Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika Wizara hii. Niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hii pamoja na Taasisi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukurani hizo, nitoe pia shukurani za pekee kwa Mheshimiwa Rais kwa kutimiza azma yake ya elimu bure kwa shule za awali mpaka sekondari, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imeweza kuwekeza katika elimu maalum katika shule nyingi katika nchi hii, karibu Mikoa yote ina vyuo vya kutolea elimu maalum, isipokuwa Mikoa mitatu ambayo ni Simiyu, Geita na Songwe, nafikiri kwa sababu ni mikoa mipya ni vizuri Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie ni lini shule hizo zitafunguliwa katika mikoa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shule hizo, nilitaka nichangie kuhusiana na mashine au vifaa vinavyotumiwa na walemavu. Tumekuwa tunazungumzia suala la masomo yao, vitendea kazi vyao lakini hatujazungumza kwa kina vifaa vyao wanavyotendea kazi au vinavyowasaidia. Mpaka sasa hivi, tuna mafundi 65 tu ambao wanashughulika na mashine za walemavu, kati ya hao sita tu ni wanawake na 59 ni wanaume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na idadi hiyo, fundi mtalaam mshauri, tunaye mmoja tu, ambaye yeye anafanya kazi Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika, ndugu Malim Kali, ambaye yuko pale Wizara ya Elimu, na msaidizi wake kidogo aliyekuwa anakuja kwa mbali, niseme kwamba Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema, alifariki mwezi wa tatu mwaka huu!

WABUNGE FULAN: Ooooh!

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, mafundi waliokuwepo, wana mafuzo tu ya awali na wengine wamepata vyeti, hatuna walimu tena, au mafundi wa kutengeneza zile mashine. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, nataka aje aniambie, wana mpango gani angalu wa kutengeneza program maalum kwa ajili ya mafundi wa kutengeneza mashine za walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, yule fundi aliyekuwa mtaalam mkuu, aliyekuwa anatengeneza mashine za viziwi, naye amestaafu, bwana Robert Lugeiyamu, amestaafu mwezi Machi, mwaka huu, ni vizuri basi Waziri atakapokuja atuambie katika walataam hao wa kutengeneza mashine hao wamejipanga vipi ili walemavu waendelee kupata huduma zao pale vifaa vyao vinapoharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya elimu maalum, wamekuwa na ushirikiano mzuri sana baina ya Tanzania Bara na Visiwani, wamekuwa wakifanya kazi kwa pamojo na kwa ushirikiano mkubwa. Ni mara nyingi utakuta mafundi kutoka bara wanakweda Zanzibar na wengine wa Zanzibar wanakuja Dar es Salaam au Mikoa mingine ya huku kuja kujifunza au kufanya kazi. Sasa nilitaka kujua, ni lini mafundi hao watapata mafunzo, nchi nzima, bila kujali huyu Mzanzibar, au huyu Mbara ili waweze kuwatumikia walemavu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hizo shule kwa Pemba, tunazo tatu, Michakaweni, Mchangamdogo na Chakechake. Kwa Unguja, kuna Moga, Umoja, Uzini, Jambiani, Suza, Haile Selassie, CCK na Kisiwa Nduwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam, tunazo tatu, Uhuru Mchanganyiko, Msasani na Kibasila. Pwani ziko mbili, Lugoba Sekondari na Mwambao Primary, ambayo iko Bagamoyo. Tunayo Morogoro, Kilosa Sekondari na Mazimbu Primary, kwa Dodoma ziko nyingi kidogo, Mpwapwa TC, Mpwapwa Sekondari, Mvumi DCT, tuna Homboro Primary na Buigiri Primary Maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga tunazo, Lushoto Maalum, Kongwe na Korogwe Grills, kwa Kilimanjaro tunayo Same, tunayo Mweleni, tunayo Moshi Technical na Saint Francis, lakini tunapokuja Arusha bado tunayo Temi, Patandi TC, Patandi Mazoezi, Lungido Primary na Longido Sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Manyara tuna moja, Kateshi Primary, lakini bado Mwanza, tuna Misungwi, Ukerewe, Kagera iko moja, Mugeza, ambayo iko Bukoba, lakini pamoja na hayo, Kigoma, wanayo Kabanga TC na Kabanga Primary. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijajinyima, tukaenda Tabora tukakuta Furaha Primary, Shinyanga iko buhangija na Shy-Bush, ambako kuna Shinyanga Sekondary, Singida kuna Ikungi, kuna Singida Sekondari na kuna Kizega Primary. Kwa Iringa ipo Lugalo, ipo Makalale na Njombe kuna Mundindi Primary, hizo zote kwa ajili ya elimu maalumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbeya tunayo Katumba Two, Katavi tunayo Azimio Primary, Rukwa tunayo Malangale Primary, Kantaramba pia, lakini Ruvuma tunayo Ruhilo Primary, Ruhilo Sekondary, Songea Boys na Songea Girls. Kwa Lindi tunayop Nyangao Primary, lakini pia na Masasi Primary na Ndanda ikafutwa! Waziri anapokuja atuambie, kwa nini Ndanda waliifuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nimeeleza mwanzo, Simiyu hakuna, Geita hakuna, Songwe hakuna, Je, wale walemavu wa kule tunawapeleka wapi kusoma, ni vizuri basi Serikali ijipange na ituambie lini itapeleka shule maalum katika maeneo hayo. (Makofi)

