Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ambayo ameiwasilisha Waziri ma Maji.

Kwanza niunge mkono hoja na kwamba nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo pamoja na kwamba kuna changamoto za hapa na pale hizo tunatarajia kwamba kutokana na haya ambayo yanayozungumzwa na waheshimiwa Wabunge yatashughulikiwa ili kusudi kazi ya kuwapelekea maji wananchi wetu kwenye majimbo yetu na kwenye halmashauri zetu yanafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, nishukuru Serikali kwamba Korogwe mji nimeona wanasema kwamba nimo kwenye orodha ya miji ambayo itapewa maji kutoka fedha za mkopo wa India. Nikiangalia kwenye kitabu ukurasa wa 148 kwenye ile orodha waliyoiweka pale hiyo Korogwe Mji yenyewe haijawekwa imewekwa HTM lakini miji iko 29 ni namba saba na HTM nachofahamu ni mradi ambao unapelekea maji Handeni.

Mheshimiwa Spika, sasa nisije nikawa vile napewa kama hisani niombe tu waniambie watakapokuwa wanasema hapa ili wananchi wangu nitakapokuwa naenda kuongea nao ninapowaonyesha kitabu hiki kwamba tupo kwenye mradi ule wa India lakini kwenye kitabu humu hatumo imeandikwa HTM na kule wanajua HTM ni Handeni basi ni vizuri atakapokuwa ana-wind up hapo atamke kwamba huu mradi na Korogwe Mji ambako ndio kwenye chanzo cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa HTM unatoka Tabora kwenye chanzo cha maji ni Tabora kwenye kata yangu ya Korogwe. Sasa kama sionekani humu naonekana tu kwamba nipo kwa kuelezwa tu maneno na kuambiwa humo humu sijui nawaambia nini wananchi wangu wa Korogwe. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakapokuwa una-wind up hapo ni vizuri basi ukawaeleza wananchi wa Korogwe wajue kwamba hicho chanzo cha maji cha Tabora ambacho kitapeleka maji kule Handeni basi na Korogwe mtapatiwa maji kutoka kwenye hichi chanzo cha maji, nashukuru sana endapo waziri atalisemea hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nikupongeze na nikushukuru sana sana ulikuwa umepita umeenda ulifanya ziara kule Lushoto nilikupigia simu nikakuomba nikakwambia ndugu yangu naomba unipitie hapa kwenye ratiba yako haikuwemo uliweza kupita. Nikawa nimekueleza suala la mradi wa maji wa ule vijiji 10 nikushukuru sana sana kwa hatua ambazo umezichukua kwamba mradi ule wa vijiji kumi vile viwili tayari kwa maana ya kwamba Msambiazi tayari wanapata maji lakini sasa hivi wanaendelea yule mkandarasi anaendelea na ujenzi wa ule mradi wa Luengela relini na darajani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sana nakushukuru vilevile baada ya ku-raise ile certificate umeweza kumlipa yule mkandarasi hili nakushukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki na kwamba kazi inaendelea vizuri kwenye ule mradi na bahati nzuri tena wameshatuma ile certificate nyingine ili kusudi muweze kuwalipa. Nimeona ni vizuri nikakushukuru kwa sababu nisipokushukuru kwa hili nalo nitakuwa sijakutendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri nina mradi wa maji ambao tulipewa milioni 500 uko pale pale mjini, shida ya Korogwe Mji tuna mto unapita pale, Mto Pangani. Lakini tuna tatizo la maji pale mjini kana kwamba hatuna chanzo cha maji, Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo wakati ule ndugu yangu Mheshimiwa Kamwele alitembelea Korogwe akazunguka akakuta kwamba tuna mto unapita pale akaamua kwamba tuutumie ule mto ndipo akatuletea fedha milioni 500 imeshajengwa intake imekwisha imejengwa tayari chujio limemalizika. Kilichobaki sasa ni miundombinu ya kuwapelekea wananchi maji.

Mheshimiwa Spika, hivi navyokwambia Korogwe kila siku kuna kipindupindu kuanzia mwezi wa tatu wananchi wangu ni kipindupindu, mwezi wa nne, mwezi huu hivi navyozungumza watu wako vitandani ni kipindupindu wanakwenda kuchota maji kwenye mto, lakini mkitumalizia mradi huu tutapunguza hili tatizo la kipindupindu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri alitembelea mradi huu aliuona na Mheshimiwa Rais alipokuwa amekuja kufungua ile stand yetu mpya alituahidi kutupa fedha za kumalizia hiyo miundombinu bilioni 2 ili kusudi mradi ule ukamilike. Sasa wananchi wa Korogwe kila siku wanasubiri na kuniuliza Mheshimiwa Mbunge kwamba Rais alituahidi mbona huu mradi haukamiliki.

