Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Salim Hassan Turky

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpendae

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii. Na mimi nachukua fursa hii kumshukuru Allah Subhanah-Wataallah kwa kutujaalia afya njema, tuko mjengoni tunafanya vitu vya uhakika, hatujui kutukana, tunahakikisha nchi yetu inaenda mbele, uchumi unakua na wala hatutatoka hata siku moja ndani ya mjengo huu tunahakikisha Tanzania inakuwa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongesa sana Rais wetu Bwana Magufuli na hali kadhalika Rais wetu wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Shein kwa ushindi wake wa kishindo. Kwa sababu leo kama unavyojua, timu za mpira zikiitwa, timu kama haijahudhuria, timu iliyohudhuria inapewa kombe. Sasa sioni sababu ya watu kunung‟unika kwamba aah, kuna hili na lile. Umeitwa njo kwenye mechi, hujaja, shukuru Mungu jipange tena kwa mechi ijayo. (Makofi)
Mhesjimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nataka sasa nichangie katika uchumi wa nchi yetu. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na wewe nataka nikupongeze sana kwa sababu una nia ya dhati ya kutekeleza kauli aliyoitangaza mwenyewe mkubwa wa nchi hii kwamba hii safari itakuwa ni nchi ya viwanda. Na wewe umekuwa kweli askari wake wa kwanza wa kuhakikisha hili linakuwa na unajitahidi sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mawazo ambayo nataka niyatoe; tutake, tusitake Mji wetu wa Dar es Salaam, ndiyo soko kubwa la wenye viwanda, wenye biashara na kila kitu ni Dar es Salaam na hasa wazalendo wamewekeza sana katika viwanda vyetu. Naomba sana Serikali nayo kama inataka viwanda basi ihakikishe pale Dar es Salaam inajipanga kutafuta eneo na kuwaita wawekezaji wetu wa nchini kwanza waulizwe kwamba wao wana shida gani na tuweze kushirikiana nao kuona kwamba uchumi huu tunakuwa pamoja tunaendeleza vipi nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kama litawezekana Mheshimiwa Waziri, ninaamini kwamba Tanzania hii itabadilika. Vilevile nataka nizumgumze jambo lingine ambalo kwa kweli siyo Wizara husika hii, lakini nataka kusema kwamba Dar es Salaam ni mji wa biashara. Sasa hivi umefika wakati, na mimi naamini Rais wetu yule analiweza, Makao Makuu yahamie Dodoma, Dar es Salaam ubaki kuwa mji wa biashara. Pale ndiyo tutapata hali halisi ya uchumi wetu utakavyokuwa. Kwa hilo wala hatuna haja ya kutafuta fedha, majengo ya Serikali yote yale yaliyokuwepo kama utayabinafsisha kwa bei ya soko la dunia, basi pesa zile zinatosha kabisa kujenga Dodoma yetu mpya na Wizara zote zikahamia hapa. Kwa hiyo, hili nalo litazamwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika uchumi wetu baina ya Bara na Visiwani. Nataka kusema kwamba Zanzibar mara nyingi sana katika Muungano wetu tunakuwa tunaitazama Zanzibar kama mshindani katika uchumi wa Tanzania. Hii fikra nataka tuiondoe. Tanzania ni moja, kwa sababu leo kama Zanzibar itakua kiuchumi, basi tujue kwamba na Tanzania imekua ka sababu Bank of Tanzania ni moja ambayo ndiyo inahimili fedha yetu. Kwa hiyo, uchumi unapokua kokote, sote wawili tunakuwa pamoja. Kwa hili, naomba sana kwamba Wazanzibar wao mashallah wamejaliwa kwamba ni bingwa wa kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyojua Tanzania hii tuna wafanyabiashara wakubwa wawili, tuna Wachaga huku, tunao na Wazanzibar kule wakiongozwa na Wapemba. Sasa ninachotaka kusema ni kwamba lazima tupange uchumi ambao utakua kwa nchi yetu. Nimeshawahi kutoa wazo hapa, sasa hivi, vijana kama tunavyoona wanataka ajira; na ili ajira hizi zipatikane, basi Zanzibar tuitazame kama inakuwa center moja ya uchumi. Sisi sasa hivi ushindani wetu mkubwa ni Dubai. Kila kitu tukienda kununua, tunaenda