Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Nianze na kuipongeza Serikali, tumeona mambo mengi kwenye elimu imefanya vizuri, Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kazi inaonekana ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kushauri; kwanza nipongeze kwa elimu bure, elimu bure ni kitu kizuri sana kwa Taifa letu na sasa hivi kuna ongezeko kubwa sana la watoto kuanza shule za awali, shule za msingi mpaka sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana na wazazi wamelielewa hilo na kufuatana na ongezeko la watoto, kuna shule nyingi sana sasa hivi zinajenga madarasa kwa ajili ya ongezeko la watoto, lakini na wazazi wako tayari kujenga madarasa kuhakikisha watoto wanasoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema elimu bure, wazazi walio wengi sasa hivi wameanza kupata uelewa, lakini zamani uelewa ulikuwa mdogo sana, walikuwa wanajua elimu bure ni kila kitu huruhusiwi kuchangia, lakini sasa hivi elimu waliyoitoa kwa wazazi nawashukuru sana wameanza kuelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watoto wanamaliza form four, bahati mbaya hawaendi high school wanaishia form four, sasa wale wanaoishia form four kwa kwenda sasa hivi hakuna na wale watoto kwa sababu bado hawajatimiza miaka 18 hawawezi kuajiriwa mahali popote, kwa hiyo basi Serikali ili kuwanusuru wale watoto ni kuhakikisha kwamba inajenga Vyuo vya VETA katika kila wilaya kama sera inavyosema. Kuna wilaya nyingine hazina VETA kabisa, kwa hiyo Serikali lazima ijikite kuhakikisha kwamba wale watoto wanaomaliza form four hawajachaguliwa kwenda high school waweze kwenda kwenye vyuo vya VETA, ili waweze kupata ujuzi na wakimaliza huko VETA waweze kujiajiri wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la msingi sana, tulienda Arusha kwenye Kamati yetu ya Bajeti, tukatembelea viwanda pale, bahati nzuri tukakuta watoto waliomaliza VETA wamepata ajira pale, ni mafundi wazuri sana mpaka tukajifunza kwamba kumbe watoto wakipitia VETA wanaweza kupata ajira bila matatizo hata akiwa hajafika form four na anaweza akafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuboresha elimu, tukisema tunataka kuboresha elimu siyo kwamba kubadilisha mitaala kila wakati. Sasa hivi Open University – Chuo Kikuu Huria Walimu wengi sana wanapenda kujiendeleza kwa kusoma vyuo vikuu, lakini chuo kikuu rahisi kabisa ni Chuo Kikuu Huria ambao tunasema Open University. Sasa nataka niishauri Serikali ili kuongeza wingi wa Walimu wasomi na tumesema kwamba Walimu kuanzia Diploma, mpaka degree mpaka Masters, sasa hivi Walimu wenye degree wanafundisha shule ya msingi na hilo tumeliona na huko ndiyo kuboresha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali tuseme elimu bure kwa Walimu, yaani Walimu wapewe elimu bure, Mwalimu anayejitolea kwenda chuo, anaenda kufanya degree kwenye Open University asome bure kwa sababu yeye akimaliza ni faida ya Taifa, anaenda kufundisha watoto katika shule zetu. Kuna Walimu wengine kufuatana na mshahara kuwa mdogo wanashindwa kujiendeleza kusoma degree, kwa sababu mshahara ni mdogo. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, tutakuwa tumemsaidia sana Mwalimu kujiendeleza. Tunabadilisha mitaala kila wakati haitusaidii kama hatuboreshi elimu kwa Walimu wetu, hii itatusaidia sana. Kwa hiyo nasisitiza kwenye hilo na nawapongeza Walimu wale wanaopenda kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna jambo lingine ambalo siyo zuri sana, Mwalimu anamaliza Masters, anamaliza degree anarudi kufundisha shule, anakuja kupitwa mshahara na Mwalimu mwenye certificate, inamkatisha tamaa Mwalimu aliyesoma. Kwa hiyo ni lazima tuweke grading system ikae vizuri ili ku-motivate Walimu. Tumesema wafanye degree, wafanye diploma na ukiweka elimu bure na akimaliza shule aongezewe mshahara kufuatana na elimu yake, lakini anamaliza degree unampeleka shule ya msingi na mshahara ni mdogo, basi Mwalimu anakata tama, sasa hapo bado tutakuwa hatujaboresha. Nimeona hili niliongee kwa msisitizo sana kwa sababu kuna Walimu wengi sana wanapenda sana kusoma soma, nami nawapongeza ili kuhakikisha kwamba Walimu wanakuwa katika mazingira mazuri kwenye elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna hizi private school, Mheshimiwa Waziri siku moja alisema wataleta kiwango cha ada. Kuwa na private school