Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata nafasi hii. Nianze kwanza kwa kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutujaalia leo kuweza kujadili bajeti hii ya Wizara ya Afya. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli, halikadhalika nimpongeze Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Faustine Ndungulile, Katibu wa Wizara wajina wangu Zainab Chaula pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya na wala haina kificho kwa sababu tunaona na tunashuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ambalo tunaliona katika awamu hii ambayo limefanywa kwa juhudi kubwa ni Taasisi ya Moyo ambayo wameweza kupeleka vifaa vingi vya kisasa wameleta wataalam kutoka nje pamoja na wataalam wa ndani wakisimamiwa na Prof. Jannabi tunawapa pongezi nyingi sana kinachobakia hapo ni kuhakikisha wale wagonjwa ambao wako nje ya mji wa Dar es Salaam, wako nje ya mikoa wako vijijini wengi wapo wanaopata matatizo ya moyo elimu ipelekwe na utaratibu uelekezwe jinsi gani tunaweza tukawatoa kule wakaja kupata huduma hapo kwenye Taasisi ya Moyo Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo limedhihirisha kwamba Wizara yetu pamoja na Serikali imesimama kidete kuweka madaktari wengi, kuweka vifaa tiba vingi matokeo yake idadi ya wagonjwa ambao ilikuwa wanakwenda kutibiwa nje imepungua kutoka 683 2014/2015 hadi wagonjwa 62 kwa mwaka huu tunaongea leo hii inabidi tuwapongeze na ningekuwa kwenye mkutano wa nje ningesema watu wote wawapigie makofi Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye suala la matibabu lakini kupitia bima ya afya, bima ya afya ni suala ambalo ni muhimu kwa Taifa letu bado Serikali ina jukumu la kuhakikisha Watanzania wote wanapata elimu na kujua faida na umuhimu wa bima ya afya. Baadhi ya Wabunge humu ndani wamezungumza jinsi mgonjwa anavyoenda kutibiwa anakutwa na deni kubwa anashindwa kulipa maiti zinashindwa kutolewa kwa sababu ya deni lakini elimu ya bima ya afya ikitolewa vya kutosha yule mtu hatodaiwa na niseme tu kwa maiti za kiislamu lazima itangazwe anadaiwa au hadaiwi? Sasa kama anadaiwa tunamtwisha mzigo ambao haustahili nishauri tu suala la bima ya afya liendelee kutolewa elimu na ikiwezekana uwekwe utaratibu wa kuwa na bima ya afya ambayo kila mtu ataimudu, kila mtanzania atamudu na kila mtanzania ataitumia hiyo bima ya afya kokote kule isiwe tu kama mimi natoka Mkoa wa Pwani basi bima ile iishie Pwani hapana siku nikipelekwa Muhimbili nitatibiwa na tiba gani kwa hiyo naomba hilo nalo litizamwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Sera ya tiba ya wazee hili lifanyiwe bidii wakati ndiyo huu unakuta wazee wengi ukienda huko kwa watani zangu Shinyanga wengi wanapigwa wanauwawa hawana mahala pa kukimbilia mpaka wapate hifadhi kwa hiyo kuna haja ya kutengeneza sera si tu matibabu waangaliwe na mambo mengine muhimu wazee wote watarajiwa ndiyo sisi na wengine wanakuja weze kupata utaratibu mzuri wa sera ya wazee kwa ajili ya maisha yao na tiba halikadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kuhakikisha elimu ya afya ya mama mzazi mtarajiwa ilivyoboreshwa lakini bado kuna haja na kuna kila sababu hawa akinamama huko chini zahanati zetu tumeziboresha, vituo vya afya tumeboresha tuhakikishe basi wanakwenda hospitali. Nimeona takwimu kwenye jedwali humu kwamba wanatakiwa waende mara nne katika kipindi cha ujauzito lakini wengi wamekwenda mara moja wengine mara mbili bado kuna haja ya kuboresha zahanati zetu na vituo vya afya ili mama mjamzito ashawishike kwenda kwa sababu kwingine huduma hazipo zipo mbali kwa hiyo inamuwia vigumu kuna haja ya kuongeza miundombinu ya vifaa tiba na hata watumishi katika zahanati zetu katika vituo vya afya ili waweze kwenda sambamba na mahitaji ya jamii wanayowazunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nagusa kidogo kidogo kwa sababu muda hautoshi.

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)