Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliye nijalia afya na uzima na hatimaye nimeweza kusimama kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa pongezi katika Wizara ya Maji. Nisipolisema hili, Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wao watanishangaa sana, kwa sababu nimezunguka sana, katika Ofisi za Wizara ya maji na hatimaye kile nilichokuwa nakifuata kimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii, kuwashukuru sana, Wizara ya Maji na Watendaji wote, Kata ya Tinde na vijiji vyake vyote vilikuwa vimesahaulika kwenye Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria. Nilisimama humu ndani nikasema, namshukuru sana Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, alilipokea, tukaa kikao Ofisini kwake na Watendaji wake na hatimaye mradi ule sasa unakwenda kuanza kutekelezwa mwezi huu wa Mei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya, vijiji vyote vilivyopo Kata ya Tinde, vinakwenda kupata maji ya Ziwa Victoria. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa, yale yaliyofanywa na Mheshimiwa Eng. Kamwelwe uyaendeleze na mradi ule uende kukamilika. Mradi ule unaenda kutekelezwa kuanzia mwezi huu wa Mei na utafanya kazi ndani ya miezi saba, nikuombe sana, uende ukasimamie na mradi huu uweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisiishie mradi huo, nilisimama ndani ya Bunge hili lakini nimezunguka sana Ofisi za Wizara ya Maji kwa ajili ya mradi wa maji Kata ya Masengwa. Mradi huu umeanza kufanya kazi na unaendelea vizuri. Niwashukuru sana Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa lililopo, fedha kwa Timu iliyoundwa kwa ajili ya kufuatilia mradi huo wa maji hazijapelekwa hata senti tano. Hivyo, tunaipa kazi kubwa Timu ya ufuatiliaji kufanya kazi kwa kutumia pikipiki kwa sababu hawajawezeshwa kwenda kusimamia mradi huu. Niwaombe sana Wizara ya Maji wapeni Halmashauri fedha hizo ili waweze kuusimamia Mradi wa Masengwa kama ambavyo ilikuwa imepangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akini Mradi wa Masengwa wameleta hati ya madai ya shilingi milioni 94 kwa ajili ya mradi huu, malipo hayo bado hayajafanyika. Niwaombe mtoe malipo hayo ili kazi hii iweze kuendelea na kuweza kukamilika mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu katika Mradi wa Maji wa Masengwa. Mradi huu una zaidi ya shilingi bilioni nne, ni mradi mkubwa sana na kuna tenki kubwa ambalo linakwenda kujengwa. Kulikuwa na mradi awamu ya kwanza, awamu ya pili na awamu ya tatu. Awamu ya kwanza, ndiyo huu ambao unatekelezwa. Niwaombe sana Wizara ya Maji, toeni pesa kwa ajili ya usanifu kwa awamu ya pili ya Mradi wa Maji wa Masengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya Mradi wa Masengwa utakwenda kutekeleza Vijiji vya Ishinaburandi, Isela, Idodoma na Ibingo. Hawa watu vijiji vyote hivi watanufaika kupata maji katika mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumzia Mradi wa Maji wa Masengwa, naomba nijikite katika vijiji ambavyo vipo nje na Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria. Vijiji hivi ambavyo haviko ndani ya kilomita 12, haviguswi popote na Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria lakini hakuna namna yoyote ya vijiji hivi kuvipatia maji. Vijiji hivi viko 23, naomba nivitaje baadhi. Vijiji vya Mwasenge, Nyang’ombe, Nyaligongo, Bushoma, Kilimawe, Mwamala, Bugogo, Masonula, Igalamya, Singita, Chabuluba, Mwamkanga, Msalala, Supigu na Masokelo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vijiji hivi 23, vina idadi ya watu 59,241. Wizara ya Maji mmejipangaje kuhakikisha kwamba vijiji hivi 23 tunaleta mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba watu hawa na wao wanakwenda kupata maji. Akina mama wanahangaika, hawawezi kufanya shughuli zozote za kiuchumi kwa kutafuta maji, ukiangalia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria uko mbali nao, je, Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha vijiji hivi na wao sasa wanakwenda kupata maji ya uhakika ili na akina mama hawa waweze kufanya kazi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, niingie katika vijiji ambavyo viko ndani ya kilomita 12 lakini havijapata maji mpaka leo. Toka awamu ya kwanza ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria vijiji hivi havijapata maji na viko ndani ya kilomita 12. Kila nikisimama ndani ya Bunge hili huwa nasema, naomba pia nivitaje tu. Vijiji hivi viko 22 toka awamu ya kwanza ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria. Vijiji hivi vina idadi ya watu 58,465 ambao wako ndani ya kilomita 12 lakini hawapati maji ya Ziwa Victoria wanayaona yanakwenda kwa wenzao. Vijiji hivi ni Mawemilu, Buduhe, Azimio, Mwandutu, Ibubu, Mapingiri, Mwashagi, Mwamala, Mwabagehu, Mwashilugura, Mwambasha, Mwalukwa, Bulambila na Shatimba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haipendezi toka awamu ya kwanza ya Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria, hawa watu wanapewa matumaini kwamba watapewa maji, wako ndani ya kilomita 12, lakini mpaka tunakwenda awamu nyingine sasa hawajapata maji.

Je, Wizara mna mpango gani kuhakikisha vijiji hivi 22 vinakwenda kupata maji kwa sababu wanaishi kwa matumaini wakitegemea kwamba siku moja na wao watapata maji kwa sababu utaratibu unawaruhusu wako ndani ya kilomita 12. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusemea hilo, naomba niingie katika Manispaa ya Shinyanga, Mradi wa Maji wa Galamba. Mradi huu umeanza kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Shinyanga lakini kwa masikitiko makubwa, toka Agosti, 2018, Halmashauri imeleta hati ya malipo ya shilingi milioni 131 mpaka sasa hivi fedha zile hazijalipwa na mradi ule umesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunaposema Wizara ya Maji kuna tatizo huko chini angalieni. Inawezekana huku juu mko vizuri sana lakini Mheshimiwa Waziri hebu jaribu kuangalia Ofisini kwako kuna shida gani kwa sababu Wabunge wengi pia wanalalamika hati hizi zikiletwa fedha hazitolewi kwa wakati. Fikiria toka Agosti, 2018, fedha hizi hazijalipwa mpaka leo, kuna tatizo gani katika Mradi wa Maji wa Kijiji cha Galamba katika Manispaa ya Shinyanga? Nimuombe sana Waziri alifanyie kazi suala hili na nitafurahi kama nitapata majibu kabla hujahitimisha mjadala wako kujua Mradi wa Maji ya Galamba mmewapelekea pesa au unanipa majibu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Tunazunguka kukagua miradi mingi katika Halmashauri hapa nchini lakini katika miradi mibovu ambayo tunakutana nayo ni miradi ya maji. Sijui kuna tatizo gani, miradi mingi unakuta ama maji yanatoka lakini tenki linavuja. Serikali imewekeza fedha nyingi lakini unakuta mradi ule hauna tija kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi najiuliza miradi ile inasimamiwa na Wahandisi haya matatizo yanatokea wapi? Mheshimiwa Waziri jaribu kuangalia, fedha nyingi ya Serikali inakwenda kule lakini miradi mingi ina matatizo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Azza, muda wako umekwisha.

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono. (Makofi)