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara naomba basi muutembelee ule mradi Naibu Waziri aliuona upo mradi ule pamoja na kwamba mnasema mmeniweka kwenye huu mradi wa fedha za India lakini zile milioni 500 ambazo zimeshajenga intake zimemaliza na intake nzuri zimejenga chujio imekamilika, tutaufanya nini huu mradi? Hivi tuendelee kusubiri mtoto anasema nataka nguo, unasema subiri na mwenzako mama yako ana mimba subiri kwamba atakapojifungua ndio niwanunulie wote nguo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, nakuomba utembelee mradi ule Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji nakuomba utembelee mradi ule uone jinsi ulivyojengwa na hatimaye wananchi wa Korogwe Mjini waweze kupatiwa maji yaliyo safi na salama waondokane na tatizo la kipindupindu, ni aibu kusikia kila siku tuna kipindupindu Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji wanafanya kazi nzuri sana lakini kuna tatizo, tatizo liko kwa wasaidizi wao. Fedha zinazopelekwa kwenye miradi huko zinaweza zikapelekwa fedha zinaende kutengeneza mradi fulani unakuta ule mradi unaweza ukawa umekamilika lakini maji hayatoki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika niko kwenye Kamati ya LAAC tumepita kukagua miradi tumekuta matatizo ya aina hiyo, unaweza ukawa umejengwa mradi haujakamilika lakini amemaliziwa fedha zote amelipwa mkandarasi lakini mradi haujakamilika. Matatizo haya yanatokana na wasaidizi walionao huko chini wanaonekana ma-engineer wanakula pamoja na hawa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mkandarasi akalipwa fedha zote lakini mradi haujakamilika kwa nini alipwe fedha zote na hali mradi haujakamilika? Ushahidi ni pamoja na ninyi wenyewe tumewaona kabisa mnavyozunguka mnavyofanya ziara kwenye kukagua miradi ya maji mmeenda kuyakuta matatizo haya. Kwa hiyo, tukuombe sana tunakutakia kila heri Mheshimiwa Waziri tuajua unapambana unapata shida.

Mheshimiwa Spika, wapo ma-engineer wako sugu huku chini huko nyuma inaonekana walishazoea kuona kwamba miradi ya maji ni shamba la bibi, ndugu yangu jikaze funga mkanda, Katibu mkuu jikaze mfunge mkanda haya majitu yaliyokaa huku yaliyokuwa yamezoea huko nyuma yashughulikieni ili kusudi muweze kufanikiwa, msipofanya hivyo tutasema fedha hazitoshi tutatafuta fedha zitakwenda lakini zitakwenda kuliwa hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mhehimiwa Waziri na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu atakusaidia tu utafanikiwa, mkifanikiwa kuwashughulikia hawa huko chini basi nadhania hata hizi fedha tunazosema ziongezeke zitaweza kwenda kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napenda kuunga mkono suala la kutumia force account. Fedha za maji kama tutatumia force account inawezekana kabisa tukafanikisha kama tulivyofanikisha kwenye miradi ya afya, kwenye miradi ya shule. Kuna ubaya gani? Ma-engineer hawa si wapo na tukitumia hii force account kwa sababu tuna watu ambao tayari kule kwenye wilaya zetu wastaafu waliostaafu kwenye masuala ya maji watafanya hizi kazi kwa kutumia hii force account. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutashuhudia tunafanya kazi ya miradi ya maji kwa gharama nafuu kuliko sasa, sasa hivi haya mambo ya wakandarasi mradi mdogo tu kwa mfano kisima cha maji mtu anakwambia kisima cha maji ni milioni 350 kitu ambacho mradi huo unaweza ukakamilika kwa milioni 20 tu wananchi wakapata maji kwa sababu mkipeleka kwa force account hata wananchi watashirikishwa na kwa sababu wanashida watafanya kazi zile ambazo wananchi wanahitajika kusaidia kuhakikisha Serikali inawapatia maji pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naunga mkono suala la kutumia force account. Lakini naunga mkono vilevile suala la kuongezea ile shilingi 50,000 hebu tuzingatie kusimamia maazimio tuliyoyapitisha humu ndani. Tuliyapitisha wenyewe haya maazimio tukisaidia kuongeza hii shilingi 50,000 utatuna huu mfuko na hatimaye angalau hata tunayoshauri haya yanaweza yakatekelezeka vizuri.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafikiri ni vizuri basi katika hili wenzetu watusikie na wasikilize ili kuona kwamba tunaweza tukafanikisha katika kuwapatia maji wananchi wetu huko kwenye miji yetu na kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)