Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu nami niweze kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu. Kabla sijajikita kwenye hoja kwanza kabisa ningependa kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kutupatia Profesa Joyce Ndalichako. Profesa Ndalichako namfahamu, mama huyu si Mwanasiasa, kama ni siasa tumfundishe sisi humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Mama Joyce Ndalichako huyu ni mama ambaye ni result oriented character, hivyo ndivyo ninavyoweza kum-define. Kwa hiyo, Profesa Ndalichako nakupa moyo sana, kazi yako inaonekana na kwa hili tunamrudishia sifa na heshima Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye hoja za msingi. Sasa hivi pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameonesha nia dhahiri ya kuweza kuongeza fursa za mkopo kwa vijana wetu wa vyuo vya elimu ya juu, kwa maana ya kwamba kuongeza fursa za rasilimali fedha ili vijana wetu waweze kupata mikopo na kuweza kujimudu kule mashuleni, lakini pia tumekuwa na changamoto kubwa na Mheshimiwa Waziri hapa amekiri, ya masuala mazima ya urejeshaji wa fedha hizi za mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jana tu nimepata taarifa kwamba katika target za Wizara hii au Taasisi hii ya Loans Board ilikuwa ipate bilioni 37 hadi ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha huu yaani tarehe 30 Juni, lakini mpaka mwezi jana ninapoongelea tarehe 30 Aprili kumekuwa kuna marejesho ya shilingi bilioni 22 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nimsaidie Mheshimiwa Waziri, nimesikia hapa akisema pengine ni namba ya defaulters, defaulters wamekuwa ni wengi. Mheshimiwa Waziri naomba nikiri hapana, yawezekana ndiyo kuna namba ya defaulters lakini tatizo si hivyo tunavyoliona leo. Tuna tatizo kubwa ambalo nafikiri bado halina commitment ya Serikali, tatizo hili ni masuala mazima ya ajira kwa kijana mhitimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeshuhudia Mawaziri wetu wengi hapa wamekuja wamefanya mawasilisho ya bajeti. Hata hivyo, nilikuwa makini, of course nilitoka kidogo, niliporudi nikasikiliza vyema, mikakati ya kumtoa kijana aliyehitimu kuingia kwenye soko la ajira. Nikasikia mipango mingi, nimesikia pale kuna masuala ya skills mismatch program ambayo hii ni mkakati wa kuwajengea uwezo vijana wahitimu kwenda kuingia kwenye ajira. Hapa nimejiuliza kijana yupi kwa ajira ipi tuliyoiandaa hapa? Tunahitaji commitment Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumesikia plan ambayo imetoka Wizara ya Ardhi kwamba, kutakuwa na land tenant support system ambayo ina mpango wa kurasimisha kwa kuwapa wakulima wadogowadogo hati za kimila ili waweze kukopesheka katika mabenki ambayo ni mabenki ya TIB, ambayo kuna Mabenki ya Kilimo. Hata hivyo, nikajiuliza hili kijana mhitimu leo anafaidikaje kwenye dirisha hili la TIB, kijana huyu anafaidikaje kwenye mkopo huu ambao tunaambiwa wa Benki ya Kilimo kwa zile rasilimali fedha zilizowekwa pale bilioni 60? hii inakatisha tamaa, tunahitaji commitment ya Serikali kuweza kuwanasua vijana wetu kwenye suala zima la changamoto ya ajira. Tusikae tukijikita kwenye masuala ya defaulters, hakuna kitu kama hicho kuna zaidi ya hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumesikia maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu akitoa maagizo pale TAMISEMI kwamba, isitokee Ofisi ya TAMISEMI inapitisha mpango wa ardhi na matumizi unless kutaonesha ni kiasi gani cha ardhi kitatengwa katika kusaidia wakulima au vijana hawa kuingia kwenye suala zima la kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutenga ardhi tu mbona haitoshi pembejeo ziko wapi? Inasikitisha sana. Mimi nimetoka Kilimanjaro, vijana wangu pale wameshuka mabega, vijana wamepata vilema vya mabega, wamekuwa potters katika kubebea wazungu mizigo yao. Jana tumesikia hapa Kilimanjaro ilivyobarikiwa na suala zima la maliasili, lakini vijana wale wamekata tamaa, mabega yamewashuka, wameishia kuvuta bangi, ni nini hiki? Tunahitaji commitment ya Serikali kwenye suala zima la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona pale na nitamfuata kaka yangu Japhary anisaidie, Kilimanjaro nimeona pale kuna White Elephant moja imejengwa na NSSF, kama kweli kulikuwa na visibility study katika jengo lile, Jengo lile limejengwa kwa bilioni 67 lakini mpaka leo ninavyoongea, mwaka wa tatu huu, kama kurudisha lile jengo siyo zaidi ya bilioni moja. Inasikitisha sana mipango na sera hai-reflect changamoto tulizonazo katika suala zima la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesimama Waziri hapa leo akatueleza changamoto ambayo imetokana na, niseme tu mipango haiko makini katika taasisi zetu hizi. Tumesikia suala la Saint Joseph ambalo naamini kila mtu atakayesimama hapa ataliongela kwa uchungu wa aina yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TCU naifahamu vizuri, nimefanya kazi Kurugenzi ya Elimu ya Juu na nilifanya pale niki-head ile section baada ya Mama Sawasawa kuondoka. Mheshimiwa Mama Ndalichako mume wake amenifundisha kazi, Profesa wangu alikuwa pale juu asubuhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ni mdau na nasema haya kwa sababu nimeyafanyia kazi ofisi kwangu. Hii TCU imegeuka kibanda cha kuchangisha upatu kwa wananchi wasio na uwezo. Pale TCU leo unaenda kusoma nje ya nchi ukirudi ukiwa una degree yako moja unatakiwa utoe shilingi 50,000, kwa masters degree 150,000, kwa PHD unatakiwa utoe karibu 200,000. Unaambiwa hii kupata accreditation letter, accreditation letter ipi na wakati kuna list ya accredited institution unapata kwenye mtandao wa TCU kupata not even authentication letter hii ni accreditation letter ambayo tayari pale kuna list unapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaumiza sana TCU hawa wanaenda leo kuwakagua Saint Joseph tumeona, badala ya TCU wao kwenda kuwakagua wanawa-charge mpaka fees, inasikitisha sana, audit fee Saint Joseph wanalipa na wamelipa kwa miaka yote, leo hii wanawarudisha wanafunzi 489 majumbani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wanapata psychological torture na mimi kama kijana mwenzao ambaye nimesoma kwa uchungu, sitakaa kimya kwenye Bunge lako hili Tukufu, nasema kwa uchungu, naomba vijana sasa waangaliwe, hatutakubali na hatutakuwa wa kupiga makofi kama vijana hawatatengewa hazina yao, kama vijana hawatapewa stahiki yao katika hii nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoongelea TCU kuna masuala yanayonisikitisha sana, tumeambiwa hiki ni kitengo katika kuangalia ubora wa shule, tunasema quality assurance, nimejiuliza wana-insure nini? Mimi nimefanya ofisi ya postgraduate, nilikuwa napokea dissertations zote, wote mliopita hapa, nimekaa nimesoma dissertation ya kila mmoja wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti inasikitisha sana, unakuta dissertation moja inakuwa submitted pale OUT chuo kishiriki, the same dissertation inakuwa submitted in university of Dar es Salaam, tunasema tuna Board inayo-insure quality for good sake, no haiwezekani. Tumeona vitu vya kutisha kwenye Board hii, wamekaa wanacheza mchezo wa kibati halafu wanakuja kusema wana-insure quality, for good sake, hili tutalisema bila kumumunya maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wamesimamishwa hawa, tumeambiwa pale Bodi imesimamishwa lakini haitoshi. Kuna psychological torture ya vijana 489 wako mtaani. Inaumiza sana sisi tumezaa matumbo yetu yamezaa tuwasemee hawa watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vitu vinavyosikitisha, leo anatoka kijana amepata discontinuation kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; lakini mwanafunzi huyo huyo anakwenda kuwa admitted kile Chuo cha pale, kinaitwa not CBE, wanaenda kuwa admitted kwenye vyuo vingine na hali wameshafeli na wanapewa mkopo, hii inasikitisha sana. Una-transfer credit za mwanafunzi ambaye ameshafeli na Bodi inamwongezea mkopo, hii tunasema hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao vijana waliokuwa misplaced kwenye hil,i inabidi tulisemee. Leo kuna vijana waliomaliza kidato cha nne wanakwenda kusoma degree ya ualimu, kwenye fani ya sayansi, unampeleka pale Chuo Kikuu cha Dodoma; for good sake tunawafahamu, baadhi wako funded na World Bank, lakini wapo wengine wamekuwa misplaced baada ya mkorogano wa Chuo cha Saint Joseph, wamepelekwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unataka kutengeneza Mwalimu, ethics za ualimu anazipata wapi pale kwenye mihadhara ya Chuo Kikuu? Hatuwezi kujenga Taifa lililoelimika, hatuwezi kujenga uchumi wa nchi wakati tunapuuza suala zima la ujuzi na maarifa kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kupata maelezo ya kina, juzi Mama Sitta alisimama hapa akashika shilingi kwenye Bunge lililopita, tulidai tuwe na Teachers Professional Board, hili nitalidai pia, kwa udi na uvumba katika Bunge hili. Tunahitaji kuwa na chombo ambacho kita-insure quality ya elimu ya juu kwa vijana wetu hawa, inasikitisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, napenda ku-declare interest. Kuna suala zima tunaita institution charter, kile ni kivuli cha kuficha maovu ndani ya vyuo vikuu. Nilimwomba Mheshimiwa Waziri tushuke twende naye tukaone maovu yanayofanyika kule, viko vitu vya kutisha. Unakuta kiongozi wa Chuo ana magari matatu, ana gari la kubebea mbwa chakula, la kumpeleka mama kwenye kitchen party na la baba. Hatuwezi kukubali, wafanyakazi wetu wanateseka…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mmasi muda wako umekwisha.