Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SILAFI J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuzungumza machache katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipatia pumzi na afya ya kuweza kusimama tena katika mwaka huu wa 2019 niweze kuzungumza haya yafuatayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, natoa pongezi za dhati kwa mdogo wangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kujituma na kujitoa kwa maslahi ya kuhakikisha kwamba elimu bora kwa Watanzania inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuzungumza hayo lakini napenda kumuarifu Waziri wa Fedha, Wizara ya Elimu ni vyema ikaangaliwa kwa jicho la namna yake la kuhakikisha ya kwamba ukomo wa bajeti unaongezwa. Nasema hivyo kwa sababu ina miradi mingi na mizito ya kutekelezwa ili kuiweka elimu katika hali inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala zima la miradi ya maendeleo. Fedha ya miradi ya maendeleo ya mwaka 2018/2019 haikuweza kutoka yote na vilevile nina wasiwasi hata mwaka wa fedha 2019/2020 zinaweza kutoka na kukidhi mahitaji katika maendeleo ya Wizara yetu ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la maboma. Kuna maboma kadhaa ndani ya mikoa yetu ya madarasa, shule za msingi na shule za sekondari hali kadhalika nyumba za walimu. Maboma haya yamejengwa kwa nguvu za wananchi lakini Serikali yangu haijaongeza mkono wake katika kuhakikisha kwamba maboma yote yanakamilika ili watoto wetu waweze kupata nafasi ya kujifunzia. Kwa hiyo, tunaomba Wizara hii iongezewe ukomo wa bajeti ili waweze kuweka bajeti yao katika mahitaji yanayohitajika ili maboma yetu yaweze kukamilika yote pamoja na jitihada waliyofikia ya kukamilisha maboma hayo kadhaa. Kwa hiyo, tunaomba fedha za maendeleo ziweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nnapenda kuzungumzia suala la madarasa lakini shule ni choo, bila kuwa na vyoo vya kutosha kwa maana ya matundu ya kutosha kwa watoto wetu watapata maradhi mengi ya kuambukiza. Kwa hiyo, tunawaomba Wizara hii iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba vyoo vya shule vinaendana na idadi ya wanafunzi waliopo hasa ukizingatia kazi nzuri aliyoifanya Rais wa Jamhuri wa Tanzania Dkt. Magufuli kuhusu elimu bure, ni dhahiri kusema kwamba wanafunzi wameongezeka katika shule zetu lakini vyoo vimebakia vilevile. Sasa hivi vyoo vingi vimejaa, tukiwaambia Mabwana Afya wakazungukie shule bila shaka nyingi zitafungwa kwa sababu vyoo vyao haviko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuweka mkakati maalum wa ujenzi wa vyoo vya watoto shuleni. Pia tunaomba waweke choo maalum kwa watoto wetu wakubwa wa kike hasa katika shule za sekondari kwani zimekuwa na matatizo makubwa. Hali kadhalika vyoo vinavyojengwa ni maji, tunaomba utaratibu wa kuweka miundombinu ya maji katika shule zetu uweze kupewa kipaumbele ili vyoo vyetu hivyo vitakavyojengwa viwe katika hali ya usafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la idadi ya wanafunzi. Idadi ya wanafunzi imeongezeka ndani ya madarasa yetu na kufikia walimu kufanya kazi ya ziada. Kwa kweli mimi napongeza sana kazi kubwa wanayoifanya walimu wetu pamoja na hali ngumu wanayofundishia lakini bado watoto wetu wanafaulu, wanakwenda sekondari, high school na vyuo vikuu lakini kazi ya walimu ni ngumu. Katika kipindi hiki cha miaka mitatu cha ongezeko la wanafunzi katika madarasa yetu na mwalimu kujikuta ana watoto zaidi ya 60 ndani ya darasa lakini bado anaifanya kazi ile. Hata hivyo, mishahara yao haijaongezeka na ni midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibuni kila Mbunge aliyesimama hapa amezungumzia mishahara ya walimu, kweli wamefanya kazi nzuri ndani ya hii miaka mitatu, tunaomba tuangalie madaraja yao na tuhakikishe ya kwamba tunawaongezea mishahara yao ili kuwatia morali walimu hawa waweze kufanya kazi nzuri zaidi na