Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara ya Maji leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri wa Maji Prof. Mbarawa, Naibu Waziri mdogo wangu Mheshimiwa Aweso na viongozi wote wa Wizara ya Maji kwa jinsi wanavyopambana kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza mdahalo huu toka tumeanza majuzi utaona kwamba kilio kikubwa cha Wabunge ni juu ya changamoto ya miradi ya Maji ambayo haikamiliki. Mimi binafsi najiuliza, tatizo liko wapi kwa sababu ingekuwa hakuna tatizo Wabunge wasingekuwa wanalalamika juu ya miradi yetu,

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa sababu katika hotuba yake amekuwa mkweli sana kwa kuainisha changamoto za Wizara hii. Ziko changamoto kama nne hivi, mojawapo ni upatikanaji wa fedha. Mimi hii siwezi kumlaumu Mheshimiwa Waziri, hata kidogo, kwa sababu mambo mengine ni ya kiserikali zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zaidi changamoto namba mbili ambayo inasema uwezo mdogo katika usimamizi wa miradi. Hapa ndipo kwenye tatizo na lazima nikubali na tukubaliane kwamba hapa pana syndicate, kuanzia Halmashauri mpaka Mikoani. Wahandisi hawa tunaowapa miradi, mimi Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, nimeona pana mabadiliko katika Wizara pale lakini hili zoezi lazima liende mbali zaidi ikiwezekana unda timu ndogo ianzie kwenye malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba kwa nini miradi inalalamikiwa, kwa nini kuna ufisadi kwenye miradi, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kujua sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja tu na nitamwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake watafute ripoti moja tu ya CAG ambayo inahusu performance audit kwenye miradi ya maji. Ukiipitia taarifa moja utapata picha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuanzisha RUWASA kwamba ma-engineer wale wa Halamashauri moja kwa moja watawajibika Wizarani lakini inawezekana ikawa ni mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya. Watu ni walewale na utaratibu ni uleule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa aliyekuwa Waziri wa Maji alianzisha utaratibu wa kufuatilia miradi ya maji kwa kutembelea Tanzania nzima kuangalia status ya miradi ya maji. Kuonyesha pana syndicate kubwa, siku moja wakati Wizara imeitwa kwenye Kamati ya PAC nilimwambia Katibu Mkuu Profesa kwamba vijana wako hawakufika Kilindi na maafisa pale Kilindi wakasema hawa tumekutana nao Handeni tu, hawakufika. Kwa hiyo, taarifa kuhusu miradi ya maji Kilindi ni ya uongo. Hii ndiyo kuonyesha kwamba pana syndicate kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefanya ziara Jimboni Kilindi alijionea hali halisi ya changamoto ya maji na nikakuomba kwamba Kilindi haitofautiani na Handeni Vijijini na Handeni Mjini, wao wamefaidika na mradi wa HTM sasa huwa mbapa leo najiuliza hao wataalamu ambao walisema kwamba mradi wa maji ufike Handeni ambayo ina changamoto sawa kabisa na Wilaya ya Kilindi, hivi hawakuiona Kilindi? Hayo tuyaache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Waziri tunahitaji mradi mkubwa unaofanana na HTM kwa sababu Wilaya ya Kilindi tuna vijiji 102 na vitongoji 615 ni vijiji 30 tu kati ya 102 vyenye maji. Ili tuweze kupata suluhu ya kudumu ya maji lazima tupate mradi mkubwa kuanzia Mto Pangani ambao uko Korogwe sawa na ambavyo watu wa Handeni wanapata. Hii itakuwa ni suluhu ya kudumu Wilaya ya Kilindi kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hili, najua kwa bajeti ya mwaka huu haiwezekani lakini kwa mwakani ututazame kwa jicho la tatu kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Kilindi wana changamoto kubwa sana ya maji. Nadhani nilikuambia jambo hili, naomba nikukumbushe kupitia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikumbusha kwamba Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa vijiji vitatu, Vijiji vya Mtakuja na Nyamaleli lakini mpaka leo Mheshimiwa Waziri havitoi maji na uliahidi utafanya ziara kwenda kuangalia inakuwaje Serikali itoe fedha za kutosha lakini hakuna hata tone la maji ambalo linatoka pale. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kulifanyia kazi suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mheshimiwa Waziri, naomba nizungumzie namna ambavyo hizi mamlaka ndogondogo ambazo huwa hazina uwezo wa kusimamaia miradi, mathalani Kilindi na Miji mingine midogo unakuta Tanga UWASA wao wanasimamia mradi wa Kilindi, Muheza, Handeni, hii ina changamoto kubwa sana Mheshimiwa, changamoto yake ni kwamba unakuta kwamba miradi hii inakuwa ni mingi watu wa Tanga UWASA hawawezi kusimamia miradi yote kwa pamoja wakati mwingine unakuta kwamba Mhandisi au Mkandarasi analalamika kwamba watu wa Tanga UWASA hawajafika kwenye site, ni jambo zuri kabisa Mheshimiwa Waziri kwa sababu mamlaka yetu haina uwezo au mamlaka hizi za wilaya nyingine hazina uwezo, lakini lazima tutazame na namna nyingine ya kusimamia ili miradi hii iweze kwenda kwa speed nzuri sana, nilikuwa naomba Mheshimiwa utazame hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linakuja pale pale kuhusu miradi hii kuna mradi huu Mheshimiwa Waziri wa Maji wa Jiji la Arusha ambao Serikali imepata mkopo kutoka ADB African Development Bank, ni mkopo wa dola bilioni 233.9, ukizi-covert hizi ni takribani milioni 530. Lakini nikuambie mradi ule haujakaa sawa unakwenda taratibu sana, nakuomba Mheshimiwa Waziri tupia jicho pale tusisubiri ripoti ya CAG ije iseme kwamba mradi ule una ufisadi. Na mimi Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hebu katika Wizara yako anzisha kitengo cha ufuatiliaji cha tathimini na ufuatiliaji Monitory and evaluation itakusaidia sana Mheshimiwa Waziri kujua status ya miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge huku tunapata mengi sana Mheshimiwa na sisi tunapozungumza hapa yapo mengi tunayasikia mradi huu wa Jiji la Arusha uangalie sana haupo katika taswira nzuri, Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla wameona kwamba Jiji lile ni Jiji la utalii lazima maji ya uhakika lakini mambo hayaendi vizuri, mimi nakuomba sana litazame hili utapata uhalisia wa kitu hichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mheshimiwa waziri nikuombe tena ulituhaidi kutuchimbia bwawa la kisasa kwenye Kata ya Mafisa ni eneo ambalo takribani miaka 50 wananchi wale hawajawahi kupata maji, nikushukuru sana ulitupatia visima vitano, lakini kwa hali halisi ya eneo lile ni kwamba maji hayapatikani suluhu ya kudumu ya kupata maji pale ni kuchimba bwawa la kisasa kabisa katika Kata ya Mafisa ambayo ina takribani wakazi 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ulitazame hilo. Pia nikuombe tunayo Kata ya Tunguli ambayo ina wakazi takribani 10,000 sasa kuna mradi wa Kata ya Kibati ambao upo katika Wilaya ya Mvomero, ni karibia ni kilometa kumi tu. Nikuombe utume wataalamu wako waweze kuangalia namna waweze kutupatia maji sisi kutokea Wilaya ya Kilombero itaweza kutusaidia kwa sababu tuna vijiji vingi sana ukiangalia kwa asilimia maana yake vijiji 30 kati ya vijiji 102 ina maana ni asilimia 20 au 30 tu ya wakazi wa Wilaya ya Kilindi ndiyo wanaopata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri, nipongeze Taasisi hizi ambazo sizo za Kiserikali kwa kuna watu wa World Vision, AMREF, wao wamekuwa ni wadau wazuri sana, wametusaidia sana kuchimba visima kwa kweli tuwapongeze katika hili. Baada ya kusema hayo mimi naomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri nikupe moyo sana, nasema naunga mkono asilimia, ahsante sana. (Makofi)