Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa kwa ajili ya kuchangia hii Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwanza nianze kuishukuru sana Serikali hasa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii ya Mambo ya Ndani na maaskari wote kwa namna walivyodhibiti mauaji ya watoto katika Mkoa wa Njombe na Simiyu, nawashukuru sana. Naomba Mwenyezi Mungu aendeee kuwabariki na aendelee kuwalinda ili tuweze kudhibiti tabia za namna hii na hatimaye Watanzania wasiweze kupotea kupitia mauaji mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa namna wanavyofanya kazi zao hasa katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kazi ni ngumu, kubwa sana, inahitaji weledi na pia inahitaji ustaarabu mkubwa. Nashukuru Mwenyezi Mungu anawatia nguvu wanaendelea kumudu na hatimaye tunaona matokeo ya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie juu ya makazi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutoa zile bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 400 za askari wetu nchini. Tumeona zimegawanywa kwenye baadhi ya mikoa, kuna mikoa inapata nyumba 88 na mingine nyumba 20 na mgawanyo umeenda karibu kila mkoa ambao una upungufu mkubwa sana wa nyumba za askari wetu. Mkoa wa Njombe nimpongeze Mheshimiwa Rais ametupa nyumba 20 kwa ajili ya askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wetu wanafanya kazi kubwa sana usiku na mchana. Nashangaa hata wakati mwingine watu wanavyowabeza, kazi wanazofanya maaskari wetu ni kubwa sana, wanatulinda usiku tukiwa tumelala, wanalinda maduka mbalimbali, maduka yetu na mali mbalimbali za wananchi wa Tanzania, lakini pia wanatulinda hata sisi Wabunge tuliomo humu ndani. Tunaweza kuongea kwa amani na tukaishi kwa amani humu ndani na tuna uhakika ni kwa sababu askari wetu wametuzunguka huku wanatulinda. Kwa hiyo wanafanya kazi kubwa, hata wanapokosea tutumie maneno mazuri kwa sababu ni binadamu na wakati mwingine sisi wenyewe tunawakwaza na ndiyo maana wakati mwingine wanaghafilika au wanachukua hatua ambazo kidogo kama binadamu wakati mwingine wanapotoka taratibu kwa sababu ya namna sisi wananchi ambao wanatulinda usiku na mchana, wanatutumikia muda wote lakini wakati mwingine tunageuka kuwapiga mateke, tunageuka kuwatukana na kuwapa lugha mbayambaya na matusi mbalimbali. Kwa hiyo niombe tuwaheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana bado maeneo mengi, mikoa mingi, nyumba za askari haziridhishi na wakati mwingine huwa wanaenda kazini wakiwa na frustrations ndiyo maana tunasikia wakati mwingine maaskari wanajiua, wanajipiga risasi kwa sababu ya frustration ya kukosa makazi. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri pia niiombe Serikali kwa utaratibu huu ambao Mheshimiwa Rais ameuanza angalau tuanze kujenga nyumba za maaskari hawa kila mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika Mkoa wa Njombe kwa mfano, Kituo chetu cha Polisi cha Wilaya pale ni cha zamani sana, ukiangalia hata jengo la kituo lenyewe ni la zamani. Kwa hiyo haiendani na hali halisi ya hatua ilipofikia kwa maana ya ngazi iliyofikia kile kituo. Kile kituo sasa hivi kinatumika kama kituo cha Mkoa lakini hadhi ya kituo chenyewe sio nzuri. Nyumba zile ni chakavu, lakini ukiangalia hata makazi ya maaskari kwa kweli ni duni sana. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tuliangalie hili jeshi, tuangalie maaskari wetu wa Mkoa pale Njombe angalau wapate nyumba. Kukaa mitaani sio nzuri sana. Wakati mwingine wanakaa mitaani wanapanga nyumba na wakati mwingine wanaweza kuwa wanapanga nyumba na mhalifu. Inakuwa ni vigumu sana kumdhibiti huyu kwa sababu wakati mwingine wengine wanashawishika, wanaweza wasifanye kazi vizuri kwa sababu ya mazingira wanayokaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanapokaa mitaani maisha yao yanakuwa hatarini kwa sababu akishajua kwamba askari fulani ndiye aliyenikamata anaweza akamdhuru anaporudi kutoka kwenye shughuli zake ule usiku au anapoamka asubuhi kwenda kufanya shughuli zake zile. Kwa hiyo wakiishi sehemu moja, wakiishi kwenye nyumba nzuri za Serikali watafanya kazi zao vizuri na hatimaye watakuwa na morale ya kufanya kazi kwa sababu wanaishi kwenye makazi mazuri. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Kangi na Naibu Waziri na Makatibu Wakuu, nafikiri wawasiliane nao vizuri hawa ili baadaye ikiwezekana bajeti ya makazi iweze kuongezeka na hatimaye maaskari wetu waweze kupata nyumba bora, waweze kuishi vizuri na waweze kuhamasika katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Jeshi la Magereza. Ni kweli Jeshi la Magereza wanafanya kazi kubwa lakini ukiangalia kwenye bajeti yao, Fungu lao namba 29, bajeti yao ni ndogo sana kwa hiyo ukomo wao ni mdogo. Hebu tupanue, tuongeze ukomo wa bajeti ya askari magereza kwa Jeshi la Magereza ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri. Wameeleza Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba kuna shida ya sare za maofisa, hawana sare walio wengi, lakini pia ukiangalia hata maaskari hawana sare, ukiangalia Jeshi la Magereza hawana na wafungwa wetu sare zao nyingi zimechakaa. Kwa hiyo tukiongeza ukomo wa bajeti wataweza kumudu kutekeleza majukumu yao, lakini wataweza kununua vifaa na mavazi ambayo wanatakiwa wayanunue kwa ajili ya askari wetu lakini pia kwa ajili ya maafisa wetu na kwa ajili ya wafungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili litiliwe mkazo ili wafungwa wetu, pamoja na kwamba wanakuwa wamefungwa lakini wana haki ya kupewa zile sare. Vilevile maafisa wana haki ya kupewa sare zao na maaskari wana haki ya kupewa sare zao, kwa hiyo tuwatekelezee hii haki ya msingi ya angalau ya kupewa nguo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa akisema mara nyingi kwamba Jeshi la Magereza waanzishe utaratibu wa uzalishaji. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulisimamia hili. Kwanza tuya- identify magereza yetu yalipo, tuzi-identify fursa zilizopo katika magereza haya. Tujue kwamba kama ni Dodoma kuna fursa ipi wanaweza wakaifanya na mwishowe wakazalisha. Kama ni Njombe au mikoa kwa mfano yenye mvua nyingi tunaweza tukaanzisha shughuli za kilimo. Kwa hiyo kwenye mikoa hii tuanzishe shughuli za kilimo, lakini hatuwezi kuanzisha shughuli za kilimo bila kupeleka matrekta ya kulimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Kangi akae na wataalam wake wajaribu ku- identify maeneo yalipo magereza haya tuangalie ni shughuli gani wanaweza wakazifanya na hatimaye magereza yasiwe tegemezi. Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuwalisha wafungwa, lakini kumbe tukianzisha shughuli watakuwa wanazalisha na hatimaye kuipunguzia gharama Serikali ya kuwatunza hawa wafungwa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kwenye gereza la Idete, kinaweza kuanzishwa kilimo cha umwagiliaji cha mpunga na wakazalisha, halafu huo mpunga au mchele ukasambazwa kwenye magereza mengine, kwa hiyo badala ya kununua chakula basi wakapewa chakula kupitia magereza mengine. Pia kwenye magereza ambako hakuna uzalishaji tunaweza kuanzisha shughuli kama za useremala, kwa mfano, tumesema kwamba hapa Dodoma Msalato tutaanzisha useremala, basi uanze haraka ili waweze kuzalisha hizo bidhaa na waweze kuuza na hatimaye majeshi yetu yaweze kujitegemea kupitia hizo shughuli za kilimo. Kwa hiyo, tukifanya hivyo tutapunguza gharama kubwa ambazo tunazitumia kuwalisha hawa wafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ili tuweze kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani tuanzishe utaratibu wa adhabu mbadala. Badala ya wote kuwapeleka ndani, kwa mfano, wafungwa wanaokuwa na adhabu ya miezi sita, mwaka mmoja, hawa wanaweza wakatafutiwa shughuli, wakafanya shughuli za maendeleo, wakashiriki kwenye shughuli hizi za ujenzi kwa kuwa sasa hivi jeshi la magereza linashiriki kwenye shughuli za ujenzi na tumeona kazi zao wanafanya vizuri. Tumeona wamejenga hizo nyumba hapo za Mji wa Serikali. Kwa hiyo, kumbe tunaweza tukawatumia hawa wafungwa wale ambao wana vifungo vifupi, badala ya kupelekwa gerezani, wao wakapewa kazi ya kufanya kama vile kushiriki kwenye kazi za ujenzi na hatimaye tukapunguza gharama, tukapunguza msongamano…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)