Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kusema machache kuhusiana na hoja iliyo mbele yetu. Nianze kwa kusema, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Profesa Mheshimiwa Mbarawa, Naibu wake Mheshimiwa Aweso, timu nzima ya Wizara ya Wataalam ikiongozwa na Profesa Mkumbo na msaidizi wake Engineer Kalobelo, viongozi wote, watendaji na wataalam. Ni miongoni mwa Wizara ambazo kusema kweli zinafanya kazi nzuri, ni kwa sababu tu ya rasilimali fedha zinakuwa zinatuangusha. Tuwatie moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na ya nyumbani kidogo, maana mcheza kwao hutunzwa. Nina miradi ya siku nyingi sana ambayo haijapata fedha. Nikianza na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, kuna visima vilichimbwa tangu mwaka wa fedha 2012/2013, mpaka leo maji yapo lakini wananchi hawajanufaika na jitihada za kodi zao kupitia miradi hii. Miradi hii ipo Masewa, Igaganulwa, Sengerema, Nkololo na Igegu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nkololo ni kichekesho kusema kweli, kwa sababu tumepata msaada kutoka Serikali ya Misri na Waziri wa Ujenzi sasa hivi Mheshimiwa Engineer Kamwele alipokuwa Naibu Waziri wa Maji alienda akatembelea mradi huu. Ni mradi ambao umetoa maji mengi sana, tunataka tuwasambazie wananchi wa center hiyo kubwa ya Nkololo. Amemaliza kuwa Naibu Waziri, akawa Waziri (full minister) wa Maji, maji hayajasambazwa. Mheshimiwa Prof. Mbarawa, rafiki yangu, naomba mtusaidie kwa upande wa miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambao ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu, tuna miradi ambayo tumeleta Wizarani, imesimama miezi sita sasa. Mradi wa Sanungu, Mahina, Nyangokolwa; nilimsikia Mheshimiwa Gimbi asubuhi akiuliza swali la nyongeza, lakini ndiyo hali halisi.

Mheshimiwa Spika, pia Nyakabindi, Bupandagila, kunahitaji kuunganishiwa na kusambaziwa maji kwa ajili ya wananchi hawa na sekondari yetu kongwe ya Bupandagila, wananchi hawapati maji. Kuna Giriku, Kidali Mandam na Mbiti. Kote huko maji yapo, tunataka tu tupate fedha tuwapatie huduma wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Izunya hivyo hivyo. Kisima hiki kina maji mengi sana, tunaweza tukatoa kwa Mitaa yote ya karibu pale Nyamhimbi, Ntuzu na Chenge Sekondari. Yote haya ni mambo ambayo tungependa tuyaone. Ni ombi langu kwa Serikali tuwaone wananchi wa Bariadi kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali hili asubuhi alipoulizwa na Mheshimiwa Gimbi Masaba, naipongeza Serikali yetu kwa hatua ya msingi ya kuanza kutekeleza mradi wa kutoa maji haya Ziwa Victoria na kuyafikisha katika Miji ya Nyashimo, Bariadi, Lakangabilili, Itilima Pale, Maswa na hatimaye Meatu, Kisesa na Mwanhuzi. Huu ndiyo ukombozi kwetu. Hii ndiyo huwa naita kwa ukanda wetu kama Simiyu. Kwetu hii ndiyo royalty, ndiyo mrahaba kwetu wananchi wa Tanzania. Ahsante sana Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli. Sasa tunapata matumaini kwamba mradi huu utaanza kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye nyongeza ya saba, zipo pesa shilingi bilioni 19.5 zimetengwa kwa shughuli hiyo. Naamini tutaanza vizuri. Najua muda wangu siyo rafiki, hayo ambayo yamo humu ndani ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo wanatarajia kuyatekeleza katika mwaka ujao wa fedha iwapo pesa itapatikana kwa wakati yatatekelezwa. Ni imani yangu kwa Serikali kwamba fedha ikipatikana yatatekelezwa na ninaomba iwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nami niseme tu kwa upande wa shida ya maji nawe unajua, ni kubwa. Lazima tufanye kila linalowezekana kuunga mkono jitihada za kuwapatia huduma ya maji wananchi wetu. Wazo la kuondoa kodi kwenye mitambo ya kuchimba maji ni moja njia ya kusaidia. Tulianza vizuri huko nyuma.

Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma tulikuwa tumeondoa kodi kwenye mitambo. Hapa katikati tukajichanganya tena kwa sababu ya ombi letu, misamaha ya kodi imekuwa mingi sana na kadhalika, ndiyo ikatufikisha hapa. Naiomba Serikali tualiangalie tena suala hili. Wenzetu hapa katika East Africa, wote wameshaondoa kodi kwenye mitambo ya maji, ni sisi tu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Fedha, Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla, tumalize biashara hii na private sector isaidie katika kutoa huduma hizi. Tutaona viwango vitashuka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwa hili la hoja ya Kamati. Mimi kama Mbunge, wewe kama Kiongozi wetu, naomba sana, Waheshimiwa Wabunge mnisikilize, naomba sana…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hebu tusikilizane. Kuna lots of talking, please.

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, sisi tusimamie maamuzi yetu. Tuna Azimio la Bunge ambalo lilitaka tuongeze shilingi 50 kwa mafuta. Huu ni mwaka wa tatu mfululizo Kamati inasema; sio mimi, Kamati na ni Azimio la Bunge. Sasa sisi Bunge tusipoheshimu maamuzi yetu, nani atayaheshimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba maamuzi yetu tuyalinde kwa wivu wa hali ya juu sana. Mojawapo ni hili. Napenda sana, maana tunajenga nyumba moja, tusigombanie fito na Serikali. Sisi tumetoa pendekezo hili la kuongeza shilingi 50/= kwa kila lita ya mafuta ya petrol na diesel na tunaona figures tunazozitaka. Tunataka tufikie kiwango cha kupata shilingi bilioni 300 karibu na 20 na kitu kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Serikali itakuja na alternative ambayo inatupeleka huko, sisi tutakuwa tayari baadaye kuja kuondoa Azimio letu kwa utaratibu wa Kibunge. Kwa sasa hivi inakuwa ni very awkward kwamba sisi wenyewe Wabunge tulipitisha Azimio hapa na Serikali ilikuwepo, haikufanya mabadiliko kwenye Azimio hilo na lipo. Sasa tunataka twende kwenye force nyingine, haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, sisi tung’ang’anie kwenye shilingi 50/= kwa lita. Halafu tutaisilikiza Serikali kama ina alternative ambayo ni sustainable, endelevu ya kutufanya tuhangaike na suala zima la maji. Hizi ndiyo kura za uhakika. Unaona, ingekuwa siyo Mfuko huu wa Maji, tungekuwa mahali pabaya sana.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tuiunge mkono Serikali, lakini na Serikali ituelewe sisi kama wawakilishi wa wananchi kwamba tuna hoja ya kujenga na siyo ya kubomoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)