemei hili, mnafikiri ni sifa mnaua Watanzania, hakika hiyo laana itawarudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mlundikano wa mahabusu kwenye Magereza yetu. Nashangaa Tanzania ni nchi ya ajabu. Nyie mnafurahia kuwalundika raia Gerezani, raia ambao wangekuwa ni wazalishaji kwenye Taifa letu, mnaweka mzigo kwenye Taifa kwa kuwalundika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Segerea unakuta zaidi ya asilimia 80 ni mahabusu, tena mahabusu kesi zao nyingine zinachekesha. Kuna kesi moja alikuwa ni mfanyakazi wa ndani, anatuhumiwa eti ameiba shilingi 800,000/=, tena ni mfanyakazi wa kigogo mkubwa sana Wizarani. Eti, akaenda kufuatwa Bukoba, ametoka Dar es Salaam; wamechukua gari Mwanza wamemfuata Bukoba ndani ndani huko, amekuja wamepandishwa ndege mpaka Dar es Salaam kwa shilingi 800,000/= mnasema kwamba mnasimamia matumizi ya walipa kodi masikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukemee haya. Lazima tukemee haya. Watanzania wanaozea kule mahabusu Gerezani kwa kesi za kitoto sana. Wanakaa miaka mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi imekuja hii ya utakatishaji. Nikiwa Segerea kuna Watanzania vijana ambao wamejiajiri kwenye hizi Travel Agents, wanasemekana sijui wametakatisha shilingi milioni 10 za ATCL. Wamekamatwa vijana zaidi ya 11, wamesafirishwa kutoka Mwanza. Kuna mahakama kule! Usiku wamesafirishwa kutoka Mwanza na Maaskari wameletwa Segerea. Shilingi milioni 10 mnawaita watakatishaji, mnawanyima dhamana, vijana ambao ni wazalishaji zaidi ya 12 na kuna mama ana katoto ka miezi miwili. Yaani, basi, kama ni laana tunaipata kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sare za Magereza. Nimekuwa nikizungumza hili. Hawa Askari Magereza…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji, kusema kweli amtaje ambaye alitumia hiyo ndege na gari ili tumjue achukuliwa hatua za kisheria. Bila kumtaja haiwezekani. (Kicheko)

MWENYEKITI: Hiyo siyo taarifa. Endelea Mheshimiwa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema hao Maaskari ni wabaya tunataka tusafishe hili jeshi liwe jeshi ambalo linatumikia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu 2012 mpaka leo Askari wa Magereza hawajapewa uniform, wanajinunulia. This is a shame. Watu hawa wanawajibika kutunza watu mnaosema ni majambazi sugu, ni manani, wanaji-sacrifice wanawatunza, hata kuwapa uniform zao, hamna! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, tumekuwa tukiona majeshi yetu yanaingiliwa. Niliona hivi karibuni TISS wanatumika kukamata raia badala ya Polisi. Kwa hili I have the evidence. Hiki ni kuingilia mihimili mingine. Haya majeshi, TISS wanatakiwa wafanye kazi zao, Jeshi la Polisi lifanye kazi yake. Pia kuna malalamiko yalikuja na hata raia tuliona.

Mheshimiwa Rais alisema kabisa kwamba wakati anakwenda kukagua nyumba ambazo zinajengwa kule Ukonga na TBA ambazo Magereza hawahusiki kabisa, alitakiwa awawajibishe wale TBA, lakini kauli ya kusema CGP atatokana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kwa kweli ile kauli mpaka kesho sijui inamaanisha nini. Kwamba CGP wa Magereza atokane na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hii ina-demoralize hawa Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kwa haraka haraka ni kuhusu Askari Magereza kutumia fedha zao za mfukoni kusafirisha mahabusu na wafungwa, kama wanatoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Hii fedheha kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Wekeni utaratibu wa kuweza kuwasafirisha hawa mahabusu na wafungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wanatumia fedha zao halafu hamwalipi, inakuwa ni deni. Hii ni aibu. Askari hawa wanadai madeni ya likizo, hamwapi, wanadai na madai kibao. Mshahara hamjawapandishia, pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alisema kwenye kampeni zake, akishinda ataongeza mishahara ili wasiwe wanauza vitumbua, wasiwe wanafanya mambo ya rushwa, kitu kimekuwa ni kunyume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wa nne tunaenda hamjapandisha mshahara, mnasubiri mwakani mpandishe; na hiyo itakuwa ni rushwa. Mlitakiwa mwapandishie kuanzia mwanzo, siyo msubiri ikifika mwakani sasa mnapandisha ili kuwasogeza karibu, maana yake kule kwetu huwa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)