Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja muhimu sana ambayo ipo mbele yetu. Hoja ya maji ni hoja ya uhai na kiukweli mtu unaweza ukaishi bila chochote, lakini huwezi kuishi bila kupata maji. Kitendo cha Serikali kuendelea kutoa fedha kwenye kidogo kwenye Wizara ya Maji kwa asilimia 51 zilizotolewa kwa bajeti iliyopita, kwa mwendo huu hatuwezi kutatua tatizo la maji na ile spirit ya kumtua mama wa Tanzania ndoo kichwani haitafikiwa na spirit ya kutaka mtoto wa kike wa Kitanzania asome, apate full education, awe mtu wa maana haitafikiwa. Vile vile pia spirit ya kuona kwamba kila Mtanzania au wananchi wote wanaenda kwenye shughuli za maendeleo na kuachana na shughuli za kusaka maji haitakaa iishe. Kwa hiyo kwanza ni lazima kwenye Sekta ya Maji fedha inapotengwa kwenda kufanya kazi ya kuleta maji itoke kikamilifu ikafanye kazi ya kuleta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono Wabunge wote waliosimama kusema kwamba Mfuko wa Maji uongezewe; Mfuko wa Maji lazima uongezwe. Hatuna namna nyingine zaidi ya kuhakikisha kwamba kuna fedha ya kutosha kupeleka maji kwa wananchi wetu. Tumeona mfano mdogo wa REA, sasa hivi kila Mbunge akisimama anagusia REA japo sio vijiji vyote angalau kuna kazi imefanyika imeonekana. Kwa hiyo, naiomba Serikali na naomba niungane na wale wote waliosema patachimbika Jumatatu hapa kama fedha ya Mfuko haitaongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kaliua tuna shida kubwa sana ya maji; mwanamke wa Kaliua anateseka sana, mtoto wa Kaliua hata shuleni wanakwenda kuvamia kwenye nyumba za watu kutafuta maji ya kunywa; nyumba za walimu na wananchi waliopo jirani. Wilaya ya Kaliua tunaomba kipaumbele cha hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kaliua kwanza kabisa jiografia yake na Mkoa wa Tabora hatuna maji ardhini, kwa hiyo Miradi yote ya Maji ya World Bank na visima hatunufaiki navyo kwa sababu hatuna maji ardhini. Kingine jiografia ya maeneo yetu hakuna mito kama ambayo inatamkwa Morogoro, Kaliua, Tabora hatuna mito hiyo, tuna Mito ya Igala na Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa na mpango wa kutoa maji Malagarasi kuleta Kaliua na Wilaya ya Urambo, lakini pia mradi mwingine ni kutoa maji Victoria kuja mpaka Igunga, Nzega, Tabora na Uyui. Ule mradi wa Malagarasi ambao sasa hivi ni mwaka wa nne ulikuwa umetengewa fedha kidogo kidogo ya kuanza kufanya usanifu yakinifu…. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Sakaya…

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: mpaka leo hakuna chochote ambacho kimefanyika…

SPIKA: Mheshimiwa Sakaya kidogo…

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: mwaka huu Serikali imekuja na mpango kwamba…