kazi iliyotukuka, pamoja na kazi hiyo ya kutukuka wanaifanya hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuzungumzia suala zima la kuhakikisha ya kwamba tunaongeza ajira, tunashukuru kwa hizo nafasi elfu nne, lakini nafasi elfu nne katika mahitaji ya milioni 60, kwa kweli haijafanyika kazi yoyote. Tunaomba tuongeze nguvu ya kutoa ajira kwa walimu, walimu wapo, wako kwenye mitaa yetu, hata kana kwamba walimu wengine wanashindwa kwenye maeneo hayo kutokana na mazingira, lakini bado mazingira yale tuliyokuwa nayo sisi kule hasa mikoa ya pembezoni, vijijini, wako walimu waliomaliza vyuo wako mitaani, nao hawajaweza kupata nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba basi, kama wengine hawawezi kuja kwenye mazingira yale ya pembezoni, kule vijijini, basi walewalioko kule naomba wapewe kipaumbele waweze kupata ajira ya ualimu, kwa sababu wanazoea mazingira yale na wamo ndani ya mazingira yale, waendelee kuwafundisha wenzao nao waweze kupata elimu iliyokuwa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ongezeko la ajira ya walimu, bado tuko nyumba, tunaomba mshirikiane na ndugu wa TAMISEMI, tuweze kupata ajira ya kutosha kwa walimu kwani tunawahitaji sana, hasa sisi mikoa ya pembezoni. Ninasema sisi mikoa ya pembezoni, hata shule za private kule ziko ni chache, ziko mbili tatu, kwa hiyo, bado tunahitaji walimu, kwa hiyo, tunaomba walimu waweze kupatiwa kipaumbele waweze kuongezewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nilikuwa nazungumzia upande wa watoto walemavu, kuna watoto walemavu maalbino, ambao wenye ufinyu wa uono, lakini wanahitaji kusoma, kuna baadhi ya wanafunzi albino, wamechanganyikana na wanafunzi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapokuwa wanasoma katika kuandika ama wanapokuwa kwenye mitihani, wakati wa kuandika, wao wanakwenda taratibu mno, wenzao wanakwenda harakaharaka, kwa sababu hatuna shule maalum katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba kwamba ile mitihani wao wawekwe peke yao watu wa albino, halafu wale walemavu wakae pekee yao na wale wengine wawe peke yao na pia waongezwe mudu wa kufanya mitihani yao na wao waweze kufanya vizuri kama wanavyofanya wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lililokuwa napenda kuzungumzia ni kuhusu katika mukoa wetu wa Rukwa, katika Mkoa wetu wa Rukwa, tuna bahati ya shule kama tatu zina walemavu, wa mtindio wa ubongo, maalbino, viziwi na vipofu. Shule ya Malangali, Shule ya Katandara B, na Mwenge B, lakini walimu tunakuwa nao ni wachache ambao ni walimu wa taaluma, tunaomba walimu wa taaluma wapatikane katika shule hizo za Mkoa wetu wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hawa watoto wanahitaji kupewa chakula mashuleni kwao, lakini bahati mbaya, Serikali yangu imetoa bilioni 22, chakula cha shule hizi, ambazo kwamba ni watoto kwa mwaka mzima. Wao hali halisi kwa maana ya Katandara, kwa maana ya Shule ya Mwenge B, na kwa maana ya Malangali, ni takribani bilioni 72, ndiyo hali halisia ya kuweza kupatikana kwa chakula kwa wale watoto. Lakini wanapata bilioni 22 ambazo kwamba hazikidhi mahitaji, tunaomba waongezewe ili watoto wale waweze kupata chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na shule za stadi, shule za stadi, ufundi stadi wa mashule, tunazo shule kadhaa katika Mkoa wetu wa Rukwa Katandara, Mwaze, Matai na kadhalika. Lakini shule hizi wanafunzi wale hawana vifaa vya vitendea kazi, yaani vya kufundishiwa na vya kufundishika, hawana vitendea kazi. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba wapewe vitendea kazi, wapewe vitu vya kwenda kufundishiwa pale, wale ambao kwamba hawawezi kwenda sekondari kuendelea na masomo… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. (Makofi)

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja, asilimia mia kwa mia, naomba tuangaliwe Mkoa wa Rukwa. (Makofi)