Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti, ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda pengine nianzie alipomalizia Mheshimiwa Shonza, amenikumbusha, hii hoja ya kwamba UKAWA wananyanyaswa vyuoni, ni bahati nzuri sana nimkumbushe Mheshimiwa Ally Saleh na Mheshimiwa James Mbatia, nikiwa pamoja na mimi, tulikuwa Chuo Kikuu, tukaonekana tunashiriki mambo ya siasa, tukashughulikiwa na Serikali, hatukuwa UKAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la Serikali kushughulika na wanafunzi kwenye vyuo, ni jambo linguine na suala la kushughulikia wanafunzi kivyama si sahihi kulihusisha na chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana hotuba nzuri ya Mheshimiwa Ndalichako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti imekuja katika wakati ambao ni muafaka, wakati ambao tunataka kuzungumzia suala la elimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ukurasa wa 24 wa hotuba. Ukurasa wa 24 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imejaribu kutoa majibu, kwenye hoja ambayo Mheshimiwa Chumi aliiwasilisha Bungeni hapa kama hoja binafsi, juu ya wanafunzi 489 ambao wanaonekana kwamba hawana sifa za kudahiliwa kusoma kozi ya Ualimu wa Sayansi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie ukweli Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize kwa makini, Wizara ya Elimu imekuwa na tatizo la kubomoa na kufumuafumua mifumo ya elimu katika Taifa letu. Mambo haya yanafanywa, kila Waziri anayekuja, anafumua mifumo iliyotengenezwa na Mawaziri wengine. Ni lini tutakuwa na mifumo ambayo inaheshimika? Ina maana kwamba, kwenye Wizara ya Elimu, hawa ambao ni Maprofesa wameshindwa kabisa kuja na mitaala, mifumo ambayo itatupeleka miaka mingi bila kufumuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uingereza tunasema kuna Cambridge, mpaka leo Cambridge haifi, hivi Tanzania tumeshindwa kuwa na Cambridge ya Watanzania; kila anapokuja Waziri anafumua mifumo ya elimu. Kwa nini nasema mifumo ya elimu inafumuliwa? Inaniuma sana baada ya kuwa na matatizo ya Walimu wa sayansi katika nchi yetu, tukaona kwamba kwa sababu wanafunzi wanapomaliza kidato cha nne, wanapokwenda kidato cha tano, wale ambao wanachukuliwa wamefaulu sayansi, wakimaliza forms six, hawataki kwenda kwenye kozi za Ualimu wa sayansi au kozi za Ualimu, wanaenda engineering, wanaenda kuchukua kozi zingine. matokeo yake shule zetu za Kata na shule za Serikali tumeshindwa kuwa na mikakati ya kuzalisha Walimu wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu hawa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne, wale ambao wana credit nzuri kuanzia C, ndio wanaofaulu kwenda kidato cha tano, wale wanaobaki na alama za D, ndiyo wanaonekana wamefeli. Sasa kukawa na utaratibu, kwamba kwa nini kama wanafunzi wanakwepa kusoma Ualimu wa sayansi, kwa nini tusianzishe utaratibu maalum, ambao waliuita five years integrated bachelor degree program, ili mtaala huu, uweze kuwachukua wanafunzi wa kidato cha nne, ambao wana alama za D, waweze kusoma miaka mitano na siyo miaka mitatu. Katika kipindi cha miaka mitano wawalee, wawanoe, wawapike, iwe kama wamesoma certificate, diploma mpaka degree na wanakuwa wamechujwa hapa katikati, wale wanaofeli wanaondoka, kumaliza miaka mitano tunakuwa na Mwalimu tuliyemfundisha sayansi ili wafundishe shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake Mheshimiwa Waziri anakuja hapa anatuambia kwamba hawakustahili, hawana sifa, wakati wamekuwa na sifa ndani ya mtaala maalum ambao umewasilishwa na Chuo cha Mtakatifu Joseph; kuna nini hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulipokuwa na mahitaji ya Walimu, tulianzisha Walimu wa UPE na wenyewe hawakuwa na sifa, lakini tukawa-qualify na ndiyo wametufundisha sisi, nimefundishwa na Mwalimu wa UPE mimi. Vile viel tulipoona kuna mahitaji ya Walimu, tulianzisha programu miezi mitatu, kumfundisha Mwalimu, wakabatizwa jina la yeboyebo, sijui voda fasta, yote hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya mahitaji ya Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulipokuwa na mahitaji ya Walimu tulianzisha combination ambazo unasoma HG Education, PC Education, CB Education, yote hiyo ilikuwa ni kutatua matatizo ya Walimu. Sasa leo kupitia mtaala maalum mnawaita hawa watoto ni vihiyo haiwezekani, hawa siyo vihiyo. Mheshimiwa Ndalichako, kuniambia kwamba wengine walikuwa arts, kwa nini wameenda kusoma, kwenye arts wanasoma biology pamoja na mathematics masomo mawili hayo ni sayansi hata kama wako arts, wakienda kusoma masomo hayo wamesoma sayansi, leo unasema ni vihiyo; matokeo yake umewafukuza wanafunzi 489. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haiwezekani, huu ni ukatili, unyama na kama umesema umemshirikisha Mheshimiwa Rais, umemshirikisha kwa kumpotosha. Umemweleza mambo ambayo si sahihi na ndiyo maana, Mheshimiwa Ndalichako anataka tucheze muziki anaotulazimisha kucheza sisi, haiwezekani!
Niliwahi kusema hapa kwamba, hatuwezi kukubali kuchezeshwa kama Joyce wowowo hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Ndalichako wanafunzi hawa wamedahiliwa na TCU, wamepewa mikopo na Serikali, itakuwaje wawe wahanga, muwafukuze. Hatutakubali, utakapokuja kuhitimisha, tunataka majibu kwa nini wanafunzi hawa umewafukuza, lazima muwarejeshe hatuwezi kukubali, tumepoteza fedha za Serikali kwa sababu ya matatizo yenu huko TCU, matatizo yenu yasije yakatuletea uhanga kwa wanafunzi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye ada elekezi. Hii ada elekezi mnaelekeza kitu gani? Mkitaka shule za binafsi wapunguze ada, mkitaka shule za binafsi zife ni shule za Serikali kuwalipa Walimu vizuri, kuwa na madarasa, kuwa na nyumba za Walimu, kuweka msosi yaani chakula, hakuna mtu binafsi atakayepandisha ada na ninyi kama mtaendelea kuhakikisha mazingira haya hamyajengi kila mtu ana uchaguzi kupeleka mtoto Ulaya, kupeleka mtoto shule binafsi. Shule binafsi mmezirundikia kodi nyingi sana, mara wapake magari rangi, mara sijui wafanya nini, sasa watarudishaje hizo fedha mnazowaambia wapake rangi magari, kodi kede kede, tunakwenda wapi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM ni gari kubwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni gari kubwa tukiacha gari ku….
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kangi Lugola muda wako umemalizika.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.