Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JULIANA DANIEL SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia, lakini vile vile nimpongeze Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kujadili suala la Bodi ya Mikopo. Tatizo kubwa ambalo linawa-face wanafunzi wengi wa elimu ya juu ni suala la mikopo. Tumeshuhudia katika vyuo vingi kwamba wanafunzi wamekuwa wakifanya maandamano, wakipinga Sera ya Bodi ya Mikopo ambayo kwa kweli ni tatizo kubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, tutakumbuka miaka ya nyuma ukisikia migomo katika Vyuo Vikuu, ilikuwa ni migomo ambayo inapinga sera. Kuna mgomo ambao ulifanyika 1969 ulikuwa ni mgomo wa kupinga sera ya wanafunzi kwenda JKT, kuna mgomo mwingine ukafanyika miaka ya 90, ambao moja kwa moja ilikuwa ni kupinga, suala la cost sharing katika elimu ya juu. Nisikitike kwamba migomo ya sasa hivi imekuwa ni tofauti, wanafunzi wa sasa hawapingi masuala ya sera kama ambavyo ilikuwa zamani. Agenda yao kubwa ni Bodi ya Mikopo, suala la mikopo limekuwa ni jipu kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia chimbuko la matatizo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ni Sheria ambayo imeunda Bodi ya Mikopo. Kuna vigezo ambavyo vimeainishwa, ukisoma Sheria ya hiyo, kifungu cha 17, kimeainisha vigezo vya mwanafunzi kuweza kupata mikopo, kigezo cha kwanza awe ni Mtanzania. Sote tunatambua kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi ni Watanzania, kwa hiyo, bado hiki sioni kama ni kigezo cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kingine lazima awe ni mwanafunzi ambaye anaendelea na amefaulu katika mwaka husika, bado siyo kigezo. Kigezo kingine cha tatu, lazima awe ameandika barua, sidhani kama kuna mwanafunzi nchi hii ambaye atashindwa kuandika barua. Kigezo kingine ni lazima mwanafunzi huyo awe amedahiliwa katika Chuo ambacho kimesajiliwa na Serikali. Sote, tunashuhudia katika nchi ya Tanzania kwamba, kuna utitiri mkubwa sana wa vyuo. Kwa hiyo, suala la mwanafunzi kuweza kudahiliwa bado siyo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa makini hivi vigezo ndivyo vinavyopelekea kuwa na migomo, wanafunzi wanalalamika, wale ambao wanastahili kupata mikopo hawapati na wale ambao hawastahili mara nyingi ndiyo tumekuwa tukishuhudia wakipata mikopo. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali, ni vyema ikaangalia hili suala kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna mkanganyiko mkubwa sana katika suala hili la Bodi ya Mikopo. Suala la kwanza, ni suala la kimtazamo, kwamba kama Bodi yenyewe haijajitambua, kwamba ule mkopo wanaotoa je, ni mkopo au ni hisani na ndiyo maana mpaka leo hii tunashuhudia kwamba hakuna vigezo ambavyo wameviweka, ambavyo mwanafunzi akipata mkopo, vinambana mwanafunzi huyo aweze kurejesha ili wanafunzi wengine waweze kwenda kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkanganyiko wa pili, kwamba hata yule anayepewa mikopo, bado yeye mwenyewe hajajitambua, kwamba je, huu ni mkopo au ni hisani na tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wengi ambao tupo katika Bunge hili tumesomeshwa na hizi kodi za Watanzania, lakini tuulizane ni nani ambaye ameweza kurudisha mkopo huo. Hata Mheshimiwa Waziri ameligusia asubuhi, lakini kusema kwamba Wabunge twende kulipa bado halitoshi, kusema kwamba atatoa majina kwenye magazeti bado haitoshi; lazima kama Wizara, kama Bodi ya Mikopo, mje na mkakati, mje na system ambayo itambana yule ambaye anapewa mikopo na Serikali ili basi aweze kurudisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hata kwa wafanyakazi wanaofanya kazi Serikalini, wanasema kwamba hawajaambiwa wameanza kukatwa, wanashuhudia tu kwenye salary slip wamekatwa, hawajui mikopo hiyo watakatwa mwisho lini. Hii ni changamoto kubwa ya Bodi ya Mikopo na inaonesha kwamba Bodi kimsingi haijajipanga kwa suala hili la kuhakikisha kwamba, hizi fedha wanazozitoa ziweze kuwa revolving fund, ili mtu anapopata na wanafunzi wengine waweze kuja kuzipata. Ndiyo maana tunashuhudia migomo katika nchi yetu haiishi kwa sababu Bodi ya Mikopo haijajipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ya Bodi ya Mikopo, tumeshuhudia kwamba mikopo hiyo inatolewa Dar es Saalam. Nimeshindwa kuelewa , kwamba Bodi ya Mikopo ipo Dar es Salaam, mwanafunzi atoke Mbozi, Ileje, mimi nikienda Dar es Salaam, watajuaje kama kweli Shonza ana sifa ya kupata mikopo. Siyo rahisi kuweza kumtambua, kwa