Dubai. Watu wana ma-account Dubai, wana majumba Dubai, watu wanaenda kununua magari Dubai. Hii Dubai kwa nini tusiisogeze ikawa Zanzibar yetu pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Watanzania wote tusikubaliane kwamba sasa Dubai ya Tanzania ni Zanzibar na uchumi wote uje pale magari yaje pale bidhaa zote zikae pale na ugomvi wa kudaiana ushuru baina ya Bara na Visiwani utaisha. Kwa sababu kama Zanzibar itakuwa freeport leo ukichukua mzigo Zanzibar ukileta Bara unalipa kodi kama zinavyotakiwa. Isipokuwa ukisema leo bandari hii kwamba Bagamoyo au Mtwara iwe freeport, utajizonga mwenyewe, kwa sababu utakamata vipi watu wasikuibie katika nchi moja? Bahari utai-control mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili naomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu tulisimamie kwa nguvu zetu, ikiwezekana mwaka huu tuweke azimio la kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa Dubai ya Tanzania. Hili lazima tufanye kazi pamoja na hapo ndipo uchumi wetu utakapobadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kueleza, Mheshimiwa Waziri toka ameingia madarakani FCC (Fair Competition Commission) pale kuna Bodi ambayo toka mwaka 2015 haipo. Sasa hivi tuna viwanda, tuna makampuni kibao, watu wameuziana share na kila kitu. Hatuwezi kwenda mbele kwa sababu Bodi inatakiwa iwepo pale ndiyo iamue. Sasa hivi kwa kweli ni mwaka wa pili, kesi nyingi ziko pale hazipati maamuzi. Naomba sana wewe ni mtu wa speed, hili ulisamamie kwa nguvu sana liweze kukaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka niseme, na-declare interest, mimi ni mfanyabiashara. Sasa hivi nchi yetu ina ukata mkubwa sana wa sukari. Leo inasikitisha sana kuona kwamba nchi hii watu wanahangaika kutafuta sukari. Miaka 21 iliyopita nchi hii tulibinafsisha viwanda vyetu vya sukari na watu ambao tuliwapa viwanda hivi walituahidi kwamba katika miaka mitatu mpaka mitano, Tanzania itajitosheleza kwa sukari. Leo wenye viwanda hawa inabidi tuwaulize, ni kipi ambacho kimefanya mpaka leo hatujaweza kujitosheleza? Wawekezaji wapya wakija hapa, baada ya muda unaona hawapo, ni kwa sababu gani? Isije kuwa kuna mitikasi ambayo inafanywa kuweza kuendelea na mfumo huu wa kila siku ikifika sukari hamna Tanzania, haitoshelezi. Hapa nataka Serikali iwe macho sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili jana nilikuwa na Mheshimiwa Adam Malima. Mheshimiwa Adam alipokuwepo hapa aliulizwa swali kwamba tunataka kujua cost of production ya sukari katika nchi yetu, mpaka ameondoka Wizara ya Kilimo jibu hilo halikupatikana.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, nawe nakupa swali hili, naomba ukija hapa utupe majibu ya cost of production ya sukari yetu ndani ya nchi hii ni kiasi gani? Halafu lingine mara nyingi sana watu huwa wanazungumza lugha hapa kwamba nchi nyingine zina-subsidize, lakini je, ile figure ya subsidize ni kiasi gani? Pia hatuijui?
Mheshimiwa Mwenyekiti, subsidization wanayopata kule, utakuta ni mtu anapata 10 percent to 12 percent. Leo sisi hapa tunavilinda viwanda hivi kwa kuweka 100 percent protection. Kwa nini tunaweka ushuru wa kiasi hicho? Kwanini tusiweke ushuru wa asilimia 25 au 45 mpaka 50 ili wakati bei duniani ikishuka, basi mtu aweze kufanya biashara hiyo kuweza kuwalisha Watanzania. (Makofi)
Leo katika Tanzania yetu hii, nani anayemtetea mlaji? Hebu niambieni! Sisi tuko wakulima pengine labda milioni mbili, wafanyakazi pengine milioni mbili, lakini watu milioni 40, mfumuko wa bei unawaumiza. Mishahara ambayo kwa kweli iko chini na maisha haya yakipanda kwa kweli hatumtetei haki mlaji huyu, wala hatumlindi. Naomba sana hili litazamwe kwa nguvu zote.
MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja kwa nguvu zote.