Pia nizungumzie kiwanda cha uchapaji kilichopo chini ya Wizara ya Elimu na Taasisi zake (Press A na Press B). Press A niwapongeze sana, wamefanya kazi nzuri katika mazingira magumo, vitabu hivi haa Wizara ya Elimu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Habari na Utamaduni vyote wamechapa wao. Mashine za kizamani, kazi ya kumaliza siku moja siku nyingine wanafanya siku mbili au tatu, siku nyingine wanalala huko huko, basi Waziri akija atuambie mashine zile wana mpango nazo gani, sambamba na mashine za uchapaji za Press B kwa ajili ya wasioona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nizungumzie kidgo kihusiana na suala lauwekaji wa viwango kwa walimu, viwango vya ushindishaji. Nafikiria labda viwango hivi wanaviangalia kwa watanzania, kuna baadhi ya shule za binafsi, walimu hao wapo wanaojiita walimu, lakini hawana sifa za ualimu, wanafikiria kuongea kingereza ndiyo sifa ya kuwa mwalimu. Tumefika baadhi ya shule tumeenda, tunakuta mtu, tena wanatoka nchi jirani, mwingine hana kibali cha kukaa nchini, mwingine hana kibali cha kufanyia kazi, hana sifa yoyote ya ualimu, lakini amepewa hiyo kazi, ninaomba mpite kwenye hizo shule mkakague. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huohuo nitoe pongezi zangu za dhati kwa wamiliki na wenye shule wote wa private, ambao wamekuwa watiifu na wanafanya kazi vizuri, kuisaidia Serikali kuboresha elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi mazuri yamefanywa katika Wizara hii ya Elimu, lakini kuna madogomadogo ambayo yameguswa inabidi yafanyiwe kazi na kuwekwa sawa. Katika mambo hayo, kuna masuala ya rushwa ya ngono katika vyuo na vyuo vikuu yametajwa, kuna masuala ya wizi wa mitihani, kuna masuala ya upendeleo katika usajili wa vyuo uliopelekea kusajili vyuo ambavyo havina sifa na hatimaye kuwapa wanachuo shida ya kuacha shule mapema au kuondolewa, halafu chuo kinafungwa, wanapata tabu, ni vizuri watuambie, wamejipanga vipi kudhibiti hali hiyo ya rushwa kwenye vyuo, upendeleo kwenye usajili na wizi wa mitihani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla sijamaliza, bado kuna suala lingine la kuzungumzia kuhusiana na elimu kwa redio…

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja asilimia mia kwa mia, na mwisho nasema siasa kwenye chama zinaendelea kwa sababu tunaanza chini tunakwenda juu, ahsante.