hiyo hii nayo ni changamoto kubwa sana ambayo kama Wizara ihakikishe kwamba inalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishauri Serikali pamoja na Wizara, Mama yangu Ndalichako tunatambua kwamba wewe ni mweledi, una uwezo mkubwa, lakini bado kuna upungufu mkubwa katika Wizara hii ya Elimu. Nishauri Serikali, kwanza sisi kama Wabunge lazima tukubaliane kwamba, mahali tulipofika mpaka sasa hivi ni ngumu kwa Serikali kuweza kutoa michango kwa asilimia mia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika ni ngumu na wala tusijidanganye, lazima Serikali ije na njia mbadala kuhakikisha kwamba hizi fedha ambazo zilikwishaanza kutolewa miaka mingi, kama zingekuwa revolving fund, leo hii tusingekuwa tunajadili bajeti ya mikopo humu ndani, kwa sababu fedha ambazo zimeshatolewa ni nyingi na zingekuwa zimeshazunguka na zingesaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kuishauri Serikali, la kwanza ni vyema wakahakikisha kwamba wanaanzisha mfumo wa kutoa scholarship, kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, kwamba kigezo pekee cha kuweza kupata mkopo, iwe ni ufaulu. Mwanafunzi ambaye amekaa kule Mbozi, ajue kabisa kwamba ili nipate mkopo, lazima nipate division one. Tofauti na ilivyo sasa hivi, kwamba aliyepata division three anapata mkopo, aliyepata division one hapati mkopo. Hiyo ni changamoto kubwa sana, kwa hiyo, kama Wizara tuwe na utaratibu wa kuzawadia bidii, itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nataka kuishauri Serikali ihakikishe kwamba inatoa mikopo asilimia mia kwa zile taaluma ambazo ni taaluma za huduma, kwa mfano Walimu pamoja na Madaktari. Hii itasaidia pia zaidi kuweza kuleta motisha, katika kozi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, niiombe pia Serikali, iangalie namna ya kuhakikisha kwamba Bodi ya Mikopo isihusike moja kwa moja katika kutoa mikopo hiyo. Ni vema mikopo ikatolewa katika Wilaya zetu, kwa sababu kule kwenye Wilaya kuna Taasisi za kifedha, leo hii Serikali imeingia taaluma ambayo naweza nikasema kwamba siyo ya kwake, ni taaluma ya kibenki. Taaluma ya kukopa na kukopeshana ni taaluma za kibenki siyo taaluma ya Serikali. Kwa hiyo Serika iache kufanya biashara, kwa kupitia Bodi ya Mikopo na kuna Taasisi ambazo zipo ambazo ni za kifedha, ziachiwe kazi hizo, hao ndio waratibu zoezi zima la kutoa mikopo, kwenye Wilaya zetu, kwa kuangalia kwamba ni nani anafaa ni nani ambaye hafai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, naamini kwamba itasaidia ili fedha hizo ziweze kuzunguka kama ambavyo tumeshuhudia nchi za wenzetu suala la mikopo mzazi anafanya jitihada kuhakikisha kwamba anamwepusha mtoto wake na mikopo, lakini Tanzania kwa sababu ni bure, ndiyo maana kila mtu ambaye ana uwezo, asiye na uwezo anaomba apate mkopo, kwa sababu ni bure. Naomba suala hili lifanyiwe kazi na likifanyiwa kazi masuala ya migomo yatakuwa yamekwisha katika nchi yetu, lakini wananchi wengi na wanaostahili watapata nafasi ya kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nizungumze kwamba, nimesikiliza kwa makini sana hotuba ya Kambi ya Upinzani. Wamezungumza kwamba, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo ambayo inawanyanyasa wanafunzi ambao ni wa UKAWA. Mimi niseme kwamba, hilo siyo kweli, mimi mwenyewe nilikuwa ni mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nilikuwa upande wa CHADEMA, nilishawahi kuongoza migomo na nikakamatwa nikaenda ndani siku mbili, lakini hakuna siku ambayo nilifukuzwa chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, hata Mama yangu ambaye amewasilisha hotuba hiyo tulikuwa naye pale Chuoni na alikuwa aki-support, hakuna siku ambayo mwanafunzi amerudishwa. Nami kama mwanzilishi wa CHASO katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mama yangu alikuwa akini-support vizuri sana na wala sikuwahi kufukuzwa. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuwe wa kweli. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile suala la kusema kwamba Mheshimiwa Nape amezomewa Mwanza, naomba Waheshimiwa Wabunge, sote humu ndani ni waelewa na kwa sisi ambao ni waelewa wa haya mambo tunafahamu, kwamba haya mambo wanapanga nani asiyejua CHADEMA kwamba wanawapa viroba vijana waende kuwazomea viongozi wa Chama cha Mapinduzi, nani asiyejua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Nape, wewe endelea na kazi yako, piga kazi Watanzania tuko nyuma yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.