Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi fursa ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Nami niungane na wenzangu wote kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu Bi. Ummy Mwalimu, lakini pia nimpongeze Naibu Waziri, Dkt. Faustine Ndugulile. Watendaji wote, Katibu Mkuu wa Afya, mdogo wangu Dkt. Zainabu Chaula, pongezi sana pamoja na Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niungane na maoni ya Kamati kwamba fedha zote ambazo hazijakamilishwa kutolewa katika Wizara hii zitolewe kwa wakati ili kusudi waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 121 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu mpango mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017/2018 hadi 2021/2022. Naipongeza sana Serikali kwa kuratibu na kuanzisha hizi Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawake na inasemekana mpaka sasa hivi Kamati hizi zimefikia 7,383. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, napenda tu kufahamu kwamba Wizara imejiandaaje katika kuhakikisha kwamba mpango huu unafahamika zaidi katika jamii yetu hasa kule pembezoni. Kwa sababu mpango huu dhima yake najua ni nzuri sana kuhakikisha kwamba wanawake na watoto wanakuwa hawafanyiwi ukatili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kutunga sheria ya jinsia ili kusudi sasa iweze kuangalia masuala yote kwa jicho la kijinsia. Kama tukiwa na sheria hii naamini kabisa masuala mengi ya kijinsia yanaweza yakafanyiwa utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti zimebainisha kwamba ukatili unaanzia majumbani na wengi wanaofanyia watu ukatili ni ndugu wa karibu. Wizara imejipangaje kuelimisha jamii kuhusiana na suala hili ili kusudi watu wasione tabu kulizungumzia na hatimaye wahusika wanaofanya ukatili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahiki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie kuhusu ustawi wa wazee, wenzangu wengi wamezungumzia. Suala la ile sheria na mimi pia naomba nisisitize kwamba sheria inabidi itungwe kwa sababu nchi yetu imeridhia matamko mbalimbali lakini pia mwaka 2016 Umoja wa Afrika ulikuwa umekubaliana kupitisha mwongozo kuhusu haki za wazee lakini inaelekea kwamba nchi yetu bado haijaridhia makubaliano hayo. Naomba basi ifanyike ili kusudi wazee wetu waweze kupata tija, kwa kweli wazee nao wanahitaji fursa nyingi na mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie kuhusu makao ya wazee. Kwa kweli kuna changamoto kubwa sana, haya makao ya wazee 17 ambayo ni ya Serikali bado yako katika hali mbaya sana. Naomba Serikali ifanye matengenezo yanayohitajika ili kusudi hadhi ya wazee iweze kupatikana kwa sababu inaonekana kwamba wazee wameachwa nyuma sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu masuala ya makuzi ya watoto, hii imezungumziwa katika ukurasa wa 123 hadi 132 katika hotuba hii. Sasa hivi watoto wengi sana ambao tulikuwa tukiwategemea wawe mayaya au walezi wanakwenda kusoma shule. Kwa sababu ya elimu bure watoto wengi wa kike siku hizi tena hawaendi kufanya kazi za majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa naomba nishauri ni kwamba Serikali ione utaratibu wa kufanya ili kusudi viwepo vituo vingi vya malezi ya watoto wakati wa mchana ili kusudi sasa wazazi na walezi waweze kuwapeleka watoto wao katika vituo hivi. Watoto kwa kukaa katika vituo hivi ni ili ustawi wa wale wao uwepo lakini pia waweze kuwa katika mazingira salama. Vituo hivi vitumike kama sehemu bora ya ulinzi na usalama wa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie kuhusu suala la afya ya kinywa na meno. Tatizo ni kwamba sasa hivi watu wengi sana wamekuwa na tatizo hili la afya ya kinywa na meno Serikali ituambie ina mkakati gani wa kwanza kuzuia ili kusudi watu wengi wasipate madhara na pia wataalam wengi wa masuala ya kinywa nao pia wapatikane. Kwa sababu inaonekana kwamba maeneo mengi wataalam hao hawapo, kwa hiyo, wananchi wanapata shida sana kwa ajili ya afya ya kinywa na meno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana.