Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza jina langu naitwa Japhet Hasunga, siyo Joseph.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kwanza kushukuru kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii. Pia napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa na mchanganuo mzuri ambao ameuwasilisha leo hii, kwa kweli nimefurahi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa uchambuzi wa kina walioufanya na kuiwasilisha katika Bunge lako Tukufu. Kwa kweli ni nzuri sana na imejenga msingi mzuri wa nini kinatakiwa kufanyika katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuchangia katika Sera ya Elimu ya shule za msingi na sekondari ya mwaka 2014. Sera hii ni nzuri sana ambayo imeandaliwa na iliwasilishwa na ilishirikisha wadau mbalimbali ambayo imeweka bayana hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba nchi yetu inabadilika kwa hali tuliyonayo na kwenda mahali ambapo ni pazuri. Elimu ni kitu muhimu sana, elimu ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yoyote na hii ndiyo itakayotusaidia kutufikisha kuwa nchi ya kipato cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu hii sasa hivi vijana wetu wengi ambao wamekuwa wanamaliza elimu ya msingi, wanamaliza wakiwa ni wadogo sana, wengi wanaanza darasa la kwanza wakiwa na miaka mitano, miaka sita wanamaliza shule ya msingi wakiwa na miaka kumi na mbili, kumi na tatu. Hivyo hawa-qualify kujitegemea wala hawawezi kujiajiri wala kuajiriwa, kwa sababu itakuwa ni kinyume na sheria za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo sera hii ilikuwa inasema elimu ya msingi sasa itajumuishwa na elimu ya sekondari mpaka kidato cha nne. Mtoto akianza shule ya awali aende moja kwa moja shule ya msingi, akimaliza shule ya msingi anaunganisha moja kwa moja kwenda kidato cha kwanza. Kwa hiyo, ina maana watoto wote sasa watakuwa wanakwenda mpaka kidato cha kwanza wanamaliza mpaka kidato cha nne. Hapa mpaka wanamaliza sasa watakuwa wamefikisha umri ule ambao kidogo wanaweza wakaanza kujitegemea au wakaajirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili nafikiri ni la msingi sana. Sasa nataka Wizara wakati wa majumuisho itupe maelezo ni hatua gani au mikakati gani wameiweka kuhakikisha kwamba sera hii sasa inaanza kutekelezwa kama ambavyo tulikusudia. Kwa sababu ifikapo mwaka 2018 ni kesho kutwa tu tutakuwa tumefika. Tungependa kikifika kipindi hicho watoto wote sasa wawe na uwezo wa kufika hadi kidato cha nne, badala ya kuishia darasa la saba ambapo wanakuwa kidogo hawajaandaliwa vya kutosha hilo ni la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna suala la watoto wanaopata mimba wakiwa shuleni. Mimba inapatikana kwa bahati mbaya, nasema ni kwa bahati mbaya siyo kwa makusudi, watoto wengi wamekuwa wakipata mimba kwa bahati mbaya mashuleni. Sasa watoto hawa wanapopata mimba, ni bahati mbaya unakuta kwamba baada ya muda wanaondolewa mashuleni kwa sababu eti wana mimba. Hii inakuwa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia ni kinyume na dira ya Wizara ya Elimu ambayo imeitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu, ukurasa wa nne pale, ameeleza dira vizuri sana, kwamba dira ya Wizara ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa. Hivi ndivyo dira inavyosema na hii dira haijabagua mtoto wa kike wala kiume. Kwa hiyo ina maana watoto wote ni muhimu na mtoto wa kike sasa hivi ndiyo muhimu sana kumwelimisha kuliko hata mtoto wa kiume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kabisa kwamba hawa watoto ambao kwa bahati mbaya wanapata mimba basi wapewe nafasi ya kuendelea kusoma pale wanapokuwa wamejifungua ili kusudi waendelee kuelimika maana nao ni Watanzania kama Watanzania wengine. Hili ni la msingi sana na litatusaidia kuhakikisha kwamba sasa jamii yote ya Kitanzania Watanzania wote wanapata elimu sawa na ile ambayo tulikuwa tunakusudia. Nadhani kwamba hilo ni suala la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nichangie katika hii Wizara ni kuhusu Mitaala. Mitaala ya elimu yetu kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu lazima hii mitaala iangaliwe kwa undani ili iendane na maarifa na stadi zinazohitajika sokoni. Iwaandae vijana wetu kujitegemea, iandae wataalam watakaochangia na watakaoweza kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mitaala yetu haijaainisha vipaumbele ambavyo Taifa kama Taifa linahitaji. Watu wanasoma tu wengine wanajiunga katika vyuo mbalimbali, sasa vyuo hivi viendane na mahitaji halisi ya soko, ndiyo itatusaidia sana kwenda na wakati. Hili ni la muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nilichangie ni kuhusu tafiti yaani research na project mbalimbali ambazo vyuo mbalimbali vimekuwa vikiwapa vijana wanafanya katika maeneo mbalimbali. Sasa hivi vyuo vingi havijatilia mkazo sana katika upande wa utafiti, vyuo vikuu vingi havifanyi utafiti wa kutosha. Bila kufanya utafiti wa kutosha hatuwezi kupata wataalam, hatuwezi kupata maendeleo halisi. Lazima vifanye utafiti na Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha hao wataalam wetu wanafanya utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti hizi ndizo zinatakazosaidia kuboresha mazingira na kuleta maendeleo katika nchi yetu. Kuna maeneo mengi ambayo vijana huwa wanafanya na kuna baadhi ya project ambazo vijana huwa wanapewa wakiwa mashuleni. Wanafanya project nzuri sana. Naishauri Wizara iandae utaratibu mzuri wa kuhakikisha zile project ambazo vijana wanafanya wakiwa vyuoni zingine zinafaa sana kuendelezwa, zingine zingefaa sana katika kuanzisha viwanda vidogo na kadhalika. Wanafanya ubunifu mzuri sana ambao nafikiri ni muhimu sana kama Wizara itakuwa na utaratibu mzuri, wa kuziangalia hizo project na kuangalia namna ambavyo Serikali inaweza ikazi-fund ili ziweze kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu Vyuo vya Ufundi, Vyuo vya VETA, pamoja na Vyuo Vikuu, Jimbo langu ni Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Songwe na hiyo naipongeza Serikali sana. Pamoja na kuwa ni Makao Makuu ya Mkoa sasa hivi hatuna chuo hata kimoja, hatuna chuo cha Serikali wala cha watu binafsi. Sasa ni wakati muafaka naomba Wizara yako iangalie utaratibu, iweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Vwawa hasa Wilaya ya Mbozi tuna jenga chuo cha VETA ambacho kitawaajiri vijana mbalimbali waliopo katika Wilaya ile. Wale vijana wako maeneo mengi, iwe ni katika fani mbalimbali wapate ule ujuzi ambao utasaidia sana katika kuchangia maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Vyuo vya Elimu ya Juu kikiwemo Chuo Kikuu Huria, tungeomba vianzishe matawi haraka ili wananchi wale ambao ni wengi sana katika ile Wilaya waweze kupata elimu ile ambayo inahitajika katika hili eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa nichangie ni kuhusu suala la hii SDL, hii kodi ambayo sekondari za watu binafsi na vyuo vya watu binafsi vinatakiwa kulipia, SDL ya five percent. Kwanza naomba ku-declare interest kwamba mimi ni mdau na nina maslahi katika hili, hili suala sasa hivi sekondari zote za watu binafsi pamoja na vyuo binafsi vinaendelea kudaiwa SDL kwamba lazima vilipwe, wakati navyo vinatoa mafunzo ya ufundi ambao vinawaandaa vijana wale wale na sera za nchi hizi zinasema elimu siyo sehemu ya biashara, elimu ni kutoa huduma. Sasa kama ni huduma kwa nini vidaiwe SDL badala ya kupata mgao kutoka Serikalini unaotokana na hizi fedha, wanaambiwa wao wachangie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili kwa kweli halikubaliki kabisa, ningeomba kabisa kabisa kwa dhati Serikali iliangalie upya ili hizi shule za watu binafsi, vyuo vya watu binafsi, vipewe msaada, vipewe mgawo wa hii SDL ili viweze kujenga ujuzi, stadi na maarifa mbalimbali yanayohitajika katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri haya masuala ya msingi sana na naamini tukiweka misingi mizuri ya kuimarisha elimu yetu nchi yetu itapiga hatua sana. Wale wanaobeza kwamba nchi yetu elimu yetu inashuka, hapana haishuki tuendelee kuiboresha, tuweke mikakati mizuri, tuiimarishe, naamini nchi yetu itapiga hatua sana. Wenzangu wale ambao wanategemea kwamba eti mwaka 2020 tutaishia hapa labda CCM itaporomoka, nataka niwaambie CCM mwaka 2020 tutashinda huenda Viti vyote vya Ubunge kwa sababu ya kazi nzuri ambayo tutaifanya. Hii Wizara naomba ifanye kazi nzuri na mambo yatakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.