ni jambo zuri sana na elimu bora kwenye private school ipo tunaiona, wanafundisha vizuri, lakini ada ni kubwa sana. Wewe unaweza ukaona ada ya private school mtoto analipa milioni kumi, milioni nane, jamani hicho ni Chuo Kikuu, ni shule ya sekondari, ni shule ya msingi. Wengine wanasema kama unaona mtoto wako huwezi kupeleka huko, peleka shule ya Serikali, ndiyo watu wanajitetea, lakini hiyo ni elimu na tunavyoongea hivi lazima tupime maana mtoto anataka apelekwe kuzuri na mzazi anataka ampeleke mtoto wake kuzuri ili apate elimu nzuri, lakini lazima kuwe na grading system ya ulipaji wa ada. Sasa kwa mfano, shule ya msingi mtu analipa milioni 12 unaweza kuona pale sawa ni lugha na elimu, sawa ni nzuri lakini lazima kuwe kuna fairness kwa watoto na kwa wazazi.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, taarifa kwa ndugu yako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe taarifa kaka yangu Mbunge anayezungumza kuwa hata kwenye mahoteli, kuna guest house Sh.15,000 mpaka Sh.2,000,000. Kwa hiyo, chaguo ni la kwake hawajatulazimisha, tupo nchi ya kidemokrasia hii. Kwa hiyo, kama mtoto wako unaona akasome St. Kayumba mpeleke zipo shule za private ada kuanzia Sh.300,000 mpaka hiyo Sh.10,000,000. Kwa hiyo, chagua ni lako. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kigola unaonaje hapo, patamu eeh?

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku moja nilikuwa naongea nikasema hizi taarifa tunazozitoa tuwe makini maana unaweza ukatoa mfano ambao hauendani na elimu. Sasa wewe unatoa mfano wa gesti na elimu wapi na wapi, nashangaa, hizi taarifa tuwe makini sana. Academics na vitu vya biashara kama gesti haviingiliana hata siku moja. Hivyo Mheshimiwa hapo inabidi ujipime mwenyewe na taarifa yako. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uboreshaji wa mazingira ya walimu kufundishia. Walimu lazima waishi kwenye mazingira mazuri. Kwa mfano, kuna shule nyingine unaweza kuona mwalimu ana nyumba yake pale lakini nyumba haina jiko.

Mimi nimeona kwenye jimbo langu, siwezi kuongea kitu ambacho sijaona. Kwa hiyo, tunaposema tunajenga nyumba za walimu tuhakikishe nyumba ina jiko na choo safi. Miundombinu ya nyumba ikakaa vizuri basi mwalimu anayefundisha shule ile atajisikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumesema nyumba zote za walimu ziwe na umeme, hilo ni jambo nzuri sana. Kama nyumba ina umeme ataandaa masomo jioni na atakaa vizuri lakini kama mazingira ni magumu unampa ugumu mwalimu kufanya maandalio. Kwa hiyo, hilo nalo ni suala la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la walimu wa sayansi, shule nyingi sana za sekondari walimu wa sayansi hakuna. Kuna siku moja tuliongea tukasema tutoe motisha kwa walimu wa sayansi, wale wanaosoma digrii ya sayansi wapewe mkopo asilimia 100, watu wengi watakimbia kuchukua masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu pale Mgololo mwekezaji amejenga shule nzuri sana. Bahati nzuri sana namshukuru Makamu wa Rais alikuja pale na alikubali kwamba ile shule itakuwa ni high school iatakuwa ni sayansi tupu. Sasa ikiwa ni sayansi tupu, wale wanafunzi wanaomaliza, kwa mfano mtu amesoma PCB, PCM akimaliza anaenda kusoma engineering au digrii ya ualimu wapewe mkopo asilimia 100. Sasa utaona mwanafunzi amesoma masomo ya sayansi magumu anaenda chuo kikuu mkopo hapati basi wanafunzi wanakwepa yale masomo, wanasema si nafuu tusome masomo mepesi tuendee na maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni msisitizo ingawa lina connection na TAMISEMI ni upandaji madaraja walimu, walimu wanalalamika. Mwalimu alimaliza mwaka 2012 mpaka leo hajapanda daraja, kwenye jimbo langu wapo. Kuna mwalimu mwingine amemaliza mwaka 2014 hajapanda daraja mpaka leo. Kuna mwingine amemaliza 2014 amepanda daraja, wa mwaka 2012 hajapanda daraja. Sasa yule aliyeanza kuajiriwa hajapanda daraja aliyekuja kuajiriwa baadaye amepanda daraja, tayari yule ambaye hajapanda daraja inakuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya kupandisha madaraja vitolewe. Ikitokea ongezeko la mshahara lazima yule aliyekuja kuajiriwa baadaye atapata mshahara mkubwa zaidi kwa sababu ndiye aliyeanza kupanda daraja yule aliyeajiriwa mwanzoni anakuwa na mshahara mdogo, kwa hiyo, inaleta shida kwa walimu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)