SPIKA: Mheshimiwa Sakaya kidogo tu, Waheshimiwa Wabunge hebu tupunguze sauti, hata sisi wenyewe tunaweza kusikia hasa upande huu wa CCM, kwa nini CCM hatusikilizi? Tutulie kidogo hata kama unaongea na mtu, ili mjadala uwe na maana, lakini sasa maeneo haya, ni kama mikutano ya hadhara kabisa. Endelea Mheshimiwa.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuona kwamba mradi ule wa Malagarasi utakuwa na gharama kubwa, umekuja na mpango mwingine wa kuweka Kaliua na Urambo kwenye mradi wa miji 29. Nashukuru kwa kuwa tumewekwa kwenye huu mradi wa miji 29 ila kwa hamu kubwa ya maji ambayo tunayo, tunaomba huu mradi uende haraka tuweze kufanikiwa kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Kaliua imewekwa kama ni sehemu ya Urambo, nakubaliana kweli Wilaya ya Kaliua tulizaliwa kutoka Urambo lakini ni Wilaya inayojitegemea, inayosimama, tuandikwe kama Wilaya na sio mtoto wa Urambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa tumepata mradi huu ambao ni wa miji 29, lakini bado kwa mradi alivyosema Mheshimiwa Waziri ni kwamba, utalisha kilomita 12 kutoka barabarani kuja Wilaya ya Kaliua. Jiografia ya Wilaya ya Kaliua ni kubwa sana, kutoka Makao Makuu ya Wilaya kuna mwananchi anayeishi kilomita 120, kilomita 90, kilomita 60, kilomita 30 mpaka unafika. Kwa hiyo, mwananchi huyo ambaye anaishi kilomita 60 atapata wapi maji? Huyu wa kilomita 90 na kilomita 120 watakunywa wapi maji? Naomba waifahamu jiografia ya Kaliua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba pamoja na mradi huu ambao wa miji 29, lazima uwepo mradi mwingine wa kuweza kutoa angalau maji kutoka Mto Ugala ambao ni mto pekee ambao tunao Kaliua uweze kulisha wananchi ambao wapo mbali ambao hawatanufaika na mradi wowote, aidha ni Malagarasi hautawafikia au ni huo wa kutoka Mjini Tabora hautawafikia. Kwa hiyo, ni lazima kuwepo na mpango wa kuhakikisha wale ambao hawanufaiki na mradi huu uliopo wanapataje maji kwa sababu na wenyewe ni Wanakaliua na ni Watanzania, wana haki ya kupata maji na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia kuna mradi mdogo ambao unaendelea pale Kaliua Mjini ambao ni wa Kata ya Kaliua na Kata ya Shokora, naomba pia Serikali itoe fedha kwa wakati mradi huo ambao ni mradi wa Kata mbili tu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mradi mwingine ambao tunaomba Serikali itusaidie, tumepata kisima kimoja kimechimbwa na GTI pale Kijiji cha Usindi, Kata ya Ushokola. Maji yale ni mengi sana, tunaomba Serikali isaidie kuyasambaza yaweze kulisha eneo kubwa, kwa sasa hivi yamelisha kijiji kizima cha Usindi. Tunaomba iwekwe nguvu ya kutosha na GTI wapo tayari kusaidiana na Serikali uweze kusambazwa, uweze kulisha angalau kata nzima, inawezekana na ni kisima cha kwanza katika Wilaya ya Kaliua kuweza kuchimbwa kikawa kina maji ya kulisha angalau kata nzima. Kwa hiyo, naomba Serikali iweke nguvu zake pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye Wakala wa Uchimbaji; mwaka 2016/2017, Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa walikuja Kaliua wakafanya utafiti katika maeneo mengi, wakaainisha maeneo tisa ya kuchimba mabwawa na wakasema kutokana na jiografia yetu, watafanya haraka kuweza kuja kutusaidia kuchimba mabwawa ili tukusanye maji ya mvua, lakini mpaka leo ni mwaka wa tatu hakuna kilichofanyika. Kwa hiyo, naiomba Serikali wale Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa waje Kaliua, tayari walishakuwa na mpango ule, waweze kuhakikisha kwamba maeneo yale yaliyoainishwa yanachimbwa mabwawa tuweze kukusanya maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni uvunaji wa maji. Bajeti ya mwaka 2017/2018, Serikali ilikuja na mipango mizuri sana hapa Bungeni kwamba ilikuwa imetoa maagizo kwenye Halmashauri zote nchi nzima na kutunga sheria ndogo kuzitaka taasisi za kijamii, asasi na watu binafsi kujenga miundombinu ya kuvuna maji. Pia wakati huo huo ikatuambia kwamba Serikali ilikuwa imetoa mafunzo kwa wananchi karibu 795 kwa ajili ya kutumia mbinu sahihi na nyepesi kuvuna maji.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali ikasema ilikuwa imejenga matenki makubwa 29 na 59 na ukubwa tofauti kukusanya maji katika Wilaya mbalimbali. Sasa nategemea Waziri akija ku-wind up atuambie huu mpango umefikia wapi? Wananchi wangapi wameendelea kupewa elimu na matenki mangapi yameendelea kujengwa? Pia tujue kwamba maagizo yaliyotolewa kwenye Halmashauri mbalimbali yametekelezwa kwa kiasi gani.

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa mtu anayetoka nje kuiona Tanzania, akiona mvua zinaponyesha maji yanavyosambaa yanavyoharibu miundombinu akisikia tunalia maji hapa Bungeni, atatuona kama tumechanganyikiwa kiasi fulani kwa sababu hakuna juhudi ya kukusanya maji haya, hatuyakusanyi kabisa, yanakwenda kuharibu barabara, nyumba na kila kitu lakini kilio cha maji kipo pale pale. Kwa hiyo, kwa maana nyingine lazima Serikali ijipange kikamilifu kukusanya maji ya mvua, hii ni neema wakati mwingine, tuitumie kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo la maji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)